Mzee, unapenda movies kali? (Session 04). Weekend hii ruka na hizi!

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
5,800
2,000
Habari zenu wandugu? Ni kitambo kidogo sasa hatujakutana kwenye hiki kijiwe chetu cha movies kutokana na mambo ya hapa na pale lakini natumai kila kitu kipo poa!

Pasipo kupoteza muda, leo tutazamia ‘session ya 04’ kwenye huu mfululizo wetu wa kuhamasishana kutazama filamu mbalimbali kwa kuelezana kwa ufupi stories zake ama mambo kadhaa kuzihusu, yote kwa lengo la kujipatia hamasa.

Movies ni tamu aisee! Ila kwa anayejua sasa. Ni njia bora sana ya kujifunza na kufurahia muda wako.

MIDSOMMAR ya 2019.

Midsommar_(2019_film_poster).png


Kama wewe ni mtazamaji mzuri wa movies utagundua kuwa katika movies nyingi ni jamii ya watu weusi ama Amerika kusini ndo’ huwa wanaonyeshwa kuwa na utamaduni wa ajabu unaohusisha kutoa watu sadaka na kuamini miungu, mfano mdogo APOCALYPTO ya Mel Gibson.

Lakini kwa upande wa hii filamu, mambo yamegeuka kidogo ambapo humu ndani ni jamii fulani ya watu wa Sweden, yaani wazungu sasa, ndo’ ambao wameonyeshwa kuwa na utamaduni wa kikatili wa kuachisha midomo wazi! … utamaduni ambao huwezi amini kama watu hawa wanaojinasibu wamestaarabika wanaweza kuuhodhi kabisa!

Mbali na hilo, filamu hii ni ‘horror’ ya kitofauti kidogo ambapo humo ndani, tofauti na horrors zingine, hutoona majini, mashetani wala mizimu! Hamna makaburi wala maruwani. Ni binadamu tu wa kawaida wakionyesha namna gani ambavyo wanaweza kuwa hatari kuliko majini yenyewe.

Lakini mwisho japo ni muhimu, ni filamu inayoonyesha namna ukosefu wa familia na mapenzi dhabiti unavyoweza kupelekea mtu kuwa mnyama kabisa. Namna sisi binadamu tunavyohitaji huruma toka kwa wengine (empathy), hisia za mapenzi na uwepo wa watu kwa ujumla. Punde tunapokosa vitu hivyo basi utu wetu hugeuka na kuwa unyama.

MAMBO YAPO HIVI: Msichana anayeitwa Dani anakumbwa sana na shida za kihisia kutokana na mambo ya familia yake kutokuwa sawa. Dada yake anayejitahidi kumtafuta kwa muda sasa, hapatikani hewani wala mtandaoni. Na baba na mama yake pia haijulikani nini kimewakuta kwani hawarudishi tena ‘messages’ zake.

Sasa kutokana na hali hii, Dani anakuwa msumbufu sana kwa mpenzi wake aitwaye Christian kwani anahitaji faraja sana. Anapiga kila saa pasipo kusahau na messages pia. Usumbufu huu unakithiri na kumchosha Christian, na sio yeye tu, hata rafiki zake pia wamechoshwa.

Juu ya malimbikizo hayo ya matatizo, Dani anakuja gundua kuwa dada yake aliyekuwa anamtafuta pasipo mafanikio, na wazazi wake wake aliokuwa anawatafuta mara kwa mara, wote walikuwa wamekufa! Hivyo anazidi kuwa kwenye huzuni kubwa kupita kiasi. Bwana ‘ake, Christian, anajitolea kumpa faraja lakini unaona kabisa jamaa kachoka. Jamaa hayupo tena kiviiile, si unajua tena. Na kutihibitisha hili, Christian pamoja na rafiki zake wakawa wameazimia kwenda Sweden pasipo hata Christian kumwambia mpenzi wake Dani.

