Mwandishi Ni Mjumbe, Hauawi ( Makala, Raia Mwema) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mwandishi Ni Mjumbe, Hauawi ( Makala, Raia Mwema)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Sep 6, 2012.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Sep 6, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa,

  HUWEZI kutawala miili ya watu ukaacha mioyo yao. Ndiyo, mjumbe hauawi, ni kauli ya hekima ya tangu enzi za wahenga wetu.

  Mwandishi wa habari na Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa Habari mkoani Iringa, Daud Mwangosi ameuawa. Polisi wanatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

  Jumapili ya Septemba 2, 2012 itabaki katika kumbukumbu za Watanzania kwa mamilioni kwa kufikiwa na taarifa za kutisha za mauaji ya mwandishi wa habari. Haya yanaingia katika historia kuwa ni mauaji ya kwanza kwa mwandishi wa habari kufanyika hadharani tangu nchi hii ipate Uhuru.

  Wengi watakuja kukumbuka walikuwa wapi na walifanya nini siku walipopata taarifa hizo za kutisha. Binafsi, taarifa ile ya mauaji ya Daud Mwangosi siku ile ya Jumapili ya huzuni kwa Taifa ilinikuta nikiwa Iringa, umbali wa mwendo wa saa moja kwa gari kufika eneo la tukio, Nyololo, Mufindi.

  Jioni ile nilikuwa nikifundisha soka ya watoto. Mara baada ya kupata taarifa zile kwa simu, nilisitisha mazoezi yale ya watoto. Nikawapa taarifa zile. Nilipowaambia kuwa nimepata taarifa sasa hivi kuwa mwandishi wa habari ameuawa Mafinga, mtoto mmoja akaniangalia na kuniuliza; “ Kwanini?”

  Ndiyo, swali la mtoto yule ndilo umma wa Watanzania unapaswa kujiuliza sasa; KWA NINI?

  Mwandishi wa habari ni mjumbe katika jamii. Anapokuwa akifanya kazi yake hapaswi kuwa na hofu ya kudhuriwa kwa kukusudia na waliopata mafunzo ya kutumia silaha. Ndivyo ilivyo kwa watumishi wa Msalaba Mwekundu, wanapokuwa kazini kwenye maeneo hata ya vita.


  Askari asiyejua kutofautisha kati ya mwanahabari aliyeshika kamera, mtu wa Msalaba Mwekundu aliyeshika mkoba wa Huduma ya Kwanza na raia anayefanya vurugu au adui aliyeshika silaha vitani, huyo hawezi kuwa ni askari makini.


  Polisi katika nchi ni moja ya viungo muhimu vya dola kuu. Polisi ni mkono mrefu wa dola ( State's extended arm). Inapofika mahali, mkono huu muhimu unapoonyesha udhaifu wa ndani katika mfumo wa utendaji kazi wake, basi, umma nao unakosa imani na mkono huu mrefu. Ndipo hata raia wa kawaida niliyemsikia kwenye runinga ya ITV akitamka; ” Kama polisi si makini, basi ni heri wasiwepo watuache wenyewe tuendeshe mambo yetu, maana sisi wananchi tunaishi kwa amani na utulivu”.

  Kauli kama hizi ni kiashiria cha umma unaopungukiwa imani na dola na viungo vyake, ikiwamo polisi. Hili haliwezi kuwa jambo jema.

  Na hakika, kama Taifa, tunafanya makosa kuamini, kuwa nchi yetu ni ya amani kwa vile wananchi wetu hawagombani.


  Kama watu hawagombani basi maana yake ni nchi ina amani yaweza kuwa tafsiri potofu ya maana nzima ya amani. Maana, kama watu hawagombani mahali pasipo na haki, usawa na uadilifu wa viongozi; mahali palipojaa dhuluma,unyanyasaji na maovu mengine wanayotendewa au wanaotendeana wanajamii, basi, amani hiyo itakuwa ni ya muda tu.


  Maana, kwa watu wenye kuishi kwenye mazingira hayo bila kugombana wala kutokea uvunjifu wa amani, hiyo itakuwa na maana ifuatayo; ama watu hao hawaelewi kuwa wanaishi katika mazingira hayo ya dhuluma na maovu mengine wanayotendewa au kutendeana, au wamejawa na hofu.


  Hivyo basi, kwa hilo la mwisho, itakuwa ni amani iliyojengeka katika misingi ya hofu. Na hofu hiyo haiwezi kuwa ya kudumu. Kuna siku mwanadamu hufikia ukomo wa kuhofia. Ukimwandama sana mjusi, mwisho hugeuka nyoka! Ndipo hapo tunapoona nchi zinalipuka na watu kuchinjana.


  Tumefika mahali hata wawakilishi wa wananchi kwa maana ya wabunge , wanatiwa mbaroni na polisi katika mazingira ya kudhalilisha, tulishuhudia hili likimtokea Mbunge wa Viti Maalumu, CUF, Tabora Mjini. Mbunge ni mwakilishi wa wananchi. Mbunge ni mjumbe aliyetumwa na wananchi. Ana kinga ya kikatiba.

  Kwa polisi kumdhalilisha mjumbe wa wananchi ina maana pia ya kuwadhalilisha waliomtuma. Haya ni matendo ya aibu.

  Kilichomtokea mwandishi Daud Mwangosi ni aibu pia ya Taifa hata kimataifa. Kupunguza aibu hii ni kufanyika kwa uchunguzi huru, na kwa wote watakaobainika kuhusika na aibu hii wachukuliwe hatua za kisheria. Na wenye kustahili kuwajibika wawajibike kulinda heshima ya serikali iliyo madarakani.

  Hii ni nchi yetu. Katika tofauti zetu hizi za kiitikadi tusifike mahali tukashindwa kuongea kama Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania. Kuna umma uliopo na unaokuja. Umma unaotegemea sana busara katika uongozi wetu.

  Tuanze sasa kujenga utamaduni wa kuitumikia nchi yetu kwa kufanya na kuamua yale yenye maslahi kwa Tanzania. Hivi vyama vya siasa vipo leo na kesho havipo. Vinakuja na kuondoka, lakini Tanzania kama nchi itakuwapo daima.


  Tusifike mahali tukabaki tunawaangalia wanasiasa wetu, kwa maslahi yao binafsi, ya makundi yao na vyama vyao, wakashinikiza au kuelekeza yale yenye kuchochea machafuko makubwa ya kijamii. Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa kutanguliza busara katika kila maamuzi wayafanyao.


  Na tunafanyaje pale tunapowaona viongozi wa kisiasa na watendaji wakifanya maamuzi yasiyo na busara na kusababisha Watanzania wenzetu kupoteza uhai na hata kuchochea machafuko?

  Jibu; Kama Watanzania wazawa na wazalendo wa nchi hii, tuna wajibu wa kuyalaani matendo yao maovu.

  Na katika nchi zetu hizi, ni kazi rahisi sana kuanzisha vurugu na kujenga mazingira ya chuki na uhasama, lakini ni kazi kubwa sana kumaliza vurugu na kuondosha mazingira hayo ya chuki na uhasama. Na nchi yetu kamwe haiwezi kupiga hatua za maana za maendeleo katikati ya mazingira ya vurugu, chuki na uhasama, uwe wa vyama vya siasa au wanajamii.


  Kihistoria, Watanzania tumeishi kwa amani na upendo bila kuwa na chuki na uhasama miongoni mwetu unaotokana na tofauti zetu za kidini na kikabila. Tunaziona sasa, dalili za baadhi ya wanasiasa, kwa malengo ya kisiasa, kutaka kupandikiza miongoni mwetu uhasama na chuki kwa kutumia tofauti zetu za kidini na kikabila, tofauti zetu za kiitikadi. Wanafanya hivyo mara ile wanaposhindwa kujenga hoja za kisiasa kwenye majukwaa ya kisiasa. Hawa ni watu hatari sana kwa maslahi ya taifa letu.


  Katika nchi zetu hizi, ni wanasiasa wa aina hii ambao, katika kufanikisha malengo yao, huwa tayari hata kuwalipa vijana wasio na ajira na kuwavutisha bangi ili washiriki vurugu za kisiasa, kidini na kikabila. Tumeyaona hayo Liberia, Ivory Coast na hata katika nchi jirani na kwetu.


  Tusipokuwa makini, yako karibu kupisha hodi kwenye nchi yetu, kama si tayari kuwa yameshaingia ndani ya nchi yetu.

  Hii ni nchi yetu. Tutafanya makosa makubwa kuwaachia viongozi wa kisiasa pekee, jukumu la kulinda maslahi ya nchi yetu. Tunapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate Uhuru.

  Dunia imebadilika, na nchi yetu inapitia kwenye kipindi cha mabadiliko. Hakuna mtu au chama cha siasa kinachoweza kuyazuia mabadiliko haya. Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja amani yetu. Tuna jukumu la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara, kuipitisha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko.

  Maana, tukiingia kwenye machafuko, basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote tutashindwa.

  Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika.
  0788 111 765
  Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
   
 2. kookolikoo

  kookolikoo JF-Expert Member

  #2
  Sep 6, 2012
  Joined: Mar 9, 2012
  Messages: 2,537
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 135
  well said. lakini maneno matupu
  hayavunji mfupa. napata taabu kuuelewa msimamo wako wa kutounga mkono
  wenzako kususia habari za polisi iringa!
   
 3. Mohamedi Mtoi

  Mohamedi Mtoi R I P

  #3
  Sep 6, 2012
  Joined: Dec 11, 2010
  Messages: 3,326
  Likes Received: 44
  Trophy Points: 0
  Nimesoma makala hii lakini baada ya kukutana na Pumba zinazolaumu wana siasa kwa mauwaji nimeamua kuishia njiani maana muandishi ameanza kuifanya kazi itikadi ya gamba lake.
   
 4. m

  maggid Verified User

  #4
  Sep 6, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Kookooliko,

  Asante sana. Mimi pia ni mwandishi, ni mjumbe pia. Nami pia huwakilisha ujumbe wa kijamii. Ni jamii yenye kuhoji mengi, yenye kuhitaji majibu ya maswali yao. Nami ni sehemu ya jamii hiyo. Na kuna wanaojitahidi ' kuniua' badala ya kujadili hoja ninazowakilisha kama mjumbe.

  Naheshimu mawazo ya wengine hata kama wengine hawaheshimu mawazo yangu. Na kama nina hoja ninayoiamini, basi, nitaisimamia mpaka atokee mwenye uwezo wa kuibomoa hoja yangu kwa nguvu za hoja.

  Maggid,
  Iringa.
   
 5. M

  Molemo JF-Expert Member

  #5
  Sep 6, 2012
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 13,287
  Likes Received: 580
  Trophy Points: 280
  Naona hapa anatumika kusafisha polisi na kuchafua CDM
   
 6. Matola

  Matola JF-Expert Member

  #6
  Sep 6, 2012
  Joined: Oct 18, 2010
  Messages: 36,045
  Likes Received: 13,266
  Trophy Points: 280
  Leo ndio ilikuwa siku yangu ya Mwisho ya kusoma makala za huyu Pimbi na hata Blog yako nimeaga rasmi leo, kamwe hutoniona huko milele kama nilivyoiblock blob ya michuzi. mnafki mkubwa wewe.
   
 7. m

  maggid Verified User

  #7
  Sep 6, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Mjengwablog Inachangisha Pole Ya Kumsaidia Mjane Wa Daud Mwangosi Kuendesha Biashara Ndogo...

  Ndugu zangu,

  Daud Mwangosi ambaye pia alikuwa ' Mwanakijiji' mwenzetu hapa Mjengwablog hatunaye tena.
  Nimemfahamu Daud Mwangosi tangu mwaka 2004 nilipofika Iringa. Tangu wakati huo, amekuwa akiinipa ushirikiano mkubwa kwenye kazi ya kutangaza shughuli za kijamii kwenye Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi. Ni kwa kupiga picha za televisheni na kurusha habari kwenda Channel Ten; Iwe ni kwenda naye Ilula au Njombe, Daud Mwangosi alikuwa tayari kila nilipomwomba aongozane nami kwa shughuli ya kijamii.


  Mara nyingi nilimkuta Daud ofisini kwake ( Picha ya kwanza juu) akichapa kazi na huku mkewe akimsaidia kazi nyingine. Daud Mwangosi alikuwa mbunifu. Alikuwa ni mwenye kiu ya kujifunza mambo mapya kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano.


  Najua Daud Mwangosi alikuwa na malengo ya kuendeleza shughuli zake za ujasiriamali. Mbali ya mambo mengine, alikuwa na Photocopy machine ya kumwongezea kipato ambayo iliharibika mwaka jana. Akawa na ndoto ya kuwa na studio ndogo ya kupiga picha za vipande ( Passport Size). Yote ni katika kumwongezea kipato kutunza familia yake.


  Leo Daud Mwangosi hayuko nasi. Ameacha familia, mjane na watoto wanne; Itika Mwangosi ( Mjane) Nehemia Mwangosi ( 17) Kidato cha Nne Malangali Sekondari, Hetzgovina Mwangosi (12) Bathsheba Mwangosi (9) na Moria Mwangosi ( 2)
  Namini Daud Mwangosi angependa shughuli alizokuwa akizifanya ziendelee na zije kuwasaidia watoto wake pia.


  Jana na leo nimewasiliana na mjane wa marehemu Mwangosi ambaye bado yuko Tukuyu. Nikamwambia kuna ' Wanakijiji ' wa Mjengwablog walioguswa na msiba wa Mwangosi na wangependa kutoa pole yao imsaidie katika kupata mwanzo kutoka hapa alipo sasa. Mjane wa Mwangosi amefarijika sana kusikia habari hizo.


  Kwa vile tayari ameahidiwa msaada wa kusomeshewa watoto. Msaada anaouhitaji kwa sasa ni kupata photocopy machine ( Used) na kodi ya pango la ofisi. Jumla yake kwa yote hayo mawili haitazidi shilingi za Kitanzania milioni mbili na laki mbili. Hivyo msaada anaouomba kwa wenye mapenzi mema ni shilingi 2, 200,000 ( Shilingi milioni mbili na laki mbili). Shughuli hizo zitamsaidia kujikimu.


  Kutokana na hali aliyo nayo sasa, Mwenyekiti wenu napendekeza nichukue jukumu la kuratibu michango hiyo. Shime tushirikiane kufanikisha hili ili tumsitiri mjane wa mwenzetu Daud Mwangosi.
  Napendekeza ifikapo mwisho wa mwezi huu ( Septemba) tuwe tumefanikisha zoezi hili kwa yeyote aliye nacho, hata kama ni shilingi elfu tano, ni msaada mkubwa.


  Mjengwablog bado tuna rekodi nzuri katika kuchangishana kuwasaidia wenye kuhitaji. Itakumbukwa, huko nyuma, kwa pamoja, tulifanikisha kukusanya michango ile ya watoto wa Somalia na kuikabidhi UNICEF, Dar es Salaam. Ni zaidi ya shilingi milioni mbili.
  Tulifanikisha mchango wa kusaidia ukarabati wa maktaba ya Kijamii kijijini Mahango, Madibira. Zaidi ya shilingi milioni nne.
  Sasa ni zamu ya kumchangia mjane wa mwenzetu Daud Mwangosi. Kinachohitajika ni milioni mbili na laki mbili.
  Naam, kutoa ni moyo, usambe ni utajiri.
  Mwenyekiti wenu na familia yangu naanza kwa kuchangia shilingi laki moja.

  Na kama kawaida, taarifa za waliochanga na kiasi kilichopatikana kitawekwa kwenye blogu kwa kila mmoja kuona.


  Namna ya kuwasilisha michango: Tumia M-Mpesa, Tigo Pesa, Airtel Money au NMB Mobile. Kwa namba 0754 678 252, 0712 95 61 31, 0788 111 765 ( Kwa walio nje mnaweza kutuma kwa Western Union, jina la mpokeaji- Maggid Mjengwa)  Natanguliza Shukrani.


  Maggid Mjengwa,
  Iringa.
  0788 111 765
  Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
   
 8. K

  Kwame Nkrumah JF-Expert Member

  #8
  Sep 7, 2012
  Joined: Dec 2, 2008
  Messages: 887
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 45
  Niliacha kupata News kwa Michuzi siku nyingi sana nikahamia kwa Mjengwa, lakini sakata hili limefichua haswa wadhalimu wa nchi hii..wewe MAGGID MJENGWA ni mmoja wao. Hivi unavoenda huko Ulaya huoni waandishi wanavyofanya kazi kwa uhuru? Huoni demokrasia ya kweli? Kwa kua wewe upo poa basi wengine can go to hell ??
  Polisi hawa HAWATUHUMIWI !!Wameshikwa REDI HENDEDI. Una roho gani wewe ??
   
 9. Matola

  Matola JF-Expert Member

  #9
  Sep 7, 2012
  Joined: Oct 18, 2010
  Messages: 36,045
  Likes Received: 13,266
  Trophy Points: 280
  Boycott Mjengwa blog, makala zake na unafki wake wote. huyu ni Traitor hapaswi kuishi na binadamu waliostaarabika.
   
 10. M

  MIGNON JF-Expert Member

  #10
  Sep 7, 2012
  Joined: Nov 23, 2009
  Messages: 2,586
  Likes Received: 1,562
  Trophy Points: 280
  Mimi ni mshabiki na mpenzi wa makala zinazoandkwa na Maggid na kila tukipata wasaa tunajadilaina katika mambo tofauti kupitia simu.
  Nimeisoma makala hiikatika gazeti na nimeirudia tena hapa katika mtandao.
  Bado nsahindwa kuelewa kwa nini Maggid ashambuliwe kwa maneno makali wakati msimamo upo wazi na alipowataja wanasiasa hakutaja Chama.Wanasiasa wa Chama tawala inawezekana kabisa wakawa walengwa wa mkala hii na si wa upinzani kama wengi wanavyotaka ionekane.
  JF is for great thinkers na dunia nzima inaeleweka ya kuwa anayeweza kukutia hatiani ni Mahakama na kwingine kote wewe ni mtuhumiwa tu hata kama ulikamatwa na panga lenye damu.
  Wakati mwingine tupime hoja zetu.
   
 11. M

  MIGNON JF-Expert Member

  #11
  Sep 7, 2012
  Joined: Nov 23, 2009
  Messages: 2,586
  Likes Received: 1,562
  Trophy Points: 280
  Well said Maggid,keep it up.
  Watu hawasomi between the lines na inaelekea kusoma vitabu vya wana falsafa kwao ni ngumu mno.
  Usichoke Maggid,tutakupinga panapostahili na tutakupongeza kwa kauli nzuri na za kiungwana.
   
 12. Matola

  Matola JF-Expert Member

  #12
  Sep 7, 2012
  Joined: Oct 18, 2010
  Messages: 36,045
  Likes Received: 13,266
  Trophy Points: 280
  Hapo kwenye hizo RED fanya marekebisho na isomeke Nitakupinga na Nitakupongeza.
  Usitumie We kwa sababu hatujakutuma uongee kwa niaba yetu. kama una mahaba na Maggid ni wewe, tena ruksa hata kwenda kumpikia chai kwake.
   
 13. Kanyapini

  Kanyapini JF-Expert Member

  #13
  Sep 7, 2012
  Joined: Jul 25, 2012
  Messages: 299
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  :shetani::shetani::shetani::shetani::shetani::shetani:
   
 14. Ukwaju

  Ukwaju JF Bronze Member

  #14
  Sep 7, 2012
  Joined: Oct 19, 2010
  Messages: 8,287
  Likes Received: 810
  Trophy Points: 280
  Mjengwa nimekukubali unajua Mwanasiasa akipanda Jukwaani na kutamka nchi hii haitatawalika Je ? ni jukumu la nani kufuatilia matamko hayo na kuyazuia?
  Tumeona Pemba askari akichinjwa hivihivi tena kupitia kisogoni na watu wakanyamaza wala hakuitwa shujaa, Mjengwa amesema kweli tupu "Na katika nchi zetu hizi, ni kazi rahisi sana kuanzisha vurugu na kujenga mazingira ya chuki na uhasama, lakini ni kazi kubwa sana kumaliza vurugu"
   
 15. POMPO

  POMPO JF-Expert Member

  #15
  Sep 7, 2012
  Joined: Mar 12, 2011
  Messages: 6,694
  Likes Received: 14
  Trophy Points: 135
  Maggid "muuwaji" na makal;a zako za kinafiki, vipi si ulifurahi sana mwangosi kuuwawa kikatili eh? na zaidi kufungiwa mwanaHalisi naona ndio unakuwa happy na polisi wenzio.
   
 16. M

  MIGNON JF-Expert Member

  #16
  Sep 7, 2012
  Joined: Nov 23, 2009
  Messages: 2,586
  Likes Received: 1,562
  Trophy Points: 280
  Asante sana kwa masahihisho hayo lakini naamini katika kadamnasi hii ya JF kuna watu ambao watakuwa na mawazo kama yangu na hao ndo niliowalenga.
  Kupika chai imekujaje hapa?This shows the type of a person you are.Jenga hoja acha matusi.
   
 17. N

  Nambombe Senior Member

  #17
  Sep 7, 2012
  Joined: May 28, 2012
  Messages: 161
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  wewe ni kilaza tu,hauna lolote unalolijua kuhusu uandishi wa habari.Angalia hata habari zako unavyoziandika huwa hazieleweki.Wengi huwa hawazipendi makala zako kama haulijui hilo.
   
 18. K

  Kwame Nkrumah JF-Expert Member

  #18
  Sep 7, 2012
  Joined: Dec 2, 2008
  Messages: 887
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 45
  Mjenga ni mwanachama wa Iringa Press Club ambayo Marehemu alikua ni rais/mwenyeketi wake.
  Club hiyo iliyoongozwa na marehemu, ambayo Mjenga ni mwanachama hai wake imejadili na kuamua kutoandika habari za kipolisi. Mjengwa ambaye ni mwanachama wa club hiyo, iliyokua inaongozwa na marehemu, ambaye Mjengwa anadai alikua ni rafiki yake ANAPINGA MAAMUZI hayo.
  Mtetee all you want...lakini mkiwa mnajadiliana naye kwenye simu mwambie yeye ni msaliti.
   
 19. M

  MIGNON JF-Expert Member

  #19
  Sep 9, 2012
  Joined: Nov 23, 2009
  Messages: 2,586
  Likes Received: 1,562
  Trophy Points: 280
  Niliposema tupime hoja zetu niliamini umenielewa lakini inaelekea bado kuna ugumu.
  Nimeipitia makala yote sioni na bado sioni usaliti.
  Nimepitia kwenye blog yake na tayari ameshahamasisha na zimechangwa millioni tatu za kumsaidia mjane wa marehemu.
  Naomba unisaidie usaliti wake unastahili kauli kali kama zilivyoonyeshwa na baadhi ya wachangiaji.
   
 20. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #20
  Sep 9, 2012
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,461
  Likes Received: 81,711
  Trophy Points: 280
  Mkuu mohamed Mtoi Gamba liko kazini kuutafuta ukuu wa wilaya kwa udi na uvumba kwa kufanya juhudi za kuupotosha umma wa Watanzania.

   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
Loading...