Mwaka 2018 na Nyaraka 3 za Viongozi wa Dini juu ya Mustakabali wa Nchi yetu

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,880
Mwaka 2018 na Nyaraka 3 za Viongozi wa Dini juu ya Mustakabali wa Nchi yetu: Wakatoliki, Walutheri na Waislam waonya Kuhusu HAKI na Hali ya Uchumi wa Wananchi


Nimekuwa nasoma nyaraka za Viongozi wa Dini zetu Kuu hapa nchini mara Kwa mara Kwa ajili ya kupata mafunzo nikiwa Kiongozi wa Wananchi. Nimeona ni vema kuweka nyaraka hizo zote pamoja ili kuwezesha urahisi kwa mtu mwengine atakaye kuzisoma. Viongozi wetu wa Dini wameongea masuala Muhimu sana kwa nchi yetu yenye kuhitaji kufanyiwa kazi. Viongozi wamesisitiza masuala yanayohusu Haki za Raia na Uchumi wao. Kwa hakika Viongozi wetu wa Dini wamewasemea wengi. Wajibu wetu ni kuyatekeleza maono yao kutoka Kwa Mungu. Nyaraka zao hizi hapa.


Waraka wa Wakatoliki


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa ujumbe wa Kwaresma wa mwaka 2018 ndani yake likitoa msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.


Ujumbe huo ulioandikwa na maaskofu wote 35 wa TEC wakiongozwa na Rais wake, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa upo katika kitabu cha kurasa 20 ikiwa ni maandalizi ya ibada hiyo ya siku 40, kipindi ambacho ni cha mfungo wa sala kukumbuka siku 40 za Kristo kufunga na kwenda jangwani.


Hali ya kisiasa


Katika ujumbe huo, TEC imesema uamuzi wa Serikali kuzuia maandamano, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni kwenda kinyume cha Katiba ya nchi.


Baraza hilo pia limeonya hatua ya Serikali kuvibana vyombo vya habari ikiwa pamoja na kuvifungia kwa sababu mbalimbali.


“Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambamba na kuminya uhuru wa Mahakama na Bunge kwa njia ya kuminya haki wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya kikatiba.”


Alipopigiwa simu ili kutoa maoni ya upande wa Serikali kuhusu ujumbe huo, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema, “Sijaliona bado tamko husika kwa hiyo siwezi kujibu hoja ambayo sijaisoma kwa sasa.”


TEC imetoa ujumbe huo katika kipindi ambacho vyama vya siasa, hasa vya upinzani vikilalamika kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara baada ya Serikali kuipiga marufuku mpaka mwaka 2020, isipokuwa kwa wabunge walioshinda uchaguzi ambao wameruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yao.


Ugumu huo umetajwa na vyama hivyo kwamba unapunguza nguvu ya ushindani kwa vyama vya upinzani kukikabili chama tawala.


“Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge,” unaeleza ujumbe huo.


“Hata hivyo, shughuli za, siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola. Maana yake ni kwamba shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na sheria za nchi.”


Kuhusu vyombo vya habari, TEC imesema Serikali imepunguza wigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari na maoni ya kujieleza na kueleza kwamba kwa ujumla wake, mazingira hayo yatasababisha jamii kufarakana na hata kujenga chuki.


“Kumekuwapo pia hali ya vurugu katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi hizi zinaacha nyuma uchungu, hasira, tamaa ya kulipa kisasi na hata kususia chaguzi nyingine,” unasema ujumbe huo wa TEC na kuonya kuwa kama hali hiyo itaachwa, itakuja kusababisha mifarakano mikubwa itakayobomoa amani na umoja wa kitaifa.


Kiuchumi


Kuhusu uchumi, TEC imetoa mambo sita ya kujiuliza; “Tunazitumiaje mali na rasilimali nyingine tulizokabidhiwa na Mungu kama mawakili wake? Tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia huduma za jamii ambazo Serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi?”


“Wale ambao tu waajiri, tunawajali wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara ya halali? Wale ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali?”


“Wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya kodi, ushuru na ada nyingine kama tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika? Tunaepukaje na kishawishi cha rushwa, hongo, mulungula, magendo au aina yoyote ya ufisadi?”


Kijamii


Katika eneo la kijamii TEC imesema bado kuna kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii.


“Hii inajidhihirisha kwa njia ya uhasama, ugomvi, ukatili kwa watoto na wanawake, ujambazi, na maovu mengine kama hayo miongoni mwa jamii yetu. Kama wamisionari tunaopaswa kuleta habari njema kwa ndugu zetu, kwa nini turuhusu roho ya namna hii ambayo kwa kweli ni roho ya Kaini inayouliza kwa jeuri kabisa,” unasema ujumbe huo.


Mambo matatu


Katika ujumbe wake, Baraza hilo limesema, “Kwa mwaka huu wa 2018 kipindi hiki ni cha kujitafakari mbele ya Mungu na kufanya toba hususan uhai wa amani yetu kwa njia ya matendo ya huruma, haki upendo na amani kwa jirani zetu.”


Limesema hiki ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwake sababu ya mambo matatu;


“Ni katika mwaka huu ambapo Kanisa Katoliki Tanzania linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 2 Oktoba.


Mwaka huu pia utakuwa ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu na Mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi wa Serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji hapo mwakani 2019.”


Kwa sababu hizo tatu, TEC imesema, “Ni vyema tafakari yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna moja au nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo mwanadamu hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali ya binadamu mwenzake. Swali hilo ni Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw. 4:9).


Waraka wa Walutheri


"Fumbua Kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie maskini na wahitaji haki yao" (Mithali 31: 8-9).


KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT)

UJUMBE WA PASAKA KUTOKA BARAZA LA MAASKOFU WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT)

TAIFA LETU, AMANI YETU


A. UTANGULIZI

"Fumbua Kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie maskini na wahitaji haki yao" (Mithali 31: 8-9).


Wapendwa wana KKKT,


Watukuka, watu wote na familia ya Mungu katika Taifa letu, "Amani iwe kwenu!; Kristo Amefufuka (Yohana 20:19).


Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, alipowatokea wanafunzi wake wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, aliwasalimu na kujifunua kwao kwa salaamu ya kuwatakia amani. Wapendwa watu wa Mungu, katika umoja wetu, sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tunawasalimuni nyote kwa kuwatakia amani. Bwana wetu Yesu Kristo Amefufuka kweli kweli - Haleluya!. Yeye ni amani yetu, na pia ni amani kwa watu wote wenye mapenzi mema.


Kwa kufufuka kwake, upendo umeishinda chuki; unyenyekevu umeushinda ubabe; nuru imelishinda giza; haki imeshinda udhalimu; msamaha umeshinda visasi; ujasiri umeshinda hofu; na kwa hiyo uzima umeshinda kifo.


Mwaka 2017, Kanisa letu limeadhimisha miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa. Tukiwa wana Matengenezo tumekumbushwa tena kuwa mwanadamu anaokolewa kwa Neema ya Mungu tu: Wokovu Hauuzwi; Mwanadamu Hauzwi wala kununuliwa; na Uumbaji hauuzwi. Kanisa zima na dunia kwa ujumla tunaitwa kusimama pamoja na kuueleza ukweli huu unaoziweka huru dhamiri zetu (Yohana 8:31-32).


Matengenezo (Reforms) ni dhana ya kibiblia. Tangu zama za Agano la Kale, Mungu kwa nyakati mbalimbali aliteua wajumbe wake kuwasilisha ujumbe wake kwa jamii na kwa watawala wa dunia. Kwa Umungu wake, aliwainua wanawake na wanaume kwa makusudi ya kutoa unabii yaani, ujumbe wa Mungu kwa jamii au watawala. Wakati mwingine aliinua manabii kuwasemea wasiokuwa na sauti. Unabii na Matengenezo ni njia ya Mungu katika kusimika utawala wa haki na unaostawisha uhuru na amani.



Kwa namna ya pekee, manabii kama Daniel, walionya juu ya uongozi unaojenga uhalali wake katika wingi wa watu wanaokubaliana na uongozi huo hata kama ni katika makosa. Haikuwa rahisi kibinadamu kuukosoa mfumo kama huo lakini Mungu alitumia manabii kuzungumza na mfumo wa namna hiyo. Unabii wa Daniel 3:7 unasema, “Kwa hiyo watu WOTE, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari, na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebkadneza aliisimamisha”. Hapa tunaona kosa la kiongozi kutengeneza sanamu, linasababisha kosa la watu wanaokubali kuiabudu hiyo sanamu.


Tumetafakari na kusadiki kuwa, kosa la kiongozi au mfumo, haliwaondolei hatia wanaomfuata kiongozi au kuufuata mfumo, hata kama watu hao walikula kiapo cha kutii maongozi ya kiongozi huyo na mfumo wake. Mbele ya Mungu hakuna ile kanuni ya kuwajibika kwa pamoja. Kila mtu kwa dhamiri yake anawajibika mbele za Mungu. Kwa upande mwingine, pamoja na uwajibikaji wa mtu binafsi, Nabii Ezekieli anatukumbusha na kutuonya kuwa tusipoonya na kusimama katika zamu yetu, hatia na damu ya wasio na hatia, itadaiwa mikononi mwetu (Ezekiel 33: 8-9).


Adhimisho la kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka) na maadhimisho ya miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa, yanatusukuma kutafakari utume wa Kanisa katika jamii kwa nyakati zetu. Tunaalikwa kupeleka ujumbe wa amani kwa watu wote na kusimama kwa ujasiri katika kuwasemea wasio na sauti katika jamii ili kuenzi roho ya Pasaka na Matengenezo katika nyakati zetu. Kama Kanisa na kwa nafsi zetu mmoja mmoja, tunaitwa kwa upande mmoja, kufundisha, kushauri na kutia moyo. Kwa upande mwingine, tunaitwa kuonya, kukaripia, kukemea na kuelekeza kwa uvumilivu wote na upendo (2 Timotheo 4: 1-5).


Wajibu huu kwetu sisi maaskofu ni wito na utume usiokwepeka; na kwa watu wote wa imani, wajibu huu hauna mbadala. Tunaagizwa kuchochea ujenzi wa madaraja ya maridhiano katika upendo na amani, na kuwa kinyume na mifumo yote inayoendeleza chuki na marafakano. Kwa kufanya hivyo, imetupasa kusema wazi wazi ujumbe wa amani, upendo, heshima, utu, ustahimilivu na maelewano.


Mfumo wowote unaojengwa katika utii wa sheria bila upendo; heshima bila uhuru; na amani bila haki, unajengwa katika msingi usio imara. Kupuuza wito huu kuna madhara kwa jamii yetu. Ni sawa na kujenga nyumba juu ya mchanga (Mathayo 7: 26). Tunasihi kwa machozi mengi, tuwe wajenzi wenye akili wajengao nyumba zao juu ya mwamba (Mathayo 7:24). Mwamba tunaotakiwa kujenga taifa letu lenye dini mbalimbali, vyama mbalimbali, na makabila mbalimbali, umetajwa katika sala kuu ya taifa letu, yaani, "DUMISHA UHURU NA UMOJA". Bila Uhuru hakuna umoja uwezao kuleta maendeleo; na bila umoja wa kitaifa, uhuru wetu hauleti amani endelevu. Kwa sababu ya nguvu ya dhamiri safi iliyo dira ya taifa letu, tunalazimika kumtii Mungu kuliko mwanadamu (Matendo 5:29).


B. TAIFA LETU NA AMANI YETU


Tunapoadhimisha sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunatambua kuwa utume wa Kanisa letu katika taifa letu, unafanyika katikati ya changamoto kadhaa. Kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii, linaguswa na changamoto hizo. Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu, sisi maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya salaam za Pasaka, tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.


1. Jamii na Uchumi


Kiini cha Utume wetu katika jamii kinatuingiza kwa nia njema katika maisha ya uchumi na mshikamano wa kijamii. Neno la Mungu linatufundisha kuwa "Mwanadamu hawezi kuishi kwa mkate peke yake" (Luka 4:4). Pia neno la Mungu linatuhakikishia kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alikuja ili tuwe na uzima tele (Yohana 10:10). Tunawiwa katika umoja wetu wa ubaba, kuipongeza serikali yetu kwa jitihada inazofanya kuboresha maisha ya wananchi. Tumeshuhudia jitihada na nia njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa raslimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma za jamii. Hata hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunawiwa kushauri yafuatayo:


Sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo, si washindani wa serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa. Mazingira yasiyo rafiki kuhusu wadau hawa, ni kikwazo kisicholeta mshikamano kati ya serikali na sekta binafsi na mashirika ya dini katika kuleta maendeleo. Jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya serikali na wadau hawa ili kuimarisha mahusiano mema kati ya serikali na sekta binafsi.


Ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe endelevu; jitihada za kukusanya kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi. Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi katika shughuli zao za biashara. Mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi (wafanya biashara) na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza makusanyo ya kodi na kujenga ushawishi wa rushwa. Mfumo wa kodi unaowafilisi wafanya biashara, haulengi kujenga uchumi wa viwanda. Kutokana na ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira; jitihada za wazi na za makusudi zifanyike ili msukumo wa uchumi wa viwanda ufikie matumaini yanayoshikika miongoni mwa vijana wasio na ajira. Sekta binafsi, wawekezaji na wadau wengine, wahakikishiwe usalama wa mitaji

yao kisheria. Hili likifanyika ni kichocheo kizuri cha ujenzi wa viwanda.


IV. Uchumi wa viwanda (vidogo na vikubwa) uendane na uwekezaji katika sekta ya kilimo maeneo ya vijijini. Kilimo na ufugaji ndizo sekta zenye wigo mpana wa viwanda vinavyogusa maisha ya watanzania walio wengi. Utozaji holela wa kodi na ushuru wa mazao unakatisha tamaa wadau wa kilimo. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja, na wakulima/wafugaji na wawekezaji kwa upande wa pili, si kivutio cha

uwekezaji katika sekta ya kilimo.


2. Maisha ya Siasa


Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu. Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo. Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.


Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali huongozwa na katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za taifa). Serikali husimamiwa na bunge huru lililo sauti ya wananchi. Wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya bunge. Bunge halisimamiwi na ilani, chama chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati zetu, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea taifa letu. Baadhi ya matukio hayo ni:


I. Hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.


II. Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa hata uhuru wa kuabudu uko mashakani.


III. Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.


IV. Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na ubabe, vurugu, hila, na vitisho.


V. Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi. Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza migawanyiko.


VI. Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu ambalo ni chimbuko la visasi, kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi katika chaguzi na maisha ya siasa.


VII. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo "Maendeleo hayana chama". Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali.


Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja na amani ya nchi yetu.


3. Masuala Mtambuka


Kanisa ni alama ya uwepo wa utume wa kuleta na kutunza matumaini katika jamii. Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa wajibu wake. Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu tu, ni chachu ya amani na matumaini. Kwa dhamiri safi inayotokana na utambuzi wa "Wakati wa Mungu"(Kairos) katika taifa letu, tunawiwa kutambua masuala mtambuka yanayogusa maisha ya watu kipekee na kwa njia nyingi na kuyatolea ushauri ufuatao:


I. Kuhitimisha mabadiliko ya mara kwa mara katika mfumo wa elimu nchini


ili kuondoa mwanya wa kila mtendaji mkuu wa wizara kuja na sera yake. Elimu ni kitovu cha ustawi wa taifa, kisiwe kinachokonolewa chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake katika mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu.


II. Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na "ubaguzi" kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma shule binafsi na wale wa shule za serikali, n.k. Kwa kuwa huu ni mkopo, jitihada ziwekwe zaidi katika urejeshaji wa mkopo huo kwa kuzingatia kuwa huu ni mkopo kwa mtoto siyo kwa mzazi.


III. Vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji haki vionekane vinatenda haki sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila au kukomoana.


IV. Wajibu wa serikali kikatiba katika kulinda uhai wa raia wake, uonekane

unatekelezwa bila kuacha mwanya wa kuituhumu serikali. Ukiachwa

mwanya katika ulinzi wa uhai wa raia, waweza kutumiwa na mamluki kujichukulia sheria mkononi kwa niaba ya serikali. Damu isiyo na hatia ina madhara kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Mpaka sasa tumeshuhudia umwagaji wa damu unaotusuta sisi sote na mamlaka zote. Mungu anatusuta watanzania kama alivyomsuta Kaini: "Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi" (Mwanzo 4:10).


V. Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni wajibu usiokwepeka kuulinda na kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai umepotea katika mazingira yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa zitolewe kwa wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa serikali na vyombo vyake. Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia, majaribio ya kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na kutolewa taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa hofu na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya uzalendo.


VI. Ili kulipatia taifa letu ufumbuzi wa mambo yote tuliyotaja na kushauri kwa wakati huu na ujao; tunaisihi serikali ya awamu ya tano, kurejea mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya wananchi, iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya Warioba. Watanzania wengi wanaona na kuamini kuwa KATIBA MPYA ina majibu ya kukidhi mahitaji ya taifa letu kwa sasa na baadaye. KATIBA MPYA ni zao la utashi wa Watanzania kupitia tume ya Warioba iliyokuwa na uwakilishi mpana wa taifa letu.


VII. Aidha, tunawashauri raia wema, kwa njia za kidemokrasia kupitia majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai upatikanaji wa KATIBA MPYA. Itapendeza ikiwa KATIBA MPYA itapatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano yatadumu iwapo kuna KATIBA MPYA inayolinda mazuri. Kiongozi mzalendo si mbadala wa KATIBA MPYA. Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la itikadi zote, dini zote, makabila yote na makundi yote chini ya KATIBA MPYA.


C. HITIMISHO


Kufufuka kwa Yesu Kristo ni kiini cha Matengenezo ya Kanisa. Kwamba, katikati ya jamii iliyokata tamaa na kutawaliwa na hofu, Kristo alifufuka na kuleta matumaini mapya. Kwamba, katikati ya wasiwasi wa Kanisa kupoteza nguvu ya utume wake, Roho Mtakatifu aliongoza Matengenezo ya Kanisa. Kwa hiyo Matengenezo ni endelevu katika jamii ya watu na taasisi zao. Muasisi wa Matengenezo Dr. Martin Luther yungali analiwajibisha Kanisa kuzingatia utume wake unaoleta matumaini mapya kila siku. Waliobatizwa wote ni wamisionari tunaotumwa na Bwana wetu Yesu Kristo (Yohana 20:21). Imetupasa kuwa nuru na chumvi ya jamii na kuwa

mawakala wa uhuru, umoja na amani.



Taifa letu lilipata uhuru mwaka 1961 bila kumwaga damu. Roho ile ile ya majadiliano na maridhiano iliyokuwamo ndani ya waasisi wa taifa letu, inatakiwa kila wakati. Uhuru ulioletwa kwa majadiliano, utunzwe na kulindwa bila ulazima wa kumwaga damu ya watanzania. Uhuru na Umoja ndizo ngao zetu zilizolitunza taifa kwa zaidi ya miaka 50.


Sisi tulio maaskofu kwa neema ya Mungu, tunaleta wito kwenu wenye imani katika dini mbalimbali, kuliombea taifa letu. Kuwaombea wote wenye madaraka ili wajaliwe hekima, busara na upendo kwa taifa na watu wake. Kupitia jumuia ndogo ndogo na sharika zote, waombee viongozi wetu ili Mungu awajalie na kuwatunuku kiu ya kutenda haki, kusikiliza kuliko kusema, kuelekeza kuliko kuamrisha, kuunganisha kuliko kutawanya, kupenda watu kuliko kutamani kupendwa na watu, kutamani kutumika kuliko kutumikiwa (Marko 10:45), kuheshimu kuliko kuheshimiwa.


Ujumbe wa Pasaka unatuhimiza kuthamini uhai. Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kufa ili kuhifadhi uhai wetu. Kwa kufa kwake na kufufuka, amekomesha kifo na mawakala wake. Tunaitwa kuthamini uhai na kutoruhusu tena watu kuteswa na kuuawa. Kwa hekima yote na unyenyekevu, tunasihi tena, kwamba ikubalike kuwa hitaji la watanzania walio wengi kwa sasa ni KATIBA MPYA. Katiba Mpya ipatikane ili kukuza na kuimarisha mfumo wa utawala utakaolinda uhai wa watu, raslimali za nchi, tunu za taifa, uhuru wa mihimili ya dola, na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.


Tunawatakia Pasaka njema ya mwaka 2018, na Mungu awabarikini nyote.Ni sisi


Waraka wa Waislam


JUMUIYA NA TAASISIZA KIISLAMUTANZANIA


WARAKA WA EID EL FITR 1439H | 2018


Bismillahir Rahmanir Rahiim


A: UTANGULIZI


Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tunamtakia Rehma na Amani Mtume wake Muhammad (SAW). Waraka huu ni kilele cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Tunamuomba Allah atukubalie saumu yetu. Kuhusu mwezi huo wa Ramadhani Allah anatueleza: “Enyi mlioamini! Mmeandikiwa saumu, kama waliyo andikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”. (2:183). Miongoni mwa umuhimu wa mwezi huu ni tukio la kushushwa Qur’an Tukufu ndani yake kama Mwongozo kwa watu na kipambanuzi cha Haki na Batili. Ni lengo la waraka huu, pamoja na mambo mengine, kuweka msisitizo juu ya upambanuzi wa haki na batili, kama ilivyosisitizwa na Qur’an Tukufu.


Watukufu Waislamu jana Eid mosi na leo Eid pili tunaadhimisha sikukuu hii adhimu. Sisi viongozi wa Waislamu nchini, tunao wajibu wa kuitumia nafasi hii kutoa nasaha kwenu na jamii nzima ya Watanzania kuhusu mambo mema (mambo ya haki), na kuwanasishi kuacha mambo mabaya (mambo ya batili). Miongoni mwa hayo ni Uhuru,

Haki, Udugu na Amani. Mambo haya ni muhimu katika dini yetu na ni msingi wa ujenzi wa taifa letu kama ilivyotakiwa katika utangulizi wa katiba ya nchi yetu ya mwaka 1977.


Sisi viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu tumeona nchi yetu imeyumba katika hayo. Na kwa sababu hiyo imekuwa kawaida sasa kwa Tanzania kushuhudiwa mauaji ya watu na maiti kutupwa hovyo, utekwaji wa watu, ukamatwaji wa raia wasio na hatia, na baadhi yao wakipotezwa kabisa.


Tunashuhudia watuhumiwa wote wa ugaidi wanakuwa ni Masheikh, Walimu wa Madrasa na Waumini wao. Jambo baya zaidi, ni kesi zao, ambazo karibu zote ni za kubambikiwa na kusingiziwa, hazisikilizwi kabisa – na hivyo wamenyimwa hata nafasi ya kupata haki mahakamani. Imekuwa jambo la kawaida Waislamu kuteswa na kuuwawa bila ya hatia. Serikali inafanya hivyo mitaani na huenda mbali zaidi kwa kuuwa katika nyumba tukufu za Mwenyezi Mungu, Misikiti. Watoto wa madrasa na walimu wao wamekuwa wakivamiwa na vyombo vya ulinzi kama wahalifu, kukamatwa na kuteswa kwa kisingizio cha ugaidi au kutokusajiliwa kwa Madrasa wanazosoma. Imekuwa kawaida kwa viongozi wa taifa letu kutoa amri na matamko yanayokiuka misingi ya haki, utu, sheria na demokrasia.


Zaidi Waislamu ni sehemu ya jamii ya Watanzania, mambo yote ya nchi yetu nasi ni sehemu yake, tunaguswa na changamoto za nchi yetu hatuwezi kujiweka pembeni bila ya kushiriki kuzishughulikia. Katika kutimiza wajibu huo, siku zote tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe hekima na busara, ili atupe maarifa ya kuzitafutia majawabu

changamoto hizo, hasa wakati wa kuunasihi umma na kuwashauri viongozi wa Taifa letu kama tunavyofanya kupitia waraka huu.


Kwa muktadaha huo, Ramadhani 29, sawa na Juni 14, 2018, viongozi wa kiislamu nchini kupitia jukwaa lao kongwe la JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU TANZANIA, tulikutana Jijini Dar es Salaam kujadili na kutafakari kuhusu masuala mbalimbali ya kidini na ya kijamii. Ujumbe huu wa Eid ni matokeo ya kikao hicho muhimu.


B. HAKI NA AMANI


Jamii ya Watanzania imejengwa na wafuasi wa itikadi, imani na mila tofauti. Hata hivyo sote tutabaki kuwa ni watu wa jamii moja ambayo yapo mambo yanayotuunganisha. Kati ya mambo hayo muhimu ni suala la amani na utulivu. Uislamu ni dini ya amani hivyo viongozi wa Waislamu tunao wajibu wa kuimarisha amani kwa jamii yetu, ili kudumisha umoja wetu wa kijamii. Lakini pia tunao wajibu wa kuonya

pale tunapoona kuna dhulma, na hakuna haki, na hivyo kuwepo kwa dalili au viashiria vya kutoweka kwa amani. Sisi viongozi wa Waislamu, tunatambua kuwa uongozi bora, wenye kuheshimu haki na utu wa watu ni msingi madhubuti wa kuongoza maisha ya watu kwa ujumla. Lakini kwa bahati mbaya, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo

kinyume na misingi iliyolilea taifa letu. Baadhi ya matukio hayo ni yafuatayo:


1. Haki ya uhai:


Kwa siku za karibuni nchi yetu imekumbwa na matukio mbalimbali

mabaya yanayotoa viashiria vya haki ya uhai na kuishi kuanza kutoweka nchini. Matukio hayo mabaya na yasiyo ya kitanzania yamehusisha utekaji na uteswaji wa raia, kuokotwa kwa miili ya watu waliouawa ikiwa kwenye viroba kwenye fukwe mbalimbali za mito, maziwa na bahari nchini, kupotea kwa watu mbalimbali huku pakiwa na viashiria vya ushiriki wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kupotea kwao, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kiislamu na viongozi wa kisiasa, hasa wa vyama vya upinzani nchini, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi aidha za kidini au kisiasa, vitisho kwa wote wanaoonekana kuwa na maoni mbadala juu ya uendeshaji wa nchi yetu, ubambikiziaji wa kesi hasa zinazohusu masuala ya ugaidi na

uraia kwa wote wanaoonekana kupingana na serikali, na zaidi matumizi mabaya, na ya nguvu kupita kiasi, ya vyombo vya dola dhidi ya raia.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ichukue hatua madhubuti kurudisha imani ya wananchi juu ya uwezo Serikali wa kulinda haki zao ya uhai na kuishi. Kwa kuwa vyombo vya Dola vilivyopaswa kulinda raia na kufanya uchunguzi juu ya uhalifu navyo ni sehemu ya wanaotuhumiwa na

kulalamikiwa kusababisha kutoweka kwa haki ya uhai na kuishi, ni wakati muafaka sasa wa kuwa na TUME YA KIJAJI ya kuchunguza masuala yote yanayohusu kutekwa, kupotezwa na kuuawa kwa watu, ili ukweli ujulikane na wanaohusika na masuala hayo wachukuliwe hatua. Pia tunashauri Jumuiya ya Kimataifa, Bunge na Taasisi za Kiraia za kutetea haki za binaadamu kuibana serikali kuhusu kuundwa tume hiyo muhimu kwa taifa. Pia tunatoa unatoa rai kwa waislam wote na kila mtanzania kuchukua ahadi, yeye na kizazi chake, kuendelea kuilinda haki hii ya Uhai na Kuishi, yake binafsi, ya jamii nzima, bila kujali imani ya dini au mrengo wa siasa.


2. Haki ya kuabudu:


Sehemu ya jamii nchini, hasa sisi jamii ya waislamu, imeathirika

zaidi na kuminywa kwa haki ya kuabudu nchini, hasa kwa waumini na viongozi wetu kutekwa, kuuawa, kupotezwa, kufungwa, kufunguliwa mashtaka na kudhalilishwa wakiwa katika mikono ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini. Mateso yote hayo huikuta jamii ya Waislamu kwa kisingizio cha mambo ya ugaidi. Yapo matukio kadhaa ya kuonyesha madhila tunayofanyiwa, tukio kubwa zaidi ni la Julai 21, 2017, la kushambuliwa kwa risasi, kuuwawa, kujeruhiwa, kuteswa na kisha kutekwa na kupotezwa kwa waumini 10 wa wakiwa kwenye ibada katika Msikiti wa Ali Mchumo, Kilwa, Mkoani Lindi.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaitaka Serikali iache kutumia kisingizio cha Ugaidi kuminya haki ya kuabudu kwa baadhi raia wake, jambo hili likiendelezwa litachochea uhasama wa kidini nchini na kujenga chuki kati ya jamii inayoondolewa uhuru wake wa kuabudu dhidi ya Serikali. Pia ni muhimu serikali ifanye uchunguzi wa kina juu ya kadhia ya Msikiti wa Ali Mchumo, mpaka leo

waumini wenzetu haijulikani hatma yao, hili ni jambo tete kwetu waislamu, na ni jambo linalojenga chuki na hasira za waislamu dhidi ya Serikali yao. Zaidi Serikali iiandike upya sheria ya Ugaidi, au iifanyie marekebisho makubwa kuondoa vipengele vyote vinavyosababisha haki za raia (hasa za kuabudu) kuvunjwa. Sheria hii ya Ugaidi

ilipokuwa inajadiliwa Bungeni mwaka 2002, Mbunge wa Lindi, Mohamed Abdulaziz alisema yafuatayo: “Sheria hiyo ikipitishwa thamani ya maisha ya mwanadamu haitakuwepo”. Maneno haya yametimia sasa, na kwa bahati mbaya jamii inayoathiriwa zaidi na sheria hiyo ni jamii ya waislamu. Mwisho tunashauri Mahakama,

Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Sheria na Mkurugrnzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kuhakikisha kuwa kesi zote za watuhumiwa wa ugaidi zinasikilizwa kwa haraka na watu hao kuapata haki yao, kwani “Haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa”.


3. HAKI NA UHURU WA HABARI NA KUJIELEZA:


Taifa letu sasa linaelekea katika kutoweka kwa haki na uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kanuni za maudhui mbalimbali zinazoongoza na kusimamia uendeshaji wa sekta ya habari nchini zinatumika zaidi kuua kabisa uhuru wa kupata habari na kujieleza kwa wananchi.


Sisi Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, pamoja na waumini tunaowaongoza, kama sehemu ya jamii ya Watanzania inayopunguziwa uhuru wa kujieleza na kupata habari, nasi ni waathirika wa hali hiyo.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali iwe na uvumilivu wa kusikia hata maoni isiyoyapenda. Jamii inayo haki na uhuru wa kutoa maoni juu ya namna serikali yao inavyofanya kazi zake, maoni hayo yanaweza kutumiwa na serikali ili kuboresha utoaji huduma wake. Lakini pia jamii inao uhuru wa kusoma, kuangalia na kusikiliza naoni hayo ya ukosoaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini. Kupunguza uhuru wa watu kujieleza na kupata habari si njia nzuri ya kuongoza Taifa letu.


4. UHURU WA BUNGE NA MAHAKAMA:


Tumeshuhudia kubanwa na kupungua kabisa kwa Uhuru wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kufutwa kwa haki

ya wananchi kuona matangazo ya moja kwa moja ya wawakilishi wao wakiwa bungeni kama ambavyo ilizoeleka, kisha kwa matendo kadhaa ya Bunge na Serikali yanayopunguza hadhi na uzito wa mhimili wa Bunge kwa nchi. Kwa kiasi fulani Uhuru wa Mahakama nao umepungua mno, utendaji kazi wake na uwezo wake wa kujiendesha kifedha umewekwa mtegoni na Serikali, kwa kuwekewa masharti ya

kumalizwa, kupelekwa kwa haraka au kutolewa kwanza hukumu za madai ya kikodi katika kesi zinazoihusisha Serikali.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ifuate Katiba na Sheria za Nchi, na iache Bunge na Mahakama vijiendeshe na kufanya kazi zake kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria na katiba. Serikali haipaswi kutoa vitisho na maelekezo kwa mihimili hiyo ya nchi yetu. Na pia ni muhimu fedha zinazopitishwa na Bunge kwaajili ya uendeshaji wa shughuli za Mahakama zitolewe kama zilivyopangwa, na zitolewe kwa wakati, bila masharti. Mwisho tunashauri wananchi warudishiwe haki ya kuona moja kwa moja wawakilishi wao wakiwa bungeni kama ilivyokuwa awali.


5. UHURU WA KUCHAGUA:


Tumeshuhudia kukosekana kwa mazingira ya haki na huru ya kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali nchini mwetu. Hali hiyo imetokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC kutokuwa huru, na pia kuendesha na kusimamia chaguzi mbalimbali kwa misingi isiyo ya Haki na Usawa.


Ushahidi ni chaguzi kadhaa za karibuni ambazo NEC kwa Dhahiri walishindwa kuziendesha, na hivyo kusababisha vyama kadhaa kugomea chaguzi hizo pamoja na kutokea kwa vurugu. Sababu kuu ya yote hayo ni NEC kuwatumia wanachama wa chama tawala, walio Wakurugenzi wa Halmashauri, kama wasimamizi wakuu wa chaguzi hizo, kushindwa kuwaondoa hata pale malalamiko ya upendeleo dhidi yao yalipoibuliwa nk. Mambo hayo yote yameondoa dhana ya Uchaguzi wa Haki, Uwazi na Usawa, badala yake ni chaguzi zetu kugubikwa na ubabe, hila, vitisho, vurugu, matumizi makubwa ya nguvu ya dola, watu kujeruhiwa, na hata vifo.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanaznia, tunaishauri Serikali, NEC, Vyama vya Upinzani pamoja na wadau wote, kukaa pamoja kujadili changamoto za mazingira ya sasa ya chaguzi zetu, ili kupata namna bora ya kuwa na chaguzi huru, za haki na zenye usawa. Pia ni muhimu yafanyike mabadiliko makubwa ya Sheria zetu za Uchaguzi, yenye lengo la kuongeza uhuru, uwazi na ufanisi wa NEC. Mabadiliko hayo ya sheria za uchaguzi yahakikishe kuwa muundo wa NEC, upatikanaji wa Viongozi na Watendaji wake, pamoja na uwezo wake wa kuwa na watumishi wake wa kudumu katika ngazi ya Halmashauri vinapatiwa ufumbuzi utakaotoa nafasi ya kuwa na Tume

Mpya Huru ya Uchaguzi.


6. UTII WA KATIBA NA SHERIA:


Tumeshuhudia pia kukosekana kwa utashi wa kutii sheria mbalimbali pamoja na katiba ya nchini yetu, hasa kwa Serikali na viongozi wake. Mifano mikuu ni Serikali kutokuheshimu Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGA’s), kuziingilia, kupunguza uwezo wake wa kujitegemea kimapato, Serikali kufanya matumizi ya fedha za umma kinyume na sheria na nje ya utaratibu wa kibajeti, Serikali kutokufuata sheria na taratibu ilizojiwekea ikiwa ni pamoja au kutosukumwa na udini, itikadi au ukabila katika uteuzi wa viongozi mbalimbali wa Serikali, na

Serikali kutokufuata sheria katika ukamataji na ushikiliaji wa watu mbalimbali unaofanywa na vyombo vya usalama.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali iwe mfano katika utii wa sheria na katiba ya nchi yetu, ili wananchi nao waige mfano huo. Pia ni vyema Serikali iziache Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zifanye kazi zake kwa mujibu wa sheria, iache uingiliaji wake ulio kinyume na sheria na unaoleta

migogoro, pamoja na kuacha kuziondolea uwezo wa kimapato mamlaka hizo kunakorudisha nyuma utekelezaji wa shughuli zake za maendeleo.


7. UHURU WA KISIASA:


Tumeshuhudia kutoweka kabisa kwa Uhuru wa mfumo wa Siasa

za vyama vingi nchini, tangu tuurudishe mwaka 1992. Serikali, kinyume na sheria zetu, inazuia kabisa mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa vya Upinzani nchini, huku viongozi wa Serikali ambao pia ni viongozi wa chama tawala wakiwa na uhuru wa kufanya mikutano hiyo. Zaidi tumeshuhudia viongozi wa kitaifa wa vya vyama vya Upinzani nchini wakizuiwa kufanya ziara za kutembelea wafuasi

wao na hata kutembelea maeneo waliyopewa ridhaa ya kuyaongoza nchini, kinyume na viongozi na wa Chama Tawala walio na fursa ya kufanya yote hayo bila kubughudhiwa. Jambo baya zaidi, tumeshuhudia, kwa mara ya kwanza nchini kwetu, Mbunge wa Upinzani akipigwa risasi akiwa kwenye eneo la Bunge, na mpaka sasa

kukiwa hakuna uchunguzi wowote wa tukio hilo uliofanyika, wala kutiwa mbaroni kwa waliohusika.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanaznia, tunaishauri Serikali kwanza iondoe zuio la mikutano ya hadhara na maandamano ya Vyama vya Upinzani, ambalo ni kinyume cha Sheria na Katiba ya nchi yetu. Pili Serikali, Vyama vya Siasa nchni (Tawala na Upinzani) wafanye “KIKAO CHA MASHAURIANO CHA KITAIFA”, ambacho sisi Viongozi wa dini tutakisimamia ili kujadili kwa kina changamoto za

kisiasa nchini, na kuleta suluhu kati ya Serikali, Chama Tawala na Vyama vya Upinzani nchini, na kuendeleza uhuru wetu wa kisiasa na kidemokrasia wa tangu mwaka 1992.


7. HAKI ZA KIMAHAKAMA:


Tumeshuhudia Viongozi mbalimbali wa Kiislam katika maeneo mbalimbali nchini wakicheleweshewa au kukoseshwa kabisa haki za

kusikilizwa na kuhukumiwa na Mahakama zetu nchini. Mfano hai ni Masheikh wa Uamsho, Masheikh wa Arusha, pamoja na mamia ya waumini wengine waliofurika katika magereza ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na magereza mengine huku kesi zao zikiwa hazisikilizwi kwa miaka kadhaa sasa. Mbaya zaidi mahakama zikikataa hata kusikiliza malalamiko yao juu ya udhalilishwaji na mateso mbalimbali wanayokumbana nayo mikononi mwa vyombo vya usalama na magerezani.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali (DPP) pamoja Mahakama watimize wajibu wake wa kutoa haki kwa watu, matendo haya dhidi ya Viongozi wa Waislam nchini yakiachwa yaendelee, jamii nzima ya Waislam itakosa Imani na Mahakama zetu, jambo ambalo si zuri kwa ustawi wa haki

nchini.


C. JAMII NA UCHUMI

Tumeshuhudia jitihada, ari na nia njema ya Serikali katika ukusanyaji Kodi nchini, usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, kupinga rushwa pamoja kusimamia uvunaji na umilikaji wa raslimali za nchi kwa manufaa ya Taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato na kodi ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma za kijamii nchini. Hata hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunapenda kusema yafuatayo:


1. Kodi:


Yapo malalamiko kutoka kwa walipa kodi nchini, hasa sekta binafsi, juu ya namna ukusanyaji kodi huo unavyofanyika. Maeneo makubwa ya malalamiko hayo yakiwa ni mazingira yasiyo rafiki ya kikodi, ukadiriaji wa kodi kubwa kuliko uwezo wa kibiashara wa walipa kodi, ubabe wa watoza kodi, pamoja na ukomoaji wao kwa wafanyabiashara.


Mamlaka za utozaji kodi nchini nazo zinayo malalamiko mbalimbali

juu ya wafanyabiashara wasio waaminifu na wanaokwepa kulipa kodi, na hivyo kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuboresha huduma za jamii na kuleta maendeleo kupitia mapato hayo ya kodi.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania tunaamini kuwa Wafanyabiashara na Sekta Binafsi kwa ujumla si adui wa Serikali, shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa nao zinapaswa kuboreshwa zaidi ili kupanua wigo wa ajira pamoja na ukusanyaji kodi wa Serikali. Hali ya mahusiano mabaya iliyopo sasa inaua biasahara

zao, na hivyo kupunguza mapato ya Serikali. Tunaamini kuwa mambo yote hayo yanapaswa kuzungumzwa ili kuboresha mfumo mzima wa utozaji kodi nchini. Pia Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania tunaamini kuwa pamoja na kuboresha mahusiano kati ya watoza kodi na walipa kodi, jambo jingine endelevu la kutilia muhimu ni elimu juu ya umuhimu wa ulipaji kodi nchini.


2. SHUGHULI ZA UCHUMI:


Kwa sasa tunaona kuuwa lipo tatizo kubwa la kukosekana kwa ajira nchini, hasa kwa vijana. Tunatambua dhamira ya Serikali ya kuifanya

Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati, unaoendeshwa na viwanda, lakini uchumi huo wa viwanda tunaoujenga bado hatujauhusianisha na sekta za kiuchumi zinazowagusa wananchi wengi wa Taifa letu, ambazo ni kilimo, ufugaji na uvuvi.


Ushauri:


Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ifanye juhudi za makusudi katika kuhakikisha inatoa nafasi zinazoongeza shughuli za kiuchumi nchini, kwa mipango ya miradi maalum, uwekezaji, pamoja na sera za kikodi. Uwepo wa shughuli nyingi zaidi za kiuchumi nchini utaongeza ajira kwa vijana wetu, utaboresha uchumi wa kaya zao, pamoja na kuongeza mapato ya kikodi kwa Serikali.


Mkazo uwekwe katika uendelezaji wa shughuli mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi, kwa kuhakikisha upatikanaji wa mapema, na wa bei rahisi, wa mbegu bora, kutoa elimu ya kilimo, ufugaji, na uvuvi bora, kuongeza uwezo wa uhifadhi na usindikaji mazao, kuweka mazingira ya uwepo wa viwanda vya kuongeza thamani mazao hayo,

pamoja na uhakika wa masoko.


3. NIDHAMU YA MATUMIZI:


Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 imeonyesha kuwa lipo tatizo katika namna Serikali inavyotumia fedha za umma inazozikusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali, hasa matumizi ya nje ya Bajeti pamoja na ukopaji wa fedha zaidi ya ukomo unaowekwa na Bunge. Mambo hayo kwa ujumla wake hayaonyeshi nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, na huwafanya wananchi wahisi kuwa Serikali yao inatumia vibaya fedha zao za kodi, na hivyo kushusha ari na utayari wao wa kulipa kodi.


Ushauri:


Nidhamu ya Matumizi ya fedha za umma imewekewa misingi kwenye Katiba ya Nchi yetu na Sheria mbalimbali. Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ijiepushe na Matumizi ambayo hayakupitishwa na wawakilishi wa wananchi kwenye Bunge. Pia Serikali kutokuwa na maelezo kwa matumizi makubwa ya Serikali kunaondoa imani ya wananchi kwa Serikali kama

ilivyotokea hivi karibuni baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Umma. Serikali ikizingatia sheria kwenye matumizi ya fedha za Umma itaepusha ufisadi mkubwa wa kimfumo uliowahi kutokea kwenye nchi yetu mara kadhaa.


D. KATIBA MPYA IWE MSINGI WA MUAFAKA WA KITAIFA


Waislamu hapa nchini, kama sehemu ya jamii ya watanzania, walishiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandika Katiba mpya ya nchi yetu, mchakato uliokwama kwa sababu mbalimbali.


Ushauri:


Ni ushauri wetu sisi Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania kuwa umefika wakati muafaka sasa kwa Serikali kurejesha mchakato ule wa Katiba Mpya, ili tujenge msingi mpya wa utaratibu wa kisheria na kikatiba wa Taifa letu.


Lakini, Kutokana na uhalisia wa yaliyojiri wakati wa mchakato wa kupata Katiba hiyo mpya, ni dhahiri kuwa ipo nakisi ya kuaminiana kati ya makundi makuu mawili ya wananchi, kundi linalokubaliana na Katiba Inayopendekezwa na kundi linalokubali Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba.


Kwa mazingira hayo, tunashauri kuwa ipo haja ya kuitishwa kwanza kwa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba. Kazi kubwa ya mkutano huu iwe ni kuweka msingi wa muafaka kati ya makundi hayo, na Taifa zima kwa ujumla, juu ya namna njema ya kurejesha mchakato wa Katiba Mpya. Tunaamini mkutano mkuu wa kitaifa wa Katiba ukifanyika utapandisha kiwango cha muafaka hasa kwenye masuala ambayo bado yanabishaniwa au yamekosa muafaka wa kitaifa na yana umuhimu wa kuingizwa, kubakishwa au kutolewa kwenye katiba mpya. Pia mkutano huu unaweza kupendekeza mambo ambayo yataingizwa kwenye marekebisho ya sheria zitakazosimamia

uendelezaji wa mchakato wa katiba mpya nchini.


Mkutano huu uhusishe uwakilishi mpana wa wananchi kutoka makundi mbalimbali yakijamii, kuanzia viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa, Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia, Makundi ya Kitaaluma, Vyama vya Ushirika nk. Lengo likiwa ni kuwa na uwakilishi mpana utakaotoa taswira ya utaifa wetu. Mwisho, sisi viongozi wa dini tuko tayari kuwa daraja la kuwezesha mkutano huo wa kitaifa wa katiba, TUTUMIENI.


E. HITIMISHO


Tunahitimisha salaamu zetu za Eid–l-Fitri kwa kuwatakia Waislamu wote na Watanzania kwa ujumla kheri na fanaka ya sikukuu hii, kuwaomba waendeleze Umoja, Amani na Mshikamano kati yao, pamoja na kubeba mafunzo ya kutenda wema (haki) na kukataa ubaya (batili) yatokanayo na mwezi wa Ramadhani. Zaidi tunawahimiza

kutokukaa kimya wanapoona haki inavunjwa kwani kukemea matendo maovu ni maagizo ya Mtume wetu Muhammad (SAW). Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislamu tunataka Tanzania yenye amani na isiyo na aina yeyote ya ubaguzi, yenye kuheshimu haki na usawa wa binaadamu wote na yenye maendeleo.


Wabillahi Tawfiq


Eid Mubarak
 
Viongozi wa dini si wazalendo,wanatakiwa kusifu tu hakuna kukosoa,kuonya wala kushauri.
 
HAHAHAHA wewe nae bora ukasomee kabisa uchungaji au uaskofu au badili dini kabisa hahahaha........
 
Kama Magufuli atagoma kuwasikiliza hao watumishi wa Mungu wanachoelekeza, basi atakiwa anajitafutia laana. OVA
 
Viongozi wa dini wametimiza wajibu wao, lakini watu wanaovunja sheria na katiba kwa makusudi kwa sababu ni watawala hawawezi kuwasikiliza, ni kama farao, Musa alipotupa fimbo yake, ikawa nyoka na waganga wa farao walifanya vivyo hivyo, lakini nyoka wa Musa aliwameza wale wa farao, basi vivyo hivyo, hawa nyoka wa farao wetu watamezwa na wa Musa wetu its just a matter of time!
 
Uzi mrefu huu,wabongo tulivyokuwa wavivu kusoma,wengine wataishia njiani
 
Anajiita JIWE, na kwa kawaida jiwe halisikii, halizai wala haliendi maliwatoni, iweje lisikie ushauri wa taasisi za kidini?
 
Asanteni viongozi wetu wa dini bila ya kujali tofauti ya dini zenu endeeleni kuwanyoosha hawa viongozi wadhalimu
 
Ukiona viongozi wa dini zote wanapaza sauti, basi ujue kuna shida
 
Back
Top Bottom