Baadae Dani anakuja kugundua hilo, wanahitilafiana kidogo na Christian wake lakini mwishowe yeye ndo’ anaomba msamaha na maisha yanaendelea. Hivyo basi kwasababu Dani ashajua kuhusu safari ya Sweden, na yeye anajumuishwa safarini humo, kitendo ambacho kwa namna moja ama nyingine rafiki yake Christian, kwa jina Pelle, ambaye ndo mwenyeji wao huko Sweden, anakiunga mkono na kukifurahia.

Basi safari inafika na watu hawa wanajikuta Sweden huko wakiwa na hamu kweli ya kutaka kujifunza yanayoendelea huko haswa kwenye sherehe kubwa inayofanyika kwenye kijiji anachotokea Pelle, rafiki yake Christian. Kwenye safari hii kwa ujumla wapo watano, Christian na mpenzi wake Dani, Pelle, na majamaa wengine wawili.

Wanapofika huko wanaungana na wageni wengine wawili ambao pia wameletwa na ndugu yake Pelle, hivyo jumla ni kama wanakuwa saba hivi. Wanaingia katika kijiji cha wakina Pelle ambacho watu wake wanaishi kijamaa sana, wakiwa wamevalia nguo nyeupe na kuvalia maua karibu kabisa na kuazimisha siku ya sherehe yao.

Lakini tofauti na vile ambavyo ilikuwa ikidhaniwa kuwa mahusiano baina ya Christian na Dani yataimarika wakienda ‘tour’, ndo kwanza yakazidi kuzorota. Bwana Christian anasahau ‘birthday’ ya mpenzi wake na kama haitoshi anaanza kuonekana hajali tena hisia za Dani, mpenzi wake.

Sasa mambo yanakuja kuwa tafrani baada siku iliyofuata toka wafike, wageni wanapelekwa kwenda kuona moja ya tamaduni ya ajabu kabisa ya watu kujiua kwa kujirusha mlimani. Wageni wanakwazika na kushangazwa na tamaduni hii ya ajabu kabisa, lakini baadhi wanavutiwa kutaka kudadisi zaidi pasipo kujali tamaduni hii ni ya siri mno, hawataki mambo yao yajulikane kwenye ulimwengu mwingine, matokeo yake wanakiona chamtemakuni!

Mmoja mmoja anaanza kupotea isijulikane nini kimekumba. Kuja kutahamaki wamebaki wawili tu, Christian na mpenzi wake, Dani! Sasa huku penzi la Dani na Christian likiwa linaelekea kufa, tena Christian akiwa ameshatiliwa madawa ya haja hajielewi kabisa, jamii hiyo wenyeji inaanza kujionyesha rangi yao halisi! Chui na madoa yake.

Ni tafarani!

Na ikiwa tayari ‘too late’, ndipo inawekwa wazi kuwa wageni hawa walirubuniwa kuja huku kwa ajili ya kutolewa kafara!

Sasa nini kitawatokea Dani na Christian?

Dani ambaye sasa ni yatima atapata familia tena? Huku alipo hatma yake ni nini na hii jamii ya kikatili na huku mapenzi batili ya Christian?

Huwezi amini katika yote haya, filamu hii inaishia na tabasamu kwenye uso wa msichana, Dani. Tabasamu katika uso wa kikatili na kinyama.

13 SINS ya 2014.

13_Sins_poster.jpg


Umewahi tazama TRUTH OR DARE au NERVE? Kama ndio basi katika mahadhi hayo ndo’ filamu hii imepita. Michezo hatari ambayo humfanya mchezaji aweke roho yake rehani haswa. Michezo ya kufa ama kupona.

MAMBO NI HAYA: Bwana mmoja, kwa jina Elliot, akiwa mtu wa mauzo, anazama kwenye madeni lukuki yanayomuumiza kichwa. Mbali na hapo, siku za karibuni, anatarajia kufunga ndoa na mpenzi wa maisha yake hivyo anazidi kuhitaji pesa mno mno.

Akiwa katika njaa hiyo ya pesa, anapokea simu inayomtaarifu kuwa kuna kamera za siri zinammulika na anahaidiwa donge nono la pesa, dola za kimarekani milioni 6.2, endapo akikamilisha zoezi fulani atakalopewa … zoezi lenye hatua zake 13! Na kila hatua atakayovuka pesa inaingia kwenye account yake chap kwa haraka!

Basi bwana huyo akafanya zoezi la kwanza alilopewa japo lilikuwa la ajabu kiasi fulani. Hamaki kweli akaona dola maelfu zimeingia kwenye account! Haikuwa mzaha. Mchezo ni halisi kabisa. Lakini ubaya ni kwamba anatakiwa kumaliza majaribio yote 13 ili kupata pesa hiyo kamili. Endapo akisitisha, hata kama atakuwa amefika kwenye hatua ya 12, pesa zote zitarudishwa isibaki hata senti!

Sasa jamaa anaanza kupambana haswa kumaliza kazi ili apate pesa hiyo ndefu. Kila anachofanya kuna watu wanamtazama na kama kawaida pesa inaingia kila akifanikiwa kufanya jambo, lakini ubaya unakuja kwamba kila alipokuwa anapiga hatua kwenda kwenye zoezi linalofuata, ugumu unazidi kuongezeka maradufu!

Bwana Elliot anajikuta akifanya matendo ambayo hakuwahi kabisa kuyadhania atakuja kuyafanya maishani mwake. Matendo ya kutisha mno. Na inafikia kipindi sasa anakuwa hawezi tena kusitisha mchezo huo. Lazima kwa vyovyote vile aumalize, hata kama hatotaka!

Je, bwana huyu ataweza kumaliza majaribio haya ya dhambi kumi na tatu? Na majaribio hayo ni yapi kiasi cha kunadiwa kwa pesa kubwa kiasi hiko?

Tafuta ufurahie kazi!

I SAW THE DEVIL ya 2010.

i saw the devil.jpg

Najua ushatazama movies nyingi zenye mikasa ya visasi lakini si kama hii. Humu wanaume wanaonyeshana kazi si kitoto. Na kwa wanaomjua Lee Byung-hun basi wanajua mambo yake haswa akiwa ameweka sura ya kazi.

Nisikuchoshe, mambo yapo hivi…

Mwanamke mmoja anayeitwa Joo-yeon anaharibikiwa na gari ikiwa ni usiku wa baridi kali. Anawasiliana na mafundi kisha na mpenzi wake ambaye ni mwanausalama, kwani jina Soo-hyeon, kuhusu tatizo hilo lililomkumba. Akiwa anangoja msaada, mara anatokea mwanaume anayetaka kumsaidia.

Joo-yeon anakataa huo msaada lakini ghafla mwanaume huyo anamshambulia na kumuua kikatili kwa kumkata viungo vya mwili!
huyu si mtu wa kwanza kwa mwanaume huyu kuua. Ni kawaida yake. Huwa anawawinda watoto na wanawake kisha anawaua kinyama kuridhisha nafsi yake.

Sasa mpenzi wake na marehemu, yaani bwana Soo-hyeon, anaamua kuvalia njuga kazi hii akiapa kumtafuta na kumtendea sawa muuaji huyo kwa namna yoyote ile, hata kama si ya kibinaadamu! Anaapa atahakikisha muuaji huyo anahisi kila maumivu ambayo alimpatia Joo-yeon.

Na kweli, bwana huyu anabadilika kabisa kutoka kuwa mwanausalama mpaka mwanahatari. Anafanikiwa kumdaka mhanga wake, anamtesa na kumuachia, kisha anamtafuta tena anamtesa na kumuachia kama vile mchezo!

Lakini mwisho wa siku, pengine labda alimdharau sana muuaji huyu, bwana Joo-yeon anakuja kujutia kwanini hakumuua muuaji huyo pale alipopata nafasi ya kufanya hivyo kwani bwana huyo ni shetani!

