Muungano wa Wafanyakazi Uingereza walia na mfumo wa teknolojia wa ufahamu bandia katika ajira

Sam Gidori

Verified Member
Sep 7, 2020
93
150
Muungano wa Wafanyakazi nchini Uingereza umeonya kile ilichokiita 'mwanya mkubwa' katika sheria za ajira na matumizi ya teknolojia ya ufahamu bandia (AI) katika mchakato wa ajira.

Kutokana na mabadiliko ya teknolojia yanayoruhusu kuajiriwa au kufukuzwa kazi kwa mfumo wa kompyuta, Muungano huo unataka kuwepo kwa sheria zinazosimamia mchakato huo ili kutetea haki za wafanyakazi.

Muungano huo unataka kuwepo kwa sheria inayoweza kuhakikisha kuwa maamuzi makubwa yanayoathiri maisha ya mfanyakazi yanasimamiwa na mwanadamu badala ya kuachiwa mfumo wa kompyuta pekee.

Katibu Mkuu wa Muungano huo amesema mfumo wa ufahamu bandia unaweza kutumiwa kuongeza ufanisi katika kazi lakini si wa kuutegemea kufanya maamuzi yenye kuathiri maisha ya wafanyakazi moja kwa moja. Ametahadharisha kuwa matumizi ya ufahamu bandia yanaweza kusababisha kuongezeka kwa ubaguzi hasa kwa wale wasiokuwa katika mfumo wa ajira rasmi.

Taasisi nyingi za kibiashara zinatumia mfumo wa ufahamu bandia kuendesha mifumo ya ajira, ikiwamo Uber ambayo hutumia mfumo wa ufahamu bandia kuwapangia madereva wake kazi au Amazon ambayo hutumia mfumo huo kuwafuatilia wafanyakazi wake. Zipo pia taasisi zinazotumia mfumo huo kupunguza idadi ya waombaji wakati wa usaili katika mchujo ili kuwapata waombaji bora zaidi.

Lakini mfumo huo umetajwa kuwa na kasoro. Kampuni ya Teknolojia ya IBM iliachana na matumizi ya mfumo wa ufahamu bandia kwa kile ilichokitaja kuwa ni wa kibaguzi baada ya mfumo huo kushindwa kutambua sura za wafanyakazi wa jamii nyingine tofauti na weupe kutokana na kuwa mfumo huo ulikuwa umefundishwa kutambua sura za watu weupe pekee.

Mfumo huo pia umelalamikiwa na wafanyakazi wa Uber kufikisha vyakula majumbani (Uber Eats) kwa kuwafukuza kazi maelfu ya wafanyakazi hata walio na ubora (rating) wa 100% kutokana na kushindwa kutambua sura zao. Uber imekanusha, ikijitetea kuwa kabla ya mfanyakazi kufukuzwa kazi na mfumo wa kompyuta, kunakuwa na usimamizi na uthibitisho wa mwanadamu.

Muungano huo wa Wafanyakazi sasa unataka:
  • Ulazima wa waajiri kuyashirikisha mashirika ya kutetea haki za wafanyakazi pale wanapotaka kutumia mfumo wa ufahamu bandia kufanya maamuzi kuhusu hatima ya wafanyakazi
  • Haki ya kisheria ya kufanya mapitio yanayohusisha mwanadamu katika maamuzi yanayotolewa na mfumo wa kompyuta
  • Haki ya kisheria ya mfanyakazi 'kujitoa kazini' na kutopokea simu au kujibu barua pepe za kazi.
  • Mabadiliko ya sheria ili kuwalinda wale wanaobaguliwa na mfumo wa kompyuta.

Muungano huo unasema kuwa tayari maamuzi mengi na ya muhimu yanafanywa na mashine, na ni muhimu sana kuwepo kwa uwazi, uwajibikaji na usahihi unaolindwa na mifumo ya kisheria dhidi ya teknolojia, na ni lazima kuwepo na mipaka inayopaswa kuheshimiwa ikiwa utendaji wa mwanadamu utapunguzwa katika mifumo ya kazi.

Chanzo: BBC
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom