Mwema, Manumba, Othmani, Mganga +1 wawajibishwe!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,398
39,547
Na. M. M. Mwanakijiji

BILA shaka kuna watu ambao baada ya uchunguzi kufanyika, watawajibishwa kutokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa kumi jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.

Sitoshangaa kama watu hao kwa namna moja au nyingine watapewa mzigo wa lawama kutokana na janga hilo lililokuwa gumzo la mji.

Hata hivyo ninaozungumzia kuwajibishwa si hawa, bali ni wale ambao kutokana na vitendo vyao au kutotenda, nusura wasababishe kadhia na adha kubwa kwa taifa.

Wakati habari za ‘ungaunga’ bungeni na tetesi za ushirikina zilipoanza kuibuka nilikuwa nimetulia nikifuatilia mwitikio wa watu kadhaa kuhusu suala zima.

Ni kutokana na mwitikio huo ninajikuta nalazimika kusema kuwa, watu wafuatao ni lazima wawajibishwe au wawajibike wenyewe kufuatia kilele cha uzembe na ubutu wa uwajibikaji katika sakata la ‘ungaunga na video’ bungeni ambako ilidaiwa Andrew Chenge (CCM – Bariadi Magharibi) aliingia ndani ya Ukumbi wa Bunge akiwa na ofisa wa taasisi hiyo na kuonekana akipitia viti vya wabunge wenzake (kikiwemo cha Spika) na kunyunyiza kitu chenye asili ya unga unga.

Watu hao ni hawa wafuatao; Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkuu wa Usalama Bungeni, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dodoma.

Utaona kuwa nimetaja vyeo vyao na si majina yao kwanza ili kuonyesha kitu kimoja kuwa ni watu wenye nyadhifa hizo ndio ambao natolea hoja leo kuwa inapaswa wawajibishwe au kama watagundua uzembe wao na makosa yao wawajibike wao wenyewe.

Lakini nikitaja majina yao kwa mfuatano wa vyeo ni Saidi Mwema, Robert Manumba, Rashid Othmani, Omari Mganga na Mkuu wa Upepelezi Mkoa.

Watendaji hawa watano ambao wamedhaminiwa kwa namna ya pekee na usalama wa nchi yetu kutokana na uzembe, kutowajibika na kwa hakika kutokuwa makini wamelinusurisha taifa katika sakata lililotokea bungeni wiki iliyopita.

Ingawa hakuna madhara yaliyotokea kwa binadamu, lakini ule uwezekano kuwa jambo hilo lingeweza kusababisha madhara kwa wabunge na watu wengine.

Ugoigoi wa kutambua dharura

Baada ya habari kuwa kuna mtu alionekana akiingia katika Ukumbi wa Bunge muda wa usiku na akiwa na kitu kama unga na akitembea kutoka kiti kimoja hadi kingine hadi kile cha Spika ni habari ambazo zingeweza kushtusha jamii yoyote ile yenye kuheshimu na kujali Bunge lao.

Kwa bahati mbaya sana, suala hilo halikupewa uzito mara moja na timu ya watu hawa watano. Inasikitisha kwamba jambo hilo au habari za tukio hilo ziliibuka siku mbili baadaye na hasa baada ya hali ya Dk. Harrison Mwakyembe kutetereka siku ile ya Alhamisi.

Kinachonisumbua mimi hasa ni kuwa vyombo vyetu vya usalama kama raia wengine na wenyewe waliitikia kwa kufuata misingi ya ‘huo ni ushirikina tu’ na si uhalifu wowote au kitendo cha kihalifu. Hili ni kosa kubwa sana kwani siku nyingine kwa kudhania kuwa ni ushirikina tunaweza kugharimu maisha ya watu.

Kamera za usalama kuzimwa?

Mwanzoni mwa habari hizi zilipotoka tuliambiwa kuwa kamera nyingine za usalama zilikuwa ‘zimezimwa’, na yawezekana moja ndiyo ilinasa watu hao. Kama hili ni kweli, basi kuna kila sababu ya Mkuu wa Usalama Bungeni kuwajibishwa.

Bunge ni mahali ambako si tu pana mambo mengi, lakini ni mahali ambako viongozi wa kitaifa hukutana. Kitendo cha kuzima kamera bungeni kwa dakika yoyote ile ni cha hatari kwa usalama wa Bunge.

Unapozima kamera ina maana unaziba macho yako kuona kinachotokea. Hivi kama ingejulikana kuwa hakuna kamera yoyote iliyowanasa watu hao, hivi kuna mtu ambaye angeweza kutajwa kweli na kukiri kuwa aliyeonekana ni yeye? Sasa ingekuwaje kama walioonekana si mbunge bali ni mtu baki tu aliyetumwa na mafisadi kwenda kuweka sumu au kitu chenye madhara, na hakuna kamera iliyokuwa inaangalia? Ingekuwaje kama ile Alhamisi isingekuwa Dk. Mwakyembe aliyejisikia vibaya? Ingekuwaje kama mngesikia majina kama kina Selelii, Zitto, Slaa, Msabaha, Lowassa na wengineo.

Wote wanaanguka kuwa wagonjwa halafu mnaambiwa kuwa kulikuwa na watu waliingia bungeni usiku wa manane wakati kamera zimezimwa! Binafsi kama kuna kitu ambacho wananchi wanastahili kuhakikishiwa ni kuwa kamera za Bunge hazizimwi kamwe, lazima ziwe zinapiga kazi saa 24, kwani gharama ya kupiga picha muda huo ni ndogo sana ukilinganisha na gharama ya kuchagua wabunge wapya!

Siku nane za kupeleka ‘unga’ kwa mkemia mkuu

Kati ya vitu ambavyo binafsi vilinishangaza sana, ni kuwa iliwachukua polisi siku nane kuamua kupeleka unga unga walioupata humo bungeni kwa mkemia mkuu. Siku nane! Kama hii peke yake si ishara ya uzembe sijui nini kingine.

Hivi walikuwa wanakaa na huo unga wakati hawana vyombo vya uchunguzi Dodoma ili kiwe nini? Walikuwa wanaunusa kupima kama una madhara? Walikuwa wanawapa paka wanywe kuona kama watakufa? Ni nini kiliwafanya polisi kuchukua siku nane kupeleka unga huo kwa mkemia mkuu?

Je, kanuni zilizokubaliwa za ufanyaji kazi (standard operating procedures) zinasema nini kuhusu kukutwa kwa kitu chochote cha shaka ndani ya Bunge au eneo lake? Hivi kama wangekuta kinachoonekana kama bomu la mkono ingewachukua muda gani kuwaita JWTZ au kikosi cha kulipua mabomu? Kwa nini huu unga unga waliuangalia kana kwamba ni unga wa maandazi?

Binafsi naamini siku hizi nane zilikuwa ni siku za kilele cha uzembe ambao hakuna serikali yoyote ya utawala wa sheria na demokrasia inayoweza kuvumilia. Hivi kama ule unga ungekuwa ni mojawapo ya sumu kama kimeta au ricin au mojawapo ya sumu na walioingia si maofisa wa Bunge hivi leo tungekuwa na kilio cha namna gani?


Mafisadi wangeamua kupenya?
Kinachonisikitisha zaidi ni ukweli ambao IGP na Rashid Othman wanauelewa vizuri kuwa nchi imetekwa nyara na mafisadi ambao wametushikilia kama kwa bomu hivi.

Wote tunasikia majadiliano yalivyo motomoto bungeni na bila ya shaka kuna watu walishtuka wakati hotuba ya Dk. Slaa siku ya Jumatatu kujibu hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliposhindwa kurushwa moja kwa moja. Je, mafisadi na makuwadi wao hawawezi kufanya kitu kama hicho?

Kama mtu anaweza kuingia bungeni na kamera zikazimwa tunajuaje kama wapambe wa mafisadi wataamua kufanya kweli bungeni kwa kutumia mawakala wao ili kuweka kitu kibaya bungeni?

Ni kwa sababu hiyo basi, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa ana wajibu mkubwa sana wa kuhakikisha kuwa hakuna uharibifu wowote wa makusudi wa mwelekeo wa taifa letu.

Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1996 (pamoja na mapungufu yake) inaipa Idara ya Usalama wa Taifa jukumu la kuhakikisha inakusanya habari zozote za kijasusi na kuzichambua ili zifanyiwe kazi.

Kama tukio lililotokea bungeni lingekuwa ni lenye madhara makubwa tungewauliza Usalama wa Taifa kama walikuwa na taarifa zozote kuhusu jambo hilo na pale walipopata taarifa walichukua hatua gani? Kinachonihangaisha mimi zaidi ni kuwa, viongozi wetu wa usalama bado wanasubiri amri kutoka juu ili wafanye kazi zao. Aidha, ni kwa sababu ya mapungufu ya sheria au kutokujua nguvu zao za kisheria.

Hivi kama Spika Sitta asingepeleka suala hilo polisi na vyombo vya usalama je, vingeweza kufuatilia vyenyewe? Kama Dk. Mwakyembe asingeugua Alhamisi ile tungejua kitu kama hiki kimetokea bungeni? Tatizo langu hadi nimetengeneza hoja hii ni kuwa, bado Bunge letu halijapewa ulinzi na hadhi inayostahili kama mhimili mwingine wa Bunge. Hebu fikiria kwa sekunde chache kwamba tunasikia mke wa rais ameanguka Ikulu kwa maradhi ambayo hayajulikani wakati tunashangaa habari zinapenyezwa kwenye mtandao wa jamiiforums.com kuwa siku mbili kabla yake mke wa pili wa rais akiwa na mfanyakazi wa makazi ya rais walionekana wakipita toka chumba kimoja hadi kingine na waliweza hadi kufika kwenye chumba cha rais.

Katika shughuli yote hiyo, huyo mwanamama alionekana ananyunyiza au kupaka kitu fulani kila alikoshika. Tukiwa tunashangaa hilo limewezekana vipi, tunaambiwa kuwa kamera za usalama za Ikulu zilikuwa zimezimwa na moja tu “kwa bahati” ndiyo inaonyesha sura ya mama huyo.

Tukiwa tunashangaa tunaambiwa kuwa mke huyo alikuwa anatafuta shuka! Kwa mtu mwenye mawazo ya zamani atakimbilia kusema ‘alikuwa anawanga’ au alikuwa anampiga juju mke mkubwa! Kwa mtu mwenye kufikiria mambo ya usalama, atasema kuwa kilichotokea ni uvunjaji mkubwa (breach) wa mipango ya usalama Ikulu. Na katika mazingira hayo baadhi ya watu wangepaswa kuwajibika.

Ingawa mfano huo unaweza usiwe mzuri sana, lakini ukweli ni kuwa Bunge letu lina watu wenye maslahi mbalimbali na hasa katika kipindi hiki cha mapambano ya kifikra, hakuna jambo la kudharaulika au kupuuzwa.

Ni kwa sababu hiyo basi, narudia kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wote wawili wawajibishwe mara moja kwa kushindwa kusimamia usalama wa taasisi nyeti ya Bunge hasa katika kipindi hiki cha bajeti. Na zaidi ya yote uchelewashaji wao wa kupeleka unga unga walioukuta kwa mkemia mkuu ndani ya saa ishirini na nne ili kujue kama Bunge ni salama.

Mkuu wa Usalama bungeni naye awajibike kwa kuzima kamera za ukumbi huo au kwa kuacha watu wengine wazime kamera hizo na hivyo kutoa mwanya kwa maadui wa demokrasia yetu kuweza kufanya kitu kibaya bungeni.

Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma na Mkuu wake wa Upelelezi nao lazima wawajibike au wawajibishwe kwa kupuzia yaliyotokea bungeni badala ya kuhakikisha kuwa taratibu za kufuatilia majanga zinafuatwa.

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa ambaye tayari taasisi yake imekuwa goigoi kushughulikia taarifa za kijasusi kuhusu mafisadi kiasi cha taasisi yenyewe kuhusishwa na ufisadi ameshindwa kuonyesha kuwa taasisi yake inasimamia usalama wa taifa bungeni.

Ni kwanini taarifa za tukio hili tumezisikia kwa Spika na tena baada ya kuwaomba wanausalama hao? Hivi kwenye kuangalia kamera za Bunge (kama ilivyo Ikulu) hakuna watu wa Usalama wa Taifa?

Kama walikuwepo ni kwanini walikaa na kukodoa macho wakati mtu anapita kutoka kiti kimoja kwenda kingine kwa kisingizio cha kutafuta kiti? Hivi wanataka kutuambia kuwa huyo mhusika angekitaka kiti cha Zitto au Mwakyembe angepewa?

