Mwongozo wa kufanyia kazi Nyumbani wakati huu wa Mlipuko wa Corona

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona unaoendelea, moja ya njia kuu za kuzuia maambukizi ni watu kujitenga. Hivyo mataifa mbalimbali yanawataka watu wake kukaa nyumbani wakati huu wa mlipuko, ili kuepuka kuambikiwa au kuwaambukiza wengine.

Kwa kuwa watu wengi wanakaa majumbani, kazi inabidi zifanyike nyumbani pia. Sasa hiki ni kitu kipya kwa wengi, hawajazoea kufanyia kazi nyumbani, hivyo wanapoambiwa ghafla kwamba unapaswa kufanyia kazi zako nyumbani, wanajikuta njia panda, kwa sababu hawana maandalizi ni kwa namna gani wanaweza kutekeleza majukumu yao ya kazi wakiwa nyumbani.

Home-Work-1.jpg


Hapa tunakwenda kupata mwongozo sahihi wa kufanyia kazi zako nyumbani (Working From Home) ambao utakusaidia sana kwenye mlipuko huu wa Corona na hata kwa siku zijazo. Maana ukiweza kujijengea msingi mzuri kipindi hiki, utaweza kuutumia kwa siku nyingi zijazo.

Uzoefu wangu kwenye kufanyia kazi nyumbani.

Tangu nilipofanya uandishi kuwa sehemu ya kuniingizia kipato, mwaka 2013 kwa sehemu kubwa kazi zangu huwa nafanyia nyumbani. Ukizingatia wingi wa uandishi niliofanya mpaka sasa, vitabu 11, makala zaidi ya elfu 5 na chambuzi za vitabu zaidi ya 200 unaweza kuona ni kwa namna gani mtu unahitaji njia bora ya kufanya hili.

Hayo yote yanawezekana pale mtu unapojiwekea mkakati mzuri na kuufanyia kazi, ambao nitakwenda kukushirikisha hapa leo ili uweze kutekeleza majukumu yako vizuri ukiwa nyumbani.

Faida za kufanyia kazi nyumbani.

Kufanyia kazi zako nyumbani, iwe umeajiriwa au umejiajiri kuna faida nyingi sana, baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo;

  1. Unaokoa muda mwingi ambao huwa unaupoteza kwa kwenda eneo la kazi. Kuanzia muda unaotumia kwenda, kurudi na mwingine unaopotea, kwa kufanyia kazi nyumbani hupotezi muda wako.
  2. Unapunguza fursa za kupoteza muda zinazopatikana kwenye eneo la kazi, mfano mikutano mbalimbali ambayo hufanyika maeneo ya kazi, ambayo kwa sehemu kubwa haina tija.
  3. Unafanya kazi kwa mpango wako bila ya kusumbuliwa na wafanyakazi wengine. Japo kunakuwa na mawasiliano ya simu au njia nyingine za mtandao, ile hali ya kukatishwa na wengine wakati unafanya kazi inapungua.
  4. Kwa sehemu kubwa unakuwa na uhuru wa kupanga muda wako mwenyewe, hasa kama kazi yako haihitaji kushirikiana na wengine wakati mnaifanya. Unaweza kupanga kufanya kwa muda unaofaa kwako.
  5. Unapata muda mwingi wa kupumzika, majukumu yako unayofanya ukiwa kazini, ukiyafanyia nyumbani itakuchukua nusu ya muda unaotumia kuyafanya ukiwa kazini. Hivyo unapata muda mwingi wa kupumzika au kufanya mambo mengine.
Changamoto za kufanyia kazi nyumbani.

Hakuna kisichokuwa na changamoto, na katika kufanyia kazi nyumbani, zipo changamoto nyingi. Hapa ni baadhi ya changamoto hizo;

  1. Kushindwa kutekeleza majukumu yako kwa wakati kwa sababu hakuna anayekusimamia moja kwa moja au anayekuangalia. Unahitaji nidhamu kali sana kuweza kujisimamia mwenyewe.
  2. Usumbufu wa wanafamilia wakati unafanya kazi, wengi hawajui kwamba japo upo nyumbani pia upo kazini, hivyo kuingilia kazi zako pale wanapokuwa na mahitaji mbalimbali.
  3. Kukosekana kwa mipaka kati ya kazi na maisha. Kwa kuwa unafanyia vyote nyumbani, ni rahisi kushindwa kuweka mipaka, ukajikuta unaruhusu mambo ya kifamilia kuingia kwenye wakati wa kazi au mambo ya kikazi kuingia kwenye wakati wa familia.
  4. Wageni usiokuwa na miadi nao wanapokuja nyumbani na kujua upo, wanaingilia sana muda wako wa kazi. Wengi hawawezi kuelewa kwamba japokuwa upo nyumbani, upo kazini, hivyo kuhitaji muda wako mwingi.
  5. Ni rahisi kwa uvivu kukunyemelea, ukipatwa na usingizi kidogo ni rahisi kwenda kulala au kufanya mambo mengine ya kupoteza muda kama kuangalia tv, kuzurura mitandaoni na kadhalika.
Mkakati bora kwako wa kufanyia kazi nyumbani.

