Mwanza: Mwandishi wa Habari, Albert Sengo Kizimbani akishtakiwa kutoa maudhui mtandaoni bila ya kuwa na leseni

Influenza

JF-Expert Member
Jul 1, 2018
1,444
3,354
Mwandishi wa habari, Ndg. Albert Sengo leo Aprili 23, 2020 amefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza na kushtakiwa kwa kosa la kutoa maudhui mtandaoni bila ya kuwa na leseni kinyume na Kanuni ya 14(1, 2) na 18: Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni) za Mwaka 2018.

Mwandishi Sengo ameshtakiwa kutokana na tuhuma kwamba, Machi 24, 2020 ndani ya jiji la Mwanza alitoa maudhui mtandaoni kupitia Televisheni ya mtandaoni iitwayo GSENGO bila ya kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Wakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Hans Edwin alikuwepo mahakamani kumtetea mwandishi Albert Sengo. Wakili Hans pamoja na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Mwanza, Ndg. Edwin Soko wamefanikisha suala la wadhamini wa mwandishi huyo na ameachiwa huru kwa dhamana.

Machi 31, 2020 mwandishi Albert Sengo alipigiwa simu na askari polisi akimtaka kufika kwenye Kituo cha Polisi Kati Mwanza mjini. Aprili 1, aliripoti kituoni hapo, baada ya kufika aliwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa juu ya kutoa maudhui kupitia Televisheni ya mtandaoni iitwayo GSENGO bila ya kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Mwandishi huyo alihojiwa bila ya kuwa na wakili wake na alishikiliwa kwa muda mrefu, baadae aliachiwa kwa dhamana ya polisi. Masharti ya dhamana ilikuwa ni yeye kuripoti kituoni hapo mara kwa mara na amekuwa akifanya hivyo.

Mwandishi Albert Sengo amefunguliwa kesi hiyo katika mazingira ambayo waandishi wengi wamekamatwa, wamehojiwa na wengine kufunguliwa kesi za namna hiyo.

Mnamo Aprili 5, 2020, waandishi wa habari wawili na mmiliki mmoja wa YouTube akaunti walikamatwa na askari polisi mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumiliki blog na YouTube akaunti bila ya kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Lakini pia, Machi 4, 2020 waandishi watatu na mmiliki mmoja wa YouTube akaunti mkoani Njombe walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe kwa tuhuma za kutoa maudhui mtandaoni (blog na YouTube) bila ya kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kinyume na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta [Sura ya 306 Toleo la Mwaka 2017] na Kanuni ya 14(1) na 18: Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui Mtandaoni) za Mwaka 2018.

Tangu Januari mwaka huu 2020, jumla ya waandishi na Watetezi wa Haki za Binadamu kumi na tatu (13) wamekamatwa na kushtakiwa kwa kutoa maudhui mtandaoni bila ya kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Kati ya hao, watetezi wa haki za binadamu wawili tayari walishahukumiwa na kutoa faini.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unaamini kwamba mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya mtandaoni ni huru kwa mtu yeyote kutumia. Wamiliki wa mitandao na majukwaa hayo hawajawahi kudai malipo kutoka kwa watumiaji.

Tunawahimiza Watetezi wote wa Haki za Binadamu nchini kuendelea kupinga Kanuni hizi sababu zipo kinyume na uhuru wa kujieleza uliopo kikatiba na na kwa mujibu wa Mikataba ya Kimataifa.

Imetolewa na
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
Aprili 23, 2020
Mwanza, Tanzania
 
Mahakama ina uwezo wa kutafsiri Katiba, jengeni hoja za msingi za kuiridhisha mahakama badala ya kutafuta huruma mtandaoni.
 
hii tanzania banaa serikal imeona kama ndio sehemu ya kujipatia kipato,si bora hiyo pesa youtube ndio waseme kuwa walipwe wao.huu ni unyanyasaji wa wadhi kabisa,na hii ni sehemu ya kuwanyima uhuru watu. hii sio sawa kabisa.
 
...Mwandishi Albert Sengo amefunguliwa kesi hiyo katika mazingira ambayo waandishi wengi wamekamatwa, wamehojiwa na wengine kufunguliwa kesi za namna hiyo....
Unaposema "waandishi wengi" ni vyema ukataja na idadi, vinginevyo ni umbea tu.
 
Sasa kama hana leseni alitoa hayo maudhui kwa mamlaka au misingi gani?

Sheria za nchi ni lazima zifuatwe(hata kama ni mbaya). Kama sheria zenyewe ni mbovu unazitii kwanza halafu unafuata utaratibu wa kisheria kuzitengua.

Alichofanya huyu mwandishi ni ukanjanja. Au huenda alitaka kupima kina cha maji kwa kidole ama alifanya kwa makusudi ili akamatwe akuze jina.
 
Back
Top Bottom