Mwalimu Mkuu amuuliza Kikwete-Ukilia, nani atalisimamia Taifa? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mwalimu Mkuu amuuliza Kikwete-Ukilia, nani atalisimamia Taifa?

Discussion in 'JF Chit-Chat' started by SG8, May 18, 2011.

 1. SG8

  SG8 JF-Expert Member

  #1
  May 18, 2011
  Joined: Dec 12, 2009
  Messages: 3,198
  Likes Received: 232
  Trophy Points: 160
  Ukilia, nani atalisimamia taifa?
  [​IMG]

  Paschally Mayega ​

  [​IMG] RAIS wangu moto wanaokwenda nao CHADEMA huko mikoani hivi sasa unatisha, tunaokupenda lazima tukuambie. Wananchi wengi wamekubaliana na yale wanayowaambia.
  Kila wapitapo maandamano yao huwavuta watu wengi sana na mikutano yao hukusanya umati mkubwa wa watu. Watu hao wanakwenda wenyewe mikutanoni. CCM na serikali yake havionyeshi kuelewa au kujua kinachoendelea mikoani!
  Ndugu Rais CHADEMA wanasema suala la kuchakachuliwa kura zao za urais wamemwachia Mwenyezi Mungu kwa maana yeye ndiye mwenye haki ya kuhukumu! Lakini wameapa kuandamana ndani na nje ya Bunge kuhakikisha hali ngumu ya maisha waliyonayo wananchi inapungua makali. Kauli zao zinaonyesha kuwajali Watanzania hasa maskini.
  Wameelekeza nguvu zao katika kuonyesha jinsi wanavyoweza kuwapunguzia ugumu wa maisha Watanzania. Kauli pekee Watanzania wanataka kuisikia kwa hivi sasa kutoka kwa yeyote na wa chama chochote. CCM wao bado wananyukana wao kwa wao. Watakapokuja kumalizana watakuta na urais wenyewe wa 2015 wanaogombania umekwisha chukuliwa.
  Rais wangu kama kuna kosa kubwa kiuchumi ambalo serikali ya awamu ya nne ililifanya mara tu ilipoingia madarakani, ilikuwa ni kuongeza kodi katika nishati ya mafuta. Kosa hili limekuwa chanzo cha mfumko wa bei wa mara kwa mara.
  Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa alifaulu sana katika kudhibiti mfumko wa bei. Leo hii Watanzania wanamkumbuka. Viongozi wa serikali ya sasa hawafanyi lolote kuonyesha kama wana uwezo wa kuukabili mfumko wa bei. Au hata kuonyesha kujali.
  CHADEMA wanasema kama gharama za uchukuzi na usafiri zikiteremka lazima bei za bidhaa na huduma zitateremka.
  Wenzetu wa Kenya walipofikwa na hali kama hii waliilia serikali yao nayo ikapuunguza kodi katika nishati ya mafuta. CHADEMA inaitaka serikali yetu nayo katika Bunge la bajeti lijalo kupunguza kodi inayotoza katika nishati ya mafuta kwa asilimia hamsini ili kupunguza gharama za uchukuzi na usafiri ambako kutapelekea kupunguza bei za bidhaa na huduma mbalimbali na hivyo kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha.
  Rais wangu itakuwa ni ole wenu CCM kama wabunge wenu hawatatumia busara, wakatumia uwingi wao wakalipinga wazo hili jema! Watakuwa wamejimaliza wenyewe na chama chao! Wananchi watakifuta chama chao katika vifua vyao. Ukiwaacha wabunge, ugumu wa maisha haujawaacha wanachama wa CCM.
  CHADEMA wanasema upungufu utakaojitokeza katika bajeti ufidiwe na fedha itakayopatikana kutokana na kupunguza misamaha ya kodi kwa asilimia hamsini. Maajabu ni kwamba wanaosamehewa kulipa kodi ni wale wenye uwezo mkubwa. Kama ni lazima kuwaumiza wananchi ili mtu awekeze basi ni bora mtu huyo asiwekeze kabisa.
  Ndugu Rais wakati wananchi wanalia kwa maisha kuzidi kuwa magumu kiasi cha familia nyingine kubahatisha mlo mmoja tu kwa siku, viongozi wao wa CCM na wa serikali yao walikuwa ‘bize’ Dodoma wakielekezana.
  Ukiwaona usoni utacheka, wote walihitaji kuelekezwa. Mwenye udhu wakuwaelekeza wenzake pale hakuwepo. Aliyeonekana kuwaelekeza wenzake ndiye aliyekuwa anahitaji kuelekezwa zaidi. Waliouliza hizi semina elekezi zitalipa lini wanauliza kwa niaba ya Wananchi baada ya kuona hazina maana yoyote bali ni ufujaji mkubwa wa kodi ya wananchi. Watu wanakuwa kama hawana dini!
  Semina ilikuwa ni kuwaelekeza mawaziri na manaibu wao. Makatibu wakuu na manaibu wao na viongozi wengine wa kitaifa. Wote hawa wanaishi na kufanya kazi Dar es Salaam. Kilichowapeleka Dodoma ni nini? Wananchi wote niliowauliza kwa nini watu hawa walikwenda kuelekezana Dodoma! Wote walinijibu, “Ili walipane posho!”
  Kwa mawazo yao semina ilikuwa ni sawa na upuuzi wenye lengo la kuchotea fedha ya walipa kodi maskini! Mwingine akasema damu ya tuliowaua Arusha bila hatia imetukimbiza Arusha jiji tulilozowea kusagia kodi ya wanuka jasho bila huruma! Roho zao zilitufuata Dodoma zikimwekamweka!
  Roho za wauaji hukosa amani siku zote za maisha yao. Bado kidogo misafara yetu itaanza kulindwa na vifaru na madege ya kivita. Baada ya hapo na sisi tutawafuata lakini kwa kifo cha mahangaiko sana!
  Rais wangu ulisema mwenyewe uwaziri hausomewi, ni masomo gani uliyowasomesha mawaziri wako kule Dodoma? Watu wazima vipi wafundishwe cha kufanya? Tulidhani walipewa uwaziri kutokana na upeo wao wa kufikiri, kuelewa na kutenda! Mnapeana uwaziri kwa kutumia vigezo gani? Wanaosema serikali ni ya kishikaji wanakosea wapi?
  Ulionekana kulia sana na utendaji usioridhisha wa viongozi hawa. Baba, mzigo huu nani kawatwisha Watanzania? Yeye atakuwa mzigo mzito zaidi? Anapolia mkuu wa nchi nani atasimama ili taifa lipate kupona?
  Kuwafokea viongozi waache uzinzi leo, au ulevi inakatisha tamaa. Tunakuwa kama hatuna kitu muhimu chakuzungumza. Kuwaonyesha kuwa hutaki watumie madaraka yao vibaya ungetokeza siku ile waziri wako alipogeuza kibanda cha kuchukulia fedha ATM kuwa sehemu ya kupigia stori na mashoga zake.
  Mhudumu alipomwambia kuna wananchi wengine katika foleni wanangoja huduma pia, hivyo, ajihudumie ili nao wapate kujihudumia ilionekana kama kamtukana Mtume au Nabii! Wamwabudio shetani kwa uroho wa vyeo na mali hawakujali kama anafamilia, au ana haki ya kujitetea au hata kuonyesha tu kuwa na yeye ni binadamu kama wao, hakuna. Yasemekana alifutwa kazi mara moja!
  Sononeko la mtu huyu na familia yake linamwandama waziri huyu siku zote za maisha yake. Waziri amepoteza mvuto katika jamii huku hukumu toka kwa Muumba wao wote wawili ikisimama juu ya kichwa chake hadi siku yake ya mwisho!
  Rais wangu unaposema waziri aliyeshindwa ajiondoe mwenyewe una maana umeshindwa kuwaondoa? Huku ni kukiri udhaifu. Ndugu mmoja akaniandikia, “Rais Kikwete apewe semina elekezi ili naye ajue wajibu na madaraka yake kama rais mtendaji.
  Amekuwa mtu wa kulalamika watendaji wake wanapoboronga kana kwamba hana uwezo wa kuwawajibisha”. Mwingine akasema Kama Rais hajamwajibisha waziri hata mmoja hapaswi kulalamika. Hakutimiza wajibu wake anapaswa kuwajibika kwa kuonyesha mfano mbaya! Anangoja hata Hussein Mwinyi ajiondoe mwenyewe?
  Mwana mwema Anney Anney kutoka Arusha aliniandikia: “Nasikiliza hotuba ya Rais Dodoma. Analalamika mawaziri hawatoki ofisini. Mbona hatoi mfano wa Magufuli ambaye katika kipindi kifupi ameshazunguka nchi nzima mpaka Pinda akamfuata mpaka Chato! Rais naye akamkamatia Dar es Salaam na kumpiga stop! Sijawahi kumwona rais msanii kama huyu. Semina ya nini si juzi tu alikuwa na ziara wizarani?”
  Watu wako wanasema iweje uwalalamikie viongozi kwa wananchi hali wewe ndiye uliyewateua, pasipo kuwashirikisha? Wanauliza, unataka Wananchi wakusaidieje? Utazungumziaje hadharani udhaifu wa watendaji uliowateua mwenyewe? Hakuna vikao vya baraza la mawaziri? Huku ni kujiumbua.
  Wakaniuliza, “Mwalimu Mkuu, kati yao wale, nani wakuacha uzinzi pale au ulevi na matumizi mabaya ya madaraka? Kondomu za kujamiiana zinatolewa bure. Dawa mseto za malaria wananchi wanauziwa. Rais kuja kwetu na kutumia muda mwingi kulalamika ni kukiri udhaifu. Anaona serikali inamwelemea” Sikuwa na chakumwambia. Baba tusaidie sisi tulio nyuma yako, tuwajibu nini hawa wanaotusonga na maneno kuwa ‘Rais wenu ndiyo mzigo!’
  Kuelekeza viongozi kile wanachopaswa kufanya, na kuwataka kuacha uzinzi na ulevi hadharani kumewaondolea imani waliyokuwa nayo wananchi juu yao! Kunawafanya waonekane wahuni tu!
  Sijawahi hata siku moja kumwambia mwanangu wa darasa la tano kuwa sasa fanya ‘homework’ uliyopewa na walimu wako.
  Anajua wajibu wake, anafanya. Je, huyu si bora kuliko hawa jamaa? Hawa hawajui wajibu wao au hawataki kutimiza wajibu wao? Umefanya vema kuonyesha wazi ubovu wa mawaziri wako. Serikali iliyo na mawaziri wa aina hii lazima iondolewe kabla taifa halijaangamia!
  Wangekuwapo viongozi makini pale, baada ya kushutumiwa kwa aibu vile na kwamba wanautamani urais wake mbele ya wananchi wangejiondoa wenyewe ili kulinda heshima yao. Hawa wanayakubali yote ili walipwe posho. Watanzania wenzangu ‘uchangudoa maana yake nini kama si mtu kukubali kudhalilishwa kwa ajili ya kulipwa posho?’ Tunapowakamata changudoa tuwakamate wote!
  Waliobuni na kuzitekeleza semina elekezi ni wafujaji wa fedha za walipa kodi. Semina hizi elekezi zimethibitisha utupu wa kifikra walionao waandaaji na watekelezaji wake katika muktadha wa uongozi wa nchi.
  Ni watupu na wasiojiweza. Wananchi wangejua kuwa kodi yao itatumika kuwalipa posho viongozi kwa kazi isiyo na manufaa badala ya kununua dawa au kuwasaidia watoto wao wapate elimu bora nina hakika wananchi timamu wote wangekataa kulipa kodi.
  Matumizi haya ya kifisadi ndiyo yanayoongeza hasira katika mioyo ya wananchi, na kuwafanya wawe tayari kuwatimua, iwe kwa mawe, magongo na fimbo mafisadi wote watakaorudia ufisadi wao huo hata kama ufisadi huo utakuwa unaelekezewa katika majumba ya wananchi kama Ikulu au bungeni.
  Kofia mbili siyo kila mtu anaweza kuvaa na zikamwenea. Hili hapa limethibitishwa bila kuacha shaka. Maana yake ni kwamba, moja inapodhalilika kama hivi nyingine isahihishe.
  Kwakuwa serikali mbovu ndiyo iliyokichafua chama chake cha mapinduzi ilikuwa ni busara mwenyekiti wa chama kumwondoa rais aliyeko madarakani na kumwamuru makamu wa rais kuunda serikali ya watu safi itakayokisafisha chama mbele ya Wananchi na kukifanya kikubalike katika chaguzi zijazo.
  Hii ndiyo busara iliyotumika kwa Thambo Mbeki wa Afrika Kusini. Mkiendelea hivi hivi hali ngumu ya maisha waliyonayo Watanzania itawalazimisha kuwaondoa hata kwa mawe na silaha duni kama zilizotumika Zanzibar kumwondoa sultani. Dhiki yao haitawangojea mpaka 2015. Kwa usalama wa chama na kwa amani ya nchi, itafaa kutenganisha kofia. Kama Dk. Willibrod Slaa angepata urais pangetokea mfano mzuri wa hili.
  Rais wangu, wananchi wakiwa bado hawajaipata vizuri sera yenu ya magamba ambayo inaonekana kufa kimyakimya kwa aibu, Fred Mpendazoe amewaambia Watanzania kuwa walioiasi CCM na viongozi wao, na kuiasisi CCJ ni yeye na Nape Nnauye na wenzao wanne ambao bado wako CCM.
  Anasema alikuwa anawaibia siri za vikao vya CCM. Naye Mabere Marando akasema Nape Nnauye aliomba kugombea ubunge katika Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA. Kwakuwa hakuweza kufikia viwango alivyo navyo John Mnyika walimkataa.
  Kama maneno haya ni ya kweli au si ya kweli tafakuri yetu isijiingize huko, ila tuwapime na kuwalinganisha John Mnyika na Nape Nnauye. Upeo wa kufikiri na uwezo wa kuwasilisha kile alicho kifikiri mtu, hawa wawili wanaachana kwa mbali sana.
  Kama CHADEMA wangekosea wakamwacha John Mnyika nina hakika wananchi wa Jimbo la Ubungo wasingekosea.
  Watanzania tunalia viongozi wetu wengi wa kidunia wamepoteza hadhi ya kuwa viongozi. Viongozi waliobaki na hadhi kubwa katika jamii yetu hivi sasa ni viongozi wetu wa dini zetu zote.
  Nape Nnauye pamoja na umri wake, kuwachafua viongozi wetu wa dini tena katika ujumla wao ni kitendo cha kuwakosea adabu.
  Kunaacha shaka kubwa juu ya malezi na makuzi yake kama maadili yalizingatiwa. Wanachama wa CCM Jimbo la Ubungo waliomkataa Nape asiwe mgombea wao wa ubunge, hawakukosea! Leo wangezificha wapi nyuso zao?
  Sasa kama mwenyekiti anamfanya huyu kuwa ndiye kamanda wa kuongoza mashambulizi yake dhidi ya maasimu wake, atavuna aibu na kunywa hasara! Ndugu zangu wanachama wa CCM haya ndiyo maji mnayotaka kuyatumia kusafishia chama chenu? Kumbukeni kuwa Watanzania wanapomdharau huyu kwa kukosa adabu kwa viongozi waadilifu wa dini wanamdharau na aliyemtuma!
  Watanzania wanapokwenda wenyewe katika maandamano na mikutano ya CHADEMA si kwa sababu wanaipenda sana CHADEMA kama chama.
  Wanatafuta mtu au chombo kitakachowaunganisha ili wafikie maamuzi ya pamoja ya kujikomboa. CHADEMA hivi sasa ndiyo inayoonekana kuwaunganisha, lakini CHADEMA ni chama cha siasa.
  Tunisia, Misri na kwingineko wananchi waliamua wenyewe katika umoja wao na kusimama katika jukwaa moja lililowaunganisha bila kujali tofauti zao za kisiasa, kidini au nyingine.
  Nchi yetu sasa inahitaji jukwaa hilo. Wananchi waelewe kuwa hakuna atakayewaletea ukombozi wa kweli. Lazima wajikomboe wenyewe. Waachane na tofauti zao za uchama, udini na vyote vinavyowatenganisha, wazingatie yale yanayowaunganisha wakiwa juu ya jukwaa moja!
  Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema awajalie wana wema waliotokana na udongo wa nchi hii Jukwaa la Mwalimu-MWALIMU FORUM-MWAFO!

  Source: Tanzania Daima Jumatano
   
 2. Tajy

  Tajy JF-Expert Member

  #2
  May 18, 2011
  Joined: Apr 9, 2011
  Messages: 298
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Mpaka nikanywa maji kwanza walau nimalizie kuisoma maana ni somo zuri na semina tosha kabisa kwa kikwete!mwenye akili na upeo wa kuona mbali pamoja na hekima na uchungu wa kodi anayoilipa ataelewa na kuchukua hatua!mwenye zero memory ataleta kashfa!big up!umenifumbua macho
   
 3. Azimio Jipya

  Azimio Jipya JF-Expert Member

  #3
  May 18, 2011
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 3,370
  Likes Received: 14
  Trophy Points: 135
  RAIS anaeleweka.... ... badala ya kuchukua hatua ...ni vilio..

  1. Kuvua gamba angewafukuza watuhumiwa palepale na kukamta mali zao ... na sio kutoa vilio..

  2. Kuwatuhumu mawaziri kuwa ni wavivu, wazinzi nk ...ni kilo kisicho na msingi ..angwachukulia hatua...
   
 4. TITAN

  TITAN JF-Expert Member

  #4
  May 18, 2011
  Joined: Dec 13, 2010
  Messages: 309
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Nduguzangu mliopo kwenye serekali jaribuni ata kufata ushauri wa watu wanaoandika izi Attica's, zinaweza kuwasaidia, awandio wasomi na watu wenye mtazamo wa juu, Mtoa mada nakutakia maisha marefu atimae uone mabadiliko katika nchi yetu. lakini sikuzote waenga walisema SIKIO LA KUFA ALISIKII DAWA
  Mungu ibariki Tanzania.
   
 5. mashikolomageni

  mashikolomageni JF-Expert Member

  #5
  May 18, 2011
  Joined: Jan 5, 2010
  Messages: 1,565
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Hongera mwl mkuu, siku zote nikisoma makala yako naelimika zaidi, kweli rais hapaswi kulia anapaswa kulifanyia kazi taifa lake litokane na shida zake. Mwl kuhusu huyo Nape nadhania anakosa adabu sababu ya malezi yake maana amelelewa na mamake tu uwezekano wa mtoto kulelewa na mzazi mmoja na kuwa na adabu kama hii ya Nape ni mkubwa sana, nadhani ni muhanga wa haki hiyo
   
 6. fredmlay

  fredmlay JF-Expert Member

  #6
  May 18, 2011
  Joined: Apr 30, 2008
  Messages: 1,855
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 135
  Kwani huyu jamaa (Mzee wa kaya) huwa anasoma haya? Au hata akisoma anakubaliana na kilichomo?? Mi naona ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa
   
 7. SG8

  SG8 JF-Expert Member

  #7
  May 19, 2011
  Joined: Dec 12, 2009
  Messages: 3,198
  Likes Received: 232
  Trophy Points: 160
  Mwalimu Mkuu aliwahi kuandika makala moja huko nyuma, "tutakuja kutawaliwa na Rais ambaye hasomi vitabu, anatumia elimu yake ya zamani . Kila kukicha yeye ni kukwea pipa kwenda nje ya nchi". Nadhani alikuwa anazungumzia hiki unachokisema wewe
   
 8. THINKINGBEING

  THINKINGBEING JF-Expert Member

  #8
  May 19, 2011
  Joined: Aug 9, 2010
  Messages: 2,726
  Likes Received: 854
  Trophy Points: 280
  Nakubaliana sana na wewe Mwl.mkuu.Nikiongeza neno NITAPOTEZA LADHA.
  Jambo moja nalijua fika J.K ninayemfahamu mimi hawezi kusoma BARUA NDEFU KAMA HII.
  Tuombe Mungu.
   
 9. Dingswayo

  Dingswayo JF-Expert Member

  #9
  May 19, 2011
  Joined: May 26, 2009
  Messages: 4,011
  Likes Received: 85
  Trophy Points: 145
  Mkuu Gerrard. Naomba u edit hiyo post na kutenganisha paragraphs. Wengine tunapata shida sana ya kusoma kama maandisha yamebanana. Natanguliza shukrani.
   
 10. Manumbu

  Manumbu JF-Expert Member

  #10
  May 21, 2011
  Joined: Oct 28, 2009
  Messages: 1,751
  Likes Received: 15
  Trophy Points: 135
  very good effort...addressed to a wrong person...hence waste of resource. dawa iliyopo ni kubadili uongonzi wetu na kuubadili mfumo mzima wa uwajibikaji wa viongozi
   
Loading...