Ili kupata manufaa ya kufanyia kazi nyumbani, pamoja na kuzuia changamoto zake zisiwe kikwazo kwako, tengeneza mkakati mzuri kwako kufanyia kazi nyumbani

Zingatia mambo yafuatayo katika kutengeneza mkakati wako wa kufanyia kazi nyumbani utakaokupa matokeo mazuri.

1. Tenga eneo la kufanyia kazi.
Kitu cha kwanza muhimu kabisa kwako kufanya ni kutenga eneo la kufanyia kazi ukiwa nyumbani. Huwezi kuwa unafanyia kazi kila mahali na ukawa na nidhamu nzuri. Badala yake unapaswa kutenga eneo ambalo utakuwa unafanyia kazi zako, na ukiwa eneo hilo unachofanya ni kazi tu na siyo kitu kingine.

Hii inakuandaa kisaikolojia kuheshimu eneo hilo na unapokuwa kwenye eneo hilo unajua cha kufanya ni kazi. Kama unaishi kwenye nyumba kubwa unaweza kutenga chumba utakachotumia kama ofisi. Lakini kama huwezi kufanya hivyo unaweza kutenga eneo kwenye chumba chochote, hata kile unacholala na kulitumia kama eneo la kazi.

Kama unatenga eneo ndani ya chumba chenye matumizi mengine, hakikisha unaweka kiti na meza kwa ajili ya kufanyia kazi. Hivyo unapokaa kwenye kiti na meza hiyo, unajua kabisa hili ni eneo la kazi. Usifanye kitu kingine unapokuwa kwenye kiti na meza ulivyoandaa kwa ajili ya kazi.

Epuka kufanyia kazi kitandani au kwenye kochi, kwenye maeneo hayo hutaipa kazi uzito kwa sababu kisaikolojia unayachukulia kama maeneo ya kupumzika.

2. Tengeneza ratiba yako ya siku na ifuate.
Japokuwa una uhuru wa muda gani ufanye kazi unapokuwa nyumbani, uhuru huo una mipaka. Huwezi kufanya kazi zako pale unapojisikia, ukienda kwa mpango huo hutafanya chochote. Ndiyo una uhuru, lakini lazima utengeneze ratiba yako mwenyewe na uifuate kila siku.

Panga kabisa ni muda gani unaamka, ukiamka unafanya nini, muda gani unapumzika, unakula na unakuwa na familia. Yote hayo lazima uyapange na kisha kuyafuata.

Ukianza siku zako bila mpango, utajikuta umefanya mengi, umechoka lakini hakuna kikubwa ulichokamilisha.

Kwenye ratiba yako ya siku tenga kabisa masaa ambayo huhitaji usumbufu, hayo ni masaa ya kazi zinazohitaji umakini mkubwa.

3. Vaa kama unaenda kazini.
Unapofanyia kazi nyumbani, una uhuru wa kuvaa utakavyo au hata kutokuvaa kabisa. Lakini hilo unapaswa kuwa nalo makini, kwa sababu lina madhara ya kisaikolojia kwenye utekelezaji wa majukumu yako ya kazi. Kama umevaa nguo za kawaida utajiona kama hauna majukumu makubwa.

Hivyo unapaswa kujiandaa vizuri kama vile unaenda kazini, kwa kuvaa kabisa nguo zako za kazi na kisha kukaa eneo lako la kazi wakati unafanya kazi. Unapovaa nguo kama vile unaenda kazini, akili yako inakupa uzito wa kikazi na unatekeleza majukumu yako vizuri.

4. Watu wote wajue ratiba yako.
Ukishaweka ratiba yako ya siku, kila mtu kwenye familia anapaswa kuijua. Na waeleze wazi kwamba japokuwa upo nyumbani, lakini pia upo kazini. Kwa muda ule wa kazi, mambo yote hapo nyumbani yanapaswa kuendelea kama vile wewe haupo kabisa.

Ule muda ambao umetenga usisumbuliwe, usisumbuliwe kweli, labda kwa jambo la dharura, ambalo hata kama ungekuwa kazini basi ungepigiwa simu. Na weka kabisa vigezo vya dharura ni vipi. Usipofanya hivi, watu watatumia uwepo wako kuuliza vitu mbalimbali na hilo kuathiri kazi zako.

