MzalendoHalisi
JF-Expert Member
- Jun 24, 2007
- 4,313
- 986
Nimekuta hii habari kule Michuzi Blog- Je ungekuwa wewe ungemshauri vipi huyu mama?
Bwana Michuzi,
Naomba usome mail hii kisha ukiona inafaa uiweke kwenye blog yako wadau wanisaidie/wanishauri. Ila kama utaona haistahili, basi achana nayo, ila tafadhali usiweke e-mail yangu hadharani.
Mimi ni Mama nimeolewa na nina watoto watatu, ninaishi hapa Tanzania ninafanya kazi shirika lisilo la Kiserikali. Nimeishi na mume wangu kwa miaka mingi sasa kwa raha na karaha pia. Mume wangu alikuwa akifanya kazi shirika fulani, lakini kwa bahati mbaya aliachishwa kazi miaka miwili nyuma kutokana na sababu flani flani.
Wakati mume wangu akifanya kazi, tulikuwa tukiishi nyumba ya shirika alilokuwa akifanyia kazi, na baada ya kuachishwa, nikaomba nyumba ya shirika na nikapewa ambayo tunaendelea kuishi mpaka sasa.
Let me cut the story short;
Ni kwamba miezi kama sita baada ya mume wangu kuachishwa kazi, mara siku moja jioni natoka kazini nakuta watoto wawili wameongezeka wakiwa na bag kabisa, nikamuuliza mwenzangu ugeni wa wapi huu, akadai ni habari ndefu japo baadae alikiri ni watoto wake/wetu mtu mzima nikajua haya ni matunda ya zile siku alikuwa akilala nje nikawapokea na kuwatambulisha kwa watoto wangu kwamba na hao ni ndugu zao.
Kama hiyo haikutosha, baada ya kama miezi miwili hivi akaletwa Mama wa watoto hao (mke mwenzangu)!, Nikauliza itakuwa vipi na sisi ni wakristo wa ndoa moja tu, tutaiambiaje jamii? Yule Mama akadai hapo haondoki kwani kaja kulea wanawe na hana imani na mimi kumlelea watoto wake. Nikabeba mzigo kwamba sawa na akae lakini kwa kivuli kwamba ni ndugu wa mume wangu (nakiri udhaifu kwa hili).
Siku zikaenda kificho nje lakini ndani inajulikana na yeye ni Mama kwani hakukuwa na kificho hicho hata kwa watoto! Tuliita wazazi wa pande zote mbili kusuluhisha, siwezi kuwalaumu kwa kufuata sheria za dini kwani walidai katika kiapo cha Ndoa tuliapa kutokuachana mpaka kifo kitapotutenganisha, na kwamba nivumilie ndio mitihani katika maisha.
Nikavumilia kwamba huu ni msalaba wangu niubebe mwenyewe. Kinachoniuma sasa ni kwamba ndani ya nyumba hakuna tena maelewano kati yangu na Mume wangu, na tumegeuka maadui mimi na mkwe mwenzangu, kiasi hata kile kificho kwamba ni ndugu wa mume wangu hakipo tena kwani mbali na watu kuhisi, yeye alikuwa mstari wa mbele kutamba kwamba na yeye ni mke kama nilivyo mimi, hivyo ana haki na mamlaka ndani ya nyumba, kuwekeana nyimbo za vijembe na kuvaliana kanga za mafumbo zinazonunuliwa kwa hela yangu! Kero ni nyingi ndani ya ndoa yangu nyingine hata aibu kuzisema hadharani, na nikisema tuachane Mume wangu anakuja na visingizio kwamba ninamnyanyasa vile hana kazi na mimi nina kazi, wazazi nao wanadai sio vizuri watoto kulelewa upande mmoja, Jamani nimeshindwa na sina raha ya maisha tena nifanyeje?
Mke mwenzangu nikampa ushauri walau apange chumba nje ya nyumba yetu tutamlipia hataki, anadai atakuwa pale mume wake na watoto wake watakapokuwepo! Sijui, labda mimi sio mvumilivu vya kutosha, lakini kweli niko njia panda naomebi uhsuri nifanyeje jamani.
Sina raha tena na ndoa yangu, na maisha nayaona machungu. Ieleweke, sio kwamba vile hana kazi ndio maana nafanya hivi, hapana ila manyanyaso na vituko ndani ya nyumba nimechoka.
Samahani kwa kuwapotezea muda kuwaelezea shida zangu, naomebi msaada wenu Watanzania wenzangu.
Kwa Mume wangu, najua ukisoma ujumbe huu utajua ni wewe na familia yetu naiongelea, nisamehe kwa kuchukua uamuzi huu ni kwa sababu sina pa kukimbilia tena, acha tusikie wanajamii wengine wanasemaje then we can act on the advise.
natanguliza shukrani.