Mwinyijuma Othman, Mwanamageuzi aliyepigania uwepo wa vyama vingi anayeishi kwa kuokota makopo na hataki kuongelea siasa

Idugunde

JF-Expert Member
May 21, 2020
6,273
6,637
Alipambana kwa kila namna ili mfumo wa vyama vingi uwepo nchini
👇
--
kinaraapiic.jpg


Ukikutana naye mitaa ya Mwananyamala wilayani Kinondoni au pembezoni mwa Barabara ya Ali Hassan Mwinyi hutajihangaisha kumfuatilia.

Begani hubeba mfuko wa chupa za plastiki au wakati mwingine kuni, sawa na wale watu wanaokusanya chupa za plastiki na kwenda kuziuza kwa ajili ya matumizi mengine.

Na si rahisi kuamini utakapoambiwa ukweli kuhusu mchango wake katika kupigania mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliopo hivi sasa nchini Tanzania.

Jina la Mwinyijuma Othman Upindo (85) haliepukiki kwa yeyote anayetaka kuandika ama kujua historia ya harakati za kisiasa katika miaka ya themanini zilizochangia kuanzishwa upya kwa mfumo wa vyama vingi.

Mwinyijuma ni miongoni mwa Watanzania wachache waliojitokeza kwa ujasiri kuunga mkono hadharani harakati za kutaka mamlaka ziruhusu siasa za ushindani.

Lakini wakati Taifa likiadhimisha miaka 30 tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992 ambazo zilirejesha haki ya wananchi kuanzisha vyama vya siasa, Mwinyijuma anaishi maisha ambayo hayalingani na nafasi yake katika siasa wala mchango wake katika kupigania kurejeshwa kwa mfumo huo nchini.

Akiwa na umri wa miaka 49 na mfanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mwaka 1984, Mwinyijuma aliamua kuacha ajira na kujiunga na wanasiasa mwenzake, hasa James Mapalala kupigania haki ya kuunda chama kipya cha siasa.

Wakati huo, Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama pekee kilichoruhusiwa kufanya siasa nchini baada ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1965 yaliyofuta mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Bila kuogopa mazingira adui ya kisiasa wakati huo, Mwinyijuma alijitokeza kijasiri kusaidia kukusanya sahihi za Watanzania wanaounga mkono rai ya kubadilishwa sheria iliyozuia vyama vingi vya siasa, akitumia njia za siri na za wazi kusaka wafuasi.

Alianzaje siasa

Kwa miaka miwili tangu Septemba 1984 baada ya mshirika wake Mapalala kumwandikia mwenyekiti wa CCM, Julius Kambarage Nyerere, na Halmashauri Kuu ya chama hicho rai ya kutaka kuondolewa kwa sheria iliyozuia mfumo wa vyama vingi, Mwinyijuma alijikuta akitiwa nguvuni zaidi ya mara tatu.

Kutiwa kwake mbaroni na kutishwa hakukumfanya abadili msimamo. Aliendelea na harakati za kupigania mageuzi hadi Oktoba 21, 1986 pale yeye na Mapalala walipokamatwa na kuanza safari ya miaka mitatu ya maisha ya gerezani na uhamishoni.

Walikamatwa Oktoba mwaka 1986 chini ya Sheria ya Preventive Detention Act iliyompa mamlaka waziri kumkamata mtu anayefanya vitendo vinavyohatarisha amani kwa lengo la kumzuia asitende kosa hilo na baadaye kupelekwa uhamishoni kwa sheria ya Deportation Ordinance iliyompa rais mamlaka hayo ya kumpeleka mwananchi ukimbizini ndani ya nchi yake.

Mwinyijuma alikamatwa muda mfupi baada ya Mapalala kukamatwa. Polisi walikuwa wakiwafuatilia kwa zaidi ya siku tatu baada ya kupata habari kuwa Mapalala aliingiza nchini kadi za chama cha siasa zilizochapishwa Ujerumani.

Ufuatiliaji wa wana usalama uliwafikisha kwa Mwinyijuma ambao walibaini kuwa maboksi kadhaa yaliyokuwa na kadi hizo yalifichwa nyumbani kwake Mwananyamala Msisiri.

Baada ya kukamatwa, Mwinyijuma na mwenzake waliwekwa kizuizini kwa wiki kadhaa bila kushtakiwa kabla ya baadaye kupelekwa gerezani Lindi na Mtwara.

Wakati wenzake Mapalala akikaa gerezani Lindi kwa zaidi ya mwaka mmoja na baadae kuhamishiwa Mafia mwaka 1987. Mwinyijuma aliwekwa gereza la Ukonga kabla ya kuhamishiwa Kisiwa cha Ukerewe.

Mwinjuma alikaa gerezani kwa miaka miwili na baadaye kuhamishiwa Kisiwa cha Ukerewe ambapo aliishi hadi mwaka 1989 alipoachiwa kwa msaada wa shirika la kutetea haki za binadamu duniani la Amnesty International.

‘Yule bwana ameacha kabisa siasa’


Mwinyijuma hataki kabisa kuongelea yaliyomsibu gerezani na baadaye uhamishoni Ukerewe. Hata hivyo, jambo moja lililo wazi ni kwamba mara tu baada ya kuachiwa huru, maisha yake yalibadilika kabisa.

Mateso ya kimwili na kisaikolojia aliyoyapata akiwa gerezani na hali aliyoikuta nyumbani kwake vilibadili kabisa maisha yake. Hali hiyo imemsumbua kwa miaka mingi na kumuathiri hadi leo.

Kwa miaka kaadhaa amekuwa akikusanya kuni na magogo popote anapoyakuta na kuyajaza mbele ya nyumba yake iliyopo Mwananyamala Msisiri. Hivi sasa anakusanya zaidi chupa za plastiki na kuzirundika nyumbani kwake.

Mwandishi wa habari hizi alipokutana naye na kufanya mazungumzo mafupi, Mwinyijuma alionyesha wazi kutotaka kuzungumzia masuala ya siasa, akisema anaogopa kufanya hivyo kwa sababu mamlaka hazitaki ajihusishe na siasa na anaamini hadi leo anatafutwa amalizwe.

“Watu wa usalama wamenunua nyumba ya ghorofa baada ya nyumba yangu,” alidai.

“Wamo mule ndani miaka yote wanataka kunishughulikia mimi, wananishumbua usiku, wanataka kunipiga risasi. Usiku na mchana hawalali wananishughulikia mimi. Wanataka kuniua. Kwa hiyo nihurumie, nihurumie. Nisaidie, nisaidie tafadhali.

Kwa ujumla mtu yeyote akikuuliza kuhusu mimi mwambie yule bwana ameacha kabisa siasa, hataki kabisaaaa! “Mimi nasema hivi; duniani kote chama kinachotawala kina-dictate (kinalazimisha) mambo, asikudanganye mtu. Hata Amerika, Ulaya na sehemu za Asia hata wapi wana-dictate tu.”

Ombi lake la kutaka tusizungumzie kabisa siasa lilitutoa kwa muda katika mazungumzo yanayogusa siasa, lakini baadae mwandishi alijaribu tena kumdodosa kuhusu kukamatwa kwake na maisha yake gerezani.

“Mimi nilikamatwa siku moja na James (Mapalala). Tukapelekwa sehemu za Mtwara, huko tukakaa sana. Yeye akapelekwa Mafia na mimi nikapelekwa Ukerewe. Tulikaa gereza moja na mwenzangu lakini hatukuonana,” anasema.

Lakini ana hofu unapotaka kujua maisha yake akiwa Ukerewe.

“Don’t play with it my dear (usicheze na hilo ndugu yangu),” anasema Mwinyijuma.

“Niache tu! Ukisema yalikuwa mazuri ni mbaya tu na ukisema yalikuwa mabaya ni mbaya tu. Yaliyonikuta yamenikuta. Sasa hivi niache, sitaki matatizo.”

Uwezo mkubwa wa kushawishi

Kabla ya kufariki, Mapalala aliwahi kuzungumza na Mwananchi na kumwelezea Mwinyijuma kama mtu aliyekuwa na akili nyingi na aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza na kushawishi watu.

“Nimefanya naye kazi, ana uwezo mkubwa sana wa akili na anaijua siasa. Alikuwa mtu mwaminifu sana katika siasa,” alisema Hayati Mapalala katika mahojiano na Mwananchi kabla ya kufariki.

“Tulipofungwa ikawa mwisho kwake kufanya siasa. Alikuwa mtangazaji mzuri sana wa siasa, tena si siasa uchwara. Akisimama na kuzungumza watu walimkubali.

“Huyu mzee (Mwinyijuma) ni sehemu kubwa tu ya historia ya kudai mfumo wa vyama vingi lakini sijui kama kuna mtu analitambua hilo. Sisi kila wakati tunaangalia siasa za leo tu, kuna wakati ni umuhimu pia kuangalia historia.”

