Mwenendo wa Kesi Ya Wakili Fatma Karume na Ilipofikia

Apr 26, 2022
64
99
MWENENDO WA KESI YA WAKILI FATMA KARUME NA ILIPOFIKIA

Habari, leo nakuletea UPDATE YA KESI YA WAKILI FATMA KARUME a.k.a. Shangazi, jinsi ilivyoanza, jinsi alivyosimamishwa Uwakili kwa muda na Mahakama Kuu na baadaye kufutwa Uwakili milele kabisa na Kamati ya Maadili ya Mawakili, jinsi alivyokata rufaa Mahakama Kuu akashinda, jinsi mwanasheria Mkuu alivyojaribu kukata rufaa akanyimwa leave (ruhusa) na Mahakama Kuu - akaomba ruhusa (leave) second bite (mara ya pili) Mahakama ya Rufani,

Jinsi Fatma alivyoupinga uamuzi uliomsimamisha Uwakili Mahakama ya Rufani akashindwa kesi na uamuzi ambao unasimama hadi leo dhidi ya Bi. Fatma Karume, maana bado amesimamishwa kufanya kazi ya Uwakili Tanzania bara.

Hizi ni tips huwa natoa kwa ajili ya wanafunzi wa law school of Tanzania wanaosoma legal ethics (Mawakili watarajiwa) na wananchi wengine wanaopenda kufatilia mambo ya Sheria.

Imeandaliwa nami Zakaria Maseke
zakariamaseke@gmail.com
Wakili / Advocate (Cohort 35).
(0746575259 - WhatsApp)

Mpaka sasa kuna kesi kama saba (7) ambazo zemewahi kufunguliwa kuhusiana na Uwakili wa Bi Fatma Karume.

1: Kuna aliyokuwa Wakili wa Ado Shaibu Mahakama Kuu - Hii ndio aliyosimamishwa Uwakili kwa muda (temporary) na Mheshimiwa Jaji Feleshi.

2: Kuna aliyoshtakiwa mbele ya Kamati (ya maadili) ya Mawakili - Hii ndio alifutwa (kuvuliwa) Uwakili jumla.

3 : Kuna aliyokata rufaa Mahakama Kuu akawekewa pingamizi kwa sababu walitumia nyaraka ya “Petition” badala ya “Memorandum” lakini Mahakama Kuu ikasema hiyo haina shida.

4: Kuna hiyo hiyo rufaa yake ya Mahakama Kuu ambayo alisikilizwa on merit baada ya lile pingamizi kuhusu kutozingatia nyaraka kutupiliwa mbali - Hii ndio alishinda na maamuzi ya Kamati ya Mawakili yaliyomfuta Uwakili milele yakatenguliwa.

5: Kuna ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliomba ruhusa (leave) Mahakama Kuu alitaka kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa akanyimwa.

6: Kuna ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tena baada ya kunyimwa ruhusa (leave) na Mahakama Kuu ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa, aliomba upya kwenye Mahakama ya Rufaa (sijasema alikata rufaa aliomba upya a.k.a second bite) akawekewa pingamizi kwa sababu alisahau kuambatanisha Order (Amri) ya Mahakama anayoilalamikia akapewa muda na Mahakama ailete.

7: Kuna ya Fatma Karume mwenyewe aliyoomba Revision Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kumsimamisha Uwakili wakati anamuwakilisha mteja wake Ado Shaibu kwenye kesi ya Ado Shaibu.

SASA TUANZE KUZICHAMBUA KESI ZOTE 7, MOJA BAADA YA NYINGINE:

1: Tuanze na kesi ya kwanza ya “ADO SAHAIBU Vs. HON. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI (PRESIDENT OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA), ADELARDUS LUBANGO KILANGI AND ATTORNEY GENERAL, Miscellaneous Civil Cause No. 29 of 2018, High Court of Tanzania at Dar es Salaam Main Registry (Unreported).” - Hii ndio ambayo Mahakama ilimsimamisha Uwakili kwa muda Bi Fatma Karume.

FACTS (STORI YA KESI):

Story iko hivi, mwaka 2018 Ado Shaibu, kupitia Wakili wake, Bi Fatma Karume, alimshtaki Mheshimiwa Rais wa wakati huo, Magufuli, akidai kwamba (Rais Magufuli) alivunja Katiba kwa kumteua Mheshimiwa Adelardus Kilangi ambaye hana vigezo, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kilangi kukubali uteuzi huo huku akijua hana sifa.

Mawakili wa Serikali wakamwekea mapingamizi mbalimbali kwamba;

1: Rais hawezi kushtakiwa Mahakamani.
2: Mlalamikaji hana sababu au madai ya msingi kufungua kesi (cause of action).
3: Nafuu au stahiki alizoomba Mahakamani haziwezekaniki au haziwezekani kutolewa.
4: Kiapo (affidavit) kilichotumika kuthibitisha maombi ni batili n.k.

Kesi ilisikilizwa kwa njia ya hoja za maandishi (written submission) na aliyekuwa Jaji Kiongozi wakati huo (Dr. Judge Feleshi).

Baada ya kila upande kuwasilisha hoja zake, Wakili wa Serikali akawasilisha pia malalamiko Mahakamani kwamba, Fatma Karume, kupitia lugha na maneno yake, ameonesha utovu wa nidhamu na dharau kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati huo, kwa kumuita “Wakili mchanga mno (far too junior), mtu asiye na uzoefu” n.k.

Mahakama Kuu baada ya kuchambua hoja za pande zote mbili, ikakubaliana na baadhi ya mapingamizi ya kisheria yaliyowekwa na serikali, cha kwanza ikatupilia mbali hoja na maombi (kesi) ya Ado Shaibu, na kuamuru mlalamikaji (Ado Shaibu) ailipe Serikali gharama zote za kesi, kwa sababu zifutazo; (NB: Hapa huwa kuna swali la bill of cost, je Serikali inaweza kudai costs au ni watu binafsi (private individuals & entities) tu ndo wanaweza? - Mwanafunzi wa law school ichukue hii ukafanye research).

Tuendelee, Mahakama baada ya kuchambua hoja za pande zote mbili, ilitupilia mbali kesi ya Ado Shaibu kwa sababu zifuatazo:

1: Mlalamikaji alishtaki watu au wahusika (parties) ambao sio sahihi, alitumia majina yao binafsi badala ya vyeo vyao, mfano badala ya Rais yeye akamshtaki Magufuli kama Magufuli binafsi ambaye anaweza kuondoka madarakani muda wowote kwa sababu Urais ni ofisi. Ingawa mbele ya jina la John Pombe Joseph Magufuli, waliweka kwenye mabano (the President of the United Republic of Tanzania), bado Mahakama ikasema hayo mabano peke yake hayatoshi kumaanisha kuwa hapo Magufuli ameshtakiwa kwa cheo chake kama Rais, kama Fatma Karume alivyodai.

Na Kama Ndivyo, Mahakama ikajiuliza pia, kwa nini Ado Shaibu hajamshtaki pia na Mwanasheria Mkuu kwa jina lake binafsi alafu aweke na mabano mbele yake, yaani kama hivi “Adelardus Lubango Kilangi (Mwanasheria Mkuu)?”

Na kweli, Kesi ilikuwa (Ado shaibu) dhidi ya watu au wahusika watatu:

1: Honourable John Pombe Joseph Magufuli (The President of the United Republic of Tanzania).
2: Adelardus Lubango Kilangi na
3: The Attorney General

(Ambapo Adelardus Kilangi ndo huyo huyo aliyekuwa Attorney General).

2: Pili, Mahakama ikasema Mlalamikaji hakuwa na sababu au madai ya msingi (cause of action) ya kuwashtaki hao aliowashtaki, kwa sababu alikosea kwa kushtaki watu binafsi ambao hana mgororo nao, na ambao hawawezi kuwajibishwa wao binafsi kwa majukumu walio nayo.

3: Nafuu au haja (stahiki) alizoomba Mahakamani haziwezekaniki kutolewa Mahakamani, (SIO KWA SABABU RAIS HASHTAKIWI) ila kwa sababu ziliombwa dhidi ya mtu binafsi ambaye hatakaa ofisini milele).

(Pingamizi kuhusu kiapo (affidavit) kwamba ni batili, lilikataliwa. Mahakama ilisema hilo sio jambo la kuongelea kwenye hatua ya pingamizi la awali ila ni suala la kuongelea wakati wa kusikiliza kesi (hearing) maana litahitaji hadi ushahidi). Kwenye pingamizi la awali wanashughulika na hoja za kisheria (pure points of law) tu ambayo ikipita inamaliza kesi hapo hapo, mfano Mahakama kutokuwa na Mamlaka n.k.

Mwisho, Mheshimiwa Jaji akagusia hoja ya matumizi ya lugha isiyofaa ya Bi Fatma Karume dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ambapo Fatma Karume, alikuwa amejibu hoja za Mawakili wa Serikali kwa kusema kwamba, “The Constitution cannot be used as a shield to protect unconstitutional conduct, as article 26(1) of the Constitution requires every person including the President to uphold the Constitution.

So, mark my words, in the event this case fails on a Preliminary Point, it is not over. If the President's unconstitutional conduct is protected by the Court on the ground that he is the President, we shall test it again once he leaves office, be it in 2020 or 2025 and in the latter case, the bench will also be a different one. That is the beauty of time.” (Emphasis added).

(Tafsiri isiyo rasmi ni kwamba), Katiba haiwezi kutumika kama kinga kulinda kitendo kilicho kinyume na Katiba, kwa sababu Ibara ya 26 Ibara ndogo ya kwanza ya Katiba inamtaka kila mtu akiwemo na Rais kuilinda Katiba.

Kwa hiyo, wekea alama (hifadhi) maneno yangu, ikiwa hii kesi itashindwa kwenye hatua ya pingamizi la awali, bado haitaishia hapa. Kama kitendo cha Rais kilicho kinyume na Katiba kikikingiwa kifua na Mahakama kwa sababu eti ni Rais, tutashtaki tena akitoka Madarakani, iwe ni 2020 au 2025 na katika kesi ijayo, jopo (la Majaji) nalo litakua tofauti. Hiyo ndo raha au uzuri wa muda”

Wakili wa Serikali, Mr. Mulwambo akairejesha tena Mahakama kwenye maneno mengine ya Fatma Karume ambapo alidai Fatma amekiuka miiko ya Kitaaluma na kuonesha dharau kwa kutoa shutuma binafsi kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo.

Sehemu ya maneno yenyewe ni hii hapa:

“...this Attorney General is far too junior to garner that kind of respect from the Bar… Given his lack of experience and junior position, Adelardus Kilangi has been a woefully disappointing legal advisor to the Government at cost of the rule of law and Constitution supremacy...In this Adelardus Kilangi has failed. A matter that is not surprising given his experience ...”

Kwamba, huyu Mwanasheria Mkuu ni mchanga sana kwenye sheria hadi apewe heshima yote hiyo kutoka kwa chama cha Mawakili. Kutokana na kukosa kwake uzoefu na nafasi changa, Adelardus Kilangi, amekuwa mshauri kisheria ambaye ni tatizo (taabu) na asiye na matumaini kwa Serikali hata kuugharimu utawala wa sheria na Ukuu wa Katiba. Kwa hili, Adelardus Kilangi amefeli (ameshindwa). Jambo ambalo si ajabu, kutokana na uzoefu wake.

NB: (Naomba niweke wazi hapa, “Junior” ni nani kisheria? Iko hivi Mawakili wanapeana vipaumbele (heshima) kulingana na muda ulioandikishwa jina lako kwenye Roll. Wa kwanza kukutangulia ndiye mkubwa (SENIOR) wako na akifika Mahakamani inabidi asikilizwe kwanza. Huku ukubwa sio suala la umri ni suala la kutangulia kuwa Wakili.) Nadhani sasa umeelewa Fatma Karume alikuwa anamaanisha nini.

(Ukizungumzia Bi Fatma Karume na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati huo (Kilangi), Bi Fatma alitangulia kuwa Wakili. Lakini hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni Wakili namba Moja (ndiye mkubwa) wa Mawakili wote, hata kama ameteuliwa leo, hata kama ulimtangulia kuapishwa kuwa Wakili.

(Sasa tuendelee, maana mimi nasimulia summary ya kilichotokea kwenye kesi, siko hapa kusema nani alikuwa sahihi au alikosea).

Mahakama ikasema, kwa kuwa Fatma Karume hajapewa nafasi ya kusikilizwa kuhusu madai ya utovu wa nidhamu yaliyotolewa dhidi yake, basi ni busara apelekwe kwenye chombo kinachohusika kuwawajibisha Mawakili, ili akajitetee huko.

Mheshimiwa Jaji (Feleshi) kwa kutumia mamlaka aliyo nayo kisheria, akamsimamisha Fatma Uwakili kwa muda (temporary) hadi pale suala lake litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi kwenye chombo husika.

Msajili wa Mahakama akaambiwa alipeleke hilo suala la madai au tuhuma za utovu wa nidhamu wa Bi Fatma Karume kwenye KAMATI YA NIDHAMU YA MAWAKILI (ADVOCATES DISCIPLINARY COMMITTEE). Hiyo ilikuwa ni tarehe 20/09/2019.

Naomba kutoa maelezo binafsi ili msomaji uelewe. Iko hivi, Jaji wa Mahakama Kuu ana mamlaka ya kumsimamisha Wakili kwa muda (temporary) kufanya kazi za kisheria (Uwakili), ikiwa utovu wa nidhamu huo utafanyika mbele yake wakati wa kusikiliza kesi, na kisha kulipeleka suala hilo kwenye MAHAKAMA KUU ambayo itathibitisha, kubadilisha au kutengua uamuzi huo.

Mamlaka hiyo ipo kwenye kifungu cha 22(2)(b) cha Sheria ya Mawakili. Baada ya Mahakama Kuu kuamua, ikiwa Wakili hataridhika, atakata rufaa kwenda kwenye KAMATI YA MAWAKILI.

FATMA KARUME BEFORE THE ADVOCATES COMMITTEE (FATMA MBELE YA KAMATI YA MAWAKILI):

2: Tunaingia Kesi ya pili ambayo citation yake ni “The Honourable Attorney General v Fatuma Amani Karume, Application no. 29 of 2019.”

FACTS (STORI):

Mwaka 2019, Mwanasheria Mkuu alitinga mbele ya Kamati ya Mawakili (Advocates Committee) kumshtaki Bi Fatma Karume.

NB: Kamati ya Mawakili inaundwa na Jaji wa Mahakama kuu ambaye ndo Mwenyekiti, na members wengine akiwemo huyo huyo Mwanasheria Mkuu (AG) au msaidizi wake au Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) au msaidizi wake na Wakili mmoja wa kujitegemea. (Baadhi wanalalamika kwamba muundo huu wa Kamati hauko sawa). Soma zaidi kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mawakili.

Mbele ya Kamati, Mwanasheria Mkuu aliiomba Kamati itamke kwamba, Bi Fatma Karume amefanya utovu wa nidhamu uliokithiri na pia jina lake lifutwe kwenye Orodha ya Mawakili.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) aliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali (SG) na mawakili wengine wa serikali huku Bi Fatuma Karume aliwakilishwa na Wakili Peter Kibatala.

Mwanasheria Mkuu akaleta mashahidi wanne lakini Bi Fatuma hakuleta shahidi yeyote.

Mwanasheria Mkuu akaelezea CV yake yote (wasifu wake) mbele ya Kamati, akasema madai ya Fatma Karume yalikuwa na nia ovu na yalilenga kuupotosha umma kuhusu elimu yake.

Mwanasheria Mkuu akaendelea kusema kwamba, Bi Fatuma Karume alipokuwa anamwakilisha Ado Sahaibu kwenye kesi Mahakamani, waliambiwa wawasilishe hoja zao kwa njia ya maandishi. Ambapo, Fatuma Karume alikiuka taaluma yake kwa kutumia maneno yasiyofaa kinyume cha maadili ya Mawakili.

Kwamba, Maneno hayo yalilenga kumdharau yeye (Mwanasheria Mkuu). Ambapo Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo (Jaji Feleshi) aliyafanyia kazi na kumsimamisha Uwakili kwa muda (temporary) Bi Fatuma Karume.

Na kwamba, hata baada ya kusimamishwa Uwakili kwa muda, Bi Fatuma Karume, aliendelea kuchapisha (kupost) Twitter shutuma za uongo na maneno ya upuuzi dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi (huyo Jaji Feleshi aliyemsimamisha Uwakili), Mawakili wengine, maafisa wa umma na Mahakama.

Posts za Bi Fatuma Kutoka Twitter zikaletwa na kusomwa mbele ya Kamati.

Mfano wakaleta post inasema, “Nimemalizika kwa kunifungia uwakili? Nyinyi mnaendeshwa kwa njaa ya matumbo yenu na si njaa ya HAKI! Mwambieni @ MagufullJP niko tayari KUFA kwa Demokrasia na Utawala wa Sheria, Wasiojulikana wanajua nakaa wapi waje tu Stupid!”

“Hakuna kitu kigumu kama kugombania utawala wa sheria na HAKI. Kuna watu WAPUMBAVU sana na hawaelewi umuhimu wa UTAWALA WA SHERIA mpaka pale wao au Jamaa zao yanawafikia. WaTZ wengi sana including majaji find Conceptual Thinking very difficult mpaka uwape CONCRETE ANECDOTES. Why?”

“It is so sad that so few Tanzanians even understand the legal nature of the Union between ZNZ and TNG including by the way the AG of TZ. Yeye ndio hata haelewi kwamba sio wa TNG!.”

“Walimpiga risasi Tundu ili TZ nzima ikose BRAIN kama TL. Can you imagine?”

Na kadhalika na kadhalika, (siwezi kunukuu zote hapa, ukitaka kusoma zote kasome kesi nzima, ipo mtandaoni. Ina kurasa 40 tu).

Baada ya hapo, Kamati ikampa nafasi ya kumsikiliza Bi Fatuma Karume. Wakili wa Fatma, Peter Kibatala akaiambia Kamati kwamba, Fatuma hana imani na Kamati. Kwamba aliamini ameshahukumiwa kabla hata ya uamuzi kutolewa, kwa sababu zifuatazo:

1: Muundo wa kamati, hususani uwepo wa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), kwa mtazamo wake hii ofisi ina ukaribu sana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, pia baadhi ya post walizoleta kutoka Twitter zinamgusa hadi DPP n.k., hivyo hakuona haja ya kuendelea kujitetea.

Hata hivyo Kibatala akaomba aruhusiwe kuwasilisha hoja za mwisho, akaruhusiwa.

Ingawa Bi Fatuma aligoma kujitetea, Kamati ilichukua alichojibu kwenye kiapo chake cha maandishi, ambapo mbali na kupinga baadhi ya malalamiko ya Mwanasheria Mkuu, alirudia baadhi ya maneno aliyoyasema kwenye ile kesi ya kwanza ya Ado Shaibu na kupelekea asimamishwe Uwakili kwa muda

Alisema kwamba, “That, it was my expectation that somebody who has somehow acquired such a lofty office as that of the Attorney General of the United Republic of Tanzania, so much that they refer themselves as ‘The Honourable Attorney General’ would immediately grasp such as obvious matter of fact and law.

The fact that the said Attorney General has missed such an obvious matter is to me justification for my professional opinion that Mr. Adelardus Lubango Kilangi is unqualified to hold an office previously exalted, respected and looked up to, as that of the Attorney General of the United Republic of Tanzania.”

