Hili wengine tuliandika tokea mwaka jana kwamba Mwakipesile hana mpango tena wa kugombea ubunge wa Kyela.
Sihitaji Ubunge Kyela 2010- Mwakipesile
Sunday, 07 June 2009 15:07 Na Mwandishi Wetu Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Bw.John Mwakipesile ametangaza kuwa hana mpango wa kuwania ubunge Jimbo la Kyela mwakani kwani ameridhika na heshima aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete, kumteua Mkuu wa Mkoa huo.
"Hivi ndugu zangu mimi nilikuwa mbunge kwa miaka 10 baada ya kufuatwa na kuombwa, baadaye nikashindwa kwenye kura za maoni,Rais akanipa heshima kuniteua kuwa Mkuu wa Mkoa hadi sasa, nirudi kugombea ubunge kwa ajili ya kutafuta nini? "Alihoji Bw. Mwakipesile hivi karibuni, wakati akizungumza na maaskofu wa madhehebu mbalimbali mkoani Mbeya, waliomtembelea nyumbani kwake.
Bw.Mwakipesile alitoa kauli hiyo wakati akijibu moja ya maswali ya maaskofu hao ambao aliwaalika kwa ajili ya chakula cha jioni na kubadilishana mawazo kuhusu mikakati mbalimbali ya maendeleo mkoani Mbeya.
Askofu huyo alitaka kujua mustakabali wa mkuu huyo wa mkoa kugombea ubunge Kyela kwenye Uchaguzi Mkuu ujao mwakani, baada ya kuwepo uvumi kwamba anajiandaa kurudi tena kupigania nafasi hiyo.
Bw. Mwakipesile alisema sasa ni miaka minne tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na kutokana na mshikamano mzuri na wasaidizi wake, pamoja na wananchi, wamepata mafanikio makubwa hususani katika nyanja ya elimu.
Mkuu huyo wa mkoa ,alisema kuwa alipokea uteuzi wa Rais kwa hofu na heshima kubwa, hivyo anachofanya sasa ni kuhakikisha anachapa kazi ili 'kutomwangusha' Rais Kikwete aliyempa wadhifa huo.
"Maaskofu ninyi ni watumishi wa Mungu, hivyo kama naongopa katika ahadi yangu hii nianguke kwa kuwa hapa nazungumza na Mungu kutokana na uzito wa nafasi yenu. Nasema sina mpango tena kuwania ubunge Kyela kama ambavyo baadhi ya wanasiasa waoga wamekuwa wakinizushia,"alisema Bw. Mwakipesile.
Aliwataka wanasiasa kuacha malumbano yasiyo na msingi na kuchapa kazi waliyotumwa na wananchi na yeye kama Mkuu wa Mkoa, kazi yake kubwa ni kusukuma gurudumu la maendeleo katika wilaya,kata na vijiji vyote vya Mkoa wa Mbeya bila upendeleo wa aina yoyote.
Aliwahakikishia maaskofu hao kuwa kutokana na msimamo wake, hana ugomvi na mwanasiasa yeyote bali na anafanyakazi na wote
kuhakikisha wananchi wanapata maisha bora kama alivyo ahidi Rais Kikwete ambaye ndiye mwajiri wao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwenyekiti wa maaskofu hao, Mhashamu John Mwela, alieleza kufurahishwa na makaribisho ya mkuu huyo wa mkoa na kwamba ni kielelezo cha namna anavyowatambua na kuthamini mchango wao. Walimwahidi kuzidi kumpa ushirikiano mzuri katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Mbeya na Watanzania kwa ujumla.