TataMadiba
JF-Expert Member
- Feb 7, 2014
- 9,866
- 5,742
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE
07/01/2014
MWENYEKITI WA CHADEMA WILAYA YA TEMEKE ATEKWA
NYARA, ASHAMBULIWA NA KUTUPWA VICHAKANI
SOMA YOTE HAPOP CHINI---------------
Jeshi la Polisi kanda maalum Dsm, linafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio la kutekwa nyara, kupigwa na kujeruhiwa na hatimae kutupwa vichakani dhidi ya mtu aitwaye JOSEPH YONA miaka 32 mkazi wa Temeke Mtoni kwa Azizi Ally. Imegundulika kwamba mtu huyo ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke ambaye pia ni Mtaalam wa Maabara Chuo Kikuu cha Elimu (DUCE) kilichopo Chang’ombe.
Mnamo tarehe 7/1/2014 saa 5.00 usiku eneo la Ununio, mlalamikaji aitwaye Joseph Yona alienda kuomba msaada kwa mlinzi binafsi aitwaye ISMAIL SWALEHE ili aende Kituo cha Polisi kuripoti. Mlinzi alimuona Joseph Yona akiwa katika hali mbaya ya kujeruhiwa. Aliamua kwanza ampeleke kwa mwenyekiti wa serikali za mitaa Ununio. Mwenyekiti wa Ununio alipopatikana aliwasiliana na Mkuu wa Polisi Kawe ambaye alifika eneo la tukio akifuatana na RPC Kinondoni ACP. Camilius Wambura na kundi la wapelelezi. Maofisa wa Polisi walimhoji mlalamikaji kuhusu majeraha aliyonayo usoni na sehemu mbali mbali za mwili wake. Mlalamikaji aliweza kujieleza vizuri kwamba yeye ni mkazi Mtoni kwa Azizi Ally wilaya Temeke na kwamba ilipofika saa 5.oo ya tarehe 6/1/2014 alikuwa akipata vinywaji katika grocery ya Mgumbini eneo la Mtoni kwa Azizi Ali akiwa na wenzake watatu walikuwa wakimalizia vinywaji. Ghafla walijitokeza watu sita ambao walijitambulisha kuwa ni Maafisa wa Polisi na walimtaka aende nao Kituo cha Polisi cha Kati. Hata hivyo kati ya watu hao sita aliweza kumtambua mmoja wapo kwa sura na jina (limehifadhiwa) kwamba ni mwanachama mwenzake wa Chadema na alipojaribu kuulizia kuhusu huyo mtu aliyemtambua, haraka walimwingiza ndani ya gari Land Cruiser na kumfunga kitambaa usoni na kuondoka naye.
Kutokana na maelezo ya mlalamikaji waliomteka nyara walianza kumhoji ni kwa nini anaendelea kumshabikia Zito Kabwe wakati ni mtu anayeharibu chama chao? pili walimtaka akawaonyeshe rafiki yake ambaye anajulikana kwa jina HABIBU MCHANGE. Mlalamikaji JOSEPH YONA alianza kushambuliwa baada ya kudai kwamba ni kwa nini hapelekwi Polisi Kati (central) kama ilivyodaiwa awali. Aliendelea kuhojiwa na kupigwa hadi alipopoteza fahamu. Hatimaye usiku wa manane alipozinduka alijikuta yupo vichakani sehemu asiyoifahamu na ndipo alipoanza kutangatanga na kutafuta msaada huku akiwa katika hali ya maumivu makali katika mwili wake. Baada ya muda alifanikiwa kumpata mlinzi, mwenyekiti wa serikali za mitaa na hatimaye kuhojiwa na Maafisa wa Jeshi la Polisi.
Uchunguzi wa awali unaonyesha wazi kuwa tukio hili lina uhusiano wa moja kwa moja na mgogoro unaoendelea katika Chama cha Siasa Chadema. Aidha kabla ya tukio hili, mlalamikaji amekuwa katika hali ya hofu kutokana na kupokea simu nyingi na ujumbe mfupi (sms) wa vitisho kutoka kwa viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chadema ambao anadai anawafahamu. Pia jana ofisi ya Chadema Wilaya wa Temeke ilifungwa saa 10.00 jioni kwa kile kilichodaiwa kuwa ni maagizo kutoka katika ngazi za juu katika chama cha Chadema. Kutokana na tukio hili nimeunda jopo la wapelelezi waliobobea wa fani mbali mbali wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ACP. Jaffari Mohamed ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa na kuwachulia hatua kali za kisheria. Wakati huo huonatoa onyo kali kuwa vitendo vya utekaji nyara pamoja na madhara yanayofuata baada ya hapo hayavumiliki katika jamii ya Kitanzania. Yeyote atakayegundulika kujihusisha na matukio kama haya ajue wazi kwamba atachukuliwa hatua kali za kisheria bila ajizi na bila kujali nafasi yake katika jamii. Ni vizuri kila mtu au kundi lolote lenye matatizo au mgogoro lifuate taratibu za kisheria katika kutanzua migogoro badala ya kutumia vitisho, nguvu au utekaji nyara kama huu.
Natoa wito kwa mtu yeyote ambaye ni raia mwema mwenye taarifa sahihi kuhusu tukio hili awasiliane nasi ili tusaidiane kukomesha vitendo kama hivi visirudie tena popote nchini Tanzania.
(S. H. KOVA – CP)
KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM