Muhimu kwa wote

Abdull Kazi

JF-Expert Member
Dec 29, 2012
322
255
CHADEMA mnatambua imani ya Watanzania kwenu?

03/11/2013 | Posted by Abdallah Khamis | Makala


ZAIDI ya miaka 20 iliyopita Watanzania waliingia katika mfumo wa vyama vingi, ikiwa ni mara ya pili baada ya mfumo huo kufutwa awali na utawala wa Awamu ya Kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa nyakati tofauti matumaini ya wananchi wengi yalijikita katika vyama vilivyokuwa na nguvu kwa wakati huo. Tuliona jinsi NCCR-Mageuzi ilivyosimama na kubeba matumaini hayo, ikaja TLP, Chama cha Wananchi (CUF) na sasa CHADEMA.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kila chama hususan vya upinzani vilijiwekea malengo ya kuwafikia watu wengi hasa wa vijijini, wakiamini uelewa wa watu hao ndio utakuwa msingi mzuri wa kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.

Kila chama kwa wakati wake kilifanya juhudi hizo na hatimaye CHADEMA ikachomoza na kuwa juu ya vyama vingine vya upinzani nchini, baada ya mikakati ya muda mrefu ya kujikita kwa wapiga kura. Matokeo ya mikakati hiyo yalidhihirishwa na idadi ya kura za jumla walizopata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, viti vya ubunge, udiwani wenyeviti wa mitaa na vitongoji, hakika matumaini ya wengi yalisimama kwao kama yanavyoendelea kujidhihirisha leo na itakavyokuwa kesho na kesho kutwa.

Namna wabunge wa chama hicho wanavyopambana bungeni kwa ajili ya kupigania masilahi ya wananchi ni sababu nyingine inayowafanya CHADEMA waendelee kujiamini juu ya kuungwa mkono na wananchi katika uchaguzi wowote utakaotokea dakika moja ijayo kuanzia sasa.

Kwa hakika Watanzania wamejenga na wataendelea kujenga imani kubwa zaidi kwa CHADEMA iliyo moja yenye mshikamamo na yenye kuwajibishana kwa misingi ya haki. Watanzania hawatakuwa na imani na CHADEMA iliyo vipande vipande, ambayo viongozi wake hawatakuwa na umoja na mshikamano, wala watakaokuwa hawaaminiani wao kwa wao.

Ukiwa mjini au vijijini katika masuala ya kijamii utakutana na watu wenye kuhoji masuala ya msingi kwa viongozi wao, hii yote ikiwa ni misingi iliyowekwa na vyama vya upinzani. Katikati ya mafanikio hayo ya CHADEMA moja ya matatizo yanaanza kujidhihirisha, ni dharau kwa viongozi waliofikisha chama hapo kilipo.

Kibaya zaidi, aina ya dharau inayooneshwa kwa viongozi wa CHADEMA inafanywa na watu wanaojulikana, wapo wanaomkashifu mwenyekiti, katibu mkuu na naibu katibu mkuu katika mitandao ya kijamii, hadharani na sirini, lakini bado hawachukuliwi hatua.

Athari ya matendo haya ni kuvunja nguvu na umoja juu ya utendaji na ujenzi wa chama. Kuna hatari ya wale wanaokashifiwa kuhisi kubaguliwa ndani ya chama hicho iwapo kauli za kukemea tendo hilo hazitatolewa, huku wahusika wa kauli hizo za kebehi wakiwa ni wafuasi au wanachama wa CHADEMA.

Kwa maana athari yoyote itakayotokana na dharau juu ya kiongozi wa chama haitamuathiri kiongozi anayekashifiwa peke yake, bali athari hizo zitakiathiri chama pia.

Katika hali ya kawaida watu wanaoendesha kashfa kutengeneza migogoro na hata kuliona kundi moja ndani ya uongozi uliopo ni tatizo, watakuwa hawakitakii mema chama chao na hasa hawayatakii mema matumaini ya Watanzania yaliyojengwa kwa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA.


Tanzania ni kubwa na inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi, kisiasa na mambo mengine, kwa hiyo sitegemei chama tawala au chama kinachotarajia kuongoza nchi kiwe chama legelege. Ni lazima chama hicho kitapitia katika vipimo vya usaliti, migogoro na vitimbi vingine.

Katika mazingira kama haya, umakini wa chama kinachotarajia kushika dola ni kitakavyopita katika mtihani huo na kuushinda kwa ustadi mkubwa na kubakia salama.

Ni wakati wa viongozi wa CHADEMA kutambua matumaini ya Watanzania kwao na namna yoyote ya kuyafifisha matumaini hayo utakuwa ni usaliti dhidi ya mabadiliko.


Mtazamo wangu ni kuwakumbusha CHADEMA kuwa mafanikio waliyofikia leo hayakuja kama mvua kutoka angani, bali ni mipango mikakati na uwekezaji wa mabadiliko katika mioyo ya watu, kazi iliyofanyika kwa zaidi ya miaka 20 na kwamba fursa iliyopo sasa ikipotea itavilazimu vyama vya upinzani kuchukua zaidi ya miaka 50 kurejea katika hali ya kuaminiwa.

Chanzo Tanzania Daima Novemba 3/2013
 
Back
Top Bottom