“Kwamba, nilitarajia kwamba mtu ambaye kiasi fulani amepata ofisi ya juu kama hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama wanavyojiita wenyewe ‘Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu’, angeleewa kwa haraka hiyo hoja ya wazi kabisa ya kisheria na fact.

Ukweli kwamba Mwanasheria Mkuu huyo ameshindwa kutambua hoja hiyo ya wazi kabisa, kwangu ni uhalalisho wa maoni yangu ya kitaaluma kwamba, bwana Adelardus Lubango Kilangi hana sifa za kushika ofisi ambayo hapo nyuma ilikuwa imetukuka, iliheshimiwa na kuangaliwa, kama hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Pia akasema, “It is true that Mr. Adelardus Lubango Kilangi is a Junior Member of the Bar, his Roll Number is 2022, while Mine is 848. Mr. Adelardus Lubango Kilangi has many Advocates ahead of him, some admitted as recently as 2010. I have personally spoken to many Advocates who have told me that Mr. Adelardus Lubango Kilangi, unlike all previous Holders of the Office, has miserably failed in advising the Government in many pertinent issues.”

Kwamba, “ni kweli kuwa bwana Adelardus Lubango Kilangi ni Wakili Mchanga kwenye chama cha Mawakili, Roll Number yake ni 2022, wakati ya kwangu ni 848. Bwana Adelardus Lubango Kilangi ana Mawakili wengi waliomtangulia, wengine wameapishwa hivi karibuni mwaka 2010. Nimeongea binafsi na Mawakili wengi ambao wameniambia kwamba, bwana Adelardus Lubango Kilangi, sio kama Wanasheria wakuu waliopita, yeye ameshindwa vibaya sana kuishauri serikali kwenye mambo mengi ya msingi.”

Kamati inasema Fatuma aliendelea kusisitiza kwamba bwana Adelardus Lubango Kilangi hakuwa na sifa za kuwa Mwanasheria Mkuu. Fatuma aliamini kwamba bwana Adelardus Lubango Kilangi alipaswa kuapishwa kuwa Wakili miaka 15 kabla ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu.

(Msomaji pengine ungetamani kujua sifa na vigezo vya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Lakini siwezi kuandika hapa kila kitu. Unaweza kusoma Katiba Ibara ya 59 au kasome hii kesi yote, utakuta kila kitu. Lakini Kamati inasema iligundua kwamba, Mr. Adelardus Lubango Kilangi alikuwa na sifa zote za kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali).

UAMUZI WA KAMATI (YA MAADILI) YA MAWAKILI:

Kamati ilikuwa na mambo matatu ya kuamua.

{i}: Je, hizo post za Twitter ziliandikwa na Wakili Fatuma Karume?
{ii}: Kama ziliandikwa na yeye, je kuna kosa lolote la utovu wa nidhamu?
{iii}: Ni suluhisho (remedy) gani inaweza kutolewa?

Kamati iliridhika kwamba akaunti ya Twitter yenye hizo post ni ya Bi Fatuma mwenyewe na kwamba yeye ndiye aliyeandika hizo posts. Pia kulikuwepo na ushahidi mwingine wa video you tube.

Hata hivyo Bi Fatuma alikana kumiliki akaunti ya Twitter yenye hizo posts.

Kamati ikasema, ni kweli Bi Fatuma alikuwa anamtetea mteja wake kwenye ile kesi ya Ado Shaibu, lakini alipaswa kuwa muadilifu na kuwa kitaaluma kwa kutokumshambulia Mwanasheria Mkuu.

Hata kama bwana Adelardus Lubango Kilangi hakuwa na sifa za kuwa Mwanasheria Mkuu, lakini maneno aliyoyatumia Fatuma hayakufaa, ni kinyume na taaluma (ya Sheria) pia ni utovu wa nidhamu.

Pia Kamati ikasema kwamba, bwana Adelardus Lubango Kilangi, kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alikuwa ni Wakili namba moja kwenye orodha ya Mawakili, haijalishi kwamba Fatuma alimtangulia kuapishwa.

Kamati ilisema kwamba, Fatuma pia alionesha utovu wa Nidhamu mbele ya Kamati. Wakati anaingia ndani, alikaribishwa na Katibu aliyemuita kwa jina la “Fatma.” Akajibu kwa ukali, usiniite Fatma, niite Fatma Karume.

Wakati wa kusikiliza kesi, alikuwa anaingilia mara kwa mara kwa kusimama na kumpazia sauti Wakili wake na Kamati, na hata alitishia kabisa kumkataa Wakili wake aliyekuwa anajaribu kumtuliza.

Na ingawa wakati kesi inaanza, wahusika wote walionywa kwamba, kesi hii inasikilizwa chemba (kwa siri) hivyo hairuhusiwi kuongea kinachoendelea huko nje, lakini dakika chache baada ya Fatma kutoka nje, akaenda kupost Twitter kwamba:

“Leo nimeitwa kwenye Kamati ya Maadili, Adelardus kasema nimemkejeli. Jaji anaandika RECORDS kwa English. Sasa ninaomba kuelewa hilo neno kalitafsiri vipi, Jibu lake ‘kwani wewe si MTZ? Nimewaacha waendelee tu. Maana Jaji anashindwa kusema KEJELI kalitafsiri vipi?” Hiyo ilikuwa saa 11:55 AM tarehe 22/06/2020.

Ilipofika saa 14:22 PM siku hiyo hiyo akapost tena kwamba: “Sijiapata kuona watu waliokuwa hawaelewi wanachokifanya kama Mahakama ya TZ. Unamsuspend wakili, halafu eti unamshitaki kama wakili kwenye KAMATI ya MAADILI? They are not serious. Mtanisuspend mara ngapi? Siendi tena. Wafanye watakalo.”

Na saa 15:03 siku hiyo hiyo akapost tena, “I know that they want to INTIMIDATE me. They failed to think. Intimidation only works when you have something to lose. They took my practicing licence illegally and they want to INTIMIDATE me? They can keep it for all I care! I left the building a long time ago @judicarytz.”

Kuhusu ipi ni suluhu (adhabu) dhidi ya Wakili Fatma, Kamati ya Mawakili ilimtia hatiani Bi Fatuma Karume kwa utovu wa nidhamu uliokithiri. KAMATI IKAAMURU WAKILI FATMA KARUME AONDOLEWE JUMLA KWENYE DAFTARI LA ORODHA YA MAWAKILI kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria ya Mawakili.

Kwa hiyo Bi Fatuma Karume akawa amevuliwa Uwakili milele na Kamati ya Mawakili. Hiyo ilikuwa tarehe 23/09/2020 Dar es Salaam.

FATMA AKAKATA RUFAA MAHAKAMA KUU.

3: Tunaingia kesi ya tatu inaitwa “FATMA AMANI KARUME Vs. THE ATTORNEY GENERAL AND THE ADVOCATES COMMITTEE, CIVIL APPEAL NO. 02, OF 2020.” Hii ndiyo aliyokata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya Uamuzi wa Kamati uliomvua Uwakil imilele, akawekewa pingamizi la kisheria kwa sababu alitumia Petition badala ya Memorandum. (Bado aliwakilishwa na Wakili Msomi Peter Kibatala).

Hapa ameshatoka kwenye Kamati ya Mawakili akarudi tena Mahakama Kuu. Iko hivi, baada ya kuvuliwa Uwakili milele na Kamati (Advocates Committee), Fatma alikata rufaa Mahakama Kuu mbele ya Jopo la Majaji watatu (Full Bench). Mawakili wa Serikali wakamuwekea mapingamizi ikiwemo hoja kwamba:

{i}: Rufaa yake haijakamilika au sio sahihi kwa sababu hakutoa taarifa ya kukata rufaa (notice of appeal), kinyume cha kanuni ya 17(1) ya Kanuni za Mawakili za Nidhamu na Mashtaka Mengine - Advocates (Disciplinary and Other Proceedings) Rules, 2018.

{ii} Kwamba Fatma amekosea kukata rufaa kwa kuchanganya nyaraka zinazotakiwa ambapo badala ya kutumia “Petition of appeal” yeye aliandika “Memorandum of Appeal” kinyume cha Kanuni ya 17(2) ya Kanuni nilizotaja hapo juu na,

{iii} Kwamba rufaa ya Fatma ni mbaya kisheria kwa sababu hakufata utaratibu. Ambapo, alifungua rufaa moja kwa moja Mahakama Kuu kinyume cha Kanuni ya 17(5) ambayo inataka rufaa ianzie kwa Katibu (Secretary) wa Kamati ya Mawakili na kisha Katibu ndo aichukue na kuipeleka Mahakama Kuu.

Wakili wa Fatma Karume kwenye hii kesi, Peter Kibatala, akapewa nafasi ya kujibu hizo hoja zote za mapingamizi.

Kiufupi, mapingamizi yote yalishindwa na kutupiliwa mbali. Mahakama Kuu ikaamuru kesi (rufaa ya Fatma) iendelee kusikilizwa kama kawaida. (Ukitaka kujua ubishani uliokuwepo kati ya pande zote mbili na Mahakama ilijibuje kwa kila pingamizi kasome kesi yote - ina kurasa 35 tu). Hiyo ilikuwa ni tarehe 17/12/2020

KUSIKILIZWA KWA RUFAA YA FATMA:

4: Hii ni Kesi ya nne jina ni lile lile kama nilivyotangulia kutaja huko juu kwenye kesi iliyopita namba 3 - wakati wanasikiliza mapingamizi - ni “FATMA AMANI KARUME V. THE ATTORNEY GENERAL AND THE ADVOCATES COMMITTEE, CIVIL APPEAL NO. 02, OF 2020.” Jina ni moja lakini zimetenganishwa kila moja imeandikwa kwa wakati wake.

Hii ndiyo sasa ile rufaa yake aliyokata Mahakama Kuu akasikilizwa on merit baada ya yale mapingamizi kutupiliwa mbali* -.

Rufaa hii ilisikilizwa na jopo la Majaji watatu (full bench). Sheria inasema hivyo, kwamba rufaa kutoka Kamati ya Mawakili, lazima isikilizwe na Jopo la Majaji wasiopungua watatu (3).

Moja ya sababu aliyotumia Bi Fatma Karume kukata rufaa na iliyompa ushindi ni kwamba, Kamati ya Mawakili ilikosea kusikiliza na kuamua suala ambalo lilifunguliwa kwenye Kamati kinyume cha amri au agizo la Mahakama.

Wakili wa Fatma, Peter Kibatala akasema, Mahakama iliagiza kwamba, suala la Bi Fatma Karume lipelekwe kwenye Kamati na Msajili wa Mahakama Kuu, kwa hiyo ilikuwa ni makosa kwa Kamati kupokea malalamiko mapya kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kibatala akaiomba Mahakama Kuu itengue uamuzi wa Kamati, kwa kuwa Kamati haikuwa na mamlaka kisheria wakati inasikiliza suala la Bi Fatma Karume, pia suala la Fatma lilipelekwa kwenye Kamati na mtu ambaye hakua na mamlaka ya kufanya hivyo, ukizingatia kwamba agizo lenyewe la Mahakama bado lilikuwa palepale halijatenguliwa na Mahakama yenyewe.

Upande wa Mwanasheria Mkuu, Wakili wake akasema kweli kuna agizo la Mahakama kuhusiana na malalamiko dhidi ya Fatma Karume. Lakini akasema, hilo agizo halizuii kufungua malalamiko mapya kwenye Kamati.

Kwa sababu, malalamiko ya mwanzo yaliyotolewa agizo na Mahakama, yalihusu utovu wa nidhamu uliotokea wakati wa kusikiliza kesi (ya Ado Shaibu) Mahakamani tu. Lakini malalamiko mapya ya Mwanasheria Mkuu mbele ya Kamati, yaliongezea hadi makosa mengine ya nidhamu aliyofanya Bi. Fatma baadaye.

Hata hivyo, waheshimiwa Majaji walikubaliana na hoja ya Wakili Peter Kibatala. Wakasema, kwanza ni Mwanasheria Mkuu mwenyewe kupitia Mawakili wake aliyeanza kulalamika Mahakama Kuu kuhusu Fatma Karume, na kupelekea Fatma asimamishwe Uwakili hadi itakapoamuliwa vinginevyo na Kamati.

Na mwanzo kabisa, Mahakama iliagiza Msajili ndo alipeleke hilo suala kwenye Kamati ya Mawakili. Hata kama waliongezea makosa mengine aliyofanya Fatma baadaye, bado hakuna namna ambayo Mwanasheria Mkuu angeweza kufungua hayo malalamiko mapya akiunganisha na yale yaliyomo kwenye agizo la Mahakama bila kukiuka agizo la Mahakama.

Majaji wakasema, kama Mwanasheria Mkuu alitaka kufungua malalamiko mapya, alipaswa asubiri hadi yale malalamiko aliyowahi kuyatoa Mahakamani yapelekwe kwenye Kamati ya Mawakili kwa namna ilivyoelekezwa na Mahakama ama sivyo alitakiwa afungue malalamiko mengine mapya ambayo hayagusi kile alicholalamikia mwanzo na kutolewa agizo Mahakamani.

Waheshimiwa Majaji wakasema, hatua aliyoichukua Mwanasheria Mkuu ilikuwa inapelekea kukwamisha agizo na maelekezo ya Mahakama.

Hivyo Mahakama ikasema, malalamiko ya Mwanasheria Mkuu kwenye Kamati ya Mawakili hayakuwa sahihi na yalitakiwa kutupiliwa mbali.

Fatma Karume akashinda rufaa. Maamuzi ya Kamati ya Mawakili kumfuta Uwakili jumla au milele yakatenguliwa na kuwekwa kando. Kisha Mahakama Kuu ikaagiza tena Msajili achukue suala la Karume alipeleke kwenye Kamati ya Mawakili sawasawa na agizo la mwanzo la Mahakama kwenye kesi ya mwanzo ya Ado Shaibu. (Hiyo ilikuwa tarehe 17/06/2021).

(Kwa wanafunzi: Ikiwa reference for disallowance inaenda Mahakama Kuu, hapa tunaona full Bench wanaingia kwenye mtego ule ule (same trap) nao wanaamuru matter iende kwenye Kamati badala ya Mahakama Kuu kama Jaji mwenzao wa kwanza kwenye kesi ya Ado Shaibu. Section 22(2)(b) ya Advocates Committee).

MWANASHERIA MKUU KUKATA RUFAA KWENDA MAHAKAMA YA RUFANI (ambayo ndo Mahakama ya juu na yenye uamuzi wa mwisho Nchini).

5: Kesi ya tano, jina ni “THE ATTORNEY GENERAL & THE ADVOCATES COMMITTEE DHIDI YA (Vs) FATMA AMANI KARUME, MISC. CIVIL APPLICATION NO. 08, OF 2021 (HC).”

Baada ya kushindwa kesi, Mwanasheria Mkuu akaenda kuomba ruhusa (leave) ya Mahakama ili akate rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa. (NB: Kwa wasiosoma sheria, kuna baadhi ya rufaa (mwaka 2021) ilikua lazima uombe ruhusa ya Mahakama).

Wakili wa Fatma Karume, Peter Kibatala na Dr. Nshalla (Rais wa TLS wa wakati huo), wakapinga na kutoa sababu kwa nini ruhusa isitolewe. (Sitazieleza hapa, ila unaweza kusoma kesi yote ukitaka kuziona hizo sababu - kesi ina kurasa 12 tu).

Mahakama Kuu ikakataa kumpa Mwanasheria Mkuu ruhusa ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa, ikiwemo kwa sababu kwamba walishindwa kuonesha hoja za msingi zinazokidhi kujadiliwa huko Mahakama ya Rufani (arguable issues). Kesi ikafutwa. (Hiyo ilikuwa 17/12/2021)

6: Kesi ya sita ni “THE ATTORNEY GENERAL & THE ADVOCATES COMMITTEE Vs FATMA AMANI KARUME CIVIL APPLICATION NO. 694/01 OF 2021 (CAT).” Uamuzi wake ulitoka tarehe 08/09/2023.

-Hii ndio Mwanasheria Mkuu (AG) aliomba leave second bite (ruhusa mara ya pili) Mahakama ya Rufani baada ya kunyimwa leave mara ya kwanza na Mahakama Kuu.

(Ukitaka kujua kilichotokea itafute mtandaoni usome ina kurasa 20 tu)

7: Kesi ya Saba ni “FATMA AMANI KARUME Vs THE ATTORNEY GENERAL & THE JAJI KIONGOZI, HIGH COURT OF TANZANIA, CIVIL APPLICATION No. 434/01 OF 2019, (CAT).”

Hii ndiyo Fatma aliupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliomsimamisha Uwakili mbele ya Mahakama ya Rufani akashindwa kesi. Yeye aliupinga kwa kutumia njia (remedy) ya revision, Mahakama ya Rufani ikasema alikosea, kwa mujibu wa sheria alitakiwa arudi Mahakama Kuu pale pale aombe uamuzi huo kutenguliwa (disallowance) chini ya kiufungu namba 22(2)(b) cha Sheria ya Mawakili (Advocates Act).

Hizi kesi mbili za mwisho utasoma vizuri kwa wakati wako mwenyewe. Zina mambo mengi mi nimeeleza kwa ufupi sana. KAMA UNATAMANI KUFAULU LAW SCHOOL UTASOMA TU.

SASA NINI HATIMA YA MISS FATMA KARUME KWENYE HIZI KESI?

Mahakama Kuu ilishatengua maamuzi ya Kamati ya Mawakili (Advocates Committee) yaliyomvua Uwakili milele kwa sababu aliyetakiwa kupeleka hilo suala kwenye Kamati ni Msajili sio Mwanasheria Mkuu. Na Mahakama ikaagiza Msajili wa Mahakama Kuu ampeleke Fatma kwenye Kamati ya Mawakili , lakini mpaka leo naandika Makala hii Msajili hajafanya hivyo na kama amempeleka kimyakimya basi uamuzi haujatoka.

Kwa hiyo Baada ya kutengua maamuzi ya Kamati ya Mawakili (Advocates Committee) uliomvua uwakili milele, FATMA BADO HAJAREJESHEWA UWAKILI, bado ule uamuzi wa kwanza wa Mahakama Kuu (kwenye kesi ya Ado Sahaibu) uliomsimamisha Fatma Uwakili kwa muda (temporary) ndio unaendelea hadi leo, hadi hapo Msajili wa Mahakama atakapompeleka Fatma kwenye Kamati ya Mawakili ambapo anaweza kupewa adhabu yoyote au asipewe adhabu yoyote au hadi Fatma atakapo challenge huo uamuzi Mahakamani na kufanikiwa.

------Mwisho-------

Natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili.

Unaruhusiwa kabisa kushare lakini usibadili au kuhariri yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya.

Tafsiri hii ya Kesi Maarufu ya Miss Fatma Karume, imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke
zakariamaseke@gmail.com
Wakili / Advocate (Cohort 35).
(0746575259 - WhatsApp)
(0754575246 - Normal Texts/Calls)

Kwa wale wa law school, kesi ya Fatma Karume ni kati ya swali linalopendwa sana kuulizwa kwenye mitihani ya law school. Unatakiwa utafute hizo kesi zote uzisome ujue kwenye kila hatua ana nafuu (remedy) gani, sehemu gani ya kupeleka malalamiko yake, grounds (sababu) zake zitakua zipi na nyaraka (documents) muhimu.