Hivi karibuni Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates aliwafukuza kazi Mkuu wa Jeshi la Anga la nchi hiyo na Katibu wa Jeshi hilo la Anga ambao ndio viongozi wakubwa kabisa katika tawi hilo la Jeshi la Marekani.

Kosa lao ni uzembe ulioonyeshwa na watu walio chini yao kiasi cha kuruhusu marubani wa ndege za kivita pasipo wao wenyewe kujua kuruka katika anga la Marekani wakiwa na silaha za nyuklia. Kitendo cha ndege kurushwa na silaha za nyuklia kilikuwa ni kilele cha uzembe na kilisababisha (pamoja na hao viongozi wawili) kuondoka kwa makanali watatu.

Katika maelezo yake ya kuwatimua maafisa wao Waziri Gates alisema kuwa ‘maofisa hawa walishindwa si tu kwa vitendo vyao wenyewe, bali pia kwa kushindwa kutambua matatizo ya mfumo, kuyashughulikia na pale ilipokuwa juu ya madaraka yao basi kuwajulisha wakubwa wao juu ya matatizo hayo.

Wote waliofukuzwa hawakulia ‘bangusilo’ au kulia kuwa ‘ni njama za wabaya’ wao. Walikubali kujiuzulu kwa sababu wao wanawajibika kwa kushindwa kusimamia silaha hizo za nyuklia.

Wakati umefika kwa viongozi wetu wa kiraia kuanza kutumia madaraka yao kuwawajibisha viongozi wazembe hasa linapokuja suala la usalama wa taifa. Tusipoanza sasa kuna siku taifa letu litaamka si na msiba mmoja bali mingi, na hapo ndipo tutakapoona viongozi wakinyosheana vidole.

Kilichotokea bungeni si jambo dogo na si la kupuuzia kama wengine wanavyochukulia. Kilichotokea ni jambo kubwa ambalo kuna watu lazima wawajibishwe au wao wenyewe kama wana chembe ya uongozi ndani yao kukubali kuwajibika na kuachia ngazi mara moja.

Hiyo ndiyo hoja yangu na ninaisimamia.
 
Sasa ni nani atawawajibisha?

Rashid ameteuliwa na raisi, halikadhalika Said Mwema.

Huyo wa Bungeni atakuwa ameteuliwa na Spika.

Na hao juniors ndio labda kati ya Rashid Othman na Said Mwema ndio wamewateua.

Kwa mtazamo wangu hili ni latizo kwani limekuatanisha wigo mpana wa kiutendaji na nani anawajibika kwa yupi.

Kama majambo yote yaliyotokea yangefuatiliwa kwa undani ni dhahiri watu wangewajibishwa, lakini na nani.? Maana mpaka sasa nahisi kuna kugongana mabega katika "corridors of power".

Pia kama bado Tanzania hatuna "joint intelligence na security committees" ambazo kwa vyovyote vinawakutanisha hao waliotajwa hapo juu, basi hatuwezi kudhibiti dharura yoyote ile isipokuwa kwa executives na VIPs.

Ni kaazi kwelikweli!
 
Yaani haya makelele yangekuwa yanapata msikilizaji naona tungekuwepo mbali lakini wana itikadi ya watasema mchana usiku watalala na yao yanawaendea ,maana hakuna wa kukusikiliza na kufuatilia undani kila mmoja analinda mlo wake ,sasa nani ataanza kutekeleza yote hayo ,nionavyo utekelezaji wanachukua ikiwa unahatarisha interest zao zipo target ukizilenga basi zinaweza kuangushwa mara moja.Sasa unataka sheria zichukuliwe kwa wanaotumiwa kupoteza ushahidi ,hivi jambo hilo linawezekana ? Wacha muungwana apite huenda tukapata mwengine aliepiga hatua mbele kwani kila Raisi anakuja na aina zake za utawala.
 
Nafikiri watasoma ujumbe na wataelewa, na nafikiri hata wabunge watasoma pia. Ni jambo la hatari sana kama hata aliyeingiza unga hatashugulikiwa ili kulinda heshima ya bunge.

tatizo sasa hivi naona anataka kujifanya kuwa hakuingia, hila waliona mtu mweupe kama yeye.
 
tuendelee kupiga kelele, siku moja watasikia. Kuna wakati watoto wanapiga kelele unawapuuzia lakini zikizidi inabidi utoke nje aidha uwakataze wasipige kelele, au utaangalia wanachopigia kelele ni nini ukiondoe.. in whatever case utakuwa umerespond kwa kelele zao.
 
Kelele muhimu ziendelee.. na katika mkondo husika, yule 'starring' katika kumwaga unga-unga awajibishwe kisawasawa pia!
 
tuendelee kupiga kelele, siku moja watasikia. Kuna wakati watoto wanapiga kelele unawapuuzia lakini zikizidi inabidi utoke nje aidha uwakataze wasipige kelele, au utaangalia wanachopigia kelele ni nini ukiondoe.. in whatever case utakuwa umerespond kwa kelele zao.

Mkuu Wangu Heshima mbele, sometimes none respond ni better kuliko wanapojibu, si unajua Kobe akiinama akwa kimyaa huwa anakuwa anatunga sheria!
 
Kwani mnadhani hawazisikii wanazisikia sana wanajifanya hawasikii ila sisi tunajua wanasikia ingawa wapo kimya. Inakuwa kama vile maandishi yameendikwa somewhere huwezi kuyasoma kwa sauti ingawa kimoyomoyo unayasoma.
 
Hata kama hatutafaidi matunda lakini wajukuu wetu watayala kama sio watoto na pia kusema ni kutimiza wajibu mbele za Mola.

Asante M.M.J
 
MWKJJ mkuu wa kaya alishasema kelele za mlango hazimzuii mwenye kula kuendelea kula upo hapo?
 
mkuu JK anaweza kusikia kelele zetu na kuunda tume, ambayo itatakiwa kutoa kuchunguza kelele zetu na kutoa taarifa kamili baada ya miezi sita.
tume ikishakutoa jibu, itaundwa tume nyengine kujadili ni kwa vipi mapendekezo yaliyotolewa na tume ya kwanza yanaweza kufanyiwa kazi. nayo itapewa muda wa miezi sita mengine.
 
mkuu JK anaweza kusikia kelele zetu na kuunda tume, ambayo itatakiwa kutoa kuchunguza kelele zetu na kutoa taarifa kamili baada ya miezi sita.
tume ikishakutoa jibu, itaundwa tume nyengine kujadili ni kwa vipi mapendekezo yaliyotolewa na tume ya kwanza yanaweza kufanyiwa kazi. nayo itapewa muda wa miezi sita mengine.

akiendelea hivyo anaweza kujikuta anamteua mmoja wetu kumuambia hataki kuwemo kwenye tume.
 
Huwa wanarespond kwa mfano spika alivyorespond kuwa yeye sio fisadi, Milton Mahanga alivyorespond kuhusu ATC na dege lao bovu la Air bus 320, Mtoto wa muungwana, IGP alivyodai JF ni chombo cha kigaidi. Tena hapa mimi nadhani kabla ya kuanza hizo kazi zao lazima waangalie ni kipi kinachojiri especially JF. Sema tu muda wao haujafika Bob Marley anasema "TIME WILL TELL".
 
Its youmwanakijiji with a bomb shell!wape wape vidonge vyao hao walinzi wa mafisadi!
 
Na. M. M. Mwanakijiji

Hebu fikiria kwa sekunde chache kwamba tunasikia mke wa rais ameanguka Ikulu kwa maradhi ambayo hayajulikani wakati tunashangaa habari zinapenyezwa kwenye mtandao wa jamiiforums.com kuwa siku mbili kabla yake mke wa pili wa rais akiwa na mfanyakazi wa makazi ya rais walionekana wakipita toka chumba kimoja hadi kingine na waliweza hadi kufika kwenye chumba cha rais.

Katika shughuli yote hiyo, huyo mwanamama alionekana ananyunyiza au kupaka kitu fulani kila alikoshika. Tukiwa tunashangaa hilo limewezekana vipi, tunaambiwa kuwa kamera za usalama za Ikulu zilikuwa zimezimwa na moja tu “kwa bahati” ndiyo inaonyesha sura ya mama huyo.

Tukiwa tunashangaa tunaambiwa kuwa mke huyo alikuwa anatafuta shuka! Kwa mtu mwenye mawazo ya zamani atakimbilia kusema ‘alikuwa anawanga’ au alikuwa anampiga juju mke mkubwa!.

Mkjj,
Acha uchokozi.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom