Mwafrika Utamjua anapohama

mchonga

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,233
247
mjengwa-jamiibc.jpg


Na Maggid Mjengwa

Disemba 29, 2010

UKITAKA kumjua Mwafrika, basi, mwangalie siku anapohama. Ndivyo tulivyo. Hata kwenye uongozi, ni hivyo hivyo. Mwangalie kiongozi wa Afrika anapoingia na anapotoka kwenye madaraka.

Ndiyo,; hana tofauti sana na Mswahili anayehama kutoka Mwananyamala kwenda Magomeni. Mswahili wa Mwananyamala, hata kama atahakikishiwa, kuwa anakohamia Magomeni vyumba vyote vina taa za balbu na pazia za madirishani na milangoni, bado, Mswahili huyu atahakikisha, kabla ya kuhama, anang’oa balbu na pazia zote kutoka nyumba anayohama. Mpangaji mpya atakayekuja atajua mwenyewe! Huyo ndiye Mwafrika, ingawa si wote, hata ukimchanja kwenye damu yake, utakuta chembe chembe za ushamba uliochanganyika na hila.

Hakika, hizo ni hulka za Mwafrika, hata azaliwe na kukulia Ulaya au Marekani. Si tumesikia majuzi, Waziri aliyepoteza ubunge alihakikisha anahamisha mpaka pazia kutoka kwenye ofisi ya mbunge jimboni kwake. Naambiwa, kuwa Waziri huyo kakulia Marekani. Kumbe, kukulia Marekani hakumwondolei Mwafrika hulka zake.

Watanzania tumefanya kosa kubwa. Ni pale tuliporuhusu mfumo wa vyama vingi bila kufanya marekebisho makubwa katika Katiba. Maana, katika nchi zetu hizi, uongozi umekuwa wa awamu. Kiongozi anaingia madarakani na kukaa kwa miaka mitano mpaka 10. Kwa Mwafrika, hapa ina maana ya kuhamia na kuhama kutoka nyumba za mamlaka. Ndiyo, tumejikuta tunaingiza wapangaji kwenye nyumba zetu bila kuwekeana mikataba. Na kama kuna mkataba, basi umeandikwa na mpangaji mwenyewe. Hapo utatarajia nini?

Katiba iliyofanyiwa marekebisho makubwa ingetusaidia kwenye kuwadhibiti ’ wapangaji’ wetu kwa maana ya viongozi tuliowapa dhamana za uongozi. Badala yake, leo Afrika utakumkuta kiongozi anayejigamba hadharani, kuwa ameukwaa uongozi kwa vile ni swahiba na kiongozi mkuu. Kwamba ana miaka mitano au kumi ya ’ulaji’. Maana, hata jirani zake watasema ’ jamaa kapata ulaji’. Na magazeti pia yataandika hivyo, kana kwamba uongozi una maana ya ulaji na si utumishi wa umma.

Na Afrika wapangaji waliongia kwenye nyumba (mamlaka) kwa staili hiyo huwa wagumu sana kutoka hata pale wenye nyumba wanapoona wakati umefika wa kuwaondoa. Wamekwishakuonja tamu ya madaraka. Na kama wataondoka, basi, watataka wao waingize wapangaji wapya wa kulinda maslahi yao. Hawataki kazi hiyo ifanywe na wenye nyumba kwa maana ya wananchi wenyewe. Angalia mfano wa Laurent Gbagbo wa Ivory Coast, kuna mifano mingi mingine.

Tatizo ni sisi Waafrika kukosa imani na Waafrika wenzetu tuliowaweka madarakani. Kikubwa ni kukosekana kwa maadili ya uongozi. Viongozi Afrika wamekuwa ni watu wenye tamaa ya madaraka na mali. Usipokuwa na katiba yenye kuwadhibiti wanapokuwa madarakani, basi, nchi wanaigeuza ’ shamba la bibi’. Kama mbweha, watakula minofu huku wakifuta damu midomoni. Ndiyo, watakula wakilindana, kwa katiba waliyoiandika wenyewe.

Kwa baadhi yao, miaka mitano au 10 kwenye uongozi ina maana ya kujilimbikizia mali, kana kwamba nchi nayo inahama baada ya miaka 10. Na siku za kuhama madarakani zikikaribia, itaongezeka, kasi ya kuvuna vilivyobaki kwenye ’ shamba la bibi’. Yale yale ya Mswahili anayehama Mwananyamala. Watakaokuja watajua wenyewe!

Swali ni je, Waafrika tuweje? Ni swali la kifalsafa. Inahusu virtue, kwa maana ya maadili na kutenda yalo ya haki. Kutenda yalo mema. Mtu mwenye maadili mema utamwamini, ndivyo pia wasemavyo Waingereza; a virtuous person is someone you can trust.

Mzazi anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kisiasa anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kidini anapaswa kuwa a virtuous person, Mwandishi wa habari anapaswa kuwa a virtuous person, vivyo hivyo mwalimu.

Kwa hilo la mwisho, mahusiano ya mwalimu na mwanafunzi kati ya Mwanafalsafa Socrates na mwanafunzi wake Plato yasingepata umaarufu yaliyonao sasa kama Plato angebaki kuwa ‘mwanafunzi’ tu. Kubaki kuwa kivuli cha mwalimu wake Socrates. Na Socrates alitambua, kuwa jukumu la mwalimu ni sawa na la mkunga. Mwalimu ni mkunga.

Katika mijadala ya siku hizi tunaona hata wale wanaojiona ni viongozi wasivyo tayari kukosolewa. Wasivyo tayari kuyaona mapungufu yao. Inasikitisha, kuona baadhi ya viongozi hawa ni vijana sana. Wamekuwa wabinafsi zaidi huku wakijiita ni viongozi. Wanajiita viongozi ilhali, kwa namna nyingi, hawawatendei haki wanaowaongoza, wanatanguliza zaidi tamaa ya mali na mamlaka.

Yumkini, kiongozi mtenda maovu kwa watu wake ni ama mjinga au mgonjwa. Kama ataambiwa bayana, kuwa anatenda maovu, au ana mapungufu ya kiutendaji, basi, huenda tutamsaidia kujirekebisha. Lakini, kamwe usishangae, kama kiongozi huyo atatingisha mabega na kucheka tu. Atacheka na kutushangaa siye tunaomkosoa.

Katika machapisho yake ya "Republic", yaani , "Jamhuri", Plato anazungumzia kwa kina juu ya ubinafsi na maadili. Je, kuna sababu gani nzuri na za kimsingi za kuwa mtenda haki na si kinyume chake, yaani mtenda maovu? Glaucon, ndugu wa Plato anajibu; "Binadamu wote kwa asili yetu tu wabinafsi, tunajijali sisi wenyewe kila tunapopata nafasi ya kufanya hivyo. Bila kujali kama jambo hilo si la haki kiasi gani kwa wengine. Lakini, kwa bahati mbaya, nasi pia hufikwa na hali kama hiyo kwa kufanyiwa yasiyo haki na wengine. Jambo hilo huwa si la kufurahia." Anasema Glaucon.

Katika jibu la Glaucon, Plato anatafuta namna ya kuikabili hali hiyo. Na ubinafsi wa viongozi Afrika huchagizwa na ulevi wa madaraka. Walevi wa madaraka wako dunia nzima. Katika nchi za wenzetu, wao walau wana njia za kuwadhibiti, kupitia Katiba zao. Lakini, Afrika ni bara lenye kuongoza kwa kuwa na walevi wengi wa madaraka.

Katiba zetu tulizorithi kutoka kwa wakoloni zinachangia kuongeza idadi ya walevi hawa wa madaraka. Ulevi wa madaraka Afrika ni sehemu ya jibu la swali; Kwa nini sisi ni masikini?”

Hivyo basi, ili kuwapo na mazingira ya kuishi kwa amani na usalama ni vema, kwa mujibu wa mwanafalsafa Plato, kukawapo na taratibu za kuishi kistaarabu. Ndipo hapa dhana ya kuwapo kwa Mkataba wa Kijamii (Social Contract) ikaingia akilini kwa mwanadamu. Ndiyo chimbuko la katiba za nchi. Chimbuko la misingi ya utawala bora.

Tunaumaliza mwaka huu na mjadala wa Katiba mpya. Madai ya Watanzania kupata Katiba mpya ni madai muhimu na ya kihistoria. Maana, mwaka kesho nchi yetu inatimiza miaka hamsini tangu tupate Uhuru. Ni kitu kikubwa kwa nchi yetu.

Fikiria. Kijana wa Kitanzania aliyekuwa na miaka 30 siku ya Uhuru, kama yuko hai, basi, mwaka ujao atatimiza miaka themanini. Naamini, hakuna zawadi kubwa tutakayojipa Watanzania katika kusheherekea miaka 50 ya Uhuru kama kuanzisha mchakato wa kuifanyia marekebisho makubwa Katiba.

Na Watanzania wenye mapenzi na nchi yenu, msikae mkafikiri, kuwa madai ya kupata Katiba mpya ni kazi nyepesi. Ni kazi ngumu sana, hata kama mnaowataka wawasaidie kupata Katiba hiyo ni Waafrika wenzenu na si wakoloni.

Ilivyo Afrika, kwanza mtaletewa na walio kwenye mamlaka, ’Katiba mpya’ iliyofanyiwa marekebisho madogo kwa maana katiba iliyoongezewa viraka. Haitawafikisha kwenye uchaguzi salama. Kuna kuandamana na hata watu kufa kutakakofuatia. Kuna akina Ocampo wa Mahakama za Kimataifa watakaokuja kuwanyofoa wahusika wa vurugu zitakazozua mauaji ya raia.

Kisha itakuja Katiba mpya. Ni njia mbaya na ya kusikitisha, lakini inaepukukika, kama kuna utashi wa kisiasa. Ndiyo, Afrika kudai Katiba mpya yaweza kuwa ni kazi ngumu kuliko kudai uhuru kutoka kwa mkoloni.

Hata hivyo, wahenga walinena; "Kazi ngumu ianze!". Kama kazi ya kudai Katiba mpya tutaianza sasa, ina maana, kuwa kama ni kazi itakayochukua miaka 20, tutakuwa tumebaki na miaka 19. Na nani ajuaye, kwa vile madai ya Katiba mpya ni madai ya haki, kama sauti za wenye kudai zitakuwa nyingi, upo, uwezekano wa kuipata Katiba Mpya ndani ya miaka mitano ijayo. Na hapa ielekewe, Katiba iliyofanyiwa mabadiliko makubwa nayo ni Katiba mpya, na ndiyo yenye kuhitajika kwa sasa. Ndiyo, kuipata ni kazi ngumu. Kufanikisha kuipata ni kuianza kazi hiyo, sasa.

Heri ya Mwaka Mpya.
 
Back
Top Bottom