Asanteni, Mungu awabariki.
By Advocate Zakaria Maseke
 
Sijuu kwanin watu wamekalia kimya bandiko hili. Lakini bwana Zakaria, naomba nikupongeze. Mimi najua sheria chache za barabarani tu lakini umenifanya nkaelewa hii kesi.
Kila la kheri mkuu. Nashukuru kwa taarifa. Ubarikiwe
 
MWENENDO WA KESI YA WAKILI FATMA KARUME NA ILIPOFIKIA

Habari, leo nakuletea UPDATE YA KESI YA WAKILI FATMA KARUME a.k.a. Shangazi, jinsi ilivyoanza, jinsi alivyosimamishwa Uwakili kwa muda na Mahakama Kuu na baadaye kufutwa Uwakili milele kabisa na Kamati ya Maadili ya Mawakili, jinsi alivyokata rufaa Mahakama Kuu akashinda, jinsi mwanasheria Mkuu alivyojaribu kukata rufaa akanyimwa leave (ruhusa) na Mahakama Kuu - akaomba ruhusa (leave) second bite (mara ya pili) Mahakama ya Rufani,

Jinsi Fatma alivyoupinga uamuzi uliomsimamisha Uwakili Mahakama ya Rufani akashindwa kesi na uamuzi ambao unasimama hadi leo dhidi ya Bi. Fatma Karume, maana bado amesimamishwa kufanya kazi ya Uwakili Tanzania bara.

Hizi ni tips huwa natoa kwa ajili ya wanafunzi wa law school of Tanzania wanaosoma legal ethics (Mawakili watarajiwa) na wananchi wengine wanaopenda kufatilia mambo ya Sheria.

Imeandaliwa nami Zakaria Maseke
zakariamaseke@gmail.com
Wakili / Advocate (Cohort 35).
(0746575259 - WhatsApp)

Mpaka sasa kuna kesi kama saba (7) ambazo zemewahi kufunguliwa kuhusiana na Uwakili wa Bi Fatma Karume.

1: Kuna aliyokuwa Wakili wa Ado Shaibu Mahakama Kuu - Hii ndio aliyosimamishwa Uwakili kwa muda (temporary) na Mheshimiwa Jaji Feleshi.

2: Kuna aliyoshtakiwa mbele ya Kamati (ya maadili) ya Mawakili - Hii ndio alifutwa (kuvuliwa) Uwakili jumla.

3 : Kuna aliyokata rufaa Mahakama Kuu akawekewa pingamizi kwa sababu walitumia nyaraka ya “Petition” badala ya “Memorandum” lakini Mahakama Kuu ikasema hiyo haina shida.

4: Kuna hiyo hiyo rufaa yake ya Mahakama Kuu ambayo alisikilizwa on merit baada ya lile pingamizi kuhusu kutozingatia nyaraka kutupiliwa mbali - Hii ndio alishinda na maamuzi ya Kamati ya Mawakili yaliyomfuta Uwakili milele yakatenguliwa.

5: Kuna ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliomba ruhusa (leave) Mahakama Kuu alitaka kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa akanyimwa.

6: Kuna ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tena baada ya kunyimwa ruhusa (leave) na Mahakama Kuu ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa, aliomba upya kwenye Mahakama ya Rufaa (sijasema alikata rufaa aliomba upya a.k.a second bite) akawekewa pingamizi kwa sababu alisahau kuambatanisha Order (Amri) ya Mahakama anayoilalamikia akapewa muda na Mahakama ailete.

7: Kuna ya Fatma Karume mwenyewe aliyoomba Revision Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kumsimamisha Uwakili wakati anamuwakilisha mteja wake Ado Shaibu kwenye kesi ya Ado Shaibu.

SASA TUANZE KUZICHAMBUA KESI ZOTE 7, MOJA BAADA YA NYINGINE:

1: Tuanze na kesi ya kwanza ya “ADO SAHAIBU Vs. HON. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI (PRESIDENT OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA), ADELARDUS LUBANGO KILANGI AND ATTORNEY GENERAL, Miscellaneous Civil Cause No. 29 of 2018, High Court of Tanzania at Dar es Salaam Main Registry (Unreported).” - Hii ndio ambayo Mahakama ilimsimamisha Uwakili kwa muda Bi Fatma Karume.

FACTS (STORI YA KESI):

Story iko hivi, mwaka 2018 Ado Shaibu, kupitia Wakili wake, Bi Fatma Karume, alimshtaki Mheshimiwa Rais wa wakati huo, Magufuli, akidai kwamba (Rais Magufuli) alivunja Katiba kwa kumteua Mheshimiwa Adelardus Kilangi ambaye hana vigezo, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kilangi kukubali uteuzi huo huku akijua hana sifa.

Mawakili wa Serikali wakamwekea mapingamizi mbalimbali kwamba;

1: Rais hawezi kushtakiwa Mahakamani.
2: Mlalamikaji hana sababu au madai ya msingi kufungua kesi (cause of action).
3: Nafuu au stahiki alizoomba Mahakamani haziwezekaniki au haziwezekani kutolewa.
4: Kiapo (affidavit) kilichotumika kuthibitisha maombi ni batili n.k.

Kesi ilisikilizwa kwa njia ya hoja za maandishi (written submission) na aliyekuwa Jaji Kiongozi wakati huo (Dr. Judge Feleshi).

Baada ya kila upande kuwasilisha hoja zake, Wakili wa Serikali akawasilisha pia malalamiko Mahakamani kwamba, Fatma Karume, kupitia lugha na maneno yake, ameonesha utovu wa nidhamu na dharau kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati huo, kwa kumuita “Wakili mchanga mno (far too junior), mtu asiye na uzoefu” n.k.

Mahakama Kuu baada ya kuchambua hoja za pande zote mbili, ikakubaliana na baadhi ya mapingamizi ya kisheria yaliyowekwa na serikali, cha kwanza ikatupilia mbali hoja na maombi (kesi) ya Ado Shaibu, na kuamuru mlalamikaji (Ado Shaibu) ailipe Serikali gharama zote za kesi, kwa sababu zifutazo; (NB: Hapa huwa kuna swali la bill of cost, je Serikali inaweza kudai costs au ni watu binafsi (private individuals & entities) tu ndo wanaweza? - Mwanafunzi wa law school ichukue hii ukafanye research).

Tuendelee, Mahakama baada ya kuchambua hoja za pande zote mbili, ilitupilia mbali kesi ya Ado Shaibu kwa sababu zifuatazo:

1: Mlalamikaji alishtaki watu au wahusika (parties) ambao sio sahihi, alitumia majina yao binafsi badala ya vyeo vyao, mfano badala ya Rais yeye akamshtaki Magufuli kama Magufuli binafsi ambaye anaweza kuondoka madarakani muda wowote kwa sababu Urais ni ofisi. Ingawa mbele ya jina la John Pombe Joseph Magufuli, waliweka kwenye mabano (the President of the United Republic of Tanzania), bado Mahakama ikasema hayo mabano peke yake hayatoshi kumaanisha kuwa hapo Magufuli ameshtakiwa kwa cheo chake kama Rais, kama Fatma Karume alivyodai.

Na Kama Ndivyo, Mahakama ikajiuliza pia, kwa nini Ado Shaibu hajamshtaki pia na Mwanasheria Mkuu kwa jina lake binafsi alafu aweke na mabano mbele yake, yaani kama hivi “Adelardus Lubango Kilangi (Mwanasheria Mkuu)?”

Na kweli, Kesi ilikuwa (Ado shaibu) dhidi ya watu au wahusika watatu:

1: Honourable John Pombe Joseph Magufuli (The President of the United Republic of Tanzania).
2: Adelardus Lubango Kilangi
na
3: The Attorney General

(Ambapo Adelardus Kilangi ndo huyo huyo aliyekuwa Attorney General).

2: Pili, Mahakama ikasema Mlalamikaji hakuwa na sababu au madai ya msingi (cause of action) ya kuwashtaki hao aliowashtaki, kwa sababu alikosea kwa kushtaki watu binafsi ambao hana mgororo nao, na ambao hawawezi kuwajibishwa wao binafsi kwa majukumu walio nayo.

3: Nafuu au haja (stahiki) alizoomba Mahakamani haziwezekaniki kutolewa Mahakamani, (SIO KWA SABABU RAIS HASHTAKIWI) ila kwa sababu ziliombwa dhidi ya mtu binafsi ambaye hatakaa ofisini milele).

(Pingamizi kuhusu kiapo (affidavit) kwamba ni batili, lilikataliwa. Mahakama ilisema hilo sio jambo la kuongelea kwenye hatua ya pingamizi la awali ila ni suala la kuongelea wakati wa kusikiliza kesi (hearing) maana litahitaji hadi ushahidi). Kwenye pingamizi la awali wanashughulika na hoja za kisheria (pure points of law) tu ambayo ikipita inamaliza kesi hapo hapo, mfano Mahakama kutokuwa na Mamlaka n.k.

Mwisho, Mheshimiwa Jaji akagusia hoja ya matumizi ya lugha isiyofaa ya Bi Fatma Karume dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ambapo Fatma Karume, alikuwa amejibu hoja za Mawakili wa Serikali kwa kusema kwamba, “The Constitution cannot be used as a shield to protect unconstitutional conduct, as article 26(1) of the Constitution requires every person including the President to uphold the Constitution.

So, mark my words, in the event this case fails on a Preliminary Point, it is not over. If the President's unconstitutional conduct is protected by the Court on the ground that he is the President, we shall test it again once he leaves office, be it in 2020 or 2025 and in the latter case, the bench will also be a different one. That is the beauty of time.”
(Emphasis added).

(Tafsiri isiyo rasmi ni kwamba), Katiba haiwezi kutumika kama kinga kulinda kitendo kilicho kinyume na Katiba, kwa sababu Ibara ya 26 Ibara ndogo ya kwanza ya Katiba inamtaka kila mtu akiwemo na Rais kuilinda Katiba.

Kwa hiyo, wekea alama (hifadhi) maneno yangu, ikiwa hii kesi itashindwa kwenye hatua ya pingamizi la awali, bado haitaishia hapa. Kama kitendo cha Rais kilicho kinyume na Katiba kikikingiwa kifua na Mahakama kwa sababu eti ni Rais, tutashtaki tena akitoka Madarakani, iwe ni 2020 au 2025 na katika kesi ijayo, jopo (la Majaji) nalo litakua tofauti. Hiyo ndo raha au uzuri wa muda”

Wakili wa Serikali, Mr. Mulwambo akairejesha tena Mahakama kwenye maneno mengine ya Fatma Karume ambapo alidai Fatma amekiuka miiko ya Kitaaluma na kuonesha dharau kwa kutoa shutuma binafsi kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo.

Sehemu ya maneno yenyewe ni hii hapa:

“...this Attorney General is far too junior to garner that kind of respect from the Bar… Given his lack of experience and junior position, Adelardus Kilangi has been a woefully disappointing legal advisor to the Government at cost of the rule of law and Constitution supremacy...In this Adelardus Kilangi has failed. A matter that is not surprising given his experience ...”

Kwamba, huyu Mwanasheria Mkuu ni mchanga sana kwenye sheria hadi apewe heshima yote hiyo kutoka kwa chama cha Mawakili. Kutokana na kukosa kwake uzoefu na nafasi changa, Adelardus Kilangi, amekuwa mshauri kisheria ambaye ni tatizo (taabu) na asiye na matumaini kwa Serikali hata kuugharimu utawala wa sheria na Ukuu wa Katiba. Kwa hili, Adelardus Kilangi amefeli (ameshindwa). Jambo ambalo si ajabu, kutokana na uzoefu wake.

NB: (Naomba niweke wazi hapa, “Junior” ni nani kisheria? Iko hivi Mawakili wanapeana vipaumbele (heshima) kulingana na muda ulioandikishwa jina lako kwenye Roll. Wa kwanza kukutangulia ndiye mkubwa (SENIOR) wako na akifika Mahakamani inabidi asikilizwe kwanza. Huku ukubwa sio suala la umri ni suala la kutangulia kuwa Wakili.) Nadhani sasa umeelewa Fatma Karume alikuwa anamaanisha nini.

(Ukizungumzia Bi Fatma Karume na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati huo (Kilangi), Bi Fatma alitangulia kuwa Wakili. Lakini hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni Wakili namba Moja (ndiye mkubwa) wa Mawakili wote, hata kama ameteuliwa leo, hata kama ulimtangulia kuapishwa kuwa Wakili.

(Sasa tuendelee, maana mimi nasimulia summary ya kilichotokea kwenye kesi, siko hapa kusema nani alikuwa sahihi au alikosea).

Mahakama ikasema, kwa kuwa Fatma Karume hajapewa nafasi ya kusikilizwa kuhusu madai ya utovu wa nidhamu yaliyotolewa dhidi yake, basi ni busara apelekwe kwenye chombo kinachohusika kuwawajibisha Mawakili, ili akajitetee huko.

Mheshimiwa Jaji (Feleshi) kwa kutumia mamlaka aliyo nayo kisheria, akamsimamisha Fatma Uwakili kwa muda (temporary) hadi pale suala lake litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi kwenye chombo husika.

Msajili wa Mahakama akaambiwa alipeleke hilo suala la madai au tuhuma za utovu wa nidhamu wa Bi Fatma Karume kwenye KAMATI YA NIDHAMU YA MAWAKILI (ADVOCATES DISCIPLINARY COMMITTEE). Hiyo ilikuwa ni tarehe 20/09/2019.

Naomba kutoa maelezo binafsi ili msomaji uelewe. Iko hivi, Jaji wa Mahakama Kuu ana mamlaka ya kumsimamisha Wakili kwa muda (temporary) kufanya kazi za kisheria (Uwakili), ikiwa utovu wa nidhamu huo utafanyika mbele yake wakati wa kusikiliza kesi, na kisha kulipeleka suala hilo kwenye MAHAKAMA KUU ambayo itathibitisha, kubadilisha au kutengua uamuzi huo.

Mamlaka hiyo ipo kwenye kifungu cha 22(2)(b) cha Sheria ya Mawakili. Baada ya Mahakama Kuu kuamua, ikiwa Wakili hataridhika, atakata rufaa kwenda kwenye KAMATI YA MAWAKILI.

FATMA KARUME BEFORE THE ADVOCATES COMMITTEE (FATMA MBELE YA KAMATI YA MAWAKILI):

2: Tunaingia Kesi ya pili ambayo citation yake ni “The Honourable Attorney General v Fatuma Amani Karume, Application no. 29 of 2019.”

FACTS (STORI):

Mwaka 2019, Mwanasheria Mkuu alitinga mbele ya Kamati ya Mawakili (Advocates Committee) kumshtaki Bi Fatma Karume.

NB: Kamati ya Mawakili inaundwa na Jaji wa Mahakama kuu ambaye ndo Mwenyekiti, na members wengine akiwemo huyo huyo Mwanasheria Mkuu (AG) au msaidizi wake au Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) au msaidizi wake na Wakili mmoja wa kujitegemea. (Baadhi wanalalamika kwamba muundo huu wa Kamati hauko sawa). Soma zaidi kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mawakili.

Mbele ya Kamati, Mwanasheria Mkuu aliiomba Kamati itamke kwamba, Bi Fatma Karume amefanya utovu wa nidhamu uliokithiri na pia jina lake lifutwe kwenye Orodha ya Mawakili.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) aliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali (SG) na mawakili wengine wa serikali huku Bi Fatuma Karume aliwakilishwa na Wakili Peter Kibatala.

Mwanasheria Mkuu akaleta mashahidi wanne lakini Bi Fatuma hakuleta shahidi yeyote.

Mwanasheria Mkuu akaelezea CV yake yote (wasifu wake) mbele ya Kamati, akasema madai ya Fatma Karume yalikuwa na nia ovu na yalilenga kuupotosha umma kuhusu elimu yake.

Mwanasheria Mkuu akaendelea kusema kwamba, Bi Fatuma Karume alipokuwa anamwakilisha Ado Sahaibu kwenye kesi Mahakamani, waliambiwa wawasilishe hoja zao kwa njia ya maandishi. Ambapo, Fatuma Karume alikiuka taaluma yake kwa kutumia maneno yasiyofaa kinyume cha maadili ya Mawakili.

Kwamba, Maneno hayo yalilenga kumdharau yeye (Mwanasheria Mkuu). Ambapo Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo (Jaji Feleshi) aliyafanyia kazi na kumsimamisha Uwakili kwa muda (temporary) Bi Fatuma Karume.

Na kwamba, hata baada ya kusimamishwa Uwakili kwa muda, Bi Fatuma Karume, aliendelea kuchapisha (kupost) Twitter shutuma za uongo na maneno ya upuuzi dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi (huyo Jaji Feleshi aliyemsimamisha Uwakili), Mawakili wengine, maafisa wa umma na Mahakama.

Posts za Bi Fatuma Kutoka Twitter zikaletwa na kusomwa mbele ya Kamati.

Mfano wakaleta post inasema, “Nimemalizika kwa kunifungia uwakili? Nyinyi mnaendeshwa kwa njaa ya matumbo yenu na si njaa ya HAKI! Mwambieni @ MagufullJP niko tayari KUFA kwa Demokrasia na Utawala wa Sheria, Wasiojulikana wanajua nakaa wapi waje tu Stupid!”

“Hakuna kitu kigumu kama kugombania utawala wa sheria na HAKI. Kuna watu WAPUMBAVU sana na hawaelewi umuhimu wa UTAWALA WA SHERIA mpaka pale wao au Jamaa zao yanawafikia. WaTZ wengi sana including majaji find Conceptual Thinking very difficult mpaka uwape CONCRETE ANECDOTES. Why?”

“It is so sad that so few Tanzanians even understand the legal nature of the Union between ZNZ and TNG including by the way the AG of TZ. Yeye ndio hata haelewi kwamba sio wa TNG!.”

“Walimpiga risasi Tundu ili TZ nzima ikose BRAIN kama TL. Can you imagine?”

Na kadhalika na kadhalika, (siwezi kunukuu zote hapa, ukitaka kusoma zote kasome kesi nzima, ipo mtandaoni. Ina kurasa 40 tu).

Baada ya hapo, Kamati ikampa nafasi ya kumsikiliza Bi Fatuma Karume. Wakili wa Fatma, Peter Kibatala akaiambia Kamati kwamba, Fatuma hana imani na Kamati. Kwamba aliamini ameshahukumiwa kabla hata ya uamuzi kutolewa, kwa sababu zifuatazo:

1: Muundo wa kamati, hususani uwepo wa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), kwa mtazamo wake hii ofisi ina ukaribu sana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, pia baadhi ya post walizoleta kutoka Twitter zinamgusa hadi DPP n.k., hivyo hakuona haja ya kuendelea kujitetea.

Hata hivyo Kibatala akaomba aruhusiwe kuwasilisha hoja za mwisho, akaruhusiwa.

Ingawa Bi Fatuma aligoma kujitetea, Kamati ilichukua alichojibu kwenye kiapo chake cha maandishi, ambapo mbali na kupinga baadhi ya malalamiko ya Mwanasheria Mkuu, alirudia baadhi ya maneno aliyoyasema kwenye ile kesi ya kwanza ya Ado Shaibu na kupelekea asimamishwe Uwakili kwa muda

Alisema kwamba, “That, it was my expectation that somebody who has somehow acquired such a lofty office as that of the Attorney General of the United Republic of Tanzania, so much that they refer themselves as ‘The Honourable Attorney General’ would immediately grasp such as obvious matter of fact and law.

The fact that the said Attorney General has missed such an obvious matter is to me justification for my professional opinion that Mr. Adelardus Lubango Kilangi is unqualified to hold an office previously exalted, respected and looked up to, as that of the Attorney General of the United Republic of Tanzania.”

