BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 497
- 1,200
Kati ya hoja zilizobainishwa na mdau katika dokezo lake ni kuwa suala hilo linaingilia faragha za watu na kufanya watu kupata huduma ya haja kwa hofu. Jambo hilo binafsi nilimuunga mkono, kuwa sio sawa kuweka camera maeneo ya vyoo vya umma.
Lakini katika hali ya kusikitisha, nimeshangazwa kwenda eneo hilo na kukuta camera hizo bado zipo kama ilivyoripotiwa awali karibia Mwezi mzima uliopita.
Najiuliza, hivi Muhimbili hawakuona taarifa hiyo, au waliiona wakaendelea kuchukulia poa kama vile ni jambo la kawaida, licha ya kugusa faragha za watu.
Ni vyema Muhimbili wakatoka hadharani wakauleza umma sababu zenye mantiki za kuweka na kuendelea kubakiza Camera hizo kwenye vyoo vya umma vilivyopo kwenye wodi ya wagonjwa wa nje (OPD).
Suala hilo linaleta utata, kuna ambao wanadai kuwa ziliwekwa kwa ajili ya kuepusha wizi wa mabomba kwenye vyoo , lakini kupitia dokezo lililoletwa na mdau wengine katika kuchangia (comment) walidai kuwa Hospitali hiyo uenda inafanya utafiti maalum.
Sasa ili kutuondoa hofu ni vyema viongozi kwenye Hospitali hiyo wakajitokeza na wakaeleza kinagaubaga sababu zenye mantiki zaidi zinazopelekea kuendelea kuwepo kwa camera hizo, ambazo uenda zina umuhimu zaidi kuliko kulindwa kwa faragha zetu.
Lakini kwa kuwa kumeendelea kuwepo kwa ukimya bila hatua za wazi kuchukuliwa wala kutolewa ufafanuzi kwa wakati ni busara Waziri wa Afya Ummy Mwalimu au viongozi wengine wenye mamlaka ya juu wakalimulika kwa jicho la tatu suala hilo.