Mwanshina: Taarifa ya ofisi ya mbunge Jimbo la Nzega kuhusu mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo

HKigwangalla

JF-Expert Member
Feb 6, 2008
717
971
Taarifa kwa Umma Kuhusiana na Upotoshaji Uliofanywa na Taasisi ya Tanzania Chamber of Minerals and Energy (TCME)


Machi 28, 2014.

Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega imesikitishwa na kufadhaishwa na taarifa ya uongo na isiyo na uzalendo hata chembe, iliyotolewa na taasisi ya TCME siku ya tarehe 26, Machi, 2014. Hii imedhihirisha kuwa, hawajui wanalolifanya ama wanatumiwa vibaya na watu wenye maslahi ovu kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Nzega na wa Tanzania kwa Ujumla. Taarifa za namna hii hazina maksudi mengine zaidi ya kusababisha chuki na mfarakano usio na sababu za msingi baina ya makundi ambayo yangepaswa kufanya kazi pamoja kutafuta suluhu ya mgogoro huu.

Mbunge wa Nzega amekuwa ni mtu anayependa kutoa fursa ya mazungumzo na wabia wote wa maendeleo jimboni kwake na yuko tayari kusikilizana na yeyote yule, inashangaza ni kwa nini wadaua hawatumii vizuri fursa hizi kwa faida ya wote. Mbunge wa Nzega ni muwekezaji yeye mwenyewe binafsi na anatambua umuhimu wa wawekezaji kwa ukuaji uchumi na maendeleo ya jamii ya watu wake, na ndiyo maana amekuwa siku zote mstari wa mbele kuvutia wawekezaji mbalimbali katika jimbo lake. Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) si mchukia wawekezaji hata kidogo. Yeye ni mtetezi wa haki za kila mtu, hata za askari polisi na magereza.

Tamko la Shrikisho la Wachimbaji na Watafutaji Madini na Nishati Tanzania (TCME) lingepaswa kuwa la ukweli na lenye weledi wa kutosha, lakini inasikitisha limekuwa ni tamko lisilo na uadilifu na hata chembe ya ukweli. Hata kama taasisi hii inawawakilisha na kuwatetea mabepari, isitetee uongo na dhulma ya wazi. Inapaswa ifahamu kuwa, Ubepari utakaoweza kufanya kazi Tanzania ni ubepari wenye sura ya kijamaa, unaothamini utu, udugu na umoja wetu.

Kwanza, Kwamba, Mbunge aliongozamaandamanoharamukuelekeaeneolaMwanshina, si kweli. Ukweli ni kwamba, Mbunge wa Nzega na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, Dr. Hamisi Kigwangalla, hakuongoza maandamano yoyote yale siku ile bali alifanya mkutano halali, na alikuwa na ratiba ya mikutano miwili jimboni mwake katika Kata zake mbili, Kata ya Nzega Ndogo (Kijiji cha Zogolo) na Kata ya Lusu(Kitongoji cha Mwashina), ambayo ni maeneo yanayohusisha mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Mwanshina.

Mikutano hii ilitolewa taarifa polisi na mamlaka nyingine mbali mbali wilayani Nzega, kwa mujibu wa Sheria, na Ofisi ya Mbunge iliomba na kupewa ulinzi halali wa polisi. Baada ya kumaliza Mkutano mmoja, wananchi pamoja na Mbunge wao waliazimia waelekee kwenye Mkutano wa pili, yaani eneo la Mwanshina, na walitembea kwa miguu wakiongozwa na polisi, na hakukuwa na vurugu, matusi na wala dalili yoyote ile ya uvunjifu wa amani ama uharibifu wa mali za watu.

Kama kwenu watu wa Shrikisho kutembea kwa miguu ni Maandamano basi hamuelewi mfanyalo, maana hata waendao mazishini, harusini, watokao uwanjani kuangalia mpira, ama watokao misikitini ama makanisani, ama kwenye mikutano ya mahubiri, ama jaji/hakimu anavyotoka na mahakama kwenda kuangalia eneo la tukio huwa ni kwa makundi, basi na wao ni waandamanaji!

Pili, Kwamba "Ni vizuri jamii ikajulishwa kwamba eneo lililovamiwa na wachimbaji wadogo linamilikiwa na kampuni ya uchimbaji na utafiti wa madini ya Resolute (Tanzania) Limited, ambao wana leseni halali ya kuchimba madini katika eneo hilo, leseni namba SML19/97)", inasema taarifa yao. Kauli hii ni ya mtu asiyejua sheria ya ardhi ya Tanzania, na kama huu ndiyo uelewa wenu haishangazi kwa ninyi kutoa tamko la uongo na upotoshaji namna hii. Resolute ‘hamiliki' eneo la Mwanshina, anamiliki leseni ya kuchimba dhahabu tu! Eneo la Mwanshina ni mali ya wananchi wakazi wa eneo lile, waliozaliwa pale na ndiyo maana hata yeye hakuliweka kwenye uzio wa maeneo yake. Na ndiyo maana hata leo hii akitaka kuchimba pale hawezi kufanya hivyo zaidi ya kutumia nguvu za jeshi la polisi tu. Na hichi ndicho kitakachopingwa na wananchi siku zote.

Tatu, katika taarifa ya TCME wanasema "Kitendo cha Kiongozi cha kuhamasisha wachimbaji wadogo kuvunja sheria ni mfano mbaya sana kwa jamii yetu na ni kitendo hatarishi kwa amani na utulivu". Ni vema TCME wakataja ni kiongozi gani amehamasisha wachimbaji wadogo wadogo wavunje sheria? Ni lini, wapi na kwa kauli ipi alihamasisha uvunjani huo wa sheria? Ni Mbunge aliyeenda kuwasikiliza wananchi waliofukuzwa kuchimba ama ni Naibu Waziri Nishati na Madini, Mhe. Stephen Massele, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ndg. Fatma Mwassa, na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Ndg. Bituni Msangi, waliowarudisha wachimbaji hawa katika eneo lile na baada ya wiki 2 tu kuwaondoa? Wananchi hawa walianza kuchimba dhahabu eneo lile mwezi Desemba mwaka 2013, wakazuiliwa na serikali mwezi wa kwanza na walitii agizo hilo.

Mbunge aliongea na Naibu Waziri na wakakubaliana kuwa atazungumza na Resolute wazirudishe leseni za eneo la Mwanshina kwa serikali hata kabla hazijamaliza muda wake, kwa kuwa wao wanaondoka na hawachimbi tena dhahabu pale, ili Serikali iwakatie wananchi leseni zao na kwamba wajiunge kwenye vikundi na SACCOS ili muda ukifika tu wapewe! Je, ni nani hasa aliyewarudisha wachimbaji hawa kwenye eneo la ‘Resolute' kabla ya utaratibu huu kukamilika? Na wakati anawarudisha aliwasiliana na Mbunge? Wakati anawarudisha hakujua kuwa hawana leseni na kwamba eneo lile ‘linamilikiwa na Resolute'? Ni kwa nini tena aliyewarudisha, akawaacha wakawekeza ‘vijisenti' vyao, na baada ya muda wa wiki mbili hata hawajafika popote anakuja anawaondoa tena? Ni nani atawalipa fidia ya nguvu, muda, na mitaji yao waliyowekeza pale? Ama uwekezaji wa watanzania maskini hauna maana kabisa kwenu? Wenye maana ni utafiti wa Resolute tu? Resolute mwenyewe alipokuja takriban miaka 15 iliyopita alikuta wenyeji wakichimba, mbona wao hawakulindwa dhidi yake? Maana na wao si walitafiti na kugundua uwepo wa dhahabu eneo lile na wakaanza kuchimba kabla yake?

Hivi ni wapi wachimbaji wadogo wadogo wamepewa maeneo yao na wanachimba dhahabu nchini mwao huku wakiwa na leseni? Ni kule Rwamgasa, Mwime ama Mwabomba? Kule wametumia vigezo gani kuwaruhusu watumie leseni za Barrick na mashirika mengine, na hapa Nzega wanawakataliaje? Ama ni kudhirisha madai kwamba kuna baadhi ya viongozi wa serikali wana maslahi yao na hili eneo la Mwanshina?

Hakuna anayekataa uwekezaji mkubwa kwenye maeneo yetu bali hakuna atakayekubali wawekezaji wachukue kila kitu na wenyeji wakose kabisa. Hakuna atakayekubali wenyeji wanyanyaswe na wapoteze mali yao kwa sababu kuna maslahi ya viongozi wachache. Miaka 15 iliyopita walipoteza mali yao na hawakulipwa fidia, leo hii hatutakubali wadhulumiwe tena!

Mwisho, rai yetu ni kwamba, viongozi wa Serikali watumie busara na hekima ya hali ya juu mara zote panapotokea migogoro baina ya wawekezaji na walalahoi ili kuondoa dhana kwamba wawekezaji wana thamani zaidi ya wenyeji, badala ya nguvu za kijeshi, uonevu, mabavu na vitisho, hususan kwenye mgogoro kama huu ambapo kwa kiasi kikubwa ni viongozi wa Serikali waliouanzisha kwa kuzuia uchimbaji pale awali, na kisha kuruhusu bila kufuata sheria.

Aidha Serikali iwafutie kesi wachimbaji wote wadogo wadogo na Raia waliokamatwa wakipita eneo lile siku hiyo bila kujua nini kimetokea pale, kwa vile tunaamini hakuna kosa walilofanya na pengine ni uonevu kuwashitaki hao wachache waliokamatwa. Pia, ni busara Serikali ikaongeza kasi ya kutafuta suluhu ya jambo hili kwa kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo leseni kama makubaliano ya awali yalivyokuwa na pia mwongozo wa uchimbaji wenye tija na ufanisi.
Imetolewa na,

Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega.
Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB).
 
Mkuki kwa Nguruwe------!

Wakati CDM walpokua wakiandamana na kupigwa huku wakiwa na vibali halali ulionaje na ulikuwa unasema nini?
Leo hii wewe ndio unaona unaonewa?

Unafiki wenu wana CCM ndio uliotufikisha hapa.Laiti kungekuwa na fair play kwenye siasa haya mambo yasingekuwepo.
 

nategemea wewe kama kijana uwe mfano kuwa vijana tunaweza,
lakini muda mwingi unageuka kuwa kituko,
acha kulamba matapishi, kama CDM walikuwa wanakosea kuandamana
iweje wwe ufanye hivyo???
Na tutawapiga tu........by M.K. Pinda
 

nategemea wewe kama kijana uwe mfano kuwa vijana tunaweza,
lakini muda mwingi unageuka kuwa kituko,
acha kulamba matapishi, kama CDM walikuwa wanakosea kuandamana
iweje wwe ufanye hivyo???
Na tutawapiga tu........by M.K. Pinda


Tatizo la watu wengi wa JF ni upofu unaosababishwa na siasa za mahaba kwa vyama vyetu, na siyo Utaifa, hivyo wakati mwingine tunakosa hoja kabisa, tunaishia kubwabwaja tu na kutoa povu jingi badala ya ku-argue kwa hoja!
 
Back
Top Bottom