“Kwamba, nilitarajia kwamba mtu ambaye kiasi fulani amepata ofisi ya juu kama hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama wanavyojiita wenyewe ‘Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu’, angeleewa kwa haraka hiyo hoja ya wazi kabisa ya kisheria na fact.

Ukweli kwamba Mwanasheria Mkuu huyo ameshindwa kutambua hoja hiyo ya wazi kabisa, kwangu ni uhalalisho wa maoni yangu ya kitaaluma kwamba, bwana Adelardus Lubango Kilangi hana sifa za kushika ofisi ambayo hapo nyuma ilikuwa imetukuka, iliheshimiwa na kuangaliwa, kama hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Pia akasema, “It is true that Mr. Adelardus Lubango Kilangi is a Junior Member of the Bar, his Roll Number is 2022, while Mine is 848. Mr. Adelardus Lubango Kilangi has many Advocates ahead of him, some admitted as recently as 2010. I have personally spoken to many Advocates who have told me that Mr. Adelardus Lubango Kilangi, unlike all previous Holders of the Office, has miserably failed in advising the Government in many pertinent issues.”

Kwamba, “ni kweli kuwa bwana Adelardus Lubango Kilangi ni Wakili Mchanga kwenye chama cha Mawakili, Roll Number yake ni 2022, wakati ya kwangu ni 848. Bwana Adelardus Lubango Kilangi ana Mawakili wengi waliomtangulia, wengine wameapishwa hivi karibuni mwaka 2010. Nimeongea binafsi na Mawakili wengi ambao wameniambia kwamba, bwana Adelardus Lubango Kilangi, sio kama Wanasheria wakuu waliopita, yeye ameshindwa vibaya sana kuishauri serikali kwenye mambo mengi ya msingi.”

Kamati inasema Fatuma aliendelea kusisitiza kwamba bwana Adelardus Lubango Kilangi hakuwa na sifa za kuwa Mwanasheria Mkuu. Fatuma aliamini kwamba bwana Adelardus Lubango Kilangi alipaswa kuapishwa kuwa Wakili miaka 15 kabla ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu.

(Msomaji pengine ungetamani kujua sifa na vigezo vya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Lakini siwezi kuandika hapa kila kitu. Unaweza kusoma Katiba Ibara ya 59 au kasome hii kesi yote, utakuta kila kitu. Lakini Kamati inasema iligundua kwamba, Mr. Adelardus Lubango Kilangi alikuwa na sifa zote za kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali).

UAMUZI WA KAMATI (YA MAADILI) YA MAWAKILI:

Kamati ilikuwa na mambo matatu ya kuamua.

{i}: Je, hizo post za Twitter ziliandikwa na Wakili Fatuma Karume?
{ii}: Kama ziliandikwa na yeye, je kuna kosa lolote la utovu wa nidhamu?
{iii}: Ni suluhisho (remedy) gani inaweza kutolewa?

Kamati iliridhika kwamba akaunti ya Twitter yenye hizo post ni ya Bi Fatuma mwenyewe na kwamba yeye ndiye aliyeandika hizo posts. Pia kulikuwepo na ushahidi mwingine wa video you tube.

Hata hivyo Bi Fatuma alikana kumiliki akaunti ya Twitter yenye hizo posts.

Kamati ikasema, ni kweli Bi Fatuma alikuwa anamtetea mteja wake kwenye ile kesi ya Ado Shaibu, lakini alipaswa kuwa muadilifu na kuwa kitaaluma kwa kutokumshambulia Mwanasheria Mkuu.

Hata kama bwana Adelardus Lubango Kilangi hakuwa na sifa za kuwa Mwanasheria Mkuu, lakini maneno aliyoyatumia Fatuma hayakufaa, ni kinyume na taaluma (ya Sheria) pia ni utovu wa nidhamu.

Pia Kamati ikasema kwamba, bwana Adelardus Lubango Kilangi, kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alikuwa ni Wakili namba moja kwenye orodha ya Mawakili, haijalishi kwamba Fatuma alimtangulia kuapishwa.

Kamati ilisema kwamba, Fatuma pia alionesha utovu wa Nidhamu mbele ya Kamati. Wakati anaingia ndani, alikaribishwa na Katibu aliyemuita kwa jina la “Fatma.” Akajibu kwa ukali, usiniite Fatma, niite Fatma Karume.

Wakati wa kusikiliza kesi, alikuwa anaingilia mara kwa mara kwa kusimama na kumpazia sauti Wakili wake na Kamati, na hata alitishia kabisa kumkataa Wakili wake aliyekuwa anajaribu kumtuliza.

Na ingawa wakati kesi inaanza, wahusika wote walionywa kwamba, kesi hii inasikilizwa chemba (kwa siri) hivyo hairuhusiwi kuongea kinachoendelea huko nje, lakini dakika chache baada ya Fatma kutoka nje, akaenda kupost Twitter kwamba:

“Leo nimeitwa kwenye Kamati ya Maadili, Adelardus kasema nimemkejeli. Jaji anaandika RECORDS kwa English. Sasa ninaomba kuelewa hilo neno kalitafsiri vipi, Jibu lake ‘kwani wewe si MTZ? Nimewaacha waendelee tu. Maana Jaji anashindwa kusema KEJELI kalitafsiri vipi?” Hiyo ilikuwa saa 11:55 AM tarehe 22/06/2020.

Ilipofika saa 14:22 PM siku hiyo hiyo akapost tena kwamba: “Sijiapata kuona watu waliokuwa hawaelewi wanachokifanya kama Mahakama ya TZ. Unamsuspend wakili, halafu eti unamshitaki kama wakili kwenye KAMATI ya MAADILI? They are not serious. Mtanisuspend mara ngapi? Siendi tena. Wafanye watakalo.”

Na saa 15:03 siku hiyo hiyo akapost tena, “I know that they want to INTIMIDATE me. They failed to think. Intimidation only works when you have something to lose. They took my practicing licence illegally and they want to INTIMIDATE me? They can keep it for all I care! I left the building a long time ago @judicarytz.”

Kuhusu ipi ni suluhu (adhabu) dhidi ya Wakili Fatma,
Kamati ya Mawakili ilimtia hatiani Bi Fatuma Karume kwa utovu wa nidhamu uliokithiri. KAMATI IKAAMURU WAKILI FATMA KARUME AONDOLEWE JUMLA KWENYE DAFTARI LA ORODHA YA MAWAKILI kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria ya Mawakili.

Kwa hiyo Bi Fatuma Karume akawa amevuliwa Uwakili milele na Kamati ya Mawakili. Hiyo ilikuwa tarehe 23/09/2020 Dar es Salaam.

FATMA AKAKATA RUFAA MAHAKAMA KUU.

3: Tunaingia kesi ya tatu inaitwa “FATMA AMANI KARUME Vs. THE ATTORNEY GENERAL AND THE ADVOCATES COMMITTEE, CIVIL APPEAL NO. 02, OF 2020.” Hii ndiyo aliyokata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya Uamuzi wa Kamati uliomvua Uwakil imilele, akawekewa pingamizi la kisheria kwa sababu alitumia Petition badala ya Memorandum. (Bado aliwakilishwa na Wakili Msomi Peter Kibatala).

Hapa ameshatoka kwenye Kamati ya Mawakili akarudi tena Mahakama Kuu. Iko hivi, baada ya kuvuliwa Uwakili milele na Kamati (Advocates Committee), Fatma alikata rufaa Mahakama Kuu mbele ya Jopo la Majaji watatu (Full Bench). Mawakili wa Serikali wakamuwekea mapingamizi ikiwemo hoja kwamba:

{i}: Rufaa yake haijakamilika au sio sahihi kwa sababu hakutoa taarifa ya kukata rufaa (notice of appeal), kinyume cha kanuni ya 17(1) ya Kanuni za Mawakili za Nidhamu na Mashtaka Mengine - Advocates (Disciplinary and Other Proceedings) Rules, 2018.

{ii} Kwamba Fatma amekosea kukata rufaa kwa kuchanganya nyaraka zinazotakiwa ambapo badala ya kutumia “Petition of appeal” yeye aliandika “Memorandum of Appeal” kinyume cha Kanuni ya 17(2) ya Kanuni nilizotaja hapo juu na,

{iii} Kwamba rufaa ya Fatma ni mbaya kisheria kwa sababu hakufata utaratibu. Ambapo, alifungua rufaa moja kwa moja Mahakama Kuu kinyume cha Kanuni ya 17(5) ambayo inataka rufaa ianzie kwa Katibu (Secretary) wa Kamati ya Mawakili na kisha Katibu ndo aichukue na kuipeleka Mahakama Kuu.

Wakili wa Fatma Karume kwenye hii kesi, Peter Kibatala, akapewa nafasi ya kujibu hizo hoja zote za mapingamizi.

Kiufupi, mapingamizi yote yalishindwa na kutupiliwa mbali. Mahakama Kuu ikaamuru kesi (rufaa ya Fatma) iendelee kusikilizwa kama kawaida. (Ukitaka kujua ubishani uliokuwepo kati ya pande zote mbili na Mahakama ilijibuje kwa kila pingamizi kasome kesi yote - ina kurasa 35 tu). Hiyo ilikuwa ni tarehe 17/12/2020

KUSIKILIZWA KWA RUFAA YA FATMA:

4: Hii ni Kesi ya nne jina ni lile lile kama nilivyotangulia kutaja huko juu kwenye kesi iliyopita namba 3 - wakati wanasikiliza mapingamizi - ni “FATMA AMANI KARUME V. THE ATTORNEY GENERAL AND THE ADVOCATES COMMITTEE, CIVIL APPEAL NO. 02, OF 2020.” Jina ni moja lakini zimetenganishwa kila moja imeandikwa kwa wakati wake.

Hii ndiyo sasa ile rufaa yake aliyokata Mahakama Kuu akasikilizwa on merit baada ya yale mapingamizi kutupiliwa mbali* -.

Rufaa hii ilisikilizwa na jopo la Majaji watatu (full bench). Sheria inasema hivyo, kwamba rufaa kutoka Kamati ya Mawakili, lazima isikilizwe na Jopo la Majaji wasiopungua watatu (3).

Moja ya sababu aliyotumia Bi Fatma Karume kukata rufaa na iliyompa ushindi ni kwamba, Kamati ya Mawakili ilikosea kusikiliza na kuamua suala ambalo lilifunguliwa kwenye Kamati kinyume cha amri au agizo la Mahakama.

Wakili wa Fatma, Peter Kibatala akasema, Mahakama iliagiza kwamba, suala la Bi Fatma Karume lipelekwe kwenye Kamati na Msajili wa Mahakama Kuu, kwa hiyo ilikuwa ni makosa kwa Kamati kupokea malalamiko mapya kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kibatala akaiomba Mahakama Kuu itengue uamuzi wa Kamati, kwa kuwa Kamati haikuwa na mamlaka kisheria wakati inasikiliza suala la Bi Fatma Karume, pia suala la Fatma lilipelekwa kwenye Kamati na mtu ambaye hakua na mamlaka ya kufanya hivyo, ukizingatia kwamba agizo lenyewe la Mahakama bado lilikuwa palepale halijatenguliwa na Mahakama yenyewe.

Upande wa Mwanasheria Mkuu, Wakili wake akasema kweli kuna agizo la Mahakama kuhusiana na malalamiko dhidi ya Fatma Karume. Lakini akasema, hilo agizo halizuii kufungua malalamiko mapya kwenye Kamati.

Kwa sababu, malalamiko ya mwanzo yaliyotolewa agizo na Mahakama, yalihusu utovu wa nidhamu uliotokea wakati wa kusikiliza kesi (ya Ado Shaibu) Mahakamani tu. Lakini malalamiko mapya ya Mwanasheria Mkuu mbele ya Kamati, yaliongezea hadi makosa mengine ya nidhamu aliyofanya Bi. Fatma baadaye.

Hata hivyo, waheshimiwa Majaji walikubaliana na hoja ya Wakili Peter Kibatala. Wakasema, kwanza ni Mwanasheria Mkuu mwenyewe kupitia Mawakili wake aliyeanza kulalamika Mahakama Kuu kuhusu Fatma Karume, na kupelekea Fatma asimamishwe Uwakili hadi itakapoamuliwa vinginevyo na Kamati.

Na mwanzo kabisa, Mahakama iliagiza Msajili ndo alipeleke hilo suala kwenye Kamati ya Mawakili. Hata kama waliongezea makosa mengine aliyofanya Fatma baadaye, bado hakuna namna ambayo Mwanasheria Mkuu angeweza kufungua hayo malalamiko mapya akiunganisha na yale yaliyomo kwenye agizo la Mahakama bila kukiuka agizo la Mahakama.

Majaji wakasema, kama Mwanasheria Mkuu alitaka kufungua malalamiko mapya, alipaswa asubiri hadi yale malalamiko aliyowahi kuyatoa Mahakamani yapelekwe kwenye Kamati ya Mawakili kwa namna ilivyoelekezwa na Mahakama ama sivyo alitakiwa afungue malalamiko mengine mapya ambayo hayagusi kile alicholalamikia mwanzo na kutolewa agizo Mahakamani.

Waheshimiwa Majaji wakasema, hatua aliyoichukua Mwanasheria Mkuu ilikuwa inapelekea kukwamisha agizo na maelekezo ya Mahakama.

Hivyo Mahakama ikasema, malalamiko ya Mwanasheria Mkuu kwenye Kamati ya Mawakili hayakuwa sahihi na yalitakiwa kutupiliwa mbali.

Fatma Karume akashinda rufaa. Maamuzi ya Kamati ya Mawakili kumfuta Uwakili jumla au milele yakatenguliwa na kuwekwa kando. Kisha Mahakama Kuu ikaagiza tena Msajili achukue suala la Karume alipeleke kwenye Kamati ya Mawakili sawasawa na agizo la mwanzo la Mahakama kwenye kesi ya mwanzo ya Ado Shaibu. (Hiyo ilikuwa tarehe 17/06/2021).

(Kwa wanafunzi: Ikiwa reference for disallowance inaenda Mahakama Kuu, hapa tunaona full Bench wanaingia kwenye mtego ule ule (same trap) nao wanaamuru matter iende kwenye Kamati badala ya Mahakama Kuu kama Jaji mwenzao wa kwanza kwenye kesi ya Ado Shaibu. Section 22(2)(b) ya Advocates Committee).

MWANASHERIA MKUU KUKATA RUFAA KWENDA MAHAKAMA YA RUFANI (ambayo ndo Mahakama ya juu na yenye uamuzi wa mwisho Nchini).

5: Kesi ya tano, jina ni “THE ATTORNEY GENERAL & THE ADVOCATES COMMITTEE DHIDI YA (Vs) FATMA AMANI KARUME, MISC. CIVIL APPLICATION NO. 08, OF 2021 (HC).”

Baada ya kushindwa kesi, Mwanasheria Mkuu akaenda kuomba ruhusa (leave) ya Mahakama ili akate rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa. (NB: Kwa wasiosoma sheria, kuna baadhi ya rufaa (mwaka 2021) ilikua lazima uombe ruhusa ya Mahakama).

Wakili wa Fatma Karume, Peter Kibatala na Dr. Nshalla (Rais wa TLS wa wakati huo), wakapinga na kutoa sababu kwa nini ruhusa isitolewe. (Sitazieleza hapa, ila unaweza kusoma kesi yote ukitaka kuziona hizo sababu - kesi ina kurasa 12 tu).

Mahakama Kuu ikakataa kumpa Mwanasheria Mkuu ruhusa ya kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa, ikiwemo kwa sababu kwamba walishindwa kuonesha hoja za msingi zinazokidhi kujadiliwa huko Mahakama ya Rufani (arguable issues). Kesi ikafutwa. (Hiyo ilikuwa 17/12/2021)

6: Kesi ya sita ni “THE ATTORNEY GENERAL & THE ADVOCATES COMMITTEE Vs FATMA AMANI KARUME CIVIL APPLICATION NO. 694/01 OF 2021 (CAT).” Uamuzi wake ulitoka tarehe 08/09/2023.

-Hii ndio Mwanasheria Mkuu (AG) aliomba leave second bite (ruhusa mara ya pili) Mahakama ya Rufani baada ya kunyimwa leave mara ya kwanza na Mahakama Kuu.

(Ukitaka kujua kilichotokea itafute mtandaoni usome ina kurasa 20 tu)

7: Kesi ya Saba ni “FATMA AMANI KARUME Vs THE ATTORNEY GENERAL & THE JAJI KIONGOZI, HIGH COURT OF TANZANIA, CIVIL APPLICATION No. 434/01 OF 2019, (CAT).”

Hii ndiyo Fatma aliupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliomsimamisha Uwakili mbele ya Mahakama ya Rufani akashindwa kesi. Yeye aliupinga kwa kutumia njia (remedy) ya revision, Mahakama ya Rufani ikasema alikosea, kwa mujibu wa sheria alitakiwa arudi Mahakama Kuu pale pale aombe uamuzi huo kutenguliwa (disallowance) chini ya kiufungu namba 22(2)(b) cha Sheria ya Mawakili (Advocates Act).

Hizi kesi mbili za mwisho utasoma vizuri kwa wakati wako mwenyewe. Zina mambo mengi mi nimeeleza kwa ufupi sana. KAMA UNATAMANI KUFAULU LAW SCHOOL UTASOMA TU.

SASA NINI HATIMA YA MISS FATMA KARUME KWENYE HIZI KESI?

Mahakama Kuu ilishatengua maamuzi ya Kamati ya Mawakili (Advocates Committee) yaliyomvua Uwakili milele kwa sababu aliyetakiwa kupeleka hilo suala kwenye Kamati ni Msajili sio Mwanasheria Mkuu. Na Mahakama ikaagiza Msajili wa Mahakama Kuu ampeleke Fatma kwenye Kamati ya Mawakili , lakini mpaka leo naandika Makala hii Msajili hajafanya hivyo na kama amempeleka kimyakimya basi uamuzi haujatoka.

Kwa hiyo Baada ya kutengua maamuzi ya Kamati ya Mawakili (Advocates Committee) uliomvua uwakili milele, FATMA BADO HAJAREJESHEWA UWAKILI, bado ule uamuzi wa kwanza wa Mahakama Kuu (kwenye kesi ya Ado Sahaibu) uliomsimamisha Fatma Uwakili kwa muda (temporary) ndio unaendelea hadi leo, hadi hapo Msajili wa Mahakama atakapompeleka Fatma kwenye Kamati ya Mawakili ambapo anaweza kupewa adhabu yoyote au asipewe adhabu yoyote au hadi Fatma atakapo challenge huo uamuzi Mahakamani na kufanikiwa.

------Mwisho-------

Natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili.

Unaruhusiwa kabisa kushare lakini usibadili au kuhariri yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya.

Tafsiri hii ya Kesi Maarufu ya Miss Fatma Karume, imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke
zakariamaseke@gmail.com
Wakili / Advocate (Cohort 35).
(0746575259 - WhatsApp)
(0754575246 - Normal Texts/Calls)

Kwa wale wa law school, kesi ya Fatma Karume ni kati ya swali linalopendwa sana kuulizwa kwenye mitihani ya law school. Unatakiwa utafute hizo kesi zote uzisome ujue kwenye kila hatua ana nafuu (remedy) gani, sehemu gani ya kupeleka malalamiko yake, grounds (sababu) zake zitakua zipi na nyaraka (documents) muhimu.

Asanteni, Mungu awabariki.
By Advocate Zakaria Maseke
Asante chief
 
Back
Top Bottom