Mungai: Takwimu zinathibitisha mafanikio yangu ya Elimu bora

Gelange Vidunda

JF-Expert Member
Aug 18, 2008
314
31
Aliyekuwa Waziri wa Elimu katika Serikali ya Awamu ya 3 ya Raisi Benjamin Mkapa, Joseph Mungai, afunguka na kujadili kwa kina kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika elimu Tanzania wakati wa kipindi chake. Ifuatayo ni nukuhu alipokaa na mwandishi wa habari Luqman Maloto, na kuchapishwa na gazeti la Mwananchi la tarehe 17 Oktoba 2016.


Mungai: Takwimu zinathibitisha mafanikio yangu ya Elimu bora


Luqman Maloto


Wizara ya Elimu kama ambavyo imekuwa ikibadilishwa majina kwa nyakati tofauti na kuunganishiwa majukumu mengine kadiri inavyompendeza Rais wa wakatihusika, ndivyo pia wamepita Mawaziri wengi walioiongoza.

Kila mmoja aliitumikia Wizara hiyo kwa kiwango chake na kutengeneza matokeo yenye kutosha kuupambanua utumishi wake. Wengi wao hivi sasa wameshasahaulika hata kamawaliwahi kuongoza Wizara hiyo.

Kuanzia mwaka 2000 mpaka 2005, katika muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Tatu, iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa, aliyebeba dhamana ya elimu nchini alikuwa Mbunge wa Mufindi Kaskazini wakati huo, Joseph Mungai.

Ni takriban miaka 11 sasa tangu aondoke Wizara hiyo, wakati huo ikiitwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, lakini bado jina la Mungai linatajwa kwa mabadiliko makubwa aliyoyafanya wakati wake.

Wadau wanamtupia lawama kwa kufanya mabadiliko makubwa ya elimu bila kutumia mtindo shirikishi kwa wataalam na wadau wengine wa sekta ya elimu. Anasemwa kwa kubadili mitaala, kufuta michezo ya Umiseta na Umitashumta, wadau hawaishii hapo wanamsema kuwa yeye ndiye chanzo cha mdororo wa sasa wa elimu nchini.

Hivi karibuni, mwandishi wa makala haya, alifanya mahojiano na Mungai ambaye ameweza kujibu maswali yote aliyoulizwa kuhusiana na lawama zote zinazoelekezwa juu yake. Kila jambo ambalo amewahi kushutumiwa amejilibu akiwa naVitabu pamoja na Nyaraka mbalimbali zenye takwimu kuthibitisha anachokizungumza.


Swali: Mheshimiwa Mungai unatupiwa lawama nyingi kwamba wakati wa uongozi wako ukiwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, ulikuwa unajiamulia kufanya mabadiliko ya elimu bila kutumia njia shirikishi, hilo unalizingumziaje?

Mungai: Tuhuma hiyo haina ukweli wowote. Mabadiliko na Maendeleo ya Elimu hayawezi kufanywa na mtu mmoja. Yanahusu wadau wengi ambao wametamkwa wazi katika Sheria ya Elimu. Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu, ubora wa elimu husimamiwa na Kamishna wa Elimu kupitia Nyaraka za Elimu.

Sera ya elimu husimamiwa na Waziri wa Elimu kupitia Sheria Ndogo au Kanuni za Elimu ambazo hutungwa na Waziri; ambaye anawajibika kwa Rais na pia kwa Bunge. Kwa hiyo Waziri hawezi kuendesha Elimu bila kujali Sheria, Bunge na maelekezo ya mheshimiwa Rais na uamuzi wa Baraza la Mawaziri.

Aidha Sheria ya Elimu inamtaka Waziri wa Elimu aendeshe Elimu kwa kuzingatia maoni na matakwa ya wananchi. Sehemu kubwa ya mabadiliko niliyoyatekeleza yalitokana na Taarifa ya Mfumo wa Elimu wa Karne ya 21 (The Tanzania Education System for the 21st Century) iliyoandaliwa na Jopo Maalumu (Task Force) la wataalamu wa Elimu waioteuliwa na Serikali ya Awamu ya Pili. Utekelezaji wangu ulikidhi matakwa ya kisheria, maelekezo ya Rais, uamuzi wa Baraza la Mawaziri na kwa kulishirikisha Bunge na Wadau wengine wa Elimu kupitia Kamati ya Maendeleo ya Elimu ya Kawaida (Basic Education Development Committee).


Swali: Lawama nyingine kubwa juu yako ni kwamba wewe ndiye hasa sababu ya kuporomoka kwa elimu ya Tanzania kutokana na mabadiliko ambayo uliyafanya, je, unaikubali lawama hii?

Mungai: Lawama hiyo haina ukweli wowote kwa sababu wakati wangu kuanzia mwaka 2000 hadi 2005 elimu haikuporomoka bali ilipanda kwa ongezeko la Wanafunzi na ubora wa Elimu kwa vigezo na takwimu muhimu za Elimu.

Uandikishaji elimu ya msingi wa rika husika la miaka 7 hadi 13 uliongezeka kutoka asilimia 59 mwaka 1999 mpaka asilimia 95 mwaka 2005. Hiyo ni rekodi ambayo haikuwa imefikiwa tangu tupate Uhuru mwaka 1961, na ilikuwa bado aslimia 5 tu kulifikia lengo namba 2 la Milenia la elimu ya msingi kwa wote ifikapo mwaka 2015.

Wanafunzi katika Shule za Msingi waliongezeka kwa asilimia 72, kutoka 4,382,410 mwaka 2000 hadi 7,541,208 mwaka 2005 wakiwa na wingi sawa wavulana na wasichana. Hivyo, lengo namba 3 la millenia la Elimu sawa kwa wavulana na wasichana lilifikiwa.

Kufaulu mtihani wa Darasa la VII kuliongezeka kutoka asilimia 19 mwaka 1999 hadi asilimia 42 mwaka 2004, asilimia 62 mwaka 2005 na asilimia 70 mwaka 2006.

Wanafunzi wa Sekondari waliongezeka karibu maradufu kutoka 266,000 mwaka 2000 hadi 524,325 mwaka 2005. Idadi hiyo ilikuwa ni ya kwanza kuvuka Nusu Milioni tangu Uhuru wa nchi yetu.

Watahiniwa wa Shuleni waliofaulu mtihani wa Kidato cha IV katika Madaraja I-III waliongezeka kutoka asilimia 26 mwaka 2000 hadi asilimia 42 mwaka 2005. Watahiniwa wa Kidato cha VI waliofaulu katikamadaraja I-III waliongezeka kotoka asilimia 82 mwaka 2000 hadi asilimia 94 mwaka 2005.

Hizo ndizo takwimu muhimu za mafanikio yangu ya Elimu bora; na SIYO bora Elimu. Hayo ni mafanikio makubwa ndani ya miaka yangu mitano 2000-2005 ya Uwaziri wa Elimu. Anayeweza kusema mimi nilididimiza Elimu ni mtu asiyejua vigezo vya ubora wa Elimu. Nashauri vyombo vya habari viepuke kuchapisha au kutangaza maneno ya wasiojua takwimu na wasiofahamu vigezo vya Elimu bora.


Swali: Katika jibu lako la kwanza umezungumzia Sheria ya Elimu kuwa inaelekezaWaziri asifanye uamuzi wowote ambao hauzingatii maslahi ya Watanzania. Je, unakumbuka ni yapi uliwahi kuyakubali au kuyakataa kwa kujali maslahi ya Watanzania?

Mungai: Katika uamuzi wangu wote nilijitahidi sana kujali maslahi na matakwa ya Watanzania hususan wazazi. Kwa mfano niliombwa na washabiki wa Elimu ya Sekondari kwa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwanza niwape kibali cha kuanzisha Shule ya Sekondari ya majaribio itakayotoa elimu kwa Kiswahili, pili kuwapa wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Niliwaambia naweza kuwakubalia ombi la kwanza lakini siyo la pili. Niliwaambia naweza kuwapa kibali cha kuanzisha Sekondari ya Kiswahili na ningeliagiza Baraza la Mitihani liwatahini wanafunzi wao kwa Kiswahili, lakini watangaze wenyewe na wapate maombi ya wanafunzi wanaopenda wenyewe, siyo kupitia kweye kuchaguliwa kutoka Shule za Msingi. Niliamua hivyo kwa kutambua kuwa hakuna mzazi ambaye angekuwa tayari mtoto wake asomeshwe Sekondari kwa Kiswahili.

Nilipowakatalia kuwapa wanafunzi hawakuendelea na majaribio hayo ya Sekondari kwa Kiswahili kwa sababu walijua kwa matangazo yao, wasingepata Wanafunzi . Sikuona sawa kuwapanga watoto wa watu kwenye majaribio ya Sekondari ya Kiswahili. Naamini Watanzania walio wengi wanataka watoto wao waelimishwe kwa ajili ya soko la ajira la ndani na nje, hivyo Kiingereza ni kipaumbele chao.

Aidha niliwakatalia kata kata kwa hoja nzito washabiki wa utoaji wa Elimu yote kwa Kiswahili.


Swali: Kwa jinsi unavyojieleza inaonekana yapo mambo mengi chanya uliyofanya, sasa ni kwa nini ulaumiwe kuporomosha elimu, na hayo uliyofanya mbona hayazungumzwi?

Mungai: Kwa bahati mbaya wapo watu wenye tabia ya hovyo ya kulaumu bila ushahidi wa takwimu. Vipo vyombo vya habari visivyojali kuchapisha au kutangaza mambo ya uongo. Ukweli uko wazi kuwa kutokana na mafanikio ya Elimu bora ya wakati wangu nilipokuwa Waziri wa Elimu ya kuongeza ufikiaji wa lengo la Elimu ya Msingi kwa wote kutoka asilimia 59 mwaka 2000 hadi asilimia 95 mwaka 2005, kwa usawa wa wasichana na wavulana, Tanzania ilipewa Tuzo na Umoja wa Mataifa mwaka 2010 kwa kufikia malengo ya Elimu ya Milenia iliyopokelewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.

Mimi binafsi nilijisikia vizuri sana nchi yangu ilipopewa Tuzo na Umoja wa Mataifa kwa kufikia malengo ya Elimu ya Milenia yaliyofikiwa wakati wangu kutokana na kazi nzuri tuliyoifanya chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa. Tanzania ilipewa Tuzo na Umoja wa Mataifa lakini mimi naishia lawama za uongo mtupu na uongo ukirudiwa mara nyingi unaweza ukadhaniwa ni ukweli.


Swali: Ipi sababu iliyokufanya ufute michezo Shuleni wakati ulipokuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni? Je, ni kweli wewe siyo mpenda michezo?

Mungai: Hakuna ukweli wowote wa mimi kufuta michezo Shuleni. Nilichofanya ni kufuta mtindo wa hovyo wa michezo badala ya masomo nilioukuta umeshamiri katika Shule za Msingi na Sekondari kupitia vilivyoitwa vyama vya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) na Umoja wa Michezo Shule za Sekondari Tanzania (Umiseta).

Vyama hivyo viliundwa chini ya Sheria ya Michezo ya Wizara inayosimamia michezo kwa lengo la kuendesha kila mwaka mashindano ya michezo ya Shule hizo kuanzia ngazi ya Kata, Tarafa, Wilaya, Mikoa na Taifa. Mashindano hayo yaliendeshwa siku za Shule na saa za masomo. Mimi nilikuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, Michezo haikuwa chini yangu.

Sikukurupuka; niliunda kamati kuainisha mashindano hayo yalichukua siku ngapi kwa mikoa mbali mbali. Taarifa ya kamati hiyo iliainisha kuwa mashindano ya Shule yalichukua kati ya siku 60 hadi 75 za masomo katika siku 199 za masomo kwa mwaka za walimu kufundisha na wanafunzi kujifunza madarasani kama ilivopangwa na Kamishna wa Elimu. Waendesha mashindano hayo wa kutoka Wizara inayosimamia michezo kupitia Umiseta na Umitashumta hawakujali kabisa siku za Shule na vipindi vya masomo.


Swali: Nini ulikuwa uamuzi wako baada ya kamati kukupa majibu hayo? Na ilikuwaje Umiseta na Umitashumta vikapotea?

Mungai: Kutokana na taarifa ya kamati niliyoiunda niliridhika kabisa kuwa mashindano ya Shule ya Michezo kila mwaka yalichangia kudidimia kwa Elimu nilikokukuta kwa sababu wanafunzi walioshiriki mashindano hayo siku 60 hadi 75 walikosa masomo ya siku hizo; Walinu waliokwenda na wanafunzi kwenye mashindano, vipindi vyao Shuleni vilikosa Walimu na kuathiri ufundishaji kwa wanafunzi waliobakia.

Timu za Shule zilizokwenda kwenye mashindano zilifikia katika mojawapo ya Shule na kulala madarasani. Kwa hiyo Shule mwenyeji ilifungwa muda wote wa mashindano.

Rais Mkapa aliponiteua aliniambia anataka awe na cha kuwaambia Watanzania kuhusu maendeleo ya elimu ya watoto wao anapomaliza muda wake mwaka 2005. Kwa hiyo niliamua bila kuchelewa kuziba mianya ya walimu kutofundisha na wanafunzi kutojifunza madarasani. Aidha niliagiza Walimu kupangwa upya Shuleni kufuata ikama na kuondoa mara moja mrundikano wa Walimu Mijini.

Ili kutoziingilia zile siku 199 za masomo kwa mwaka, niliagiza michezo shuleni iwe baada ya vipindi vya masomo na siyo badala ya Masomo. Mashindano ya Shule yawe baada ya masomo, au siku za Jumamosi na Jumapili au wakati wa likizo.

Kutokana na maagizo yangu Kamishna wa Elimu alitoa Waraka wa Elimu wa kuvifuta vyama vya Umitashumta na Umiseta. Waraka huo ulifuta pia mchango wa Sh.1,000 kwa mwanafunzi kwa ajili ya mashindano ya michezo. Jumla zilikuwa zinakusanywa zaidi ya Sh.4.3 bilioni ambazo hazikuwa na risiti wala ukaguzi wa Serikali. Sehemu kubwa zilienda mifuko binafsi ya viongozi wa Elimu na mashindano hayo ambao niliwaudhi sana nilipoyafuta. Hao ndio wanaendelea kutangaza Mungai alifuta michezo Shuleni. Wanazililia zile Sh. Bilioni 4.3 hadi leo!


Swali: Mambo yapi ambayo yanakupa nguvu na kujisikia fahari katika sekta ya elimu kwa sababu uliyafanya mwenyewe wakati wako?

Mungai: Kutokana na hatua nilizochukua bila kuchelewa ilipofika Mwaka 2005, Rais Mkapa aliweza kuwaambia Watanzania kuwa asilimia 95 ya watoto wao wa rika la Elimu ya Msingi wapo Shuleni na ufaulu wao Darasa la VII umepanda mwaka hadi mwaka kufikia asilimia 62 mwaka 2005 na itakuwa asilimia 70 mwaka 2006. Aidha Watoto wao zaidi ya nusu milioni walikuwa Shule za Sekondari na zaidi ya asilimia 40 wanafaulu Kidato cha IV katika Madaraja I-III na asilimia 94 wanafaulu Kidato cha VI katika Madaraja I-III.

Tulibuni na kuanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) mwaka 2004 -2009 uliopanua Elimu ya Sekondari kuwafikia angalau nusu ya rika lengwa la miaka 14-18. Tulianzisha Vyuo Vikuu Vishiriki vya Elimu vya Chang’ombe na Mkwawa kwa lengo la kufundisha walimu kwa ajili ya utekelezaji wa MMES. Upanuaji wa Elimu ya Sekondari ulipangwa kuendana na upanuaji wa mafunzo ya Walimu wa Sekondari

Najivunia kufuta ada na kuifanya Elimu ya Msingi kuwa ya bila malipo na ya lazima kwa kila mtoto wa miaka 7 hadi 13. Mzazi alibakia na wajibu wa kumpa mtoto wake malazi, mlo na mavazi. Nilipiga marufuku michango yote ya wanafunzi na wazazi wao. Michango ya Ujenzi wa Shule ni jukumu la wote wenye uwezo wa kufanya kazi; na siyo Wazazi wa Wanafunzi peke yao.


Serikali ilitoa Ruzuku ya Uendeshaji wa Shule za Msingi ya Shs. 10,000 kwa kila mwanafunzi ya kununulia vifaa vyote vya kufundishia na kujifunzia, vikiwemo vifaa vya michezo. Baada ya kufuta mchango wa Sh.1,000 ya mashindano ya Shule; Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya michezo baada ya masomo.

Najivunia kuandaa na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) 2002-2006 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) 2004-2009 iliyotoa ruzuku za maendeleo na uendeshaji kwa wananchi wanaojenga na kuendesha Shule. Nilisimamia kupunguzwa kwa ada ya Sekondari za Serikali za kutwa kwa aslimia 50 kutoka Sh.40,000 mpaka Sh.20,000, na tuliongeza ruzuku maradufu ya kuwasomesha Sekondari bila ada watoto wa familia zisizo na uwezo. Hatukuona sababu youote ya elimu ya Sekondari ya bure kwa watoto wa Wazazi wenye uwezo.

Najivunia kuanzisha mafunzo ya Teknolojia ya Habari naMawasiliano (Tehama), katika vyuo vyote vya ualimu.

Aidha najivunia kusimamia marekebisho na kuanza kutekeleza mtaala mpya wa Sekondari uliounganisha masomo ya michepuo (Ufundi, Kilimo, Biashara na Sayansi Skimu) na masomo ya Kawaida. Mtaala huo Mpya ulitekeleza kwa ukamilifu mapendekezo ya Taarifa ya Mfumo wa Elimu ya Tanzania unaofaa kwa Karne ya 21 (The Tanzania Education System for the 21st Century).

Swali: Hili la mtaala nalo limezungumzwa sana na ni eneo ambalo unasemwa ulibadii bila kushauriana na wataalam wa Wizara, hili lipoje?

Mungai: Nilifuata utaratibu mzuri kabisa. Nilichofanya ni kutekeleza Taarifa ya Mfumo wa Elimu ya Tanzania kwa Karne ya 21 (The Tanzania Education System for the 21st Century) ya Mwaka 1993. Hiyo ni Tarifa ya Jopo la Wataalam (Task Force) wa elimu waloteuliwa mwaka 1990 na Waziri wa Elimu Amran Mayagila wa Serikali ya Awamu ya Pili kufanya kazi ya kuchunguza na kupendekeza mfumo bora wa elimu kwa nchi yetu kwa Karne ya 21. Mwenyekiti wa Jopo hilo alikuwa Profesa Hernes Mosha na Katibu Mkuu wake alikuwa Profesa Justinian Garabawa ambao kwa nyakati tofauti wamewahi kuwa Wakuu wa Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wajumbe walikuwa wasomi maarufu wa taaluma ya elimu na ualimu. Benki ya Dunia na DANIDA waligharamia kazi ya jopo hilo.

Taarifa ya jopo hilo iliwasilishwa Novemba 1992 kwa Mhe. Charles Kabeho Waziri wa Elimu na Utamaduni; na Mhe. Benjamin Mkapa Waziri wa Sayansi Teknologia na Elimu ya Juu wa Serikali ya Awamu ya Pili. Kutokana na Taarifa hiyo; Serikali iliandaa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (The Education Sector Development Pragramme - ESDP) na kupitishwa na Serikali. Mimi niliikuta na kuisoma Tarifa na Programu hiyo nikazifanyia kazi hadi kuandaa mtaala Mpya unaofaa kwa Tanzania ya Karne ya 21. Sehemu kubwa ya Maboresho ya Elimu niliyoyasimamia yalitokana na Taarifa hiyo; ambayo pamoja na mengineyo ilikosoa sana ufundishaji wa Masomo ya amali Shuleni kabla watoto hawajaiva katika Masomo ya kawaida ya Shule. Aidha ilikosoa kuwa Masomo ya Sekondari Tanzania ni mengi mno bila sababu kulinganisha na Nchi nyingine hususan za Jumuia ya Afrika ya Mashariki.

Katika mtaala mpya wa Sekondari masomo ya michepuo ya Biashara, Kilimo, Ufundi na Sayansi Skimu yaliondolewa. Masomo hayo yaliachiwa VETA na Vyuo vingine vya Amali. Aidha wingi wa masomo ya Sekondari ulipunguzwa ili kuongeza vipindi vya masomo ya elimu ya Sekondari ya kawaida (basic secondary education subjects) ya Hisabati, Lugha za Kiingereza na Kiswahili, Sayansi za Biologia Fizikia na Kemia ambapo Kemia na Fizikia vikiwa somo moja kidato I na II, kisha kuwa tofauti kidato cha III & IV. Masomo ya Hisabati na ya Sayansi yalirekebishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania kuzingatia Elimu ya Kujitegemea.

Vivyo hivyo vipindi viliongezwa kwa Masomo ya Sayansi ya Jamii ya Historia, Jiografia na Uraia. Aidha lilibuniwa somo maalum la muundo wa lugha ya Kingereza (English Structure) la lazima kwa wanafunzi wote wa kidato cha V na VI ili kuwaandaa kwa Elimu ya Chuo Kikuu. Hatua hiyo ililenga kurekabisha kasoro kubwa ya wenye Shahada za Vyuo Vikuu ya kutokujua vizuri Kingereza.

Katika hatua nyingine niliamua kurejesha mtindo wa kupanda darasa kwa kuhitimu (achievement based progression). Walimu Wakuu wa Shule za Msingi walikumbushwa wajibu wao wa kukalilisha kwenye madarasa ya Kwanza na Pili watoto ambao hawajajua zile "K" tatu, yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Mtindo wa zamani wa kukalilisha Darasa la IV na Kidato cha II wasiofikia kiwango kulichowekwa ulirejeshwa.

Serikali ya Awamu ya Tatu tuliboresha Elimu kwa kupandisha alama za kufaulu Darasa la IV, Darasa la VII na Kidato cha II. Nilizitunga upya Kanuni za Elimu (Education Bye Laws) ili kuyapa uzito wa kisheria mageuzi niliyoyasimamia. Tuliimarisha vigezo vya utoaji wa Elimu bora kwa kupanga wanafunzi wasizidi 45 kwa darasa na wawe wa umri mmoja na shule isizidi wanafunzi 945. Nyaraka za Elimu maalumu zilitolewa na Kamishna wa Elimu kuelekeza vigezo vya Elimu bora ambavyo lazima vizingatiwe vikiwemo vya wingi wa wanafuzi Darasani usizidi 45; ukubwa wa Shule usizidi mikondo minne yenye wanafunzi 945; kuondoa mrundikano wa Walimu Mijini; Kupanga Walimu kwa usawa kwa kuzingatia ikama; kuandikisha kila mwaka watoto wote wa miaka 7 kuanza Darasa la kwanza; na Kupanda kutoka Darasa la IV na Kidato cha II kwa kufaulu Mitihani ya Kitaifa. Hizo ni hatua za kuongeza ubora wa elimu na siyo za bora Elimu.


Swali: Wakati unaondoka wizarani, kuna mambo gani ambayo ulitamani kuendelea kuyafanyia kazi lakini hukuyapatia nafasi kwa sababu baada ya utawala mpya, kutoka Rais Benjamin Mkapa mpaka Dk Jakaya Kikwete, ulihamishwa wizara?

Mungai: Nilipenda sana kuendelea kusimamia maboresho ya Elimu kupitia utekelezaji wa mtaala mpya unaofaa kwa Tanzania ya Karne 21. Lakini Rais Kikwete aliniteua kuwa Waziri wa Kilimo na baadaye kidogo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Niligundua baadaye kuwa kulikuwa na shinikizo la Chama cha Walimu nisiendelee kuwa Waziri wa Elimu. Sikupendwa na Walimu kwa sababu niliwabana mno. Chama cha Walimu CWT walimuambia Mgombea Urais wa CCM wa mwaka 2005 kuwa wanamuunga mkono lakini Mungai asiendelee kuwa Waziri wa Elimu.

Rais Kikwete akaamua kuwafurahisha zaidi Walimu kwa kumteua aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Mhe Margaret Sitta kuwa Waziri wa Elimu wa baada yangu. Hivo ndivo mchezo wa Siasa ulivyo.


Swali: Ulipoondoka Wizara ya Elimu, yapo mambo mabadiliko makubwa yalifanyika baada yako, je, uliyaunga mkono au uliyakataa?

Mungai: Serikali ya Awamu ya Nne iliamua kuufuta Mtaala Mpya wa Elimu unaotekeleza Mfumo wa Elimu ya Tanzania wa Karne ya 21. Masomo ya Michepuo ya Kilimo, Ufundi, Biashara na Sayansi Sikimu niliyoyafuta yalirudishwa. Hata lile somo la "English Structure" lililoanzishwa la lazima kwa kidato cha V na VI likafutwa. Wingi wa masomo ya sekondari ukarudi upya. Kwa ufupi elimu yetu ilirudi kule kama ilivokuwa Karne ya 20.


Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Mkapa iliienzi na kuitekeleza kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Pili ya Rais Mwinyi ya kuandaa Taarifa ya Mfumo wa Elimu wa Karne ya 21. Kama Waziri wa Elimu wa Kwanza wa Karne ya 21 nilisimamia utekelezaji wa maboresho yaliyopendekezwa katika Taarifa hiyo. Matokeo yalikuwa mazuri: Elimu ya Msingi ilipanuliwa hadi aslimia 95 ya wote wa rika husika; na Elimu ya Sekondari angalao hadi kwa Nusu ya wote wa rika husika; na wakati huo huo ubora wa Elimu uliongezeka. Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Kikwete iliyafuta maboresho hayo katika mwaka wake wa kwanza. Cha kushangaza Serikali zote hizo mi za CHAMA kile kile!!!


Mabadiliko hayo ya kurudi nyuma niliyakosoa sana, bila mafanikio. Nilichogundua ni kuwa waliohusika na uamuzi wa kurudi tulikotoka walikuwa hawajawahi kuisoma na hawaijui kabisa Taarifa tuliyoitekeleza na Rais Mkapa ya Mfumo wa Elimu ya Tanzania wa Karne ya 21; wala ile Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (Education Sector Development Programme - ESDP) ya utekelezaji wake. Uamuzi wa kurudi tulikotoka haukutokana na Uchunguzi wala Taarifa yoyote. Ulikuwa usmuzi wa kisiasa uliofanywa na Wanasiasa. Hata Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) yenye jukumu kisheria ya kurekabisha mitaala haikuhusishwa.



Swali: Tangu mwaka 2005, yapata miaka 11 sasa, umekuwa ukishambuliwa kuwa umeharibu elimu bila kutoka nakuzungumza chochote kujibu, ni kwa nini huzungumzi kutetea uliyoyafanya?

Mungai: Sipendi kujibizana na mjinga kwa sababu inawezekana tofauti yetu isionekane vizuri. Lakini sina tatizo kujibu maswali ninayoulizwa na mtu mwenye akili na ujuzi kama haya ninayoyajibu leo.

Wapo wanaonishauri niandike kitabu cha kueleza kile hasa ambacho tulifanya nikiwa Waziri wa Elimu; na mafanikio yangu ya Elimu bora. Nashawishika kufanya hivo ili kuweka rekodi ya kazi nzuri na mbinu zilizotumika kupanua Elimu ya Msingi kwa wote ndani ya miaka Mitano na wakati huo huo kuongeza ubora wa Elimu

Swali: Kipindi mabadiliko ya mfumo wa elimu yanafanywa mwaka 2006, wewe ulikuwa kwenye Baraza la Mawaziri kama Waziri wa Kilimo, ulijisikiaje kwa mabadiliko hayo?

Mungai: Kama nilivyosema, nilijiisikia vibaya kuona kazi nzuri tuliyoifanya chini ya uongozi wa Rais Mkapa inabomolewa mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne. Nilisononeka sana. Pamoja na utu uzima wangu sikusikilizwa.

Niliwatahadharisha wahusika kuwa matokeo mabaya ya uamuzi huo watayaona baada ya miaka kadhaa. Matokeo yakawa kama nilivyosema. Baada ya mwaka 2007 matokeo ya mitihani ya Darasa la VII na Kidato cha IV yalianza kushuka mwaka hadi mwaka. Wanaofeli waliongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia kilele cha asilimia 60 mwaka 2012. Kama ilivyo ada ikaundwa Tume ya kuchunguza sababu za matokeo mabaya. Cha kushangaza Tume hiyo iliyoongozwa na mtu ambaye hajawahi kusomea taaluma ya elimu na ualimu.

Wakati huo huo Vyuo Vikuu viliendelea na vinaendelea hadi sasa kupokea wanafunzi wasiojua vizuri lugha hususan ya Kiingereza kutokana na kulifuta hata lile somo la "English Structure" kwa wanafunzi wote wa kidato cha V na VI. Kwa hiyo wenye Shahada za Chuo Kikuu wasiojua vizuri Kingereza wanaongezeka.


Swali: Je, kipindi chako ukiwa Waziri wa Elimu ulikuwa unafanya kazi na wabunge pamoja na wataalamu wa wizara? Kama jibu ni ndiyo ni kwa nini shutuma zote zinaelekezwa kwako?

Mungai: Mafanikio niliyoyaeleza yasingekuwepo bila ushirikiano wa Bunge lililopitisha Bajeti ya Wizara yangu bila mgogoro miaka yote mitano. Nilishirikiana sana na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii. Mtaala Mpya baada ya kuandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) tuliujadili na kamati hiyo katika vikao maalumu mara mbili. Mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi mwaka 2002-2007 na ya Sekondari mwaka 2004-2009 ilipitishwa na Baraza la Mawaziri na kuombewa fedha bungeni.

Tulikuwa na Mkutano Mkuu wa Elimu wa wadau wote wa elimu kila mwaka wa tathimini na kupeana malengo. Nilikutana na Wakuu wa Shule za Sekondari kila mwaka. Nilisafiri sana Mikoani na Wilayani kuhimiza utekelezaji na kujionea hali halisi ya Elimu.



Swali: Kama nawe utatakiwa kulaumu, lawama zako utazielekeza kwa nani kuhusu mfumo wa elimu kuwa butu pasipo kumsaiadia mtoto wa Kitanzania?

Mungai: Kuliko kumtafuta wa kumulaumu nadhani tukubaliane yaliyopita ni ndwele tugange yajayo. Kwa sasa ninayo matumaini makubwa kwa sababu kwa mara ya kwanza tangu Uhuru, Elimu imepata utatu mtakatifu wa Rais mwalimu; Waziri Mkuu Mwalimu; na Waziri wa Elimu mwalimu. Hapo kazi kwao. Watanzania wanawategemea sana kuokoa jahazi la Elimu linalozidi kuzama.


Swali: Baada yako Wizara ya Elimu alifuata Margaret Sitta naShukuru Kawambwa, kila mmoja unampa alama ngapi kwa kazi uliyoshuhudia akiifanya ukiwa ukiwa nje?

Mungai: Sipendi kuwa mkosoaji wala muweka alama kwa ndugu zangu tupatao 23 tuliopokezana kijiti cha Uwaziri wa Elimu tangu Uhuru mwaka 1961. Mawaziri 23 katika miaka 55 ni wastani wa chini ya miaka miwili na nusu kwa kila Waziri wa Elimu. Huenda Waziri wa Elimu kutokupewa muda wa kutosha ni sehemu ya tatizo la Elimu yetu. Rais Mkapa alinipa miaka yote mitano ya kipindi chake cha pili na naamini nilimfanyia kazi nzuri.



Swali: Una imani gani na Profesa Joyce Ndalichako? Wewe ukiwa Waziri wa Elimu, yeye alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), unavyomfahamu kikazi, anaweza kuisaidia elimu ya Tanzania?

Mungai: Wakati nilipokuwa Waziri wa Elimu alisimamia Baraza la Mitihani kwa ufasaha na weledi mkubwa. Alinisaidia sana. Yeye siyo profesa tu, bali ni profesa wa Elimu.

Swali: Je, umewahi kufikiria kukutana na Profesa Ndalichako na kuzungumza naye kuhusu hali ya elimu? Siku ukikutana naye utamshauri mambo yapi ya msingi?

Mungai: Alipoteuliwa nilimuomba anipe muda nikaenda ofisini kwake kumpongeza na kumtakia mafanikio. Tulibadilishana mawazo vizuri sana.



Swali: Tangu Serikali ya Rais John Magufuli iingie madarakani, ni mambo yapi ambayo yameshafanyika na yalikukuna zaidi katika maelendeo ya elimu? Yapi ambayo nimabovu na yalikuogopesha katika elimu?

Mungai: Muda ni mfupi mno kufanya tathimini ya maana. Lakini nimeshangazwa na Elimu ya Sekondari ya bure hata kwa watoto wa wenye uwezo Kama Mimi , Rais, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mameneja Wakuu na kadhalika, na kadhalika. Serikali ya Awamu ya Nne tuliwapa ruzuku ya ada ya Sekondari watoto wa Wazazi wasio na uwezo wa kuwalipia ada.


Swali: Kuna kashfa ya rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu 2015, ulituhumiwa kutoa rushwa lakini kesi ilipofika mahakamani ulishinda lakini tayari ilikuwa imeshakuchafua, tukio hilo lilikuumiza kiasi gani na kukuachia ujumbe gani?

Mungai: Nilizidi kujifunza kuwa kabla hujafa hujaumbika. Nilisimamishwa kizimbani kama mshitakiwa wa kwanza. Palipo na uongo ukweli hujitenga ndiyo maana sikukutwa na hatia, nilishinda. Nilishangaa tu kufanyiwa vile na Serikali ya CCM baada ya utumishi wangu kwa uaminifu katika Awamu Zote NNE!!! Niliahidiwa kusaidiwa kusafisha jina, lakini nadhani aliyeniahidi alisahau na mimi sikuona sababu ya kumukumbusha.


Swali: Wewe ni mmoja wa waliokuwa makada wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi, lakini zipo taarifa kuwa katika Uchaguzi Mkuu 2015, ulitangaza kukihama, je ni kweli?

Mungai: Sijawahi kutangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi. Nilichofanya ni kushirikiana na viongozi wa Chadema kumuombea kura mtoto wangu William (William Mungai) ambaye alikuwa anagombea ubunge jimbo la Mafinga kupitia chama hicho. Na mimi kama mpigakura wa Mafinga, niliwashawishi wenzangu tumchague William lakini hakufanikiwa.


Swali: Wadau mbalimbali wa elimu wamekuwa wakijitokeza na kuzungumza na vyombo vya habari, kuhojiwa na televisheni au hata redio, ni kwa nini hutumii fursa hiyo ili kutoa mchango wako wa elimu?

Mungai: Mimi ni Mbunge na Waziri Mstaafu. Sipendi kushinda magazetini wala redioni. Ushauri wangu ukihitajika nitautoa kwa anayeuhitaji. Nikiulizwa Maswali kama unayoniuliza nitayajibu. Hata yakiwepo ya nyongeza nitayajibu.



Swali: Je, bado unahamu ya kufanya siasa? Kama jibu ni ndiyo, unapenda ufanye siasa za namna gani?

Mungai: Sina hamu tena wala muda wa mambo ya siasa



Swali: Hivi sasa siyo Waziri wala Mbunge, Watanzania wangependa kujua ni mambo gani ambayo yakakushughulisha kwa wakati huu.

Mungai: Najishughulisha na mambo yangu binafsi ya uwekezaji wa kiuchumi pamoja na kupumzika.



Swali: Unauzungumziaje uongozi wa Dk Magufuli kwa jumla?

Mungai: Tunayasibiri kwa hamu kubwa matokeo ya uongozi wa Rais Magufuli.



Swali: Unaweza kutupa historia yako kwa ufupi?

Mungai: Nilizaliwa Oktoba 24, 1943 Kiliji cha Malangali Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa. Nilizaliwa katika familia ya Biashara na Kilimo. Nilisoma katika Shule nzuri sana. Nilianzia Shule ya Msingi Malangali mwaka 1951 mpaka 1958, yaani Darasa la Kwanza mpaka la Nane.

Sekondari nilisoma Shule ya Tabora mwaka 1959 mpaka 1962, Darasa la 9 mpaka la 12. Nikajiunga na Shule ya Sekondari ya Juu ya Mkwawa kuanzia mwaka 1963 mpaka 1964, Darasa la 13 hadi 14.

Baadaye nilijiunga na Taasisi ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Colorado, Marekani, nikasomea Diploma ya Uchumi mwaka 1979 na mwaka uliofuata nilijiunga na Shule ya Kennedy ya Serikali (Kennedy School of Government) katika Chuo Kikuu cha Harvard pia Marekani ambako nilisomea shahada ya Umahili katika Uongozi wa Umma (Master of Public Administration - MPA).

Kabla ya kuingia siasa mwaka 1970, nilikuwa kwanza Mneja Mauzo wa Kampuni ya SINGER 1965-67 na baadaye Meneja Mkuu wa Tanzania Elimu Supplies 1967-72.

Nilikuwa Mbunge miaka 35 wa Wilaya ya Mufindi: mwaka 1970 mpaka 1990 wa Wilaya ya Mufindi yote na mwaka 1995 mpaka 2010 wa Jimbo la Mufindi Kaskazini.

Nimewahi kuwa Waziri wa Kilimo kuanzia mwaka 1972 mpaka 1975, kisha mwaka 1980 mpaka 1982 na baadaye mwaka 2006 mpaka 2007. Nilikuwa Waziri wa Elimu mwaka 2000 hadi 2005 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2007 mpaka 2008. Nilikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa mwaka 1993 hadi 1995. Kimsingi nimekuwa kwenye uongozi kuanzia Awamu ya Kwanza mpaka ya Nne.

Namushukuru Mungu kunijalia kuwa katika uongozi wa Taifa letu kwa karibu nusu ya umri wangu. Niliapishwa kuwa Mbunge na Spika wa Bunge wa Kwanza, Adam Sapi Mkwawa nikiwa na umri wa miaka 26. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliniteua na kuniapisha kuwa Waziri wa Kilimo nikiwa na umri wa miaka 28 tu, wakati huo nilikuwa mdogo kuliko Mawaziri wenzangu wote.
 
alifanikiwa sn kwa kufuta michezo mashuleni na masomo ya mchepuo wa biashara... watu wengine sio lazma ujisifu wakati unajua ulifanya madudu pengine kuliko wote waliokutangulia.
 
Back
Top Bottom