Muswada Sheria ya Fedha wazua mvutano bungeni.

lodrick

Member
Dec 29, 2010
61
19
MUSWADA wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 jana ulizua mvutano bungeni kati ya Serikali na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na kusababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda kuliahirisha Bunge kwa dakika 10 kuanzia saa 10:00.Spika alifanya hivyo kutokana na mwasilishaji wa muswada huo, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuchelewa kuingia bungeni kwa wakati.

Mara baada ya Spika kuingia bungeni na kukaa kwenye kiti chake, alibaini kutokuwapo kwa Waziri wa Fedha ambaye alipaswa kuwasilisha Muswada wa Sheria wa kuidhinisha matumizi ya Sh15.1 trilioni kwa matumizi ya Serikali kutoka Mfuko Mkuu unaoishia Juni 30, 2013 na kuhamisha baadhi ya fedha.

“Hatuelewi sasa kama Waziri wa Fedha amebadilisha utaratibu ama vipi,” alisema Spika na hapohapo Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe alisimama na kutoa taarifa kuwa waziri alikuwa amechelewa kuingia bungeni kutokana na kuchelewa kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Fedha.“Huo siyo msamaha wewe umetoa tu taarifa, lakini huo si msamaha, kwa hiyo nitaahirisha Bunge kwa dakika 10,” alisema Spika.

Baada ya muda huo, Waziri Mgimwa aliingia na kuliomba radhi Bunge kwa kuchelewa kwa kuwa kulikuwa na mambo ya msingi aliyokuwa akiyamalizia.

Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zilisema kuwa kulikuwa na mvutano baina ya wajumbe na Serikali kuhusu kufutwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwenye ununuzi wa migodi, ushuru kwenye vifungashio vya maji ya kunywa na suala la umri wa magari yanayopaswa kuingia nchini.

Chanzo chetu kilisema waliamua kukubaliana kutokubaliana katika baadhi ya vifungu na yalikuwapo mawazo ya kuahirisha Bunge ili liahirishwe leo kwa kuhofia kuwa muda usingetosha.

Hata hivyo, suala la muda lilimalizwa bungeni kwa kutengua kanuni na kupunguza muda wa kuwasilisha, kuchangia na kurejea bungeni baada ya kumaliza kufuturu, ili Waziri Mkuu, Mizengo Pinda awasilishe hoja yake ya kuahirisha Bunge usiku.

Akiwasilisha muswada huo, Waziri Mgimwa alisema baada ya majadiliano ya Wizara na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Serikali imetafakari ushauri, maoni na mapendekezo ya kamati na kuridhia baadhi ya mapendekezo na kuyaingiza katika muswada huo.

Alitaja mapendekezo hayo kuwa ni pamoja na kuongeza ushuru wa bidhaa kwa juisi inayoagizwa kutoka nje ya nchi kutoka Sh83 kwa lita hadi Sh100 kwa lita ili kulinda viwanda vya juisi inayotengenezwa kwa kutumia matunda yanayolimwa hapa nchini.

Pia Serikali imeridhia kurekebisha Kifungu cha 30 (b) cha muswada ili kupanua wigo wa mahakama katika kutoa adhabu ya faini kwa kosa la kuacha kutoa stakabadhi baada ya mauzo.

Chini ya marekebisho hayo, msamaha wa Vat, kwa vifaa vya miundombinu ya maji imerejeshwa kuwa asilimia 100 badala ya asilimia 45 iliyopendekezwa ndani ya muswada kabla ya marekebisho, ili kuwezesha upatikanaji wa maji.

Pia msamaha wa Vat kwa vifaa vya umwagiliaji na vile vya uzalishaji (capital goods) na vifaa vya zimamoto imerejeshwa kuwa asilimia 100 badala ya asilimia 45 iliyokuwa imependekezwa awali.

Katika sheria hiyo, ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi kwenye simu za mikononi umeongezwa kutoka asilimia 10 kwenda 12 na magari yenye umri wa zaidi ya miaka minane yatakayoagizwa kutoka nje ya nchiyatatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 20.

Sheria hiyo imerekebisha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye pombe, vinywaji baridi, mvinyo isipokuwa bidhaa za mafuta ya petroli.

Kodi ya vinywaji baridi ambayo awali, ilipendekezwa kuwa Sh83 kwa lita sasa imebaki kuwa Sh69 iliyokuwa ikitozwa awali huku kodi mvinyo kwa zabibu inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 ikiwa imepunguzwa kutoka Sh420 kwa lita hadi Sh145 kwa lita.

Wakati mvinyo unaozalishwa kwa kutumia zabibu ya hapa nchini ukishuka, mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango cha asilimia 25 umeongezwa kutoka Sh1,345 kwa lita hadi Sh1,614 kwa lita ikiwa ni nyongeza ya Sh269.

Kodi kwa vinywaji vikali imeongezwa kutoka Sh1,993 kwa lita hadi Sh2,392 kwa lita huku kodi ya bia iliyotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa ikipanda kutoka Sh248 kwa lita hadi Sh310 kwa lita ikiwa ni nyongeza ya Sh62.

“Kodi kwa bia nyingine zote imeongezwa kutoka Sh420 kwa lita hadi Sh525 kwa lita ikiwa ni nyongeza ya Sh105 sawa na Sh52.5 kwa chupa yenye ujazo wa nusu lita,” alisema Waziri Mgimwa.Pia Muswada huo wa sheria umefuta ushuru wa bidhaa wa Sh40 kwa lita kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ili kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hapa nchini.

Punguzo hilo limezingatia ahadi ya Serikali iliyotoa mwaka 2011/2012 wakati wa kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2010 kwamba Serikali ingepunguza ushuru huo hatua kwa hatua hadi kuufuta kabisa ndani ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2010/2011.

Pia punguzo hilo la ushuru wa bidhaa Sh40 kwa bidhaa zinazohifadhi muziki na filamu zikiwamo DVD, CD,VCD na mikanda ya video na muziki iliyorekodiwa lengo likiwa ni kuwawezesha wasanii hapa nchini kupata kipato kinachostahili kwa kurasimisha biashara ya bidhaa.

Ili kutekeleza hatua hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaweka stempu kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hiyo uwe rasmi na hatua hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia Januari Mosi, 2013 ili kutoa muda wa maandalizi ikiwa ni pamoja na kuandaa kanuni za utekelezaji wake.Katika mabadiliko hayo ya sheria, kima cha chini cha kutozwa kodi kwenye mapato ya ajira kimeongezwa kutoka Sh135,000 hadi Sh170,000.

Ushuru wa bidhaa kwa magari kwa waliokuwa wananufaika na msamaha huo umefutwa isipokuwa kwa watumishi wa Serikali, miradi ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mkataba, mashirika ya dini, balozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.

Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, iliilalamikia TRA kwa kuendelea kutoza ushuru wa uchakavu kwa magari ya uzalishaji kama matrekta, malori, na mabasi kinyume na matakwa ya sheria.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge pia alishauri umri wa magari yanayostahili msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa miaka isiyozidi 10 urejeshwe, badala ya miaka minane kama inavyopendekezwa na Serikali kwenye muswada huo.

Chenge alitoa ushauri huo, kwa kuzingatia kuwa uwezo wa wananchi kununua gari lenye umri chini ya miaka 10 kuwa mdogo na kuwa sababu zilizoifanya Serikali kutunga sheria hiyo mwaka 2006 bado zina nguvu.

Bunge lilipokaa kama kamati, kifungu hicho kilisababisha mvutano, hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipoingilia kati na kusema kama suala hilo linagusa wabunge wengi Serikali haina pingamizi, hivyo umri huo wa magari unarudi kuwa miaka 10.
 
Back
Top Bottom