Miaka kadhaa nyuma niliwahi kusikia mwanamke mmoja nchini Uganda kajifungua watoto wawili (mapacha) wenye baba tofauti, hali hii ilinishangaza sana.
Hali kama hii iliripotiwa pia Septemba 9, 2022 kwenye jarida la CNBC ambapo mwanamama mmoja kutoka Minerois, Brazil alithibitika kuwa na ujauzito wa mapacha ambao baada ya kupimwa DNA zao ilibainika kuwa walikuwa wa baba tofauti.
Kisayansi, ni kweli kuwa jambo hili linaweza kutokea? Kama jibu ni ndio, linatokeaje?
Hali kama hii iliripotiwa pia Septemba 9, 2022 kwenye jarida la CNBC ambapo mwanamama mmoja kutoka Minerois, Brazil alithibitika kuwa na ujauzito wa mapacha ambao baada ya kupimwa DNA zao ilibainika kuwa walikuwa wa baba tofauti.
Kisayansi, ni kweli kuwa jambo hili linaweza kutokea? Kama jibu ni ndio, linatokeaje?
- Tunachokijua
- Ujauzito hutokea baada ya kuungana kwa mbegu ya kiume na yai la mwanamke, tendo ambalo kitaalam huitwa urutubishaji (Fertilization). Tendo hili hutokea kwenye siku maalum katika mzunguko wa hedhi ya mwanamke.
Baada ya kutokea kwa urutubishaji huu, yai pamoja na mwili wa mwanamke kwa ujumla hutengeneza mfumo imara usioruhusu kutokea kwa urubishwaji wa mara ya pili kwenye yai moja. Ni mwanzo wa takriban siku 280 za kulea ujauzito mpya hadi pindi ambapo muda wa kujifungua utafika.
Katika hali ya kawaida, ujauzito wa mwanamke huhusisha baba mmoja wa mtoto. Hii inatokana na ukweli kuwa wanawake wengi hutoa yai moja lililopevuka katika kila mzunguko mmoja wa hedhi.
Ujauzito wa watoto wawili wenye baba tofauti
Kwa mujibu wa Taasisi ya Afya ya Marekani (NHI), baadhi ya wanawake hutoa yai lililopevuka zaidi ya moja kwenye mzunguko mmoja wa hedhi.
Ikiwa mwanamke atashiriki tendo la ndoa na mwanaume mmoja kisha wakafanikiwa kufanya urutubishaji, baadae mwanamke huyo akashiriki tena tendo la ndoa na mwanaume mwingine baada ya kutolewa kwa yai lingine ndani ya mzunguko huo mmoja, urutubishaji mwingine wa mara ya pili unaweza kutokea.
Tendo hili huitwa Heteropaternal superfecundation, humaanisha kuwa mwanamke amepata ujauzito wa watoto wawili (mapacha), kwenye mzunguko mmoja wa hedhi uliohusisha mayai mawili, ambao baba zao ni tofauti.
Utafiti wenye kichwa cha habari "How frequent is heteropaternal superfecundation?" wa Wenk RE et al, unabainisha kuwa visa hivi huwa havitokei kwa namba kubwa. Mathalani, katika utafiti wao uliohusisha wazazi 39,000 wenye watoto mapacha wasiofanana, ni 2.4% ndio waligundulika kuwa na baba tofauti.
Hivyo, kwa kuzingatia rejea hizi muhimu, pamoja na mazungumzo tuliyofanya na madaktari bingwa wa Masuala ya uzazi, JamiiForums inakubaliana na hoja kuwa hali hii ipo, na inaweza kutokea kwa wanawake wachache sana.