Kuhusu wageni, kama kuna mgeni amekuja na hukuwa na miadi naye, usikutane naye wakati ambao unafanya kazi. Anapaswa kuelezwa ratiba yako na muda mzuri kwako kukutana naye. Na kama ni mgeni muhimu, unaweza kumsalimia na kumpa ratiba yako ilivyo na mkapanga muda gani mzuri wa kuwa na maongezi, kama yapo na ni muhimu.

5. Tengeneza mipaka ya kazi na maisha.
Kwa kuwa upo nyumbani na unafanyia kazi nyumbani, mpaka kati ya kazi na maisha unafutika kabisa. Wakati wa kazi utaingiliwa na mambo ya kifamilia na wakati wa familia utaingiliwa na mambo ya kikazi.

Ni lazima utengeneze mpaka kati ya kazi na maisha, ufanye kazi wakati wa kazi na maisha wakati wa maisha. Jisukume kutekeleza majukumu yako ya kazi kwa wakati uliopanga kufanya kazi na ule wakati uliopanga kupumzika au kuwa na familia basi usiruhusu kazi kuingilia wakati huo.

6. Tumia vifaa vya kuondoa usumbufu.
Kama mazingira ya nyumbani kwako siyo rafiki kwako kupata utulivu wa kazi, labda kuna kelele mbalimbali za majirani na watu wengine, basi tumia vifaa vua kuondoa usumbufu.

Hapa unapaswa kuwa na spika za masikioni (headphone au earphone) ambazo utazivaa wakati wa kufanya kazi. Kuna ambazo zina sifa ya kufunga kelele za nje zisikuingie na hivyo kukupa utulivu mkubwa wa kufanya kazi zako.

Pia kitendo cha kuvaa spika hizo, kinamfanya mtu asikusemeshe mara kwa mara, kwa sababu anajua humsikii. Pia mtu anapokusemesha, jifanye kama humsikii, hata kama unamsikia, hasa pale jambo linapokuwa siyo muhimu.

Inayoendana na hii ni kuandaa orodha ya nyimbo (playlist) zinazokupa utulivu na kuitumia wakati unafanya kazi zako. Hapa unasikiliza nyimbo hizo kwa kujirudia rudia na hilo linafanya akili yako izame kwenye kazi unayofanya na kuepuka usumbufu.

7. Jali afya yako.
Unapofanyia kazi nyumbani, kama kazi zako ni za kutumia akili na unazipenda sana, unaweza kujikuta umekaa kwenye kazi siku nzima na hujatoka kabisa nje ya nyumba yako. Pia ulaji ni rahisi sana unapokuwa nyumbani kuliko ukiwa kazini, ni rahisi kula mara kwa mara ukiwa nyumbani kuliko ukiwa kazini.

Hivyo unapaswa kuwa na mkakati wa kujali na kuboresha afya yako. Kitu cha kwanza muhimu ni kufanya mazoezi, tenga muda wa kufanya mazoezi ambayo yatakutoa jasho. Cha pili ni kudhibiti ulaji, usile kwa sababu kuna kitu cha kula, bali kula kwa utaratibu maalumu na kuwa makini na kile unachokula. Cha tatu ni muda wa kupumzika, unaweza ukakosa mapumziko mazuri japo uko nyumbani na hilo likaathiri afya yako.

8. Pangilia muda unaoendana na wewe na unaoepuka usumbufu.
Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinanisaidia sana mimi binafsi kuweza kukamilisha sehemu kubwa ya uandishi ni kutenga muda wa uandishi ambao unaendana na mimi na pia unaepuka usumbufu.

Huwa ninaamka saa kumi kamili asubuhi kila siku na baada ya kufanya tahajudi na tafakari kisha kuipangilia siku, kuanzia saa kumi na nusu mpaka saa 12 kamili huo ni muda wa kuandika tu, sifanyi kingine kwenye muda huo. Kwa muda huo, nimekuwa na uwezo wa kuandika kwa kiwango kikubwa sana, kwa sababu akili inakuwa na utulivu na hakuna usumbufu, maana watu wengine wanakuwa wamelala kwenye muda huo.

Hivyo na wewe pangilia majukumu yanayohitaji utulivu na umakini kulingana na wewe binafsi na mazingira. Yaani yapange kwenye muda ambao akili yako iko vizuri lakini pia hakuna usumbufu wa nje.

