Mwananchi: Bei ya vifaa vya ujenzi moto, wanaojenga wahaha

Kinuju

JF-Expert Member
Mar 20, 2021
2,390
5,310
Gazeti la mwananchi limekuja na habari ya kina inayoonyesha upandaji bei wa kutisha wa vifaa vya ujenzi kwa miezi 6 iliyopita.

Waziri wa viwanda Prof Kitila Mkumbo amesema hata yeye hajui kwa nini bei ya cement imepanda wakati amefanya utafiti na kugundua gharama za uzalishaji viwandani hazijapanda.

Amesema serikali itaendelea kufanyia utafiti kwenye eneo la usambazaji huenda ndio wanaopandisha bei sokoni.

---
Bei ya vifaa vya ujenzi katika baadhi ya maeneo nchini imepaa ndani ya miezi michache iliyopita, jambo lililosababisha vilio kwa wananchi wanaojenga na wafanyabiashara wa vifaa hivyo.

Mikoa ya Songwe, Njombe na na Dar es Salaam, ni kielelezo cha hali halisi ya upatikanaji wa bidhaa hizo, huku wafanyabiashara wakisema bidhaa kama mabati yamekuwa nadra kupatikana, hali inayofanya biashara kuwa ngumu.

Nao baadhi ya wananchi wanaoendelea na ujenzi, walilieleza Mwananchi kuwa kwa sasa wamesitisha ujenzi, kutokana na kupaa kwa gharama za vifaa hivyo muhimu kwenye ujenzi na kukwamisha ndoto zao za kupata makazi bora kulingana na vipato vyao.

Hata hivyo, wazalishaji wa vifaa vya ujenzi wamebainisha kwamba ongezeko hilo la bei limesababishwa na kuongezeka kwa mahitaji ya chuma katika soko la dunia wakati uzalishaji ukiwa uleule.

Alipoulizwa kuhusu ongezeko hilo la bei, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo hakuwa tayari kuelezea kwa undani. Hata hivyo, alisema:

“Huwa tunafanya survey (uchunguzi) ya bei kila wiki, sasa sijapata ripoti ya wiki iliyopita, kesho (leo) ndiyo nitaipata, kwa hiyo siwezi ku-comment (kueleza) kwa sasa.”

Hali ilivyo jijini Dar es Salam

Mwananchi lilitembelea maduka mbalimbali jijini Dar es Salaam na kubaini vifaa vya ujenzi vilivyopanda bei kuwa ni pamoja na bati, nondo, marumaru, rangi, ‘gypsum board na poda yake pamoja na rangi katika maduka mbalimbali.

Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Buguruni jijini humo, Marietha Sungura alisema vifaa vya ujenzi vimepanda bei maradufu na wateja wamepungua na kufanya biashara yao kuwa mbaya.

Alisema bati za rangi za geji 28 zimepanda bei kutoa Sh27,000 na Sh28,000 hadi kufikia Sh40,000 hivi sasa wakati zile za geji 30 nazo zikipanda kutoka Sh18,000 na Sh19,000 hadi kufikia Sh27,000 hivi sasa.

Alisema marumaru nazo zimepanda bei kutoka Sh15,000 kwa zile zenye ukubwa wa 40 kwa 40 na sasa zinauzwa Sh25,000.

Kwa upande wa ‘gypsum powder’, Marietha alisema nazo zimepanda kutoka Sh16,000 hadi kufikia Sh33,000, kiasi ambacho ni mara mbili zaidi.

“Bidhaa hakuna na wateja pia hakuna. Kwa mfano, kwenye bati, unakuta mzigo ukiisha, kuja kupatikana tena unaweza kukaa hadi mwezi mzima,” alisema mwanamke huyo mfanyabiashara huyo.

Mfanyabiashara mwingine katika eneo hilo, Kelvin Kalasa alibainisha vifaa vingine vilivyopanda bei kuwa ni gypsum boardambazo miezi michache iliyopita zilikuwa zinauzwa kwa Sh18,000 kwa kila moja lakini sasa ni Sh22,000.

Aliongeza kuwa bidhaa nyingine kama saruji na rangi nazo zimepanda, lakini siyo kwa kiwango kikubwa kama ilivyo kwenye nondo na bati. Alisema nondo zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh19,000 hadi Sh21,000 sasa zinauzwa Sh26,000 au zaidi kulingana na eneo.

“Yaani vitu vinapanda bei halafu biashara zimekuwa ngumu. Unaweza ukapata mzigo kidogo kidogo ukiisha unakaa kusubiria mwingine kwa muda mrefu, ukifika unakuja kidogo, siyo kama zamani,” alisema Kalasa.

Hali mkoani Njombe

Ongezeko la bei ya vifaa vya ujenzi siyo kwa Dar es Salaam pekee bali pia mikoani ambako wafanyabiashara wanasema bei ikipanda katika jiji hilo, nao wanaathirika kwa kuwa ndipo wanaponunua bidhaa zao.

Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi mkoani Njombe, Imasco Sanga alisema bei ya vifaa ilianza kupanda kuanzia Julai mwaka huu, lakini kabla ya hapo bei zilikuwa nzuri ukilinganisha na sasa ambapo ongezeko hilo limewashtua wateja wao.

“Viwanda vingi viko huko Dar, kwa hiyo wakipandisha huko na sisi tunaoagiza huku tunapandisha. Hali ni mbaya kwa kweli,” alisema Sanga na kuongeza kwamba bidhaa za chuma kama vile mabati na nondo ndiyo zimepanda zaidi.

Songwe nako moto

Mfanyabiashara mwingine katika mji wa Vwawa mkoani Songwe, Subiri Ndambo alisema bei ya saruji imekuwa ikipanda kila wiki kutoka bei ya Sh15,500 kwa mfuko mmoja wa kilo 50 na sasa bei ya mfuko huo inauzwa Sh16,500 kwa mfuko.

Alisema bei ya bati na nondo nayo haishikiki ambapo nondo yenye urefu wa futi 40 ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh18,000 na 22,000 mwezi uliopita, lakini kwa sasa zinauzwa Sh27,000 na bati zimepanda kutoka bei ya 18,000 na 25,000 kwa bati lenye ujazo wa geji 30.

Kilio cha wananchi

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Jackline Paschal anasema hakuamini alipoelezwa kuhusu kupanda kwa bei ya nondo ndani ya miezi mitatu tu tangu aanze ujenzi.

“Nilianza ujenzi Agosti. Nilijenga msingi kwanza halafu baadaye nikaja kuinua boma. Wakati naanza, nondo zilikuwa Sh20,000 lakini nilipofika kwenye linta na nguzo nikashangaa eti imepanda mpaka Sh29,000, sikuamini,” alisema Jackline.

Kutokana na wasiwasi aliokuwa nao baada ya kuelezwa na mdogo wake anayemsaidia kusimamia ujenzi huo, alisema kuwa alilazimika kwenda dukani ili ajiridhishe akakuta ni kweli.

“Sijui kwa nini bei imebadilika kwa kiasi kikubwa hivi. Yaani ndani ya miezi mitatu inapanda kwa Sh9,000...hii sio kawaida. Sijajua kitu gani kimebadilika mpaka hali ikawa hivyo,” alisema Jacline aliyejitambulisha kama mjasiriamali wa nafaka.

Kwa upande wake, Jimson Kiwango alisema kupaa kwa bei kumemfanya asitishe shughuli za ujenzi, akisubiri zishuke ndipo aendelee na ujenzi kwa gharama ambazo atazimudu kwa kujenga kidogo kidogo.

“Bei zinakatisha tamaa, miezi sita iliyopita wakati najenga msingi, bei zilikuwa za kawaida lakini sasa hazishikiki. Nondo kipindi kile nilinunua Sh19,000 lakini sasa zinauzwa Sh26,000. Tutajenga kweli?” alihoji kijana huyo anayeishi Gongo la Mboto.

Wenye viwanda wafunguka

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Ando Roofing Products Ltd ambao ni wazalishaji wa mabati, Ado Maimu, alisema kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi hasa mabati na nondo kumetokana na kupungua kwa uzalishaji wa chuma nchini China.

Sababu nyingine alieleza kwamba China ambayo ndiyo mzalishaji mkubwa, ilikuwa ikizalisha zaidi na kuuza nje lakini sasa nao wana mahitaji makubwa katika soko la ndani, hivyo sasa wanazalisha ili kutosheleza soko lao.

“Walipokuwa wanauza nje walikuwa wanatoa kwa wauzaji wa nje asilimia 13, ina maana walikuwa wanapata punguzo kwenye suala la kodi, sasa baada ya hiki kilichotokea zile 13 zote zimerudi. Hiki ndicho kitu kikubwa kinacholeta tatizo,’’ alisema.

Chanzo: Mwananchi
 
Na bahati nzuri limekuja na sababu,sasa unfortunately sababu zenyewe ziko nje ya uwezo wa serikali ku control,vitashuka tuu kama sukari na mafuta kwani serikali iliingilia?
 
Back
Top Bottom