Mmoja wa ndugu anayeishi na mzee huyo anasema Mwinyijuma hakuwahi kujaliwa kuwa na mtoto hivyo kubaki akisaidiwa na ndugu wengine. Ameomba watu wanaomfahamu na wenye uwezo kujitokeza na kumsaidi arudi katika hali yake ya kawaida.

“Kwa kweli ana wakati mgumu, kwa kifupi ni mtu anayehitaji kusaidiwa,” alisema Mapalala.

Chanzo: Mwananchi
 
Nchi hii ni ile ya Tenda wema uende zako usingoje shukran !! Na ukiwa ni MTU unayependa kusema ukweli ujue utasomeshwa namba hadi uone maruweruwe au usiyaone kabisa !! Wanaofaidi keki ya taifa ni wale wajanja wajanja wa kusifia sifia hata vile visivyohitaji kusifiwa !!
 
Vyama vya Upinzani viuenzi mchango wake japo kwa kumkumbuka , najua hawawezi kufanya hilo kwa sababu matambo yao bado hayajajaa vizuri,.
Akina Bibititi Mohamed ndio waliomng'oa mkoloni lakini waliambulia patupu ! Wamekuja kufaidi keki wengine kabisa !!
 
Kwani kile kituo cha Mwendokas pale Manyanya Kinondoni kuitwa Mwinyjuma ni kwa ajili yake huyu au yupo mwingine?
 
Inasikitisha sana


Huyu Bwana itakuwa kule Gerezani walimdunga sindano za kulegeza nati za kichwa au walimfanyia vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kuchukua picha kama alivyofanyiwa yule jamaa wa 'Ze Utamu' wa 2005-2010

James Mapalala hata juzi kwny maadhimisho ya miaka 30 ya Vyama vingi kwa makusudi kabisa kaachwa kutajwa katika Waasisi halisi (ukiondoa Watoto wa kijitonyama) wa Mfumo wa vyama vingi.

Waasisi halisi wa Vyama vingi wakinyofolewa na kwny nafasi hizo wakakaa watoto wa Kijitonyama kina Mzee Mabere Nyaucho Marando, Augustino Lyatonga Mrema, Wilbroad Slaa, Prof Ibrahim Lipumba na baada yao kazi hizo wamewarithisha 'watoto' wao wa kisiasa Kaka Dalali na Kaka Kamanda wa Anga

Kuna Jamaa miaka ile ya 1995 aliwahi kutuambia karatasi ya kupigia kura ya wakati huo ( 1995) ilijaa Watu wa mfumo tu…hatukuelewa kwa wakati

Waliogombea Urais 1995

Augustino Mrema, Ibrahim Lipumba, Benjamin Mkapa na John Cheyo
 
Aiseee watu wabaya sana ,gerezani sio pazuri kabisa tena serikali wakiamua kukupeleka
 
Mohamed Said tunaomba historia hapa. Au wewe umeishia kuandika harakati za uhuru tu??

Huyu babu Mwiyijuma Othman Upindo anafaa kuwekwa katika historia ya uhuru wa pili baada ya wale wa harakati za uhuru wa bendera wa kumuondoa mkoloni toka Uingereza.

Tuna uhakika ujumbe umemfikia Mzee Mohamed Said na ataweza kumshawishi Mzee Mwinyijuma kufunguka na pia jumuiya kubwa ya kiTanzania kumpatia Mzee Mwinyijuma msaada aweze kutengemaa kisaikolojia.

Picha Mzee Mwinyijuma Othman Upindo ktk mitaa ya jiji la DSM.
1657453601633.png
 
Ukweli ni kwamba serikali zilizopita zilitumia nguvu kubwa sana kuwapunguza kasi watu walioonekana wanauzidi utawala nguvu
 
Huyu mzee mitaa ya kinondoni hakosekani kabisa.

Ile barabara ya kuelekea mwananyamala ni kwa jina lake??
 
Kuna mwingine alikuwa don enzi zake mkoani Dodoma.
Akawapa Ccm jengo la ghorofa dodoma mjin,ambalo ndio ccn wilaya,
Ila yule mzee sasa hivi hana hata pa kulala.
.CCM ni wachawi
 
Wapo watu pamoja na kuwafanyia ukatili mkubwa binadamu wenzao mfano kama huyo mzee na wengine kadhaa kwa tamaa tu ya vyeo na madaraka lakini kila kukicha ndio tunawaimba kwa wema na kuwasifu kwa sifa za uongo na wengine wakitaka waitwe watakatifu!!
 
Back
Top Bottom