Mwakyusa:Pombe ina uhusiano na saratani, moyo na magonjwa ya akili

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
KWA Miaka mingi watu wamekuwa wakitumia pombe kama sehemu ya kiburudisho huku wengine wakiamini kuwa inasaidia kupunguza mawazo. Pamoja na imani hizo, wataalamu wa afya wanabainisha kuwa matumizi ya pombe katika mwili wa binadamu yana madhara makubwa.

Akizungumza katika mkutano wa pili wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa anasema pombe ina uhusiano wa moja kwa moja na magonjwa kama saratani, magonjwa ya akili na Ukimwi.

Vilevile pombe inachangia kwa kiwango kikubwa kuwepo kwa vipigo kwa wanawake... “Mtu aliyekunywa pombe huwa hana uchaguzi katika kufanya mambo, ndiyo unakuta wengine wanatukana, wanapigana na wengine kudiriki hata kujikojolea. Vitendo vyote hivi mtu hawezi kuvifanya akiwa hajalewa.”

Anasema pamoja na serikali kuzitoza kodi kubwa kampuni zinazotengeneza pombe lakini bado watu wanaendelea kunywa kama kawaida na yote hiyo ni kutokana na kutokujua madhara yake.

Mtaalamu kutoka Chama cha Afya ya jamii (TPHA), Dk Ali Mzige anasema pombe ina madhara ya aina mbili. Kwanza ni kuathirika kwa mishipa ya fahamu mwilini kote kwa kupunguza uwezo kufanya kazi na pili ni kuungua baadhi ya ogani za mwili hasa tumbo pindi mtu anapokunywa.

Kuathirika huko ni kwa aina nne za wanywaji, hatua ya kwanza ni ile ya kuchangamka, hapa mtu hujisikia mzima zaidi ya kawaida moyo unapiga haraka, tumbo linameng’enya chakula haraka na hamu ya chakula kuongezeka.

Hatua ya pili, mtu akiendelea kunywa anachanganyikiwa na kuzungumza sana, kukosa aibu, utu kubadilika, kutawala tabia za kimwili, hamu ya chakula kuongezeka na hapo ndipo walevi wanapoagiza nyama choma kwa wingi.

“Tunaposema kutawala tabia za kimwili ina maana kuwa mtu anakuwa hana maamuzi sahihi katika maamuzi. Mnywaji akiendelea kunywa pombe hucharuka kutokana na neva zake za ubongo kushindwa kumiliki mwili na mambo yote anayoyafanya huwa hayana utaratibu."

Dk Mzige anasema mnywaji huwa mkorofi na anaongea maneno yasiyo na maana. Baadhi ya wanywaji huchukulia hatua hii kama raha yao. Kinachojitokeza ni kupoteza hamu ya kula.

Hatua ya nne mtu akilewa kupita kiasi huwa hajijui analala fofofo. Huenda akajikojolea au kutapika, inategemea na kiasi cha pombe alichokunywa.

Kwa upande wa ogani, pombe huathiri zaidi viungo vinavyopata pombe nyingi kila wakati. Mfano wa viungo hivyo ni mdomo, koo na tumbo, ambavyo vyenyewe hufikiwa na pombe nyingi.

“Pombe yote mtu anayokunywa hupita katika seli za ini huku zikijaribu kuliondoa ini hilo lakini nazo zinalewa chakari na baadhi zina kufa,” anasema Dk.Mzige.

Anasema mtu akinywa sana seli nyingi zinakufa na mtu akinywa kidogo chache zinakufa kisha nafasi yake inajazwa na nyuzi nyuzi za kovu. Ini huwa na mabilioni ya seli ambazo ni imara, hata mtu akinywa pombe nusu, seli zake bado zitaendelea na maisha, kama inafikia kikomo ini linashindwa kufanya kazi na kusababisha njia za nyongo na mishipa ya damu inaziba. Kila ogani ya mwili inaumia kivyake, lakini tumbo na ini ni mifano wazi.

Dk Joseph Mbatia kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anasema pamoja na madhara yake, mpaka sasa hakuna takwimu sahihi za wangapi wameathirika au wamepata madhara kwa kuwa unywaji wa pombe ni jambo lililokuwepo tangu enzi na enzi.

“Upatikanaji wa takwimu ndiyo utakaosaidia kuionyesha jamii madhara halisi ya pombe, kuliko hali ilivyo hivi sasa maana watu wengi wanaona kunywa pombe ni jambo ambalo lipo na limezoeleka,” anasema na kuongeza:

“Zikiwepo takwimu sahihi zitawasaidia watunga sera kuandaa miswada bora ambayo baadaye inaweza kuwa sheria zitakazotekelezwa katika kudhibiti matumizi ya pombe."

Anasema hii haina maana kwamba sasa hivi hakuna sheria, la hasha, zipo ila utekelezaji wake si madhubuti ni kama hakuna kabisa huo utekelezaji wa sheria ya pombe. Kama ilivyo kwa sigara.

Dk Mbatia anasema, vifo, ulemavu au hasara ya mali inayotokana na pombe ni kubwa ingawa kwa sasa hakuna anayefahamu, kwa kuwa hakuna utafiti unaofanyika.

Kwa upande wake, Dk Bertha Maegga anayeshughulikia masuala ya utafiti kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road anasema pombe ni ugonjwa sugu ambao tiba yake ni sawa na ile ya kisukari, ambapo mgonjwa anatakiwa kufuatiliwa kwa karibu.

Anasema ulevi wa wataalamu wa sekta mbalimbali nchini ni tatizo kubwa hali inayosababisha kushuka kwa imani ya wananchi wanaotegemea huduma kutoka kwao.

Anasema utafiti mdogo uliofanyika kwenye kitengo chake umeonyesha kwamba asilimia kubwa ya viongozi wa maeneo wanaolalamikiwa kwa ulevi ni wa jinsi ya kiume.

Utafiti huo unaonyesha idadi ya walevi kuwa ni asilimia 24 ya watawala kwenye ofisi za umma, asilimia 27 ya wafamasia, madaktari asilimia 20 ambao waliripotiwa kuwa walevi zaidi hali inayotishia usalama wa maisha ya wagonjwa wao.

Anasema kuwepo kwa utafiti wa kina kutasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza madhara ya pombe, ingawa duniani kote hakuna sheria inayombana raia kutotumia kilevi kabisa.
Mwakyusa:pombe ina uhusiano na saratani, moyo na magonjwa ya akili
 
Back
Top Bottom