- Mwenyekiti Kamati ya Richmond akatiwa maji (Gazeti la Majira)
Na Rehema Mwakasese
Na Rehema Mwakasese
KAMPUNI ya Huduma ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) imemkatia maji aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza Mkataba wa Richmond na kusababisha Waziri Mkuu na mawaziri wengine kujiuzulu, Dkt.Harrison Mwakyembe, baada ya kubainika amejiunganishia maji isivyo halali.
Wengine waliokatiwa maji kwa kushindwa kulipia ankara zao ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Bw. Vicent Mrisho anayedaiwa kiasi cha sh. 600,000, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Bw. Emmanuel ole Naiko anayedaiwa sh. 791,379 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bw. Peniel Lyimo.
Vigogo hao walikatiwa huduma hiyo ya maji Dar es Salaam jana katika operesheni kata maji inayoendeshwa na mafundi wa DAWASCO katika maeneo mbalimbali jijini.
Wengine waliokatiwa maji katika operesheni hiyo mbali na vigogo hao ni Bw. Abubakari Somo, Bw. Stanford Masulube, Bw. Miradji Msuya, Bw. Dominick Palangyo, Bw. Roger Magwaza na Tanzania Christian Church.
Akizungumzia hatua ya Dkt. Mwakyembe ambaye ni mbunge wa Mbeya kukutwa amejiunganishia maji, Ofisa Uhusiano wa DAWASCO, Bi. Badra Masoud, alisema wiki moja iliyopita mkewe alikwenda katika ofisi za kampuni hiyo kwa lengo la kujaza fomu ya kuomba huduma ya maji ndipo alipoelezwa kuwa wamejiunganishia maji isivyo halali.
Bila kumtaja jina lake, Bi. Masoud alisema walipomkatalia kumpa fomu hizo wakimtaka alipe faini kwanza alikataa.
"Kwa kuwa alikataa ndio maana leo hii (jana) tumekuja kumkatia," alisema Bi. Masoud. Alitaja faini aliyotakiwa kulipa kuwa ni sh. 600,000.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa wale wote ambao wameshindwa kulipia ankara za maji au kujiunganishia maji isivyo halali watafikishwa mahakamani ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.
"Wale wote wasiotaka kulipa tutang'oa mabomba na hatuogopi vitisho vyao kwani watu wenye uwezo ndio wanaoongoza kwa kukwepa kulipia bili za maji," alisema Bi. Masoud.
Kwa upande wake Meneje wa Kituo cha Boko, Bw. Ramadhan Mtendasi, alisema walifika nyumbani kwa Bw. ole Naiko, mara nne kudai ankara za huduma ya maji aliyotumia lakini alishindwa kulipa hadi hatua ya kumkatia inafikiwa jana.
"Maji yakikatika wao ndio wanaokuwa wa kwanza kulalamika wanasahau kuwa bila kulipia ankara zao kampuni hii itakufa," alisisitiza Bi. Masoud. Hatua ya kampuni hiyo kuwakatia vigogo hao huduma ya maji ni mwendelezo wa operesheni yake ya kukata maji kwa wadaiwa sugu.
Wiki hii kampuni hiyo ilikata maji nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Matein Lumbanga, ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania Geniva Uswisi na nyumba ya aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Maokola Majogo.