Mwerevu, mjinga na mpumbavu ni sifa za binadamu sio matusi

A-town

JF-Expert Member
Oct 25, 2011
494
169
Nimeona nilete mada hii mbele yenu tujadili pamoja ili isije kuwa kama yale yaliyowahi kusemwa bungeni na David Kafulila kuwa Serikali legelege .........watu wakajaa mate midomoni kutaka kumsulubu kijana wa watu halafu mwishowe wakaishia na aibu baada ya kukumbushwa kuwa maneno yale si yake bali hata yeye kayanukuu toka kwa baba wa taifa,kusema tu hivyo wabaya wake wote hoi. Kiongozi wa mjadala ule mwana mama Jenister Mhagama akaishia kusema jamani,"Maneno ya baba wa taifa yasitumiwe vibaya"lakini ujumbe ulikuwa umefika.

Leo hebu tujiulize je ni kweli alichokisema Mbunge wa Mbeya Joseph Mbilinyi (Sugu) kwa Waziri Mkuu ni tusi? Nauliza hivi ili wajuaji mnitoe usingizini.Hivi mausi huwa ni nini? Labda hapa niseme kuwa kwa ulewa wangu na taaluma yangu katika Kiswahili kindakindaki,neno tusi linaukilia .....neno ambalo jamii ilikubaliana kuwa lisitajwe hovyo na hadharani....kwa kuwa neno hilo yumkini linataja sehemu au kiungo cha mwili kisichopaswa kutamkwa hadharani na mtu.Ni makubaliano tu ya jamiilugha.

Sasa nitudi kwenye mada,nimesikia kuwa Mbuge amemuita Waziri Mkuu "Mpumbavu" halafu msemaji akakamatwa na kutiwa mbaroni(sijui kwa muda gani) kisha akaachiwa kwa kuwa eti wakamataji hawakufuata vigezo na masharti ya kumkamata mbunge katika viwanja vya bunge.

Nijuavyo mimi wanadamu huwa katika makundi mawili mintaarafu urazini na utashi wetu,kuna MWEREVU,MJINGA na MPUMBAVU nitaeleza sifa za watu hawa.

MWEREVU, huyu ni yule anayejua na anajua kuwa anajua huyu huwa mwalimu wa wengi akitumia hekima (hekima ni uwezo wa kutafakari jema na baya ili kuchukua hatua stahiki) na busara (busara ni uwezo kutenda lililojema kutokana tafakuri sahihi) kuwaelimisha wenzake na hasa ndio huwa washauri wa viongozi wetu katika kufanya maamuzi mbalimbali. Hapa taifa hungia kwenye matatizo makubwa iwapo viongozi wa juu watakosa watu hawa wa kuwashauri.

MJINGA, huyu ni yule ambaye hajui na anajua kuwa hajui,mtu huyu huwa tayari kujuzwa na wanaojua na huwa mpole na mnyenyekevu ili apate kujua huwa hajifanyi mjuaji kwa sababu hakika hajui na analitambua hilo.Kwa tabia mtu huyu huwa habishani bali hubisha ili kuchochea utolewaji wa maarifa na yeye hufaidi kutokana na maarifa hayo. Watu wa jinsi ndio wale ambao huonekana hatari kwa werevu kwa sababu wakijua huwa werevu ambao hujitambua.

MPUMBAVU, ni yule ambaye hajui na hajui kuwa hajui basi huyu atakuwa aking'ang'ania tu kile anachofikiri kuwa ndicho kumbe sicho na hata akifahamishwa basi huwa mkali ili kulinda kile anachoamini kuwa ni sahihi hata kama sio sahihi. Mtu huyu huhitaji nguvu kubwa na muda mwingi kumfanya ajue kwa sababu huwa mjuaji,na hupenda sana kubishana badala ya kubisha lengo likiwa ni kutetea kile anachokiamini hata kama sicho.

Kwa hali hii je mtoaji wa kauli hiyo 'mpumbavu' kweli alitukana? Wanaodhani alitukana je wamejiridhisha vya kutosha kuwa neno hilo ni tusi? Hivi neno hilo na maneno ya Peter Serukamba ni yapi hasa matusi? Hivi kumfananisha mbunge na mbwa sio tusi? Hawa wote waliosema hayo walifikishwa wapi?

Chonde chonde viongozi wetu mkitaka msisemwe tendeni haki,tumieni weledi na sheria za nchi,fuateni katiba hakuna atayewasema vibaya ila mkikiuka katiba na kuvunja sheria hakika mtapatilizwa na matendo na kauli zenu.

KATIBA YA 1977 TOLEO LA 2005 INASEMA:

Ibara ya 18 kila mtu-

(a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake

Nimetumia haki yangu kikatiba.

Naomba kuwasilisha.
 
Mpumbavu limetumika kwa zaidi ya mara 650 kwenye Biblia, hasa kitabu cha Methali.
 
Back
Top Bottom