Mwenyekiti wa UVCCM Sadifah na Dr Shein wafungua matembezi ya UVCCM kuenzi Mapinduzi.

security guard

JF-Expert Member
Sep 27, 2011
799
603
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema, katika kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi, vijana hawana budi kuzingatia mafunzo ya msingi ya mwenendo wa waasisi wa Mapinduzi hayo.

Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa matembezi ya Umoja wa Vijana wa CCM kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya mwaka 1964 huko Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dk. Shein amebainisha kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 ambao yaliwakomboa wananchi wa Zanzibar yaliwezekana tu kutokana na ujasiri, mshikamano, moyo wa kujitolea na uzalendo pamoja na ukweli miongoni mwa waasisi wa Mapindhzi hayo.

Aliwaeleza mamia ya vijana kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wanaoshiriki matembezi hayo kuwa katika hali ya unyonge waliyokuwa nayo wananchi wa Zanzibar na uwezo mkubwa wa utawala wa kikoloni uamuzi wa kufanya Mapinduzi ulikuwa mgumu lakini waasisi hao hawazingatia hayo kutokana na ujasiri waliokuwa nao na umadhubuti wa mshikamano wao.

Aliwakumbusha vijana hao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni jambo la lazima kutokana na ukandamizaji waliokuwa wakifanyiwa wa nanchi huku wakifanyiwa kila aina ya njama na misukosuko wasiweze kujitawala.

“Chama cha ASP katika kipindi cha miaka 7 tangu kuanzishwa mwaka 1957 kulipitia misukosuko mingi, viongozi na wanachama wake walikabiliana na vitisho, mbuni za kuwagawa na vitendo vya hila katika uchaguzi wa mwaka 1957, Januari 1961, Juni 1961 na uchaguzi wa mwaka 1963” Dk. Shein alieleza baadhi ya visa hivyo.

Kwa hiyo alisisitiza kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa halali kwa kuwa ndio yaliyowapa wananchi wote wa Zanzibar haki ya kujitawala na kuwaondoshea kila aina ya ubaguzi.

“Ni Mapinduzi yaliyowaondoshea wananchi wa Zanzibar unyonge wa kutawaliwa kwa karibu karne na nusu, ndio yaliyowaondoshea ubaguzi katika elimu, afya, ardhi na unyonyaji kwa kutangaza huduma hizo bila ya malipo” Dk. Shein alieleza.

Alifafanua kuwa kuweka hali za wananchi sawa kwa kuondosha ubaguzi na malipo katika huduma kama afya na elimu ni miongoni mwa ahadi za chama cha ASP na ndio maana, hatua kwa hatua, tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Kwanza hadi sasa zimekuwa zikitekeleza ahadi hizo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameutaka Umoja wa Vijana wa CCM kuendelea kuyalinda Mapinduzi na Muungano vitu alivyovieleza kuwa ndio nguzo mbili kuu za msingi wa uhuru, amani na maendeleo yaliyopatikana katika miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano ifikapo Aprili, 2014.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Sadifa Juma Khamis alieleza kuwa madhumuni ya matembezi hayo ni kupeleka ujumbe wa Mapinduzi kwa jamii ili kuleta hamasa kukumbuka mchango wa vijana katika Mapinduzi hayo ambayo hayawezi kufutika katika historia ya nchi yetu.

Alisema kuwa UVCCM inathamini sana mchango wa vijana wenzao waliofanya Mapinduzi wakiwa chini ya uongozi wa Jemedari Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Mwenyekiti huyo wa UVCCM aliongeza kuwa Mapinduzi ni tukio la kihistoria katika maendeleo ya Zanzibar hivyo vijana hawana budi kufanya tathmini ya nchi ilikotoka, ilipo na inakokwenda na kuchukua nafasi yao katika kuleta maendeleo.

Aliahidi umoja huo kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kwamba umoja huo hautawapa nafasi watu wanaobeza na kutaka kurejesha nyuma Mapinduzi hayo.
 

Attachments

  • sadifah.jpg
    sadifah.jpg
    200.2 KB · Views: 98
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom