Mzimu wa Buzwagi wamvaa Mramba

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
803
Mzimu wa Buzwagi wamvaa Mramba

Alitoa msamaha wa kodi ya mafuta ‘milele’


WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Basil Mramba, akiwa Waziri wa Fedha mwaka 2005 alisamehe kodi ya mafuta kwa makampuni ya madini kwa muda wote, uamuzi ambao ulibarikiwa mwaka huu na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alipoidhinisha mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi, Raia Mwema limethibitisha.

Msamaha huo wa kodi umetolewa kwa makampuni yanayochimba madini ya dhahabu pekee na unalenga kuzuia utekelezaji wa Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta ya mwaka 1985 (The Road and Fuel Tolls Act, 1985) inayohusu utozwaji wa ushuru kwa magari na mafuta yote yanayotumika nchini.

Habari zinaeleza ya kuwa Mramba alifanya uamuzi huo Aprili 2005, kipindi ambacho viongozi wa serikali walikuwa ‘likizo’ wakiwa katika harakati za uchaguzi ikiwa ni siku chache kabla ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kufanya mkutano wake mkuu uliomteua Jakaya Kikwete kuwa mgombea wake wa urais.

Kwa mujibu wa tangazo la serikali (GN) namba 99, lililochapishwa katika gazeti rasmi la serikali la Aprili 15, 2005, Mramba alitoa nafuu hiyo ya kodi, “kwa kipindi chote cha Mkataba wa Uendelezaji Madini (MDA) ama uhai wa mgodi husika au chochote kitakachotangulia kati ya mambo hayo mawili.”

Ofisa mmoja mwandamizi wa serikali aliliambia Raia Mwema kwamba, msamaha huo ni matokeo ya udhaifu wa sheria hiyo inayompa mamlaka Waziri wa Fedha kutoa msamaha “anapojisikia kufanya hivyo” hali ambayo inaweza kutumika vibaya na kiongozi dhaifu.

Wakati kifungu cha 7 (2) kinaeleza wazi kwamba ushuru huo unapaswa kulipwa na mtu yeyote anayenunua mafuta, sehemu ya 8 inampa mamlaka makubwa Waziri wa Fedha kuweza kutoa msamaha wa kodi kwa jinsi atakavyoona inafaa.

“Waziri anaweza, kwa kutangaza katika gazeti la serikali (Government Gazette) kutoa msamaha kwa mtu ama chombo chochote (taasisi ama kampuni) ama gari lolote kuguswa na kifungu cha sheria ya ushuru wa barabara na mafuta, msamaha ambao unaweza kuwa wa jumla jumla ama unaweza kupangiwa kipindi maalumu kulingana na waziri atakavyoona inafaa,” inaeleza sehemu ya 8 ya sheria hiyo.

Anayetajwa kuanza kutumia mamlaka hayo kutoa msamaha kwa makampuni ya uchimbaji dhahabu alikuwa Daniel Yona, akiwa Waziri wa Fedha, siku ya kuadhimisha miaka 22 ya kuzaliwa kwa CCM, Februari 5, 1999, lakini yeye alitoa msamaha huo kwa mwaka mmoja wa kwanza tu baada ya kuanza rasmi kwa uzalishaji wa dhahabu.

Habari zinasema kwamba Mramba ‘alimzidi kete’ Yona, kwa yeye kuamua kutoa msamaha huo kwa kipindi chote cha uhai wa migodi ya dhahabu, jambo ambalo limeanza kugusa hisia za watendaji serikalini wakiwamo wajumbe wa kamati iliyoundwa awali kwa maelekezo ya Rais Kikwete kupitia upya mikataba ya madini.

Kamati hiyo iliyoongozwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Laurence Masha, ilionyesha wazi kutoridhika na kipengele hicho na kupendekeza mabadiliko makubwa katika kutolewa kwa misamaha hiyo.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo walitoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mipango na Uchumi na Uwezeshaji, Wizara ya Fedha, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Sheria na Katiba, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Jiolojia, Benki Kuu na STAMICO.

Kamati hiyo ilielezea jinsi ambavyo makampuni mengi ya madini yanatumia mafuta mengi kutokana na kutotumia umeme wa gridi na badala yake wanatumia jenereta za dizeli wakati wote na kushauri kuwapo kwa marekebisho katika misamaha ya kodi kwa makampuni ya madini.

Mtaalamu mmoja wa uchumi alilieleza Raia Mwema kwamba kwa siku makampuni ya mafuta hutumia zaidi ya lita 300,000 za mafuta kwa uzalishaji, kiwango ambacho husamehewa kiwango kikubwa cha fedha kwa kila lita kinachokadiriwa kuwa takriban Sh bilioni 46 kwa mwaka.

Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, hakuzingatia kabisa ushauri huo wa kamati alipokwenda kusaini mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi kati ya serikali na kampuni ya Pangea Minerals Limited, kampuni tanzu ya Barrick. Katika mkataba wa Buzwagi kifungu cha 4.4.3 kimeweka wazi kwamba Pangea hawatawajibika kulipa ushuru wa mafuta kwa kuzingatia marekebisho yaliyofanywa na Waziri Mramba.

Karamagi aliliambia Bunge mjini Dodoma kwamba mkataba wa Buzwagi umezingatia mapendekezo ya kamati ya madini iliyoundwa kwa maelekezo ya Rais.

Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) akijibu bungeni hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, aliyetaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuhusu kusainiwa kwa mkataba wa Buzwagi, Waziri Karamagi alisema mapendekezo ya kamati ya Rais yametekelezwa katika kusaini mkataba wa Buzwagi.

“Mheshimiwa Kabwe Zitto, anasisitiza kuwa zoezi la kudurusu mikataba bado linaendelea. Mtoa hoja labda anachanganya tena zoezi la kudurusu mikataba na zoezi linaloendelea na kudurusu Sheria ya Madini ya Mwaka 1998 na Sheria zinahusu mfumo wa kodi katika sekta ya madini; kitu ambacho ni kipana zaidi na kinawahusu wadau wote yaani, wawekezaji wakubwa, wawekezaji wadogo na wote wanaojihusisha na utafiti katika sekta ya madini. Akielewa hili mtoa hoja atabaini kuwa maagizo ya (kamati ya) Rais yalitekelezwa kikamilifu na matokeo yake yameshaanza kujitokeza,” alisema Karamagi.

Mbali na msamaha katika ushuru wa mafuta, Mkataba wa Buzwagi pia umepingana na ushauri wa Kamati ya Masha iliyoundwa kwa maelekezo ya Rais kuhusu ulazima wa makampuni ya madini kuishirikisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika ufunguaji wa akaunti katika offshore banks za nje. Mbali ya kuonyesha wasiwasi wake kuhusu makampuni mengi ya madini kutozingatia kipengele hicho, Kamati ya Masha ilipendekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kina chini ya usimamizi wa pamoja wa Wizara ya Nishati na Madini na BoT.

Mkataba wa Buzwagi uliosainiwa na Karamagi nchini Uingereza, unazingatia kuwapo kwa kibali cha BoT katika kipengele cha 5.1 lakini katika kipengele cha 5.2 mkataba huo unaweka wazi kwamba BoT itakaposhindwa ama kukataa kutoa ruhusa hiyo katika kipindi cha siku 30, kampuni husika itaendelea na mpango wake wa kufungua akaunti bila kuhitaji ruhusa hiyo. Sakata la Buzwagi liliibuka bungeni baada ya Zitto kuhoji, pamoja na mambo mengine, usiri wa mkataba huo ambao ulisainiwa nchini Uingereza, lakini Karamagi alitetea kwa nguvu zote akidai kwamba hakukua na ukiukwaji wowote wa sheria na taratibu na ulizingatia maslahi ya taifa.

Katika kuhoji kwake, Zitto alitoa maelezo akitaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza suala hilo, lakini hoja yake ilishindwa kwa kura na wabunge wa CCM japo sasa wengi wanaona walifanya makosa kuzuia hoja hiyo.

Hoja hiyo pia ilimponza Zitto kwani Mbunge wa Mchinga kupitia CCM, Mudhihir Mohamed Mudhihir, aliwasilisha hoja akidai kwamba Zitto alisema uongo wakati akimtuhumu Karamagi, na kupendekeza afungiwe.

Bunge kwa kura nyingi za wabunge wa CCM walipitisha uamuzi wa kumfungia Zitto, kifungo kilichomalizika katikati ya Novemba, baada ya kuigharimu CCM kwa kiasi kikubwa kutokana na wananchi wengi kuonekana kumuunga mkono Zitto na hata kuwazomea viongozi wa serikali na wale wa CCM.

Kabla hata ya Zitto kumaliza ‘kifungo’, Rais Kikwete aliunda kamati ya kupitia mikataba na sheria za madini, huku mbunge huyo kijana akiwa mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo na kuzua maswali mengi kuhusu msimamo wa Rais kuhusu suala hilo.

Source: Raia Mwema
 
Back
Top Bottom