Mwongozo (circular) ya utaratibu wa uhawilishaji wa ardhi ya kijiji katika ngazi ya k | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mwongozo (circular) ya utaratibu wa uhawilishaji wa ardhi ya kijiji katika ngazi ya k

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by MAKOLA, Aug 25, 2010.

 1. M

  MAKOLA Member

  #1
  Aug 25, 2010
  Joined: Jun 5, 2010
  Messages: 46
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 15
  YAH: MWONGOZO (CIRCULAR) YA UTARATIBU WA UHAWILISHAJI WA ARDHI YA KIJIJI KATIKA NGAZI YA KIJIJI

  Mwongozo huu unakuja kufuatana na muongozo uliotolewa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia kwa kamishna wa Ardhi unaohusu uhawilishaji.

  UTANGULIZI:
  Tarehe 1 Mei, 2001 Sheria za Ardhi Na. 4 na Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na. 5 za mwaka 1999 zilianza kutumika. Sheria hizi ni tofauti na sheria ya Ardhi ya Mwaka 1923. utekelezaji wa Sheria hizi unatakiwa kuleta ari mpya ya maendeleo hususani katika kukuza uchumi na kutoa mchango mkubwa katika juhudi za kupunguza umasikini na kukuza uchumi. Sheria ya Ardhi Na. 4 (sura 113) inaelekeza kuwepo kwa aina kuu tatu za Ardhi kwa kuzingatia mamlaka za usimamizi. Aina hizo ni:
  1.Ardhi ya kawaida inayosimamiwa na Kamishna wa Ardhi.
  2.Ardhi ya Hifadhi inayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi husika au Afisa wa Umma.
  3.Ardhi ya Kijiji inayosimamiwa na Halmashauri ya Kijiji kwa niaba ya wanakijiji wote kwa kuzingatia/kutekeleza maamuzi ya mkutano wa Kijiji.

  Halmashauri ya Kijiji ina wajibu wa kutunza mipaka ya Kijiji na kusimamia utoaji wa Hati za Hakimiliki ya Kimila. Ndani ya Ardhi ya Kijiji, hati inayotakiwa kutolewa ni Hati ya Hakimiliki ya Kimila. Sharti hili ni kwa mujibu wa sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999. hati ya Hakimiliki ya Kimila inayotolewa ina nguvu sawa kisheria na Hati ya Kumiliki Ardhi inayotolewa kwa mujibu wa Sheria Na. 4 yaani Hati inayotolewa ndani ya Ardhi ya kawaida.

  Sheria imeweka uwezekano wa kubadilisha msimamizi wa aina moja ya Ardhi kwenda kwa msimamizi wa aina nyingine. Azma hiyo ilipelekea umuhimu wa kuwepo utaratibu wa kisheria utakaowezesha jambo hilo kutekelezwa. Utaratibu huo ndio unaoitwa UHAWILISHAJI.

  Lengo la utaratibu huu ni kuwezesha kubadilisha msimamizi wa aina moja ya Ardhi kwenda kusimamia aina nyingine. Pia kuondoa uwezekano wa kutokea mgongano katika usimamizi wa Ardhi iwapo msimamizi wa aina moja ya Ardhi hatafahamu mipaka ya utawala wake.

  Utaratibu wa Uhawilishaji wa Ardhi ya Kijiji kuwa Ardhi ya kawaida au Ardhi ya Hifadhi umeelezwa katika Fungu la 4 fungu dogo 1-14 la Sheria ya Ardhi ya Vijiji. Kwa mujibu wa fungu hili Mhe. Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuhawilisha Ardhi ya Kijiji kwa manufaa ya Umma kwa kumwagiza Waziri mwenye dhamana ya Ardhi kutekeleza kusudio lake hilo. Kigezo cha msingi cha Uhawilishaji wa Ardhi ni MANUFAA YA UMMA ambapo maneno haya yamefafanuliwa maana yake kuwa ni “Maslahi kwa Taifa” yanajumuisha sababu zozote au matumizi ambayo sehemu kubwa ya jamii itakuwa na maslahi nayo au itanufaika nayo. Kinyume na maslahi ya mtu mmoja mmoja.

  Mtu anapoomba Ardhi ya Kijiji na kutaka apate hati inayotolewa chini ya Sheria Na. 4 ina maana anataka kubadilisha msimamizi wa Ardhi ya Kijiji toka Halmashauri ya Kijiji kwenda kwa Kamishna wa Ardhi. Matokeo haya hufanya Ardhi hiyo iliyomo ndani ya kijiji kuwa Ardhi ya Kawaida. Ili kutekeleza azma hiyo ya kubadili Ardhi ya Kijiji kuwa Ardhi ya Kawaida, mahitaji na hatua zifuatazo zitatakiwa zizingatiwe:

  MAHITAJI YA UHAWILISHAJI:
  1.Muhtasari wa Halmashauri ya Kijiji unaoonyesha
  i.mwombaji kupewa Ardhi katika Kijiji husika ukiwa na idadi ya wajumbe wanaoruhusu kufanyika kikao yaani itimie “coram” inayotakiwa (zaidi ya nusu ya watu wenye sifa ya kuhudhuria).
  ii.Muhtasari uonyeshe agenda za kikao,
  iii.majadiliano ya kina juu ya ombi la kupewa Ardhi,
  iv. majina ya wajumbe waliohudhuria,Wadhifa wao na saini zao, wasioweza kusoma na kuandika waweke saini za dole gumba
  2.Muhtasari wa Mkutano Mkuu wa Kijiji ukionyesha idadi ya wanakijiji wanaoruhusiwa kisheria kuhudhuria Mkutano wa Kijiji,
  i.majina ya wanakijiji waliohudhuria kupitisha ombi la Ardhi, saini zao, Vitongoji vyao,
  ii.agenda za mkutano na majadiliano ya kina na maamuzi yaliyofikiwa.
  3.Sketch au ramani inayoonyesha ukubwa wa Kijiji na ukubwa wa Ardhi inayoombwa.
  4.Halmashauri ya kijiji iwasilishe taarifa inayojadili kwa kina mambo yaliyoainishwa hapa chini na Taarifa hiyo isainiwe na wajumbe wa serikali ya kijiji wasiopungua 20:
  i.Ukubwa wa kijiji
  ii.Idadi ya wanakijiji ikionyesha, wanaume, wanawake na watoto
  iii.Idadi ya maeneo yaliyokwisha kutolewa kwa wawekezaji wengine pamoja na ukubwa wake ndani ya Ardhi ya Kijiji husika.
  iv.Shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika kijiji hicho kwa mfano kilimo, ufugaji, uvuvi, uwindaji , misitu ya hifadhi na kadhalika.
  v.Madhumuni na matumizi ya eneo linaloombwa pamoja na faida za mradi kwa wanakijiji na utaratibu wa kulipa fidia kwa wanakijiji.
  5.Kama mwombaji ni Kampuni, pamoja na mahitaji yaliyopo hapo juu Ataleta pia uthibitisho wa:
  -Uraia wa Wakurugenzi
  -“Memorandum and Articles of Association”
  -“Certificate of Incorporation”
  -Kama kampuni ni ya zamani na imebadilisha wakurugenzi, ombi hilo itabidi liambatishwe na “Annual Returns” pamoja na Andiko la Mradi.

  HATUA ZA UHAWILISHAJI:
  Utaratibu huu utaanza Kijijini, Wilayani (Halmashauri ya Wilaya husika) Kamishna wa Ardhi/Waziri na hatimaye kwa Mhe. Rais.

  ANGALIZO:
  1.Ardhi ya Kijiji inayosimamiwa na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya 1999 ISIPIMWE BILA KUZINGATIA TARATIBU ZA UHAWILISHAJI ZILIZOAINISHWA HAPO JUU.
  2.Serikali za vijiji zinapaswa kutekeleza Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya 1999, kwa kuhakikisha kuwa zinashirikiana na Halmashauri (W) ili kuwawezesha wananchi vijijini kupata Hati za Hakimiliki za Kimila.
  3.WAOMBAJI WA ARDHI KUTOKA NGAZI YA VIJIJI NI LAZIMA WAWE NA NYARAKA ZILIZOAINISHWA HAPO JUU KABLA YA KUWASILISHA MAOMBI YAO WILAYANI KWA HATUA ZAIDI.
   
Loading...