Mwafaka ndiyo pekee utakaohalalisha Katiba Mpya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mwafaka ndiyo pekee utakaohalalisha Katiba Mpya

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mwanajamii, Nov 17, 2011.

 1. Mwanajamii

  Mwanajamii JF-Expert Member

  #1
  Nov 17, 2011
  Joined: Mar 5, 2008
  Messages: 7,080
  Likes Received: 15
  Trophy Points: 0
  KINACHOENDELEA ndani ya Bunge la Muungano linalokutana hivi sasa mjini Dodoma kujadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 kimewatia hofu kubwa wananchi kiasi cha wengi kuhoji nini hasa utakuwa mustakabali wa taifa letu. Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba, badala ya kuujadili muswada huo katika muktadha wa kupata mwafaka na maridhiano ya kitaifa, wabunge wametofautiana vikali kiasi cha wabunge wa Chadema na baadhi wa NCCR kususia mjadala huo na kutoka nje ya Bunge.

  Kitendo cha wabunge wa Chadema na baadhi wa NCCR kutoka nje kilichochea vitendo visivyotegemewa kutoka kwa wabunge wa CCM na vyama upinzani vya CUF, TLP na UDP. Badala ya kujikita katika mjadala wa ajenda iliyokuwa mezani, wabunge hao waliligeuza Bunge kuwa jukwaa la matusi na vijembe dhidi ya Chadema na wabunge wake.

  Kila mbunge aliyesimama kujadili muswada huo alitumia muda mwingi kutoa kauli za kuudhi na zisizokuwa za kibunge dhidi ya chama hicho au wabunge wake, huku wenyeviti wa vikao hivyo wakikaa kimya bila kukemea vitendo hivyo au kuwataka wabunge hao wafute kauli zao. Katika kikao cha jana asubuhi, kwa mfano, mmoja wa wabunge hao aliwaita wabunge wa Chadema ‘waovu', lakini Mwenyekiti wa kikao hicho alikaa kimya.

  Tungependa kutoa hadhari kwa wabunge wote kwamba, vitendo vya aina hiyo vinalidhalilisha Bunge mbele ya wananchi. Kuzomeana na kutoleana matusi badala ya kutoa hoja zenye mashiko kwa lengo la kuuboresha muswada huo ili hatimaye taifa letu lipate katiba nzuri itakayolinda matakwa ya wananchi wote, kunachafua mchakato mzima wa kupata katiba hiyo.

  Ingefaa wabunge na viongozi wa Serikali watambue kwamba, katika kuandika katiba mpya (constitution making) mahali popote duniani, wanaobeba dhima ya kusimamia mchakato huo hulazimika kuhakikisha mwafaka wa kitaifa unapatikana katika kila jambo linalojadiliwa kwa kuzingatia dhana kwamba kila wazo ni muhimu katika mchakato huo. Vinginevyo, katiba inayopatikana hukataliwa kwa sababu huwa siyo ya wananchi, hivyo hukosa uhalali (legitimacy). Kwa maana hiyo, juhudi za makusudi hufanywa kuhakikisha makundi yote yanasikilizwa bila ubaguzi wowote.

  Ndiyo maana tunasema kwamba hoja zilizotolewa na makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwamo wanaharakati zilipaswa kusikilizwa na kupewa uzito stahiki badala ya kubezwa. Kwa mfano, hoja kwamba muswada huo haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili bungeni kama ilivyofanyika ilikuwa ni hoja yenye uzito mkubwa kwa kuzingatia ukweli kwamba, marekebisho yaliyofanyika kwenye muswada huo baada ya kuondolewa bungeni mara ya kwanza yalikuwa makubwa mno, hivyo muswada huo ulibidi usomwe mara ya kwanza ili upelekwe kwa wananchi waweze kuujadili.

  Bunge lilipourudisha muswada huo serikalini ili, pamoja na mambo mengine uandikwe pia katika lugha ya Kiswahili, wananchi waliona hatua hiyo kama fursa pekee ya kuwawezesha kuujadili kikamilifu na kwa uelewa mkubwa. Serikali na uongozi wa Bunge wamefanya kosa la kudhani kwamba kitu muhimu zaidi kwa wananchi ni kutoa mawazo kuhusu katiba wanayoihitaji badala ya kujadili muswada wa namna ya kukusanya maoni ya wananchi hao.

  Mambo mengine yaliyohojiwa na makundi ya kijamii ni pamoja na madaraka makubwa aliyopewa Rais katika mchakato wa kupata maoni ya wananchi. Yeye ndiye ataunda vyombo na kuteua watendaji wa kusimamia mchakato huo. Licha ya kuteua wajumbe 116 watakaoungana na wabunge wa Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunda Bunge la Katiba, Rais pia anapewa mamlaka ya kutoa hadidu za rejea. Baadhi ya vipengele katika muswada vinampa mamlaka ya kufanya kama anavyoona inafaa.

  Hali hii bila shaka inahitaji mjadala mzito. Hofu yetu ni kwamba, iwapo Bunge litaingia katika mtego wa kushikilia dhana ya wengi wape, nchi yetu itaingia katika mzozo mkubwa. Fursa ya kupata mwafaka na maridhiano bado ipo. Kinachohitajika ni ujasiri wa viongozi wetu kufanya hivyo.


  mwananchi.


  [​IMG] [​IMG] [​IMG] [​IMG] [​IMG] [​IMG] [​IMG] [​IMG] [​IMG] [​IMG]
   
Loading...