MWANZA: Polisi kwa kushirikiana na JWTZ wapambana na Majambazi usiku kucha

Kimong'onyole

Member
Dec 2, 2011
15
34


Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliokuwa wamejificha kwenye maandaki Milima ya Maina, Mwanza wakiwa na silaha nzito za kivita walirushiana risasi na vikosi vya ulinzi na usalama usiku kucha na hatimae wanne wameuwawa.
FFU.jpg


=====================

Habari zaidi zinasema...


Katika tukio hilo, watuhumiwa watatu waliuawa huku polisi mmoja akijeruhiwa vibaya kwenye unyayo kufuatia mapambano yaliyodumu kwa saa 16, kuanzia saa 10:30 jioni juzi hadi jana kulipopambazuka.

Tukio hilo limetokea jirani na Msikiti wa Rahman ambako Mei 19, mwaka huu, kulitokea mauaji ya kutisha baada ya watu wasiofahamika kuvamia na kuwaua kwa kuwachinja Imamu aliyekuwa akiswalisha swala ya Isha, Ferouz Elias (27) na waumini wawili, Mbwana Rajab (40) na Khamis Mponda (28).

Aidha, tukio hilo limetokea siku chache tangu taifa lipatwe na mshtuko mwingine mkubwa kufuatia kuuawa kikatili kwa watu wanane mkoani Tanga Mei 31, mwaka huu, ambao walivamiwa nyumbani usiku na kuchinjwa na watu wanaodhaniwa kujificha kwenye maeneo ya mapango ya Amboni mkoani Tanga.

Hata hivyo, licha ya kuwapo kwa hisia kuwa watu hao waliouawa katika mapambano na Polisi mkoani Mwanza juzi ni magaidi, taarifa rasmi za polisi zinasisitiza kuwa watu hao ni majambazi waliokuwa wakisakwa kwa muda mrefu.

KAMANDA WA POLISI ASIMULIA
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema mapambano dhidi ya watu hao yalianza juzi saa 10:30 jioni baada ya polisi kupata taarifa za kuwapo kwao (wahalifu) katika maeneo hayo.

“Tulituma kikosi kamili na polisi wetu walianza kushambuliwa baada ya kufika eneo hilo…mmoja kati ya polisi, alijeruhiwa kwenye unyayo kwa risasi. Hali hiyo ilituonyesha kuwa mahali hapo ni sehemu hatari zaidi,” alisema Msangi.

Alisema mapambano hayo makali yalianza baada ya polisi na vyombo vya ulinzi na usalama kumkamata Omary Kitaleti maarufu Kiberiti (28), muuza nyama buchani, mkazi wa Nyegezi Kijiweni, anayetuhumiwa kuhusika na matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwenye maduka ya miamala ya kuweka na kutoa fedha jijini Mwanza.

Alisema baada ya kuhojiwa, Kiberiti aliwataja wenzake kadhaa ambao alidai walijificha mapango ya Utemini na hivyo kupata nafasi kwa polisi kwenda kwenye milima yenye mapango hayo saa 10:30 jioni.

Hata hivyo, alisema baada ya kufika, walipokewa kwa kushambuliwa ghafla kwa risasi na watu hao.

“Risasi za majambazi hao zilimpata jambazi mwenzao Kiberiti (aliyekuwa ameongozana na polisi) na kufa papo hapo huku nyingine ikimjeruhi polisi wetu kwenye unyayo na sasa amelazwa Hospitali ya Rufaa Bugando kwa matibabu zaidi,” alisema Kamanda Msangi.

Kutokana na kuuawa kwa mtuhumiwa huyo na polisi kujeruhiwa, askari walijibu mashambulizi mara moja na kufanikiwa kumuua mtuhumiwa mmoja ambaye hakufahamika jina lake anayekadiriwa kuwa ni umri wa miaka kati ya 20 na 25.

Kamanda Msangi alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na bastola aina ya Chinese, yenye namba M.20-06436, wakati huo ikiwa imebakiwa na risasi tatu.

Alisema kutokana na giza kuingia, polisi walijipanga upya na kuzingira zaidi eneo lote la mlima huo kuhakikisha kuwa panapopambazuka mapambano yanaendelea ili kuwadhibiti wathumiwa hao.

Hata hivyo, Kamanda Msangi alisema kinyume cha walivyotarajia, walijikuta usiku kucha wakiendelea kurushiana risasi na watu hao huku (wao polisi), wakisaidiwa na mwanga wa taa za magari waliyofika nayo mahala hapo.

“Kulipopambazuka, majambazi hayo yaliamua kutumia bomu la kurusha kwa mkono ili kuwasambaratisha polisi huku wengine wakirusha risasi kwa wingi kwa nia ya kuwachanganya polisi… na kweli, kwa kufanya hivyo, walifanikiwa kuondoka maeneo hayo wakiwa watatu wakitumia bodaboda (pikipiki) kuelekea maeneo ya Nyasaka,” alisema Kamanda Msangi.

Aidha, alisema wakati watuhumiwa hao wakitoroka, baadhi ya wananchi waliwaona na kuwapa taarifa polisi ambao waliwafuatilia na kumkuta mmoja wao, Said Mbuli maarufu kwa jina la Fundi Bomba, mkazi wa Bugarika, ambaye pia alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu.

“Alipowaona polisi (Said), ghafla alitoa bunduki aina ya SMG namba 307039 akitaka kuwafyatulia risasi… lakini askari walimuwahi na kummiminia risasi mwilini na kumsababishia kifo pale pale,” alisema Kamanda Msangi.

Akisimulia zaidi, Kamanda Msangi alisema baada ya kuuawa kwa mtuhumiwa huyo, polisi walimkagua na kumkuta akiwa na risasi nane pamoja na kisu kiunoni mwake.

Aidha, alisema baada ya upekuzi zaidi kwenye mapango walikuta risasi nne, kisu chenye damu, kofia ya kuficha uso, jiko, sufuria, unga wa sembe, sukari, dagaa, ugali, ngoma na simu tatu.

Kamanda Msangi alitoa wito kwa wananchi kutulia na kuendelea na shughuli zao, lakini akiwaisihi kutoa ushirikiano kwa polisi ili kuhakikisha uhalifu unatokomezwa mkoani Mwanza.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama mkoani humu.

Mongella alisema matukio ya ujambazi yamekuwa yakiharibu na kuchafua sifa ya mkoa huo kutokana na kuwapo na vikundi vya watu kama hao waliouawa.

“Bado uperesheni hii inaendelea. Kuna watu wanaofahamika na polisi wanaendelea kuwasaka. Tutahakikisha tunavimaliza vikundi hivi na kuuweka mkoa wetu katika hali ya usalama,” alisema Mongella.

Akiwa eneo ambalo mapambano hayo yalifanyika, Mongella aliwataka wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kuwataja wahalifu wa maeneo yao na kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi.

Mongella ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani mwake, aliahidi kutoa Sh. milioni mbili kwa askari waliofanikisha ushindi katika mapambano dhidi ya watuhumiwa hao.

MWENYEKITI WA MTAA
Jukaeli Kiula, Mwenyekiti wa mtaa wa Utemini, alisema wananchi wake waliingiwa hofu kwa kuwa tukio hilo ni la pili kwa kipindi cha mwezi mmoja kutokea ndani ya mtaa wake baada ya la kuchinjwa wananchi wake watatu msikitini.

Alisema juzi, akiwa kwenye mkutano wa Injili viwanja vya Furahisha, alipigiwa simu na mmoja wa wananchi wake kuhusu kuwapo kwa mapambano makali yanayoendelea kati ya polisi na majambazi.

“Niliondoka na nilipofika eneo la tukio, nilikuta hali si nzuri,” alisema.

Aidha, Kiula aliomba polisi kushirikiana na jeshi la wananchi kwenye matukio makubwa kama hayo ili kukabiliana na watu wenye silaha nzito kama hao waliouawa.

KISA KUHUSISHWA UGAIDI
Wakati taarifa rasmi za polisi zikisisitiza kuwa tukio hilo ni la ujambazi, baadhi ya wananchi katika eneo la Utemini wameendelea kuwahusisha watu hao na ugaidi kutokana na sababu kadhaa ikiwamo muda mrefu walioutumia katika mapambano.

Akizungumza na Nipashe, mmoja wa wakazi wa eneo hilo alisema kuna mambo kadhaa yanayowapa imani kuwa waliodhibitiwa na polisi huenda ni magaidi na kubwa zaidi ni hilo la muda walioutumia kwa mapambano, silaha walizokutwa nazo na pia silaha walizofika nazo polisi katika eneo la tukio ambalo halipo mbali na eneo la msikiti palikotokea mauaji ya kinyama kwa imamu na waumini wawili hivi karibuni.

“Tunawapongeza polisi kwa kazi nzuri…lakini hisia kwamba hawa jamaa ni magaidi haziwezi kuondoka kirahisi.

Ni majambazi gani wanaoweza kupambana na polisi usiku kucha? Ni majambazi gani wanafuatwa na polisi wenye silaha kali zaidi kama ile ya kutungulia ndege? Kwakweli kuna maswali mengi yanayoibua hisia kwamba wale jamaa ni magaidi na siyo majambazi wa kawaida,” alisema mmoja wa wananchi hao aliyekataa kutaja jina lake.

SIMULIZI ZAIDI KUHUSISHA UGAIDI
Wakati taarifa za Polisi zikieleza kuwa ‘majambazi’ walinaswa kutokana na taarifa za raia wema, chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa waliouawa walikuwa na kila dalili za kujihusisha na ugaidi na kwamba, polisi walikuwa wakifuatilia nyendo zao kwa muda mrefu.

Inaelezwa zaidi katika simulizi hizo nyingine kuwa katika siku ya tukio juzi, mtu mmoja mwenye asili ya kiasia alikamatwa pamoja na mwingine, wote wakihusishwa na tuhuma za ugaidi.

Inaelezwa zaidi kuwa katika watu hao wawili, wa kwanza asiyekuwa na asili ya Kiasia ndiye aliyekamatwa wakati akienda kuchukua fedha kwa mtu huyo mwenye asili ya Kiasia ambaye ni mfanyabiashara.

“Akiwa njiani, mtu huyo akadakwa na wazee wa kazi waliokuwa wakimfuatilia nyendo zake.

Baada ya kubanwa kwa maswali, ndipo mtu huyo alipowaelekeza (polisi) kwa mfanyabiashara wa Kiasia anayeaminika kuwa ni miongoni mwa watu wanaodhaniwa kuwamo katikia mtandao wa kigaidi.” chanzo kilidai.

“Naye alipobanwa zaidi, ndipo alipowataja watu waliokuwa kwenye milima ya mawe maeneo ya Buhongwa… yeye (mfanyabiashara wa asili ya Kiasia), ndiye aliyekuwa akiwafadhili watu hao kwa chakula na mahitaji yao yote muhimu,” chanzo kilidai.

Inaelezwa zaidi kuwa baada ya kukaribia eneo la milima walikokuwa watu hao, (jamaa hao) wakashtuka na kuanza kurusha risasi kwa nia ya kujiepusha kukamatwa. Ni hapo ndipo mapambano makali yaliyodumu kwa saa nyingi yalipoanza.

Chanzo kimedai zaidi kuwa miongoni mwa watu waliouawa, yupo aliyekutwa akiwa na ‘dozi’ ya kemikali na zana nyingine za kutengeneza mabomu.

Aidha, inaelezwa kuwa katika eneo la tukio, zilikutwa silaha kadhaa nzito zikiwamo za AK47, SMG na bastola. Pia zilikutwa kemikali kadhaa za kutengenezea mabomu na daftari lenye kanuni za namna ya kutengeneza mabomu hatua kwa hatua.

Chanzo kilidai zaidi kuwa tangu mwaka jana polisi walikuwa wakiwafuatilia watu hao na kutaka kufanya operesheni kali ya kuwakamata, lakini mpango huo ulisitishwa wakati wa kukaribia uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 ili kuepuka uwezekano wa kuwajengea hofu wananchi katika kipindi hicho.

“Tukio la utata wa kuchinjwa watu watatu msikiti ulio jirani na eneo la tukio pia limechangia kufanyika kwa operesheni hii,” chanzo kilieleza katika simulizi hizo ambazo hata hivyo, zinatofautiana na taarifa rasmi ya polisi.


Chanzo: Magazetini
 
Watu wanaosadikiwa kuwa ni Alshaabab waliokuwa wamejificha kwenye maandaki Milima ya Maina, Mwanza wakiwa na silaha nzito za kivita walirushiana risasi na vikosi vya ulinzi na usalama usiku kucha na hatimae wanne wameuwawa.
Ishu ni network yao tu
 
Duuh!! Kama wiki imepita nilisikia wanajeshi walipanda Milima ya MAHINA na Mkuyuni wakisaka kitu vichakani na kwenye Nyasi.

Jana usiku milima ya Mkuyuni (Kang'anga) imechomwa moto!! Ngoja wakomeshwe hao IS.
 
Lazima waisome namba, hapa siyo Kenya. Tunawaingilia hukohuko vichakani na Mapangoni, Tumawafurusha woteeee fumbafu sana magaidi hawa.

Unachinja Binadamu kama Kitimoto?????

BACK TANGANYIKA
 
Tunaimbiwa kila siku ya kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani lakini kuna sehemu huwezi kutembea baada jua kuzama na kwa matukio yanayoendelea ni wazi kazi kubwa tunayo....

Vyombo vya usalama haswaa maaskari wajiweke tayari kimbinu na kimazoezi ,rejea tukio la kuvamiwa bank mbagala maana aliyeokoa jahazi ni mwanajeshi...

WE ARE NOT SAFE JAMANI NA WANAUSALAMA WENYE MIILI KAMA BONGO MOVIES CELEBRITIES
 
MAPAMBANO MWANZA: Mmoja auawa, mwingine ajificha baada ya kutokea majibizano ya risasi baina ya polisi na watu wenye silaha Mkolani, Mwanza usiku huu, RPC Msangi athibitisha.
 
Back
Top Bottom