Mwinjilisti: Barua kwa Rais Magufuli, kwanini umejiandaa kumwaga damu za watanzania wasio na hatia?

Francis12

JF-Expert Member
Sep 30, 2016
7,533
22,276
BARUA YA WAZI KWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI
kwanini umejiandaa kumwaga damu za watanzania wasio na hatia?
Na Mwinjilisti Kamara Kusupa: 0767 311422

Mheshimiwa Rais, naandika barua hii nikiamini kwamba endapo utaitilia maanani ukauelewa ujumbe wake utaepusha janga na maafa. Ukiipuuza usiuone umuhimu wake hilo kwangu si muhali, ninachojali ni kuufikisha ujumbe kwako na kwa Watanzania unaowatawala.

Katika barua hii natoa mifano kutoka kwenye Biblia kwakuwa naamini wewe ni mkristo, unayethamini ukweli na unayeamini yaliyoyandikwa na watangulizi wetu mitume na manabii ambao Mwenyezi Mungu aliwainua ili waseme na watu wa vizazi vyao.

Nimelitafakari kwa umakini onyo lako dhidi ya waliokusudia kuandamana tarehe 26 Aprili, 2018 wanaohamasishana kupitia mitandao na njia nyinginezo, nayo maandalizi yako ya kuwapinga waandamanaji yanaonekana wazi wazi.
Rais, umeonya kwa ukali ukisema watakaoandamana watakuona, kauli hiyo inaashiria umekusudia kuwafanyia mabaya, umejiapiza kuwa “watakwenda kuwaeleza baba zao.”

Hayo siyo maneno ya amani ni maneno ya Jemedari aliyejiandaa kupigana vita dhidi ya raia wake wasiokuwa na silaha, kwasababu tu raia hao wanataka kusema yale asiyopenda kusikia. “Wanaoiombea Tanzania na wanaokuombea wewe Rais” Awali ya yote nikiri kwamba wanaoiombea Tanzania wanafanya vyema, pia wapo wanaokuombea wewe Rais pasipo kukueleza ukweli kuhusu utawala wako na misimamo yako, hao wanafanya vibaya.

Kwasababu Mungu huwasikia wanaomsikiliza na huwakubalia (wayaombayo) hao wanaoyakubali maneno yake na kuyatii. Upo mfano hai wa Mfalme wa kwanza wa nchi ya Israeli aliyeitwa Sauli mwana wa Kishi, Mungu alimchagua ili awe mfalme na sherehe ya kumsimika ilifanyika hadharani.

Lakini huyo Mfalme Sauli alipoanza kutawala alifanya makosa yanayofanana na makosa ya Marais wengi wa nyakati zetu, Mfalme Sauli hakuwa msikivu. Mfalme Sauli hakukubali kushauriwa bali alifanya yale ambayo akili yake ilimwaminisha kwamba ndiyo yanastahili kufanywa, Mwenyezi Mungu
akamwambia Nabii Samweli (aliyemsimika na kumtawaza Sauli awe mfalme) “najuta kumchagua Sauli” (1Samweli 15:10-12).

Imeandikwa Samweli akamlilia Mungu usiku kucha, alipoamka alikwenda kumwona Mfalme Sauli uso kwa uso akampa ukweli wote. Hata hivyo huyo mfalme aliendeleza utamaduni wake wa kufanya mambo kama atakavyo badala ya kufanya mambo kama inavyotakiwa, ilifikia hatua Mungu akaishiwa uvumilivu akamuuliza Nabii Samweli hata lini wewe utamlilia Sauli?
Nani anayefaa kuwa mwalimu wako?

Inaeleweka duniani pote kwamba Urais ni kazi ambayo wanaoipata hawasomei darasani, kwahiyo hakuna yeyote anayeweza kukufundisha jinsi ya kutawala wala kukuelekeza namna nzuri. Kufanya kazi zako kama Rais. Hakuna
atakayekufundisha jinsi ya kutimiza majukumu yako ya kiutawala, kuanzia Marais wastaafu waliowahi kuitawala Tanzania kabla yako hadi wananchi wengine wasiowahi kuitawala Tanzania.

Hakuna Rais katika dunia yetu kuanzia Rais wa Taifa kubwa hadi Rais wa Taifa dogo, anayeweza kuwa mwalimu wako mzuri wa kukufundisha a, b, c, d za Urais, wala hakuna Rais wa nchi yoyote jirani anayestahili kuwa mwalimu wa
kukufundisha jinsi unavyowezakuwa Rais bora. Lakini kuna mwalimu mmoja tu anayekufaa, anaitwa Yesu atakufundisha somo muhimu liitwalo unyenyekevu wa moyo.

Kwenye Injili ya Mathayo 11:28-29 Yesu anasema “Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha, jivikeni nira yangu mjifunze kutoka kwangu kwakuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo na nira yangu ni laini.” Yeyote anayetaka Mungu wa kweli alisikie dua
lake na aweze kumpigania, anapaswa kulielewa vilivyo somo la unyenyekevu wa moyo.

Yeye asiyekuwa na huo unyenyekevu wa moyo anajidanganya mwenyewe, anaweza kukazana kumwomba Mungu kwa bidii akidhani hiyo bidii yake katika kuomba na kusali itachangia kumsukuma Mungu amsikie na kumtendea hayo ayaombayo. Wanaojidanganya kwa kumwomba Mungu kwa bidii pasipo unyenyekevu wa moyo ni wengi, kwenye waraka huu nitatoa mfano hai wa unyenyekevu wa moyo.

Maandamano ndani ya Biblia Kwenye kitabu cha 1Samweli 8: 4-7 imeandikwa
“ndipo wazee wote wakakusanyika pamoja na kumwendea Samweli huko Rama, wakamwambia tazama wewe umekuwa mzee na wanao (uliowaweka kutimiza majukumu ya kiutawala) hawaenendi katika njia zako, wanakula rushwa na kupotosha hukumu, wanatafuta faida kwenye nafasi za utawala.

Tunataka utufanyizie Mfalme atakayeamua kama ilivyo kwa mataifa mengine”
maneno yaliyo kwenye mabano ni yangu Ujumbe huo wambao wananchi walimpelekea Nabii Samweli kwenye makao yake yaliyoitwa
Rama, ulikuwa mbaya sana mbele yake Samweli na mbele ya Mungu. Lakini imeandikwa Mungu akamwambia Samweli “isikilize tu sauti ya watu hao na kila neno watakalokuambia, kwa maana hawakukukataa wewe bali wamenikataa mimi nisiwe mfalme juu yao.”

Uhalisia wa tukio hili ni kwamba watu walikusanyika pamoja na kuandamana hadi kwenye makao ya Nabii ili wamjulishe hisia zao. Tafsiri halisi ya maandamano ni watu kujikusanya pamoja na kutembea kwa pamoja hadi hapo
walipokusudia kuishia kwa lengo la kuelezea hisia zao. Haijalishi hisia hizo kuwa halali ama kutokuwa halali zikipimwa kwenye mizania na vigezo au
vipimo vya kibinaadamu.

Mwenyezi Mungu alijua hisia za waandamanaji kwamba ni mbaya sana, hata hivyo hakuwazuia wasiandamane wala hakuwahujumu kwa namna yoyote, ingawaje alikuwa na uwezo wote juu yao. Mwenyezi Mungu hakuwazuia wala
hakuwaadhibu, badala yake alimwagiza nabii awasikilize katika yote watakayomwambia.

Ingawaje maandamano yao yalikosa uhalali mbele ya Samweli na machoni pa Mungu mwenyewe, bado waandamanaji walisikilizwa na ujumbe wao ndio ulioifanya Israeli ipate ufalme. Siku aliposimikwa huyo Mfalme Sauli, nabii Samweli aliwaambia Waisraeli “tazama nimeyasikia madai yenu mmempata Mfalme, kabla sijaondoka mnishuhudie mbele ya Mungu na mbele ya Mfalme wenu (masihi wake), nilitwaa ng’ombe wa nani ama kwa mkono wangu huu
nilipokea rushwa kutoka kwa nani nami nitamrudishia.

Semeni ukweli ni nani niliyemuonea nikatoa hukumu isiyokuwa ya haki?” Watu walijibu kwamba hukuwahi kupokea rushwa wala hukutuonea, ndipo Samweli akasema kwa sasa ni wakati wa kiangazi lakini nitamwomba Mungu alete mvua ili mjue kwamba dhambi yenu mliyofanya ya kujitakia mfalme ni mbaya sana.

Nabii Samweli akaomba, Mungu akapeleka ngurumo na mvua hadi watu wakamsihi Samweli wakisema utuombee kwa Mungu wako tusije tukafa, kwakuwa tumetenda uovu kujitakia mfalme (1samweli mlango wa 12).

Maandamano katika historia ya Tanzania huru Mwezi Novemba mwaka 1966, wasomi wa Chuo kikuu eneo la mlimani wakishirikiana na wanafunzi waliokuwa kidato cha sita kutoka sekondari ya Kibaha, waliandamana hadi Ikulu ili kumjulisha hisia zao Rais wa wakati huo (hayati Mwalimu Julius Nyerere) walimweleza mambo kadhaa kuhusu utawala wake.

Miongoni mwa masuala waliyomweleza kwa uwazi ni kuhusu udikteta wake binafsi na udikteta wa chama kilichotawala (TANU), wasomi hao waliona kitendo cha kupelekwa JKT wakalitumikie Taifa kwa miezi sita na kukatwa mishahara yao pasipo kushirikishwa kwenye mjadala wa mambo yaliyowahusu ili kusikia hoja zao, ilikuwa sawa na kuwaburuza wakaita udikteta usiokubalika.

Mwandamanaji mmoja aliyeitwa Mkate alibeba bango lililoandikwa “better were the colonial days” akimaanisha ni heri enzi za ukoloni mambo yalikuwa mazuri.
Lingine ambalo mhutubiaji aliliweka wazi ni suala la utabaka na tofauti ya mapato kati ya wakubwa na wadogo, mhutubiaji alisema mbele ya Nyerere
“mishahara yenu (akimaanisha mishara ya watawala na wanasiasa) ni mikubwa mno punguzeni.”

Hayo yalikuwa maandamano ya kwanza dhidi ya utawala katika Tanzania huru, ikiwa ni miaka mitano tu tangu uondoke utawala wa kikoloni. Matunda ya maandamano hayo yakaandika historia mpya katika nchi yetu kwani ni hayo
maandamano ya Novemba 1966 ndiyo yaliyozaa Azimio la Arusha mwaka 1967.
Nyerere hakuyazuia maandamano wala hakupuuza ujumbe wa waandamanaji, ingawa maneno “afadhali ya ukoloni” yalimuuma, yalimuudhi na kumuumiza moyo, akahoji mnasema afadhali ya mkoloni!

Akawafukuza Nyerere alizikubali baadhi ya hoja za waandamanaji aliopoona zina mantiki, aliahidi kupunguza mshahara wake kwa asilimia 20% na
akawahakikishia hangewapeleka JKT watu walioiona kama kambi ya mateso, akamwagiza Waziri mkuu Rashid Kawawa ahakikishe wanafunzi hao hawarudi chuoni bali wanarudi makwao.

Mheshimiwa Rais umenukuliwa ukiwaonya watu wanaotaka kuchezea amani ya nchi ambayo unakiri kuwa ilijengwa katika misingi imara tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza, umesisitiza “msione vyaelea vimeundwa.” Kupitia waraka huu nakusihi uuone ukweli huu kwamba huko nyuma tulikotoka amani yetu Watanzania ilijengwa katika misingi ya udugu siyo uadui, uhasama wala ubabe.

Rais Nyerere hakupambana na waandamanaji wa 1966 kwa nguvu za dola, hakuthubutu kutumia Askari wenye risasi na mabomu kuwapinga waandamanaji wasio na silaha bali wenye hoja, Nyerere alikabiliana nao kihoja. Watanzania
tumejengwa katika msingi huo wa kujadiliana na kutofautiana bila kupigana.

Rais Nyerere akawathibitishia uhalali wa JKT wanafunzi waliompinga kwa kumwagiza Waziri mkuu wake Rashid Kawawa aende JKT aonyeshe mfano kwamba haukuwa mpango wa kuwakomoa waliosoma, bali mpango wa kujenga Taifa. Nyerere hakuwaepusha na JKT hata wanawe wa kuzaa, akina Anna Nyerere, Andrew (sasa hayati), Makongoro na Rose (wachache ninaowafahamu).
Waliokwenda JKT miaka ya sabini wangali wanakumbuka masimulizi yaliyohusu kisa cha Afande Vero (mwanamke aliyekuwa matata sana) jinsi alivyomzaba kofi Rashid Kawawa.

Ndani ya mwezi mmoja wa Desemba 1966 Nyerere aliutafakari ujumbe wa waandamanaji uliohusu tatizo la utabaka kati ya wachache wenye nacho waliotumia nafasi zao na madaraka yao kujitajirisha na tabaka la wavuja jasho. Nyerere akaona hayo hayafai kuwako ndani ya nchi huru, akahisi yatampunguzia uhalali wa kutawala.

Kwahiyo ilipofika Januari 26 1967 akaitisha kikao cha NEC mjini Arusha kilichoibuka na “Azimio la Arusha” ambalo kimsingi lilipiga vita utabaka, unyonyaji, dhuluma na watu kutumia madaraka yao kujitajirisha. maandamano ya Aprili 26 hayana madhara usipambane nayo Mheshimiwa Rais hakuna sababu yoyote halali inayokulazimisha kutumia nguvu kupambana na waandamanaji ifikapo tarehe 26 Aprili, 2018.

1.Kwasababu watakaoandamana hawatabeba silaha yoyote ya kuwadhuru ninyi watawala wala kuwadhuru wananchi wenzao, hali hiyo ya watu kuandamana bila silaha ndiyo inayofanya Watanzania makini wahoji inakuwaje ujiandae kutumia silaha kupambana na raia zako wasiokuwa na silaha wala wasiokuwa na madhara?

2. Maandamano ya tarehe 26 Aprili siyo ya kudumu, hayafanani na yaliyotokea Tunisia na Misri ambako wananchi walipiga kambi kuonyesha nia ya kuzikataa serikali zao.

3. Maandamano ya tarehe 26 Aprili ni ya siku moja kati ya siku 365 za mwaka, hayaizuii serikali yako isitimize majukumu yake, wala waandamanaji hawakuzuii wewe kama Rais kuendelea kuifanyia mema nchi yako. Maandamano yao hayakuzuii wewe usiwatendee mema Watanzania wanaokukubali, isipokuwa waandamanaji wanataka kuonyesha tu hisia zao kuhusiana na yale yanayogusa maisha yao ndani ya Tanzania yao chini ya utawala wako.

Kitendo cha watu kuonyesha hisia zao siyo dhambi wala siyo kosa la kuwafanya wapigwe na Askari, wavunjwe viungo vyao, waumizwe ama wauawe.

4. Sababu ya nne hao waandamanaji bado ni raia wako, hawana Tanzania nyingine isipokuwa Tanzania moja tu inayowahifadhi Watanzania wote, wala waandamanaji hawana Rais wao mwingine zaidi ya wewe Rais John Pombe Magufuli. Isipokuwa tofauti ndogo tu kwamba waandamanaji wana hisia
zao tofauti ambazo wamekusudia kuziweka wazi kupitia maandamano yao.

Hao watakaondamana hawatofautiani na Waisraeli walioandamana kumwendea Nabii Samweli kumwelezea hisia zao, maandamano ya Aprili 26 hayatofautiani na maandamano ya kihistoria ya wanafunzi ya Novemba 1966 yaliyozaa Azimio la Arusha.

Ikiwa maandamano ya Waisraeli yalizaa ufalme na maandamano ya wanafunzi ya mjini Dar es salaam yalizaa Azimio la Arusha, yaache maandamano hayo ya Aprili 26 yaandike historia tuone yatazaa nini. Usiyazuie!

5. Kuyazuia maandamano ambayo waandamanaji wamekamia kuyafanya maana
yake halisi ni kuanzisha mapambano yatakayozaa vurugu na kuondosha amani
iliyopo. Nakusihi Rais wangu usiwe chanzo cha vurugu za kuikomesha amani ndani ya nchi unayotawala, hekima ya kawaida inashauri kwamba “yeye anayeishi kwenye nyumba ya vioo asiwe wa kwanza kuwarushia wengine
mawe.”

Nakusihi waache watu waandamane kwa amani ili wapumue yanayowauma kwani hata hayati Mwalimu Nyerere aliumizwa na kejeli za “better were the colonial days” lakini ustahimilivu wake ulimwepusha kuandika historia mbaya ya kumwaga damu za raia anaowatawala. Nawe unaweza kudumisha
amani ya Tanzania kwa kutoyapinga maandamano kwa gharama kubwa na
gharama mbaya ya kumwaga damu.

Ukistahimili utaingia kwenye orodha ya viongozi makini wasioogopa hoja za
wanaowapinga bali husikiliza hoja na kuufanyia kazi ukweli unaowasilishwa kwao, wakiyaacha maneno yasiyofaa ya waandamanaji yaishie hewani.

6. Kwenye mikutano yako ya hadhara kuna Watanzania wengi wanaokukusanyikia ili kukueleza hisia zao, wapo waliodhulumiwa viwanja na wamerudishiwa, wapo walioonelewa kwa namna moja ama nyingine nawe umewasaidia kupata haki zao baada ya kuwasikiliza vilio vyao. Nakusihi uuone ukweli huu kwamba hata hao waliodhamiria kuandamana Aprili 26, bado ni Watanzania na wanayo haki ya kusikilizwa na Rais wao.

Inabidi serikali yako ijiweke kwenye mkao wa kupokea, ijue wanalilia nini? Yawezekana wanaililia Tanzania mpya na iliyo bora ambayo ukiwasikiliza utapata kilicho chema.

7. Nakusihi uuone ukweli huu kwamba thamani ya Mtanzania anayesema “ndiyo kwa Magufuli” ni sawa na thamani ya yule anayesema “hapana kwa Magufuli.” Thamani yao ni moja, Mtanzania hawezi kupungua thamani yake kwasababu tu ya kumwambia Rais hapana.

8. Unapojiandaa kukabiliana na waandamanaji kwa kutumia nguvu kubwa inabidi ujiulize unalinda nini? JE, unailinda haki ya mwananchi na uhuru wake wa kujieleza ama unalinda kiburi cha kiutawala kinachowasukuma kutokuwa tayari kusikia msiyoyapenda? Unapodhamiria kutumia nguvu kubwa kuzuia
maandamano, Je, thamani ya Mtanzania asemaye hapana itazingatiwa wakati wa
operesheni na kuchukuliwa kuwa sawa na thamani ya Mtanzania asemaye ndiyo?

Maana haiwezekani ukailinda amani ya Tanzania pasipo kuitambua thamani ya Mtanzania kwani “thamani” na “amani” ni pacha lazima viende pamoja.

9. Endapo itatokea Watanzania kadhaa wakapoteza uhai wao kwenye maandamano ya tarehe 26 Aprili 2018 JE, wewe binafsi utawaeleza nini Watanzania watakaobaki hai? Utawaeleza nini wazazi wao na ndugu wengine wa marehemu? Je, utatamba kwamba umefanikiwa kuwazimisha waandamanaji na kwahiyo waliouawa wachukuliwe kirahisi kwamba uhai wao hauna thamani, wameuliwa kama wanavyouliwa kunguni, mbu na virobota wanaostahili
kuangamizwa kuzuia magonjwa?

Mheshimiwa Rais umejiandaa kupambana na waandamanaji kwa kutumia Askari, lakini kupitia waraka huu nakutahadharisha mapema kwamba serikali yako haina kiwanda cha kufyatua Askari kama mashine inavyofyatua matofali, bali hao Askari (utakaowatumia) nao wana baba zao, wanamama zao, wana wake zao, wana waume zao, wana vijana wao, wana binti zao na ndugu zao
wengine wa damu.

Je, umefanya tathmini ya kisayansi ili kupata uhakika Tanzania yetu itakuwaje yakitokea mauaji ya halaiki? Nakufahamisha mapema kwamba damu ikimwagika itawasha moto usiozimika nchi nzima na utakuwa mwanzo wa wewe
kujiumbia upinzani wenye nguvu lakini ulio mbaya kwakuwa upinzani huo
utachanganyikana na mbegu za chuki, uhasama na uadui. Mapambano
yatakayotokana na kuzuia maandamano yatazalisha makundi ya kigaidi kila mkoa, kila wilaya na kila pahala ambapo Watanzania watakuwa wameuliwa.

Ukiwa Rais wetu watano hutatembea kifua mbele ndani ya Tanzania huru, badala yake utaifanya kazi ya Urais huku ukijificha kama nyoka anayetafutwa ili apondwe kichwa. Kwasababu hasira ya Watanzania wasiokubaliana nawe itaongezeka na kuwa kali zaidi, pia itaenea kwa kasi kwenye maeneo yote muhimu kuanzia ndani ya chama chako CCM hadi serikalini.

Upinzani utahamia kwenye vyombo vya dola, kwenye majeshi na ndani ya usalama wa Taifa watainuka Askari watakaokuwa tayari kukudhuru, tukifikia hali hiyo ujue wazi ni uamuzi wako uliokusukuma kupambana na Watanzania wenzako yaani waandamanaji wasiokuwa na silaha, ndio utakaokuwa
umezalisha hali hiyo ya hatari itakayoipotezea Tanzania amani yake.

11. Nakusihi tafadhali ukumbuke siku za nyuma Watanzania walipowapokea wageni wa Rais, huku Rais wao na mgeni wake wakitumia gari ya wazi iliyotembea taratibu kama imebeba maharusi. Rais na mgeni wake wakiwa kwenye gari ya wazi waliwapungia mikono Watanzania waliokwenda kuwapokea. Leo ninyi watawala wetu mnalazimika kusafirishwa kwenye gari za vioo vyenye giza (tinted glass) huku gari zilizowabeba zikienda kasi mkiwahofia wananchi waliokuchagueni na kukuwekeni madarakani.

Hapo ni lazima kuna jambo lisilo la kawaida limetokea, mmeiasi kanuni ya uongozi, mmekiuka mila ya utawala, hamuitendei haki historia ya nchi yetu, mnatakiwa kuwaongoza Watanzania kuurudia “utanzania” wao. Hatua unayokusudia kuichukua ya kupambana na waandamanaji ni hatua ya hatari yenye hasara nyingi kuliko faida, kwakuwa itakuongezea maadui ndani ya nchi
unayotawala.

Hatua hiyo italeta chuki penye upendo, itakomesha uvumilivu penye subira na
kuleta vilio penye kicheko, itawafanya vijana wapoteze tumaini lililoanza kuchipua baada ya ujio wako. Vijana waliokosa tumaini, wataanza kujitoa mhanga kwakuwa wataona Tanzania ni mali ya wachache walio madarakani wasiotaka kusikia lolote kutoka kwa walio chini yao.

Nayaandika haya kwa nia njema nikiamini kwamba hasara hizo zinaweza kuepukwa, ukitaka kujenga Tanzania ya Magufuli yaani Tanzania ya viwanda, ziepuke hatua mbaya zinazokufarakanisha wewe na umma, usijiongezee maadui.

Msome kwa makini Mtume Paulo, anavyowashauri wamwaminio Mungu akisema “tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu ambao
hakuna atakayemwona Mungu asipokuwa nao, mkiangalia sana mtu wa kwenu asiipungukie neema ya Mungu hadi shina la uchungu likaibuka ndani yake likamsumbua na kusababisha wengine watiwe unajisi kwa hilo” (Waebrania 12: 14 -15).

Katika kuijenga Tanzania upya unahitaji mchango wa kila Mtanzania wakiwemo wale wanaokwambia hapana, kwaajili hiyo achana kabisa na dhamira ya kuzuia maandamano badala yake serikali yako ijipange kuyadhibiti ili maandamano hayo yasichukue mwelekeo hasi wa uporaji na fujo. Askari wasiwachokoze
waandamanaji wala wasiwadhuru.

Ndimi
.....................................................
Mwinjilisti Kamara Kusupa
Magomeni Mwembechai,
Mtaa wa Mkwawa
DAR ES SALAAM
Nakala kwa:
- Vyombo vya Ulinzi na Usalama
-Vyombo vya habari
-Viongozi wa dini
-Marais wastaafu
-Viongozi wa CCM
-Viongozi wa vyama vya upinzani
-Mawaziri
- Wabunge
-Wakuu wa mikoa
-Wakuu wa Wilaya
-Wananchi wa kawaida
 
Nanukuu.....

1...Hakuna Rais katika dunia yetu kuanzia Rais wa Taifa kubwa hadi Rais wa Taifa dogo, anayeweza kuwa mwalimu wako mzuri wa kukufundisha a, b, c, d za Urais, wala hakuna Rais wa nchi yoyote jirani anayestahili kuwa mwalimu wa kukufundisha jinsi unavyowezakuwa Rais bora.

2...Yeye asiyekuwa na huo unyenyekevu wa moyo anajidanganya mwenyewe, anaweza kukazana kumwomba Mungu kwa bidii akidhani hiyo bidii yake katika kuomba na kusali itachangia kumsukuma Mungu amsikie na kumtendea hayo ayaombayo. Wanaojidanganya kwa kumwomba Mungu kwa bidii pasipo unyenyekevu wa moyo ni wengi.

3... Mwenyezi Mungu alijua hisia za waandamanaji kwamba ni mbaya sana, hata hivyo hakuwazuia wasiandamane wala hakuwahujumu kwa namna yoyote, ingawaje alikuwa na uwezo wote juu yao.

Mwenyezi Mungu hakuwazuia wala hakuwaadhibu, badala yake alimwagiza nabii awasikilize katika yote watakayomwambia.
Ingawaje maandamano yao yalikosa uhalali mbele ya Samweli na machoni pa Mungu mwenyewe, bado waandamanaji walisikilizwa na ujumbe wao ndio ulioifanya Israeli ipate ufalme.

Siku aliposimikwa huyo Mfalme Sauli, nabii Samweli aliwaambia Waisraeli “tazama
nimeyasikia madai yenu mmempata Mfalme, kabla sijaondoka mnishuhudie mbele ya Mungu na mbele ya Mfalme wenu (masihi wake).

Mwisho wa kunukuu.
 
-
Unapojiandaa kukabiliana na waandamanaji
kwa kutumia nguvu kubwa inabidi ujiulize
unalinda nini? JE, unailinda haki ya mwananchi
na uhuru wake wa kujieleza ama unalinda
kiburi cha kiutawala kinachowasukuma
kutokuwa tayari kusikia msiyoyapenda?
 
Hivi na wewe bado upo ?? Si ungepumzika tu, mbona ULISHAJICHOKEA ? Angalia gazeti uliloandika uliyemkusudia ATASOMA KWELI? Mwinjilisti jipumzishe UMESHACHOKA
 
Wacha kuchanganya dini na siasa.Kama utapewa kibali Ruksa usipopewa usiandamane tafuta chakula cha familia yako au fanya kazi zako.Mda wa kutoa kiki umekwisha
 
Bure kabisa..
Mpeleke ushauri bure wenu. Mheshimiwa Rais umejiandaa kupambana
na waandamanaji kwa kutumia Askari, lakini kupitia waraka huu nakutahadharisha mapema kwamba serikali yako haina kiwanda cha kufyatua Askari kama mashine inavyofyatua matofali, bali hao Askari (utakaowatumia) nao wana baba zao, wana mama zao, wana wake zao, wana waume zao,
wana vijana wao, wana binti zao na ndugu zao wengine wa damu.

Je, umefanya tathmini ya kisayansi ili kupata uhakika Tanzania yetu
itakuwaje yakitokea mauaji ya halaiki? Nakufahamisha mapema kwamba damu
ikimwagika itawasha moto usiozimika nchi nzima na utakuwa mwanzo wa wewe kujiumbia upinzani wenye nguvu lakini ulio mbaya kwakuwa upinzani huo utachanganyikana na mbegu za chuki, uhasama na uadui.
 
Mpeleke ushauri bure wenu.
Mheshimiwa Rais umejiandaa kupambana
na waandamanaji kwa kutumia Askari, lakini
kupitia waraka huu nakutahadharisha
mapema kwamba serikali yako haina kiwanda
cha kufyatua Askari kama mashine
inavyofyatua matofali, bali hao Askari
(utakaowatumia) nao wana baba zao, wana
mama zao, wana wake zao, wana waume zao,
wana vijana wao, wana binti zao na ndugu zao
wengine wa damu. JE, umefanya tathmini ya
kisayansi ili kupata uhakika Tanzania yetu
itakuwaje yakitokea mauaji ya halaiki?
Nakufahamisha mapema kwamba damu
ikimwagika itawasha moto usiozimika nchi
nzima na utakuwa mwanzo wa wewe
kujiumbia upinzani wenye nguvu lakini ulio
mbaya kwakuwa upinzani huo
utachanganyikana na mbegu za chuki,
uhasama na uadui.
Woga huu,pole sana
 
Na kweli hakuna Rais anaeweza kufundisha Rais mwingine kutawala
Lakini kila nchi ni lazima isonge mbele kimaendeleo.

Rais ana dini na anasali kila jumapili na nyie sasa yote hayo unafikiri hayajui.

Ila unafiki ni mbaya sana na ndio analopigania ili taifa lisonge mbele.

Tutaona rangi nyingi sana awamu hii
 
Mwaka huu ni mwaka wa nyaraka tu, jamani wasomaji tutasoma sana,
Maaskofu tayari, TEF tayari, Mwinjilisti tayari, .....

Ushauri wangu:

Mliobaki ombeni mkaonane na Rais Ikulu muongee naye ana kwa ana. Nadhani itasaidia zaidi.

Mbona wenzenu wanaomba appointment na wanaenda kumuona? Mf. Lowasa, wafanya biashara, wazungu wa ACACIA nk.
 
Back
Top Bottom