Muhidin Issa Michuzi amlilia Balozi Abdulkarim Omar Cisco Mtiro

SWAHILIYA

Member
May 13, 2017
54
150
*Muhidin Issa Michuzi amlilia Balozi Abdulkarim Omar Cisco Mtiro*

Hebu jaribu kulielezea jiji la Dar, au la Arusha, ama la Mwanza, Mbeya ama jiji lolote lile, tena kwa kutumia ukurasa mmoja tu na uwe umefanikiwa kulieleza kinagaubaga kiasi hata mtu ambaye hajawahi kufika hapo ajione kama keshafika na anapafahamu vizuri.

Basi huo ndio mtihani nilionao wakati naandika haya, tena kwa moyo mzito, nikijaribu kumwelezea rafiki yetu, kaka yetu, ndugu yetu, jamaa yetu au vyovyote vile upendavyo kumwita mtu kama Balozi Abdul Omar Cisco Mtiro.

Labda uamue kuzungumzia kamtaa kamoja tu katika kitongoji kimoja, ndipo kidooooogo unaweza kufanikiwa kueleza vitu vikaeleweka. nami ndivyo najaribu kufanya hapa, kwa kudonyoa kasehemu tu ka Braza Cisco.

Ni kweli kwamba mtu akitangulia mbele ya haki huwa kuna hulka ya kumsifia na kumuenzi mtu huyo. Lakini si uwongo kwamba haya niandikayo hapa, japo yalikuwa nyuma ya ubongo wa wengi wetu siku zote, ni halisi na wala sio kwa sababu Cisco hatunaye tena.

Kwa wengi alikuwa mkarimu na mwingi wa bashasha saa zote. *Kwa tuliobahatika kuwa karibu naye, Cisco alikuwa hivyo na zaidi. Pamoja na kuwa na wadhifa mkubwa serikalini (Balozi wetu nchini Nigeria na Malaysia katika nyakati mbalimbali na baadaye Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje), Cisco alikuwa mtu wa kujichanganya na kila mtu bila kujali hali ama mali zake*. *Hakuwa na makuu wala makidai. Alikuwa mtu mmoja 'freshi' sana, wanasema vijana wa mjini*.

*Unapomkuta na wanachama wenzie wa Klabu ya michezo ya TAZARA pale Leaders Club ama kwa Octa (kijiwe maarufu jirani na ubalozi wa Ufaransa) ilikuwa huwezi kuamini kwamba huyu mtu mchana ametoka kusuguana mabega na viongozi wakuu wa nchi na wageni wao ambao, akiwa kama Mkuu wa Itifaki, jukumu lake lilikuwa kuratibu na kusimamia kila kitu*.

*Ubaya, ama uzuri wake, hukumsikia hata mara moja akizungumzia kazi yake ama wadhifa wake*. Huko alikuwa serious kama askari wa Mjerumani. Lakini afikapo kijiweni, kama mlivyo nyinyi wakati huo, na yeye pia alijitosa kuogelea nanyi kwenye soga za siku kama vile kandanda, stori zote za mjini, pamoja na muziki ambao alikuwa anaupenda sana – hasa hasa Jazz, Classics, Old Skul na Chachacha.

Sifa yake kubwa akiwa nasi kijiweni ilikuwa ni utani na vichekesho vya kuvunja mabvu. Yaani Cisco alikuwa hakosi kuja na ‘mpya’ hata kabla ya kuketi kitini, na wakati wa kuondoka kwenda kupumzika alikuwa hakosi kuwaacha na ‘kibomu’ kingine cha kuchana mbavu. Vile vile kila ukutanapo naye lazima ‘akuchape’ na kitu kipya.

Na hiyo ilikuwa hivyo kwa takriban miongo yote miwili ambayo nilibahatika kuwa karibu naye. Angeweza kuandika vitabu lukuki vya utani na vichekesho na bado akabaki hajaishiwa.

Balaa la vunja mbavu liliongezeka maradufu pale alipokutana na marafiki wengine wa karibu kama vile *Balozi Mohamed Maharage (aliyekuja kumwachia kiti cha Mkuu wa Itifaki pale alipostaafu rasmi kazi takriban miaka mitatu iliyopita) kina Mudhihir Mudhihir, Job Juma, Max Rutihinda, David Mgwassa, Muddy Pizzaro, Makongoro Nyerere, Ronnie Mtawali, Wendo Mwapachu, Balozi Patrick Tsere, Balozi Amy Mpungwe, Zainnul Dossa, