UZUSHI Mwanaume mmoja aokolewa kutoka kwenye kifusi miezi mitatu baada ya tetemeko la ardhi nchini Uturuki

Baada ya tathmini, tumebaini kuwa taarifa hii ni ya uzushi
Picha moja iliyosambaa mtandaoni – ikiwemo hapa JamiiForums – inamuonesha mwanaume mmoja akiwa katika hali mbaya ya kiafya. Maelezo katika picha hiyo yameandikwa kwa lugha ya Kiarabu yakieleza: “Kutoka tetemeko la ardhi la Februari 6, leo ametolewa chini ya vifusi huko Antakya, Uturuki hai na akiwa vizuri. Utukufu ni wa Mungu.”

Ahmed Fake.jpg



Ahmed.jpg

Picha ya sasa ya Ahmed Al-Sousi (Chanzo: An-Nahar)
 
Tunachokijua
Uchunguzi wa JamiiForums umebaini kuwa taarifa iliyoambatanishwa kwenye picha hiyo kudai kuwa mwanaume huyo ameokolewa toka kwenye kifusi haipatikani kwenye chanzo chochote cha habari cha kuaminika. Utafutaji uliofanyika kupitia Google Image Search pia unaonesha kuwa picha hiyo haihusiani kwa vyovyote na madhara ya tetemeko la ardhi lililoikumba nchi za Uturuki na Syria mnamo mwezi Februari mwaka huu 2023.

Jambo lingine linaloongeza mashaka kuhusu taarifa hiyo ni kuwa hata baadhi ya watumiaji wa mtandao waliohoji uhalisia wake katika kurasa zilizoichapisha lakini hawakupata majibu ya kuridhisha. Kwa mfano, mtumiaji mmoja wa Twitter alihoji: “Jambo jema. Lakini chanzo cha habari ni kipi?” Majibu yalikuwa ni ya mzaha, “Niamini mimi.”

Zaidi ya hayo, JamiiForums imebaini kuwa hakuna chombo cha habari cha kimataifa kilichoripoti kuokolewa kwa mtu yeyote baada ya miezi mitatu tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi nchini Uturuki.

Hata hivyo, uchunguzi zaidi uliofanyika na JamiiForums umebaini kuwa taarifa hii imekanushwa na tovuti ya gazeti la An-Nahar ( النهار) baada ya kusambaa kwa wingi. An-Nahar ni gazeti la kila siku linalochapishwa kwa lugha ya Kiarabu nchini Lebanon. Lilianzishwa mwaka 1933. Taarifa zinanaeleza kuwa mwanaume anayeonekana kwenye picha hiyo anaitwa Ahmed Al-Sousi anayeishi huko Idlib, nchini Syria.

Taarifa pia zinaeleza kuwa picha hiyo ya Bw. Ahmed iliyopigwa takribani miaka saba iliyopita, inamuonesha akiwa anaugua ugonjwa wa ngozi uitwao Psoriasis ambao husababisha upele, muwasho na mabaka katika maeneo mbalimbali ya mwili. Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani (CDC), Psoriasis ni ugonjwa unaotokana na sehemu ya mfumo wa kinga ya mwili kuwa hai kupita kiasi (overactive) na kushambulia tishu za kawaida za mwili.

Taarifa pia zinaeleza kuwa Bw. Ahmed anapewa dozi ya dawa kila baada ya siku 45 ili kutibu ugonjwa huo, na anaeleza kuwa kwa kipindi ambacho picha hiyo ilipigwa alikuwa amedhoofika sana mwili. Pia, kwa sasa anapata shida kunyoosha vidole vyake na kwamba mguu wake wa kulia kwa sasa unampa wakati mgumu kutembea.

Kwa taarifa hizi, ni dhahiri kuwa picha na taarifa zilizosambaa mtandaoni kuhusisha picha ya Ahmed na tetemeko la ardhi nchini Uturuki ni za uzushi.
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom