Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 613
Taarifa iliyosambazwa na UONGOZI WA MEDIA SOLUTION WAMILIKI WA THISDAY NA KULIKONI:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MWANDISHI wa habari mwandamizi Godrefy Mhando (63) amefariki dunia leo asubuhi jijini Dar es Salaam kwa matatizo ya moyo.
Mhando ambaye hadi kifo chake alikuwa mhariri msanifu wa gazeti la Kulikoni, linalochapishwa na Kampuni ya Media Solutions Limited amefariki leo asubuhi muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Burhani.
Familia ya marehemu ikielezea kuhusu kutokea kwa kifo chake, ilieleza kuwa Mhando leo asubuhi alikuwa amejiandaa kuelekea kazini, lakini kabla hajaondoka nyumbani, alijisikia vibaya, hasa kubanwa na kifua na mapigo ya moyo kuongezeka, ndipo alipopelekwa hospitali ya Madonna, iliyopo Tabata.
Hata hivyo, madaktari walishauri apelekwe hospitali ya Amana, ingawa familia iliamua kumpeleka hospitali ya Burhani ambako alifariki dunia hata kabla ya kuanza kupatiwa huduma.
Mhando aliwahi kuajiriwa na Kampuni ya magazeti ya Chama Cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo ambako alifanya kazi kwa muda wa miaka 30 kabla ya kustaafu mwaka juzi kujiunga na Media Solutions Limited kama mwajiriwa wa muda (part-time staff).
Alizaliwa mwaka 1944 jijini Dar es Salaam na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Mchikichini kuanzia mwaka 1952 hadi 1955 na kuendelea na shule ya kati ya wavulana ya Uhuru hadi mwaka 1959 alikohitimu.
Kuanzia mwaka 1960 hadi mwaka 1964 alijiunga na Shule ya Sekondari Kiungani, Zanzibar na baadaye kwenda Chuo cha Kimataifa cha Mawasiliano ya Umma cha Szechoslovakia ambako alisoma uandishi wa habari na kutunukiwa stashahada.
Alirejea nchini na kuanza kazi Uhuru na Mzalendo akiwa mwandishi wa habari na mwaka 1990 hadi 1991, alikwenda Ujerumani kwa masomo ya Sayansi ya Jamii katika chuo cha Magdeburg ambako alitunukiwa stashahada.
Mhando ameacha mke na watoto kadhaa. Taratibu za mazishi zinapangwa na familia ya marehemu Mhando nyumbani kwake Tabata Segerea, eneo la Mangumi.