Sasa basi kazi inageuka kuwa mlima asoutaraji kabisa … nisikumalizie uhondo, katafute utazame mwenyewe!


DERANGED ya 2012.

deranged.jpg

Filamu hii ni kitambo kidogo hapo nyuma, lakini kutokana na janga hili la Corona imekuwa ‘relevant’ kiasi na wakati wa sasa japo kwenye hii kazi huu ugonjwa walioushukia wao ulikuwa ni moto wa kuotea mbali, Corona haikufika hiki kiwango!

Lakini zaidi, movie hii pia inaonyesha namna gani kuwa jina la ‘baba’ si la ubatizo. Baba ni majukumu. Baba ni kulinda familia kwa hali na mali hata pale muda mwingine unapotakiwa kuvuka mstari wako wa mwisho wa mpaka.

SASA MAMBO YAPO HIVI: Kabla hakujapambazuka, miili lukuki iliyokufa inaonekana ikiwa inaelea kwenye mto Han. Chanzo cha kifo kikiaminika ni parasite hatari, kwa jina Yeongasi, wanaomkalia mgonjwa na kula akili yake alafu humfanya ajihisi kiu kikali kupita kiasi ambacho hupelekea kunywa maji mengi mno yasiyokata kiu ama mwishowe kujitupia mtoni ambapo humo mtu atakufa maji!

Sasa bwana aitwaye Jae-hyuk, mfanyakazo wa maswala ya madawa, anakumbana na kisanga hiki cha aina yake ambapo familia yake nzima inaanza kuonyesha dalili za parasite hawa hatari! … akiwa anahaha kutumia ujuzi wake kutafuta namna ya kusaidia familia yake, parasite hawa wasambaa nchi nzima na kuwa janga la kitaifa!

Watu wengi wanaathirika, wanaenda kujirusha mtoni na kufa hivyo kupelekea mto kuwa kama makaburi. Serikali inachukua hatua kwa kufungua kambi nyingi za kuhifadhia wagonjwa lakini hamna kitu! Wagonjwa wanaendelea kuongezeka kiasi kwamba wanausalama wanakuwa na mzigo mzito sawa kuwamudu!

Miji inakuwa tafarani, mingine inakuwa mitupu kabisa watu wakiwa wamelala chini wamekufa! Wale walio hai wanahaha kutafuta dawa kwa gharama yoyote ile hata kwa kuua.

Katika yote hayo, bwana Jae-hyuk ataokoaje familia yake dhidi ya mdudu huyu hatari kabla hawajaenda kujitupia mtoni wakafa ama tu wakiwa hapo nyumbani wakafa kwa kiu kisicho cha kawaida?

Na je, dawa ikigundulika kutakuwa na ustaarabu mbele ya watu ambao hawajali tena kuhusu utu bali kupona tu?

Fun fact ni kwamba filamu hii, katika nchi yao, ilifunika kimauzo filamu ya Amazing Spiderman kuanzia kwenye kujaza watu kwenye majumba ya sinema mpaka kwenye manunuzi. Sasa katazame kwanini?

INSANE ya 2016.

insane.jpg


Wewe ni mpenzi wa Mystery? Zile movies ambazo akili kweli inatumika na mara nyingi huwa kuna mafumbo yanayokuja kukuacha mdomo wazi kwa butwaa kwasababu haukuwa unadhania kabisa kama kitu fulani kitatokea hapo awali? Basi karibu na hapa maana pana utamu!

MAMBO YAKO HIVI: Mwanamke aitwaye Soo-A anakamatwa ghafla na kupelekwa hospitali ya wagonjwa wa akili pasipo kujua sababu. Akiwa huko, anachomwa sindano za mara kwa mara huku akipitia shurba za mateso.

Lakini mbali nay eye pia, kuna wagonjwa wengine vilevile ambao wanapitia magumu na makali kama yeye ama kuliko yeye humo hospitalini.

Basi mwanamke huyo anaanza kuandika yale yanayotukia humo hospitali. Bahati nzuri, mwaka mmoja baadae, notebook yake inafika mikononi mwa mwandishi wa habari aitwaye Nam-so ambaye anashtushwa kweli nay ale yanayotokea kwenye hospitali hiyo lakini pia na kisa cha mwanamke huyo.

Sasa ili kujua ukweli zaidi, bwana mwandishi anahaha kumtafuta mwanamke huyo. Lakini cha ajabu zaidi, anakuja gundua mwanamke huyo hayupo tena hospitali humo bali sasa yupo jela ambapo amehukumiwa kama mtuhumiwa wa mauaji.

Kazi inapamba moto!

Moja, kwanini mwanamke huyo alipelekwa hospitali ya vichaa? Pili, yapi ambayo yanatokea ndani ya hospitali hiyo ya vichaa? Na tatu, kwanini mwanamke huyo anafungwa tena kwa tuhuma za mauaji? … tafuta mzigo huo ujiweke karantini ya kupenda.

BONUS:-

THE VANISHED ya 2018.

vanished.jpg

Katika hali ya kushangaza, maiti inapotea ndani ya mochwari isijulikane imeenda wapi. Mpelelezi anaingia kazini kutafuta majibu na kujikuta anazama kwenye dimbwi la mambo lukuki ya kushangaza na hatari! … kwanza, ni nani aliyesababisha mauaji ya maiti hiyo ilopotea mochwari? Pili, maiti hiyo imeenda wapi? Na kwanini ipotezwe?

Maswali hayo yatakufanya utazame filamu hii mpaka kikomo chake. Ni bampa after bampa!

NB: Kwa wale ambao walinichek kuhusu movies ninazozipost, huenda wakawa wanapitia ugumu kuzipata ama kupata tu-maelezo yake, basi tatizo limekwisha. Hakikisha una Telegram kwenye simu yako.

Nenda sehemu ya Search kisha andika ‘Movies na stories’ utaona channel ya free kabisa, jiunge utapata movies zote humo. Search pia ‘Chumba cha series’, humo utakuta series zote. Jiunge. FREE! Ni wewe na bundle lako tu!

Pia kuna youtube waweza kupitia kwa mambo yetu haya ya movies. tafadhali subscribe

 

Pyaar

JF-Expert Member
Feb 11, 2018
14,587
2,000
Chagua moja kati ya hizi malizia weekend yako fresh kabisa.

*Just Mercy
*Midway
*12 Strong
*13 hours secret soldier of Bengazi
*Badla
*Sicario
*15 Minutes
*Hunter Killer
*John wick
*Mile 22
*Grinch
*Peter rabbit
*6 underground
* Foxtrox Six
*Escape from Pretoria
*Pink
*Angle has Fallen
*Anna
* The courier
 

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
5,800
2,000
Chagua moja kati ya hizi malizia weekend yako fresh kabisa.

*Just Mercy
*Midway
*12 Strong
*13 hours secret soldier of Bengazi
*Badla
*Sicario
*15 Minutes
*Hunter Killer
*John wick
*Mile 22
*Grinch
*Peter rabbit
*6 underground
* Foxtrox Six
*Escape from Pretoria
*Pink
*Angle has Fallen
*Anna
* The courier
Tupe hata vitumaelezo (synopsis) mzee baba.

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Super Villain

JF-Expert Member
Jan 2, 2019
9,223
2,000
Chagua moja kati ya hizi malizia weekend yako fresh kabisa.

*Just Mercy
*Midway
*12 Strong
*13 hours secret soldier of Bengazi
*Badla
*Sicario
*15 Minutes
*Hunter Killer
*John wick
*Mile 22
*Grinch
*Peter rabbit
*6 underground
* Foxtrox Six
*Escape from Pretoria
*Pink
*Angle has Fallen
*Anna
* The courier

Hiyo 13 hours bengazi we achana na Waarabu kabisa wale watu nimenyoosha mikono juu hawapumziki masaa 13 nikama upo jehanamu vile
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom