Mzimu unaotabasamu

MZIMU UNAOTABASAMU-19

Mlinzi aliyeondoka kwa lengo la kwenda kumuita mzee Daniel alirudi huku akiwa peke yake, alimwambia mwenzake kwamba alipiga simu lakini mzee huyo alikuwa kwene kikao muhimu na hivyo hakutaka kabisa kutoka ndani ya lengo la benki hiyo. Hilo likamfanya Tim kupumua kwani kama angepambana kwa maneno na walinzi wale ilikuwa ni lazima kuwashinda na hivyo kumwachia.
Aliendelea kujitetea kwamba hakuwa mwizi na hakukuwa na kitu chochote alichoiba zaidi a kuokota chupa za maji kama alivyotakiwa kufanya. Hawakutaka kuridhika, wakampekua kuona kama alikuwa na kitu chochote kile lakini hawakumkuta na kitu chochote zaidi ya simu.
“Hii simu ni yako?” aliuliza mlinzi mmoja.
“Ndiyo bosi!”
”Una uhakika?”
“Ndiyo!” alijibu Tim.
Hakutaka kuishia hapo, ili kuwaaminisha kwamba simu ilikuwa yake akaanza kuwaambia majina yaliyokuwa ndani ya simu ile, meseji picha na kila kitu ambacho aliamini kwamba walinzi hao wangemwamini. Waliridhika na majibu yake na hivyo kumruhusu kuondoka huku wakimtaka kutokufika tena katika benki hiyo.
Hilo halikuwa tatizo, kitu alichokuwa akikihitaji alikipata, akachukua kiroba chake kilichokuwa na chupa za maji na kuondoka mahali hapo. Breki ya kwanza ilikuwa nyumbani kwake, akaoga na kuwapigia simu wenzake na kuwaambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari, alizichukua namba zile na alikuwanazo mahali hapo.
“Inabidi tuonane!” alisema Mike.
Ndani ya nusu saa tayari walikuwa wameonana, wakakaa katika chumba ambacho mara nyingi hukaa na kupanga mipango yao, Mike akaichukua simu yake na kuanza kudukua namba iliyokuwa katika pleti ile.
Namba zikatoka, za juu zilisomeka 01 na chini kulikuwa na namba iliyosomeka 4. Hii ilimaanisha kwamba katika mtiririko wa namba walizipata namba mbili, namba ya kwanza ambayo ilikuwa hiyo ya mzee Daniel ambayo ni namba 4 na namba ya Cecilia ambayo ilikuwa ni ya tatu katika mtiririko wa namba walizokuwa wakizihitaji ambayo ilikuwa ni namba 9.
Bado kulikuwa na namba mbili walizokuwa wakizihitai, kulikuwa na namba ya Sebastian Kanayo na mwanamke aliyeitwa kwa jina la Pamela Ogwu. Kuhusu kuipata namba ya Sebastian haikuonekana kuwa kazi kubwa kwani tayari David aliweka ukaribu na mzee huyo na kuamini kwamba kama angeutumia vizuri basi angeweza kuipata bila matatizo.
Kitu cha kwanza kabisa walichotakiwa kufanya kilikuwa ni kwenda kuaribu ofisini kwake kwa kuamini kwamba inawezekana pleti yake ilikuwa ofisini. Mipango ikapangwa na hivyo Joshua akatakiwa kuongozana na David mpaka ofisini kwa mzee huyo na kuzungumza naye huku wakiwa na lengo la kuichukua namba aliyokuwanayo katika pleti yake.
Asubuhi ya siku iliyofuata David akampigia simu Cecilia na kuzungumza naye sana. Alimwambia kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi, alimwambia jinsi alivyokuwa akimpenda na mwisho kabisa alimwambia kwamba alihitaji msaada mkubwa kutoka kwake.
“Msaada gani mpenzi?” ilisikika sauti ya Cecilia kwenye simu.
“Nina rafiki yangu ninafanya naye biashara, anahitai kuonana na mzee Sebastian,” alisema David.
“Hilo si tatizo, anaweza kuonana naye.”
“Hapana. Najua anaweza, nimekuomba wewe kwa kuwa ndiyo unaua muda wake, ni muda gani anakuwa na nafasi lakini pia ningependa utupeleke mpaka ofisini kwake, nyie watu wakubwa bwana,” alisema David na kumalizia kwa kumsifia kidogo.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, akamwambia kila kitu kuhusu ratiba ya mwanaume huyo na mwisho wa siku akamwambia kwamba angemsaidia mpaka kuonana naye, hivyo alitakiwa kwenda ofisini.
Simu ilipokatwa, haraka sana David akampigia simu Joshua na kuomba kuonana naye,. Hakukuwa na tatizo, wakaonana na kuyapanga, walipomaliza wakaanza kuelekea katika beki hiyo kwa lengo la kuonana na mzee huyo.
Huko, tayari Cecilia alikuwa amekwishayapanga, hawakupata tabu, walipofika tu, haraka sana akawachukua na kuwapeleka ofisini kwa mzee Sebastian na kuanza kuongea nayo. David hakuwa na haja ya kujitambulisha, alifahamika na mzee huyo kwani haikuwa mara yake ya kwanza kuingia ndani ya ofisi hiyo.
Huku wakiendelea na mazungumzo, Joshua akatoa simu yake na kuifungua programu ya Pentagon 2.4 na kuanza kuangalia kama ilishika pleti ile.
“Yes!” alijikuta akisema kwa sauti kiasi kwamba kila mmoja akamwangalia.
“What is wrong?” (kuna tatizo gani?) aliuliza mzee Sebastian.
Joshua akajua kwamba alikosea na ilikuwa ni lazima kudanganya. Akawaambia kwamba kulikuwa na ombi la biashara ya kuingiza pembejeo nchini Nigeria aliliomba serikalini na muda huo alitumiwa barua pepe kuambiwa kwamba serikali ilikubaliana naye na ndiyo maana akashangilia mara baada ya kuiona barua pepe hiyo.
Kila mmoja akamwamini japokuwa David alijua kabisa rafiki yake huyo alidanganya. Programu ile ikaanza kudukua namba kutoka katika pleti ya Sebastian aliyokuwa ameiweka katika sanduku la kuhifadhia pesa tena huku akiwa amefunga kwa kutumia namba maalum.
Hilo kwao hakukuwa na tatizo, hawakutaka kufungua sanduku hilo bali ile programu iliweza kuidukua vizuri pleti ile na kuanza kuhesabu namba, ilikasoma asilimia, ilipofika asilimia mia moja, ikaandika completed ikiwa na maana kwamba imekamilika. Hapohapo akamkanyaga David kwa chini kama ishara ya kumwambia kuwa kazi ilikamilika.
“Tutakuja kuzungumza vizuri kesho, kuna mambo mengi sana kuhusu biashara tutaongea ila la muhimu ni kuhitai mikopo,” alisema David.
“Hakuna shida. Mnakaribishwa sana. Halafu hukuniambia harusi lini,” alisema Sebastian.
“Bado hatujapanga ila tutakujulisha,” alisema David, hapohapo akamwangalia Cecilia na kumkonyeza.
Wakaondoka ofisini hapo huku wakiwa na furaha tele, hawakuamini kama kweli kuipata namba ya pleti hiyo ilikuwa rahisi kama vile. Walipofika nyumbani, wakawapigia simu wenzao na kuanza kuifanyia kazi namba namba ya pleti ile.
Programu yao ikaonyesha namba ya juu kuwa ni 04 na ya chini ilisomeka 3. Wakafanikiwa kwa kiasi kikubwa mno, kwa kuzipata namba za watu watatu na kubaki mmoa ilionyesha dhahiri kwamba wangekwenda kufanikiwa na hivyo kuanza kuiba pesa kama walivyokuwa wamepanga.
“Amebaki mtu mmoja ambaye ni Pamela Ogwu. Huyu ni mwanamke mtu mzima, ameokoka, anaishi na mume wake, ni mwanamke anayemwamini sana Mungu,” alisema Mike, alionekana kumjua sana mwanamke huyo.
“Ameokoka? Tutaweza kufanikiwa kweli?” aliuliza David.
“Ndiyo! Tutafanikiwa kwa urahisi sana. Kwa kuwa kuipata pleti ya mwanamke huyu ni jukumu langu, naomba nilifanyie kazi,” alisema Mike.
“Utafanyaje?”
“Nitajifanya mimi ni mchungai kutoka nchini Ghana ambaye nitakuwa na mkutano wa kimataifa hapa Nigeria, tutatengeneza matangazo na kuomba kanisa lao ndilo linipokee, nitaifanya nimetoka nchini Marekani, tutatengeneza tovuti ya uongo ya kuonyesha miujiza yangu huko nilipokuwa,” alisema Mike.
“Mmh!” aliguna Mercy.
“Ndiyo hivyo! Mercy utakuwa mke wangu,” alisema Mike.
“Haina shida, tufanye hivyo!” alisema Mercy.
Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutengeneza tovuti ya muda ya kumzungumzia mchungaji huyo wa kimataifa. Wakanunua ndevu za bandia, wakamvisha, wakamuwekea nguo na kuzifunga vizuri tumboni ilio ionekane kama kitambi. Walifanya kila kitu na kumpiga picha na kuziweka katika tovuti ile na baada ya siku mbili wakaanza kumtangaza kwamba alikuwa mchungaji aliyekuwa akifanya miujiza mikubwa duniani.
****
Mchungaji Philip Ogwugwu wa Kanisa la God’s Power nchini Nigeria alipokea barua pepe kutoka kwa mtu aliyeitambulisha kwa jina la Nehemiah Waka. Aliifungua barua pepe hiyo alikuta ikiwa inahusu mkutano mkubwa uliotakiwa kufanyika jijini Lagos ambapo mchungai huyo wa kimataifa angekwenda kuifanya huduma hiyo nchini humo.
Jina la mchungai huyo lilikuwa geni, hakuwahi kumsikia lakini baada ya kutumiwa video ya kutengeneza ikionyesha jinsi alivyokuwa akifanya huduma yake katika mikutano mbalimbali nchini Japan, Misri, Uingereza na sehemu nyingine duniani kote akajikuta akishikwa na hamu ya kumuona mchungaji huyo akifanya huduma.
Barua pepe hiyo ilieleza kwamba kwa kipindi chote ambacho angekaa nchini Nigeria kwa lengo kuhubiri neno la Mungu angependa kufikia katika kanisa lake na kutoa huduma hilo huku akilitaka kanisa hilo lisimamie maandalizi yote.
Hilo halikuwa tatizo, kwa mchungaji Philip kwake ilionekana kama baraka mojawapo, akakubaliana naye na hivyo haraka sana kuwaambia washirika wake kwamba baada ya wiki moja kungekuwa na mkutano mkubwa wa injili hapo Lagos hivyo watu walitakiwa kujiandaa.
Siku hiyo hiyo matangazo yakaanza kubandikwa kila kona, kwenye vituo vya redio matangazo kuhusu mkutano huo yakaanza kutangazwa, kila mtu alishangaa, hakukuwa na mkutano uliokuwa ukitangazwa kwa ukubwa kama huo ambao ulitarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini humo.
Kwa kuwa walikuwa na pesa, Mike akamtumia mchungaji huyo kwa ajili ya kufanya kila kitu. Hawakuwahi kuonana sehemu yoyote ile lakini kwake, mchungaji huyo wa kimataifa alionekana kuwa kila kitu, alijawa upako na nguvu kubwa ya Mungu.
Baada ya siku mbili, mchungaji Nehemiah Waka ambaye ndiye alikuwa Mike akaanza akaingia nchini Nigeria huku akiongozana na mkewe, Mercy aliyejiita kwa jina la Maggie.
Washirika wote wa Kanisa la God’s Power walikuwa uwanjani hapo, kila mmoja alikuwa akiimba kwa furaha, kitendo cha kutembelewa na mchungai huyo kwa lengo la kufanya huduma kwao kilionekana kuwa baraka kubwa kwani kulikuwa na makanisa mengi nchini humo ila yote hakuyaona akaliona kanisa lao.
Alipoteremka ndani ya ndege, washirika wakachukua khanga na kwenda kuziweka chini, Mchungaji Nehemiah hakutakiwa kukanyaga chini, alitakiwa kutembea juu ya khanga mpaka anaingia ndani ya gari. Alipoingia tu, gari likawashwa na kuondoka uwanjani hapo huku nyuma washirika wa kanisa hilo wakilifuata kwa kuimba nyimbo za kusifu jina la Mungu aliye hai.
“Wamekwisha! Yaani mbwembwe zote hizi kisa pleti! Hakuna atakayepona,” alisema Mike huku akicheka, kila kitu kilichofanyika kilikuwa kweli ila kwake, kila kitu aliona kama maigizo alichokitaka ni kuona akifanikiwa kwa kile akitakacho tu.
***
Kila mmoja aliamini kwamba mtu aliyekuwa amefika nchini Nigeria alikuwa mchungaji kweli. Muonekano wake, jinsi alivyoongea kila mtu alihisi kabisa kwamba Mike alikuwa mtumishi wa Mungu. Watu wengine waliokuwa wakimfuata na kuzungumza naye walimfuata kwa unyenyekevu kiasi kwamba mpaka yeye mwenyewe alishangaa.
Matangazo yalizidi kubandikwa mitaani kwamba hatimaye mchungaji huyo wa kimataifa alifika nchini Nigeria na ni mahubiri tu katika mkutano wa injili ndio uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa. Wale waliokuwa nje ya Jiji la Lagos wakaanza kulisogelea jiji hilo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo ambao uliaminika kuwa mkubwa mno kufanyika jijini humo.
Kwa wagonjwa, wakajitolea kwenda kwa ajili ya kuombewa, kwa watu wasiokuwa na ajira, kila mtu aliona kuwa hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yake na ilikuwa ni lazima kwenda katika mkutano huo.
Lengo kubwa alilokuwa nao Mike ni kukutana na mwanamke aliyeitwa kwa jina la Pamela Ogwu kwa ajili ya kuchukua namba kutoka katika kifaa kidogo kilichokuwa na umbo kama andazi ambapo ndani yake kulikuwa na namba walizokuwa wakizihitaji.
Siku hiyo usiku yeye na Mercy wakalala katika hoteli nzuri ya nyota tano. Huko, wakawapigia simu wenzao na kuwaambia kilichokuwa kimeendelea. Kila mtu alifahamu, walifuatilia kwa karibu kila kitu kilichokuwa kikiendelea na hivyo walijipanga kwa ajili ya kupokea namba yao ya mwisho kwa mikono miwili na hatimaye waweze kufanya uhalifu katika Benki Kuu hapo Nigeria.
Mipango ikasukwa upya, ilikuwa ni lazima wahakikishe kila kitu walichokuwa wakikihitaji wakikipata haraka sana. Usiku wa siku hiyo ulikuwa ni wa kupanga mipango tu na siku iliyofuata Mike akataka kuonana na mchungaji Phillip ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wake, alitaka kukaa na kuzungumza naye kutokana na kile kitu ambacho alionyeshwa ndotoni.
Asubuhi ya siku hiyohiyo haraka sana mchungaji Phillip akaelekea kwenye hoteli hiyo, alipomuona Mike aliyekuwa akijulikana kwa jina la Nehemiah, akamsalimia na kukaa sehemu ya maongezi na kuanza kuzungumza.
“Mungu amenionyesha jambo moja kubwa sana nilipokuwa katika maombi yangu usiku,” alisema Mike huku akimwangalia mchungaji huyo.
“Kitu gani mtumishi?”
“Kuna mwanamke anasali kwako, amekamatwa kwa nguvu za giza. Ameolewa, amefungwa kizazi, amebahatika kupata mtoto mmoja tu, ndoa yake imekuwa ya masimango, ndugu wanamchukia, hana matumaini ya kupata mtoto mwingine. Mungu amenionyeshea mwanamke huyo yupo kanisani kwako,” alisema Mike huku akimwangalia mchungaji huyo.
Alimfahamu Pamela, historia ya maisha yake ilikuwa mikononi mwake, aliyajua matatizo aliyokuwanayo na alitaka kuyatumia hayohayo ili ionekane kwamba alikuwa mtumishi wa Mungu kweli. Mchungaji Phillip alipojifikiria, kweli kulikuwa na mwanamke huyo aliyekuwa na matatizo hayo yote.
“Ni Bi Pamela!” alisema huku akionekana kushangaa.
“Haleluyah! Ni huyohuyo. Ni mwanamke mwenye uwezo kifedha, si ndiyo?” alisema Mike na kuuliza.
“Ndiyo!”
“Mungu anataka kufanya jambo, anataka kumpatia furaha yake iliyopotea kwa kipindi kirefu,” alisema Mike.
Mike alijua kuzungumza, aliyafumba macho yake kama mtu aliyekuwa akiongea kwenye hisia kali mno. Mchungaji Phillip akamwamini kwani mwanamke aliyekuwa akimtaja alimfahamu kabisa, alikuwa Pamela, mwanamke aliyekuwa na pesa ambaye alikuwa akifanya kazi zake katika Benki Kuu nchini Nigeria.
Siku hiyohiyo Mike akataka kuonana naye kwa lengo la kufanya naye maombezi. Hakukuwa na tatizo, mwanamke huyo akapigiwa simu na kuonana kanisani ambapo huko akafanyiwa maombezi huku muda wote Mercy akiwa bize na simu yake kuangalia kama pleti ile ilikuwa imesoma.
Japokuwa walikuwa wamewahi sana lakini siku hiyohiyi Mike alitaka kukamilisha kila kitu. Akamwambia mwanamke huyo kwamba alitaka kwenda nyumbani kwake kwa lengo la kumfanyia maombezi kwani shetani alikuwa ameifunga nyumba kwa ujumla na ndiyo maana hakukuwa na furaha ndani ya ndoa yake.
Muda wote aliokuwa akiambiwa na Mike, Pamela alikuwa akilia tu, moyo wake ulikuwa ukimuuma kwani kila kitu alichokuwa akikizungumza Mike kilikuwa ni ukweli kabisa.
“Mungu ana mipango na maisha yako, ana mipango na ndoa yako. Umekosa furaha, anataka kukurudishia furaha,” alisema Mike huku akimwangalia mwanamke huyo.
Alipomaliza, akamwambia apige magoti na kuanza kumuombea. Pamela alikuwa na imani na mchungaji huyo, wakati ameshikwa kichwa na kuanza kuombewa, alihisi kabisa mwili wake ukiingia kwenye mabadiliko yaliyomfanya kuamini asilimia mia moja kwamba watu hao walikuwa watumishi wa Mungu kwa asilimia mia moja.
Walipomaliza, wakamwambia kwamba ilikuwa ni lazima kwenda nyumbani kwake na kufanya maombezi ya nyumba nzima kwani shetani alikuwa ameweka nguvu zake katika nymba hiyo. Hilo halikuwa tatizo, wakaondoka na kuelekea nyumbani huko huku njia zima Pamela akiwa analia tu kwani ali
“Mungu anakwenda kutenda muujiza Pamela, Mungu anakwenda kuzungumza nawe katika maisha yako,” alisema Mike kwa sauti ya chini kabisa.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika nyumbani kwake. Muda wote Mercy alikuwa kwenye simu yake, alikuwa akiangalia kama pleti ile ilikuwa ikisoma katika programu ile waliyokuwanayo au la. Gari liliposimamishwa, wakateremka na kuanza kuelekea ndani.
Muda wote walipokuwa wakitembea Mike alikuwa akiomba tu, hakutaka kunyamaza, kwa maigizo aliyokuwa akiyafanya ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba mwanamke huyo anamwamini kwa asilimia mia moja.
Wakafika sebuleni, bado programu ile haikuonyesha kitu chochote kile. Mercy akampa ishara Mike kwamba bado mambo hayakuwa yamesoma pale walipokuwa. Hilo halikuwa na tatizo, waliamini kabisa kwamba ile pleti ilikuwa ndani ya nyumba hiyo. Alichokifanya ni kumfanyia maombezi pale sebuleni na kisha kumwambia kwamba waende chumbani kwa lengo la kufanya maombezi huko kwani shetani alikuwa amefanya mambo mengi maovu katika nyumba hiyo.
“Bado Mungu ana kazi na wewe, ni lazima twende tukafanye maombezi kila kona ya nyumba hii,”alisema Mike.
Hilo halikuwa tatizo. Walipohakikisha wamefanya maombezi sebuleni wakaanza kuelekea chumbani huku wakiwa na mchungaji Phillip ambaye muda wote alionekana akiomba na kuona kwamba Mike alikuwa mchungaji kweli na si mwizi kama ulivyokuwa ukweli wenyewe.
Walipoingia tu, programu ile ikakubali, ikaonyesha maneno yaliyosomeka Plate Accepted yaani pleti imekubali. Hapo hapo Mercy akampa ishara Mike kwamba pleti imekubali na hivyo kubaki chumbani humo wakifanya maombezi huku programu ile ikiendelea kupakua namba za kwenye pleti hiyo iliyokuwa ndani droo ya kitanda.
Asilimia zikaanza kupanda, wakati Mercy akiwa bize na simu yake, Mike alikuwa akifanya maombez kuiombea nyumba hiyo. Pamela alikuwa akilia, moyo wake ulimuuma mno, maisha yake yalikuwa yenye kuumiza, kila alipokuwa akiwafikiria ndugu zake walivyokuwa wakimsema, alisikia kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake.
Waliendelea kubaki chumbani humo mpaka Mike alipomaliza maombezi, Mercy akamshtua kama kumpa ishara kuwa programu ilimaliza kazi yake na hivyo walitakiwa kuondoka. Hakukuwa na muda wa kupoteza, haraka sana wakaelekea sebuleni ambapo huko akawaambia kwamba lingekuwa jambo jema kabisa kama siku inayofuata wangekutana tena kanisani.
Wakaondoka! Njiani walikuwa wakizungumza, waliziangalia namba zilizokuwa kwenye pleti ile huku wakiwa garini. Walifurahi, walikuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Namba ya juu ilikuwa ikionyesha 02 na ya chini ilikuwa ikionyesha 7.
Huo ndiyo ulikuwa mtihani wa mwisho waliokuwa wamepigana nao kwa kipindi kirefu. Hatimaye namba zikawa zimekamilika, wakazipanga kama zilivyotakiwa kuwa na kusomeka namba 4793. Hizo ndizo zilikuwa namba za kuingilia katika database ya benki hiyo.
Ikawapa uhakika wa kupata utajiri mkubwa. Walipofika hotelini, hawakutaka kukaa, mchungaji Phillip alipoondoka tu nao wakatoka na kuelekea nyumbani ambapo huko wakakutana na wenzao na kuwaambia kwamba walifanikiwa kuipata namba waliyokuwa wamebakiza na hivyo mtitiririko kusoma 4793.
“Well done,” (kazi nzuri)
Wakapongezana kwa kazi kubwa waliyokuwa wamifanya, hawakutaka kuchelewa, kila kitu kilitakiwa kufanywa haraka sana. Siku iliyofuata wakakaa chumbani huku kila mmoja akiwa na kompyuta yake aliyoiunganisha internet. Walikuwa wakipekua huku na kule, waliingiza codes, wakafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanaingia katika database ya Benki Kuu ili waweze kufuta mafaili na kuhamisha pesa katika akaunti zao za siri.
Haikuwa kazi ndogo, ilikuwa kubwa iliyowasumbua mno. Mpaka yanakatika masaa matano bado hawakuwa wamefanikiwa kwani wataalamu wa kompyuta ambao walihakikisha database hiyo inakuwa salama waliweka ulinzi wa uhakika uliowafanya kushindwa kabisa.
Hawakutaka kukubali, walipambana usiku na mchana, wakakesha wakiwa na kompyuta zao, walihakikisha wanafanya kazi kwa umakini kabisa. Hakukuwa na mtu aliyelala, wakati mwingine walipochoka walifanya kazi nyingine lakini baadaye kurudi na kuendelea na kazi yao.
Mpaka siku ya tatu inaingia, bado hawakuwa wamefanikiwa, walikuwa wakiendelea kuingia ndani ya database. Codes zilikataa, kila walipofanya hivi na vile, codes ziliwaambia kwamba walitakiwa kufanya hili na lile.
Vichwa vyao vikachoka, wakaona dalili za kukosa pesa hizo zikionekana waziwazi. Ilikuwaje wafanye kazi kwa siku nyingi halafu siku za mwisho washindwe na wakati tayari walikuwa na namba? Hilo liliwauma lakini hawakutaka kuacha. Naila bilioni tano ziliwachanganya, wakaongeza kasi ya kufanya kazi kuhakikisha wanapata pesa hizo na kuwaliza viongozi wa benki hiyo.
 
Back
Top Bottom