Watu tumegawanyika kwenye makundi mawili; kuna ambao wanaweza kuamka asubuhi na mapema na akili zao zikawa vizuri (early birds) na kuna ambao wanachelewa kulala na muda wa usiku ndiyo akili zao zinakuwa vizuri (night owls). Jijue wewe uko kundi gani, kisha tenga muda ambao wengine wamelala na ufanye kuwa wa kazi.

Mfano kama uko vizuri kwenye kuamka asubuhi basi amka asubuhi na mapema sana, labda saa tisa au saa kumi na kisha tumia masaa mawili ya kwanza kwenye kazi inayohitaji umakini wako na utulivu. Muda huo wengi wanakuwa wamelala na hivyo usumbufu unakuwa mdogo.

Na kama unachoelewa kulala basi tenga masaa mawili ya usiku mnene ambapo wengine wamelala na akili yako imetulia kufanya kazi.

Ukiweza kutenga masaa mawili ambapo akili yako imetulia na ina umakini na hakuna usumbufu wa nje, kisha kuyaweka masaa hayo mawili kwenye kazi, utatekeleza majukumu makubwa kuliko anayefanya kazi siku nzima kwenye ofisi isiyo na utulivu.

Rafiki yangu mpendwa, huu ndiyo mwongozo sahihi kwako kwa kufanyia kazi nyumbani wakati huu wa mlipuko. Tumia muda huu vizuri na kama ukiweza kuzalisha matokeo bora katika kipindi hiki, unaweza kuifanya hayo kuwa maisha yako kama umejiajiri au kumshawishi bosi wako akupe siku zaidi za kufanyia kazi nyumbani kama umeajiriwa.

Kikubwa unachohitaji ili uwe na ufanisi na uzalishaji mkubwa unapofanyia kazi nyumbani ni nidhamu kali na isiyoyumba, ukishapanga fuata ulichopanga, usiruhusu uzembe wowote uingilie mipango yako.
Huduma ya ukocha ya kukuongoza unapofanyia kazi nyumbani.

Rafiki, kama bado hujaweza kujijengea nidhamu ya kufanyia kazi nyumbani na kutekeleza majukumu yako kama ulivyopanga, nimekuandalia huduma ya ukocha ambayo itakusukuma kufanya kile ulichopanga kama ulivyopanga mwenyewe.

Huduma hii inaitwa DAILY COACHING PROGRAMU, inafanyika kwa njia ya mtandao na unashirikisha kile ulichopanga kufanya kwenye siku na kutoa ripoti ya utekelezaji wake, unafanya hivyo kila siku.

Hivyo kama unakutana na changamoto kwenye kujisimamia mwenyewe, programu hii itakusa msaada mkubwa sana kwako.

Kujiunga na programu hii, tuma ujumbe wenye maneno DAILY COACHING PROGRAM, kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 na utapewa maelekezo ya kujiunga na programu hii.

Karibu sana twende pamoja ili uweze kupata msukumo wa kutengeneza na kutekeleza ratiba yako ya kila siku.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
 
Kufanyia kazi nyumbani kunapoteza sana umakini uwezi kufanya kwa ufasaha sana kama ambavyo ungefanya kazini hata urahisi wa kupata vitendea kazi Utakuwa mgumu tena na internet yetu hii bongo ni hatari
 
Kufanyia kazi nyumbani kunapoteza sana umakini uwezi kufanya kwa ufasaha sana kama ambavyo ungefanya kazini hata urahisi wa kupata vitendea kazi Utakuwa mgumu tena na internet yetu hii bongo ni hatari
Ukijipanga vizuri hakuna linaloshindikana.
 
~ kwenye mavazi....ukivaa msuli au pajama na carwash! Kazi haziendi hadi uvae manguo ya wazungu?
 
~ kwenye mavazi....ukivaa msuli au pajama na carwash! Kazi haziendi hadi uvae manguo ya wazungu?
Kikubwa ni unachukuliaje mavazi kisaikolojia. Kama umezoea kwenda kazini na nguo za aina fulani, tayari akili yako imeshahusianisha kazi na aina hiyo ya nguo.

Hivyo ukivaa nguo za aina nyingine unapokuwa nyumbani, akili yako haipi kazi umakini unaostahili.
 
Kikubwa ni unachukuliaje mavazi kisaikolojia. Kama umezoea kwenda kazini na nguo za aina fulani, tayari akili yako imeshahusianisha kazi na aina hiyo ya nguo.

Hivyo ukivaa nguo za aina nyingine unapokuwa nyumbani, akili yako haipi kazi umakini unaostahili.
Asante sana.
 
Walimu wenyewe wameambiwa warudi shule wakapambanie kombe

Sent from my TECNO LB6 using Tapatalk
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom