Mwageni hisia zenu ndugu Wabunge hakuna cha muongozo -Sitta

Lunyungu

JF-Expert Member
Aug 7, 2006
8,873
1,894
Date::7/13/2009Spika Sitta atoa uhuru zaidi kwa wabunge
spika.jpg
Spika wa Bunge la Muungano, Samuel Sitta, ametoa uhuru zaidi kwa wabunge kuonyesha hisia zao wakati wakichangia hoja bungeni.
broken-heart.jpg
*Ashauri wanasiasa kuwa wenye ngozi ngumu

Na Kizitto Noya Dodoma

SPIKA wa Bunge la Muungano, Samuel Sitta ametoa uhuru zaidi kwa wabunge kuonyesha hisia zao wakati wakichangia hoja mbalimbali bungeni baada ya mkutano wa 15 wa muhimili huo wa nchi kutawaliwa na maombi ya mara kwa mara ya kutaka mwongozo wake dhidi ya kauli zinazotafsiriwa kuwa za kuudhi na za matusi.

Spika Sitta, ambaye amekuwa na wakati mgumu kukabiliana na hisia kali za wabunge katika mkutano unaoendelea mjini hapa kiasi cha kuonekana anapendelea baadhi ya wabunge, pia alisema wanasiasa hawana budi kuwa na "ngozi ngumu ya kustahimili mikwaruzo ya kisiasa" na kwamba wabunge ni binadamu wanaoweza kukasirika na kutoa maneno makali.

Kwa ufafanuzi wake, Spika Sitta alimweka huru mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye Juni 24 aliyaelezea majibu ya Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari, kuwa ni "ya ovyo ovyo", lakini akasema mbunge huyo anatakiwa kumuomba radhi mwenyekiti aliyeongoza kikao hicho, Zuberi Ali Maulid kwa kutotii amri ya kutakiwa kukaa.

Mkutano wa 15 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano umetawaliwa na maneno makali yanayotolewa wakati wabunge wanapochangia bajeti za wizara mbalimbali na maneno hayo yamesababisha baadhi, hasa kutoka CCM na Ofisi ya Waziri Mkuu, kutaka mwongozo wa spika mara kwa mara.

Lakini Spika Sitta jana alisema si maneno yote yanayoweza kuchukuliwa kuwa ni makali na ya kuudhi na hivyo kulazimisha yafutwe au waliyoyatoa waombe radhi.

"Kwa kuwa malalamiko haya yamekuwa yakijirudiarudia na imefikia hatua ya kupoteza maana kamili ya lugha ya kuudhi (unparliamentary language), nimeamua nitoe ufafanuzi na mwongozo kuhusu suala hili," alisema Spika Sitta baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

"Katika Kanuni za Bunge letu, kanuni ya 64 inaainisha mambo yasiyoruhusiwa bungeni katika mijadala. Miongoni mwa mambo yasiyoruhusiwa ni kutumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha wengine.

"Uamuzi kwamba maneno gani ni ya kuudhi na yapi si ya kuudhi uko ndani ya kiti kwa kuzingatia hali halisi ya mjadala; hulka ya mbunge mchangiaji na utamaduni wa mabunge yenye mfumo kama wetu.
Haya yote matatu ni lazima yazingatiwe."

Spika Sitta aliendelea kusema: "Mathalani tumekuwa na mbunge ambaye ana hulka kama ya uchekeshaji. Sasa anapotamka, hata kama neno linakuwa gumu kidogo, sisi hatuwezi kusema kwamba ameudhi. Ni jambo la kawaida kwamba katika mazingira ya pekee pale ambapo mjadala unapopamba moto, mzungumzaji anaweza akajikuta akitumia maneno makali.

"Waheshimiwa wabunge, pamoja na waheshimiwa mawaziri ni binadamu na wanaweza kuwa na hisia kali katika mambo wanayoyajadili. Kwa hiyo kutafsiri kanuni hii inayozuia maneno ya kuudhi kwa wigo finyu, kuna hatari ya kuminya ule uhuru wa majadiliano uliopo katika ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Isitoshe Bunge ni uwanja wa siasa za ushindani ambapo katika kutetea maslahi ya kiuwakilishi, mgongano wa mitazamo na utata wa lugha haiwezi kuepukwa. Ukiwataka waheshimiwa wabunge wazungumze bungeni mithili ya mashahidi mahakamani, utakuwa umeiondoa ladha yote ya mijadala bungeni."

Spika, ambaye ni mbunge wa Urambo Mashariki, alikuwa akizungumza huku akipigiwa makofi na hasa wakati akitoa mifano ya mabunge mengine kadhaa, ambako mawaziri waliwahi kufananishwa na hata na konono aliyechoka, akisema kwa tafsiri finyu yangechukuliwa kama ni ya kuudhi.

Pia alitoa mfano wa waziri mkuu wa Uingereza katika karne iliyopita ambaye aliwahi kuitwa mwizi wa mawazo na akili za wenzake na kwamba maisha yake yote yalikuwa ni ya ubinafsishaji wa maoni ya wenzake. Mbunge huyo alimuelezea waziri mkuu kuwa hakuna mwanasiasa aliyekuwa hodari katika uhalifu wa wizi mkubwa wa ajenda za wengine kama yeye.

"Waheshimiwa wabunge, kwa mifano hiyo, si nia yangu kuwashawishi mtumie maneno kama hayo, au maneno mengine makali na yanayoweza kuumiza wengine," alisema Sitta.

"Hata hivyo, kama nilivyowahi kuwaasa siku za nyuma, mwanasiasa, hasa kiongozi, anatakiwa awe na ngozi ngumu inayohimili mikwaruzo ya maneno makali ya siasa bila ya kuchubuka kwa urahisi.

"Aidha, katika mkutano huu maneno yaliyosemekana ya kuudhi humu bungeni, si makali zaidi kuliko hayo niliyoyanukuu na kwa hiyo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa wahusika wala hawakutakiwa kuyafuta."

Spika aliendelea kusema: "Kwa mfano kumsema mbunge fulani kwamba kasema ovyo ovyo, au hata waziri fulani alaaniwe kwa sababu anajipendelea, haifikii kiwango cha athari cha kutakiwa maneno hayo yafutwe.

"Kikubwa hapa ni kuangalia ikiwa ipo nia mbaya, nia mbaya na ya dhati ya kudhalilisha. Je, anayeongea kwa nia ya dhati anataka kumdhalilisha mwingine."

Akirejea suala la Zitto, Spika Sitta alisema: “Kwa kuzingatia misingi hiyo miwili niliyoieleza, tarehe 24 Juni, 2009 Mheshimiwa Kabwe Zitto hakuathiri kanuni yoyote kwa kutamka kwamba mheshimiwa waziri fulani alijibu ovyo ovyo.

"Tatizo hapa ni kwamba Mheshimiwa Zitto aliendelea kuyakaidi mamlaka ya kiti kwa kauli. Kwa hilo namuagiza amuombe radhi Mheshimiwa mwenyekiti Zuberi Ali Maulid humu bungeni. Amuombe radhi humu bungeni na kwa kufanya hivyo shauri hili litakuwa limefungwa."

Zitto alikuwa akichangia hotuba ya Wizara ya Fedha na Uchumi Juni 24 wakati alipoelezea majibu ya Waziri Sumari kuwa ni ya ovyo ovyo wakati akijibu swali la mbunge wa Karatu, Dk Willibrod Slaa kuhusu kampuni ya Meremeta Gold na kusababisha mbunge wa Nkati (CCM), Ponsiano Nyami kuingilia kati na kuomba mwongozo wa spika kuhusu lugha hiyo ya mbunge wa Chadema.

Pia mbunge wa Nzega, Lucas Selelii aliliombea Baraza la Mawaziri lilaaniwe kwa kuwa limezidi kujipendelea, wakati akichangia hotuba ya bajeti kuu kuhusu mgawanyo wa fedha za miradi ya barabara.

Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa alitaka maelezo ya spika kuhusu kuhalalisha matumizi ya maneno yanayoonekana ni makali, akisema mengine si ya utamaduni wa Watanzania, ambao alieleza kuwa wanaeleweka duniani kote kuwa ni watu wa amani.

Lakini Sitta alimjibu kuwa hawezi kutoa mwongozo mwingine na kwamba "anayetazamia kwamba mazungumzo humu yawe kama ya mashahidi mahakamani, basi hapa sio mahali pake. Maana yake siasa ni mikiki mikiki."
Alisema: "Sasa jambo la kweli umelizungumza mwaka wa kwanza, halikutekelezwa, mwaka wa pili; unakaribia kupigiwa kura, halafu ulizungumze tu kama vile ni jambo la kawaida; ohn samahani. Hakuna kitu cha namna hiyo."
Tuma maoni kwa Mhariri
 
Back
Top Bottom