Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Kufujwa ni kitendo cha mpenzi mmoja kuwa na mamlaka aliyojipa dhidi ya uhuru na haki ya mwenzake. Inaweza kuwa ni kusimanga, kukosoa kupita kiasi kumuita mwenzie mjinga, mbumbumbu n.k. Pia naweza kusema ni kile kitendo cha mpenzi mmoja kumuumiza mwenzake kwa kauli zake au kimwili mara kwa mara. Kwa bahati mbaya sana wanaokubali kufujwa ni wanawake ukilinganisha na wanaume. Miongoni mwa matatizo ya ndoa ambayo mtu hashauriwi kuendelea kuyavumilia ni kufujwa. Ndani ya kufujwa kuna maumivu makubwa ya hisia na mwili.
Kuna ufujaji wa aina kadhaa ukiwemo ule ambao kwa mazoea huwa hautazamwi kama ufujaji hasa. Mazoea maana yake ni kwamba, unafanywa sana na ni kama vile jamii imekubaliana nao kwa njia moja ama nyingine, ingawa una maumivu na madhara yakutosha.
Hapa chini nitataja baadhi ya aina za ufujaji:
1. Ufujaji wa kimwili: Huu ni ufujaji ambao mpenzi anatumia nguvu za mwili dhidi ya mwenzake, ambapo mara nyingi, humwacha anayefujwa akiwa ameumia au kumweka katika mazingira ya kuumia. Ufujaji huu hutofautiana kutoka kukwaruzwa kwa mwili au kupigwa hadi kifo kwa mhusika. Na hii hufanyika kwa kupigwa, kusukumana, kumtupa mtu chini, kupiga mateke, kupiga vibao, kuminya, kugonga, kukaba, kutikisa, kung'ata, kubamiza, kubonyeza na kudhuru kwa kutumia silaha, kisu bunduki, bastola, kumwagia mwenzake maji ya moto au mafuta ya moto au wakati mwingine kuchoma nyumba moto wakati mwenzake akiwa ndani amelala…
2. Ufujaji wa kihisia: Kufuja kisaikolojia au kihisia kunaweza kuwa kwa kauli au bila kauli. Tabia zinazooneshwa hapa zinaweza kuwa zimejificha sana kiasi kwamba si rahisi mtu kubaini kwamba kuna ufujaji unaendelea katika uhusiano huo. Ufujaji huu unaelezwa kwamba ni mbaya zaidi ya ule wa kimwili kwani makovu ya ufujaji huenda ndani kwa kina kirefu sana. Ufujaji huu huhusisha masimango, kutisha kwa maneno, uharibifu wa mali za mpenzi, au hata wanyama wa ndani kama paka, ikiwa ni juhudi za mfujaji kumtisha mpenzi ili afuate yale anayotaka. Kwa kifupi tunaweza kusema ni matumizi ya ‘mkwara'. Pia kuna kupiga kelele, kutukana kwa kashfa, majibu ya mkato na dharau, kudhalilisha kwa maneno ya kebehi, kutania kwa lengo la kuudhi na kumbeza mpenzi akiwa peke yake au mbele ya watu wengine wa familia au hadharani….. Pia kukosoa, kutoamini uamuzi wowote au ushauri wa mpenzi na wakati mwingine kumdharau waziwazi, kujitahidi kuthibiti, kumchonganisha mpenzi na ndugu au na marafiki zake, kumdhalilisha mpenzi kwa maneno wakati mfujaji akiwa amelewa na baadaye kusingizia pombe. Lengo la ufujaji wa aina hii ni kumfanya mfujwaji ahisi kushtakiwa na dhamira na kukubaliana na yale anayotendewa na mfujaji.
3. Ufujaji wa kimapenzi: Ufujaji wa aina hii huweza kubainika kwa vitendo kama hivi vifuatavyo: Kumlazimisha mfujwaji kufanya mapenzi nje ya utashi wake, kumlazimisha kufanya ngono isiyo salama, kulazimisha kufanya mapenzi yenye kudhalilisha (hususan kulawiti), kujaribu kumwekea mpenzi mipaka ya uchaguzi wake kimapenzi au uzazi. Pia kukagua simu kuona ni akina nani mpenzi anawasiliana nao, kuulizia habari za wapenzi wa zamani kwa marafiki au ndugu zake. Hapa ndipo ambapo neno, ‘malaya' hutumiwa sana na mfujaji. Kwa kawaida mwanamke anayefujwa anakuwa hana kauli kuhusu mwili wake mwenyewe na suala zima la mapenzi. Mwanaume mfujaji ndiye anapanga lini, kwa vipi na kwa nini tendo la ndoa lifanyike. Ndiye ambaye anapanga lifanyike au lisifanyike. Ndiye ambaye anapanga kuhusu watoto wangapi wapatikane kwenye ndoa na lini wapatikane. Lakini pia tendo la ndoa huweza kutumiwa kumdhalilisha mwanamke. Kwa mfano. Kumwambia mke, ‘unazaa kama panya tu,'au ‘nina wasiwasi mtoto huyu siyo wangu,' au ‘unanizalia wahudumu wa baa tu,' kufuatia ndoa kujaaliwa watoto wa kike mfululizo. Kuna suala la mwanaume kulinganisha mkewe na hawara zake, 'Kwa kweli humfikii fulani kwa vitimbwi vyake kitandani, ndiyo maana na nafikiria kumwoa,' mume anaweza kumwmabia mkewe maneno hayo bla wasiwasi….
4. Ufujaji wa kiuchumi: Huu ni pamoja na kumnyang'anya mpenzi nguvu na uwezo wa kudhalisha, kutumia njia ya wizi au kuharibu pato la mpenzi. Je hujawahi kusikia mume anamkataza mkewe kufanya biashara au ametuma majambazi kuvamia shughuli ya mkewe ya biashara ili asiwe na nguvu ya kuzalisha? Kama hujasikia, kwa taarifa yako tu ni kwamba, mambo haya yapo sana kutoka kwa wanaume wafujaji. Lakini kingine ni pamoja na kumnyima mpenzi kama adhabu au kwa sababu nyingine mahitaji ya msingi kama chakula, nguo, matibabu na kumwachisha mpenzi kazi kwa ushawishi au kwa nguvu.
5. Ufujaji wa kiroho: Ni pale ambapo mpenzi anatumia dini au imani ya mwenzake kumwendesha. Kuna wakati mpenzi anabaini kwamba, kwenye imani yao au ya mpenzi wake kuna kipengele anachoweza kukitumia kumkandamiza mwenzake, ambapo hukitumia. Kwa mfano, kama imani ya mwenzake au imani yao inasema mwanamke amtii mumewe, basi kipengele hicho kitapindwapindwa na mpenzi hadi mfujwaji akubali yale anayotaka mfujaji kupitia kipengele hicho. Lakini pia humzuia mpenzi kushiriki kwenye ibada au maombi au huduma yoyote ya imani yake. Kuzuia huku kunaweza kuwa ni kwa moja kwa moja au kwa mbinu za kulaghai na kukashifu. Mara nyingi hata hivyo kashfa, matusi, kebehi na matumizi ya nguvu hutumika katika suala hili. Kuna wakati watoto hulazimishwa kufuata imani ambayo mzazi mmoja haitaki na ambayo pengine haikuwa imani ya yeyote kati ya wapenzi wawili. Mpenzi mmoja kabadili dini wakiwa tayari kwenye ndoa, halafu analazimisha watoto kufuata hiyo dini yake mpya, bila makubaliano na mwenzake ambaye yeye hajabadili dini. Mara nyingi hii hufanywa na wanawake………. Hii ni aina ya udhalilishaji kupitia dini au imani ambao ni udhalilishaji wa kiroho. Imani inatumika kutoa maumivu kwa mwingine………