Mzee Mwinyi katika hili la kuongeza muda wa Asante kwa Rais Magufuli hapana, tunakukatalia kwa nguvu zetu zote

Missile of the Nation

JF-Expert Member
May 24, 2018
13,483
51,056
Mzee wetu mzee Mwinyi, Shikamoo

Mimi ni mtanzania, kwa umri niseme labda ni mjukuu wako, ni Mtanzania, naipenda nchi yangu na ningependa iwe na mustakbali mwema.

Mzee wetu nimekusikia mara kadhaa ukieleza hamu yako ya kumuona Rais aliyeko madarakani akiongezewa muda wa kutawala kinyume cha katiba ya sasa inavyotaka.

Mzee wetu, mimi kama mtu mzalendo, mwenye uchungu na nchi hii, nimeitafakari kauli yako, hapo mwanzo nilitaka niiache kama ilivyo lakini nikaona nitakuwa sijaitendea haki nchi yangu kama nitaiacha hilo suala lipite hivihivi bila kulizungumzia, hususan baada ya kuona kuwa hilo suala linaweza kuwa sumu ya amani ya nchi yetu na mustakbali wake, Mheshimiwa rais mstaafu baba yetu mzee Mwinyi hebu tusemezane katika haya yafuatayo kuhusu suala hilo:

1. Je, ni nini lengo la kuweka ukomo wa utawala katika katiba?

Mzee Mwinyi bila shaka ulikuwepo wakati Baba yetu wa Taifa alivyoongoza Taifa letu katika mchakato wa mabadiriko ya katiba yaliyohakikisha kuwa tunaweka ukomo wa madaraka katika katiba mwaka 1984, Kwa hakika Baada ya vuguvugu la wananchi katika Afrika kutaka kubadiri serikali zao kwa njia za amani na iliposhindikana kujaribu kutumia nguvu za kijeshi, busara ilimuingia raisi wetu wa wakati huo baba wa Taifa letu mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa ipo haja na ulazima wa kuweka Transition ya amani ya madaraka kutoka generation moja kwenda nyingine. Na hii ilifuatia majaribio kadhaa ya mapinduzi dhidi yake.

Mzee wetu mzee Mwinyi unataka kuturudisha kwenye utaratibu wa utawala wa maisha?. Je mzee wetu unadhani tukimruhusu rais wa sasa aendelee kutawala tutaweza kweli kuwazuia na marais wajao kuendelea kutawala kwa kisingizio kuwa wanafanya kazi vizuri?, Je mzee wetu unataka kuwaandalia mazingira Watanzania utaratibu wa kufanya machafuko ili kumtoa rais ambaye watadhani hawafai, raisi ambaye atakuwa anatawala kwa katiba inayomruhusu kutawala bila ukomo?

Mzee wetu usidhani ukibadili katiba kwa ajili ya Magufuli, hiyo katiba itaishia kwa Magufuli tu, hata Magufuli baada ya kutawala tani yake akaamua kubadili katiba tena na kurudisha utaratibu wa zamani, atakayemfuata naye anaweza kuibadili tena naye akatawala tani yake!. Mzee wetu hayo ndiyo unayoyataka?

2. Mzee wetu, kumbuka Msisitizo wa Baba wa Taida kukutaka usibadili ukomo wa kutawala

Mzee wetu, mwaka 1999 pale uwanja wa Taifa kwenye msiba wa mwalimu, ulikuwa miongoni mwa watu waliopewa nafasi ya kumzungumzia Mwalimu, ulieleza mambo mengi, ulieleza jinsi alivyokuwa Mlima wa fikra na uongozi n. k na uliahidi kulinda yale mazuri yote aliyotuachia. Sasa mzee wetu mzee Mwinyi, hata hili la ukomo wa madaraka nalo unaliwekea question mark?. bado una chembe ya shaka juu ya umuhimu wake?

Mzee wetu mzee Mwinyi labda nikukumbushe tu namna mwalimu alivyotueleza wazi Watanzania kuwa wakati wa utawala wako, walikuwepo watu na harakati za kukutaka wewe ubadili katiba ili uendelee kutawala baada ya miaka kumi, Mwalimu alielezea jinsi alivyokuwa concerned na suala hilo na akatueleza kuwa jinsi wewe binafsi ulivyomhakikishia kuwa huna nia hiyo.

Sasa mzee wetu mzee Mwinyi, unadhani Mwalimu hakupenda usiendelee kutawala kwa sababu alidhani wewe hufai au alidhani kuwa wazo hilo siyo jema kwa mustakbali mpana wa nchi yetu?. Je Mzee wetu mzee Mwinyi, mbona basi na wewe unakuwa kama wale watu waliokuwa wanasukumasukuma mambo ili wewe uendelee kutawala kinyume cha ukomo wa vipindi kipindi cha utawala wako?.

Au mzee wetu mzee Mwinyi wakati ule ulikubaliana kishingo upande na mwalimu lakini wewe binafsi siyo muumini wa ukomo wa vipindi vya utawala?

3. Mzee wetu Mzee Mwinyi, Je una maslahi binafsi na utawala wa Magufuli?

Jana kwenye mkutano mkuu, Raisi Magufuli alituibia siri kuwa mwaka 2015 alikuwa yeye binafsi amempendekeza mwanao Hussein Mwinyi ili awe mgombea mwenza, Pia Mwanao Hussein Mwinyi amepata nafasi ya kuwa Mgombea wa CCM kwa tiketi ya Uraisi Zanzibar katika kipindi hiki ambapo Magufuli ni rais.

Sasa sisi tunajiuliza, hivi je mzee wetu unataka kulipa Shukrani kwa Magufuli kwa kumfanyia makubwa mwanao?, Je una maslahi binafsi yanayokusukuma kutaka Magufuli aendelee kuwa raisi, Je unamuandalia njia njema zaidi Mwanao kwa kutaka tuendelee na kile ambacho waswahili walisema kwenye methali "Zimwi likujualo"?

4. Mzee wetu, Mzee Mwinyi kumbuka hotuba ya baba wa Taifa kuhusu Nyufa zilizoikumba nchi yetu

Kabla ya uchaguzi wa mwaka 1995, baba yetu wa Taifa alizungumza nyufa mbalimbali ambazo zilianza kuikumba nchi yetu, na miongoni mwa mambo aliyoyasema ni suala la kutoheshimu katiba.

Mzee wetu mzee Mwinyi, mimi binafsi nilisikitishwa sana kusikia ukisema, Katiba tuiweke pembeni ili tumpe tena Rais wa Sasa miaka mitano kama Ahsante. Mzee wetu hata kama Rais Magufuli angeleta maendeleo ya namna gani, Je unataka tutoe ahsante kwa mtu aliyetimiza wajibu wake tuliomtuma afanye kupitia kuvunja katiba?. Mzee wetu mzee Mwinyi, wewe si uliapa kulinda katiba, Mwenzio naye si aliapa kulinda katiba, Sasa unamshawishi avunje katiba?

5. Mzee Mwinyi, Ushauri wako haujengi, ni mbaya na unatuma meseji mbaya kwa vizazi vijavyo

Mzee wetu mzee Mwinyi, wewe ni mtu mkubwa sana, wewe ni role model wa wengi, fahamu kwamba kauli zako zinawekwa kwenye rekodi na huenda zikawa rejea vizazi na vizazi hata miaka maelfu ijayo. Kauli za "huba" unazozitoa juu ya mtawala wa sasa hata kutaka katiba ipindishwe kwa ajili yake, wapo watu watakaokuja huko mbeleni watazitumia kama rejea ili kufanya hayahaya ambayo unatamani Taifa lifanye kwa ajili ya Magufuli, Watasema mbona miaka 50 iliyopita Rais wa awamu ya pili alitaka rais wa awamu ya tano naye aendelee kutawala?, basi kwa nini na sisi tusifanye?. Kwa kweli mzee wetu katika hili hauko sahihi kabisa, haujalitendea haki Taifa kabisa

Hitimisho
Ni dhahiri ushauri wa mzee wetu mzee Mwinyi ni ushauri mbaya kabisa kwa Taifa letu, ni ushauri usiozingatia hekima bora kabisa ya baba wa Taifa letu mwalimu Nyerere aliyeamua kuingiza ukomo wa utawala kwenye katiba, kitu ambacho leo hii tunajivunia Taifa letu kubadirishana uongozi kwa amani.

Mzee wetu Mzee Mwinyi akumbuke tu, Wakati mwalimu Nyerere anamuachia kijiti hapo mwaka 1985,Mwalimu alikuwa ni "kijana" kabisa wa miaka 63, pamoja na hali ngumu ya uchumi tuliyokuwa nayo wakati huo, Mwalimu alikuwa na uwezo wa kwenda kwenye uchaguzi na bado akashinda kwa kishindo, lakini aliona busara pana ni kung'atuka na kumuachia mtu mwingine kijiti.

Sasa swali la kujiuliza ni hili, kama Mwalimu asingeng'atuka mwaka 1985 yeye angekuwa rais?, Mkapa asingeheshimu mihula ya utawala Kikwete angekuwa rais?, Kikwete asingeheshimu katiba juu ya mihula ya Utawala Je Magufuli angekuwa rais?. Tunamuomba Mzee wetu alifikirie sana suala hili

Ama kuhusu Ahsante anayotaka tumpe Magufuli, Kama kuna ahsante yoyote ya kutoa kwa mtawala basi Watanzania wangetoa ahsante kwa mwalimu Nyerere kwa kuwaletea uhuru. Hakuna kitu kikubwa kilichofanywa katika nchi hii kuliko uhuru wetu. Lakini wananchi hawakuona eti wamfanye Mwalimu mfalme kisa katuletea uhuru.

Kama ni ahsante kwa sababu mtawala kaitendea jema familia, hata Mwalimu alikuwa na watoto pia akina madaraka Nyerere, Makongoro Nyerere, Rose Nyerere, lakini baba yetu wa Taifa hajawahi kuwa nice kwa mtawala teyote aliyekuja baadae ili watoto wake watendewe mema.

Mwisho kabisa nimpongeze katibu mkuu wa CCM ndugu, Bashiru Ally kwa kuzungumza wazi kupitia mahojiano na Tido Mhando kuwa suala la kubadili katiba ili kuongeza mihula ya utawala halimo katika ajenda ya CCM na si sera ya chama hicho na kwamba likiibuka CCM watalikataa. Mimi nasema hiyo ni busara kubwa sana

Pia nimshukuru rais Magufuli Mwenyewe ambaye yeye Mwenyewe kwenye mkutano mkuu alionyesha kutokubaliana na wazo hilo la mzee Mwinyi waziwazi, na ambaye mara kadhaa ameongea na kusema kuwa hana mpango huo

Mwisho kabisa ningependa Watanzania wote tulikatae wazo hilo la mzee Mwinyi, ni wazo baya, si jema kwa nchi yetu na halina mustakbali mwema kwetu na vizazi vyetu
 
Ndio hapo sasa watu wanaolazimisha kua kila analoongea au kushauri mzee basi lizingatiwe! ...mambo mengine ya tamaduni hayana maana kabisa mtu anaongea kitu kisicho na maana asifiwe tu kisa mzee wakati hakuna substance!
 
Back
Top Bottom