Mwandosya aonya CCM isitafute mchawi wa uchaguzi uliopita

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC), Profesa Mark Mwandosya amesema viongozi wakianza kutafuta mchawi aliyesababisha washindwe uchaguzi uliopita katika baadhi ya maeneo, mwaka 2015 utakuwa mgumu kwao.

Amewataka viongozi hao bila kutaja chama, lakini katika kikao cha CCM, wajikite zaidi kuchapa kazi ili kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwa 2015 sio mbali na waliahidi wananchi mambo mengi.

"Ndugu zangu muda ni mfupi sana wa kutimiza yale tuliyoahidi kwa wananchi kwani sasa siyo miaka mitano tena, bali ni miaka minne na miezi tisa tu tuliyobaki nayo, tunapaswa kufanya kazi ya ziada kumaliza kero zilizopo," alisema Prof. Mwandosya.

Prof. Mwandosya ambaye pia ni Waziri wa Maji alisema hayo jana wakati alipokuwa akipokea taarifa ya maendeleo ya CCM katika Mkoa wa Tabora.

“Haitasaidia kuanza kuulizana wewe au nani alifanya tushindwe eneo fulani, haina tija na haiingii akilini katika kusaidia wananchi,” alisema na kuongeza ahadi katika uchaguzi ni kitu muhimu na wanapaswa kukamilisha yote.

“Itafikia mahali muda umekwenda, halafu tunaanza kuulizwa na wananchi kila kona kuwa tulisema hivi, lawama zitaturudia wenyewe kwa kushindwa kumaliza ahadi zetu.

“Hakuna kitu kibaya kama wananchi kuamua kufanya uamuzi ambao kwetu itakuwa majuto na lawama,” alisema Prof. Mwandosya na kusisitiza kuwa jambo lisilo na tija kwa wanachama na viongozi kuanza kusaka mchawi katika baadhi ya sehemu ambazo CCM ilishindwa.

Aliwataka viongozi wa vyama mbalimbali kuacha malumbano, bali watekeleze Ilani ya CCM ya 2010-2015 na kuwaletea maendeleo wananchi.

"Sasa ni muda wa kazi tu,tena kwa kujipanga tusipofanya hivyo mwaka 2015 hali kwetu itakuwa mbaya sana huu ni ukweli usiopingika kabisa tujitahidi kukamilisha ilani ya uchaguzi kwa yale yaliyopo," alisisitiza.

Alisema itashangaza zaidi kuwa baadhi ya viongozi na wanachama kuanza kutajana majina kuwa fulani alifanya hivi, kiongozi fulani alitusaliti na kuonya hiyo ni kujitafutia ama kujiletea mazingira magumu katika kusukuma maendeleo.

Alisema kama viongozi wa chama, wanachama wanataka kuuona mwaka wa uchaguzi wa 2015 mgumu kwao, basi waendelee kusaka wachawi ndani ya chama.

“Tutashindwa kufanya kazi na badala yake muda utakwisha tunarudi kwa wananchi mikono mitupu na mbaya zaidi tutaulizwa tumefanya nini katika kipindi cha miaka mitano,” alionya.

HabariLeo | Mwandosya aonya CCM isitafute mchawi wa uchaguzi uliopita
 
Back
Top Bottom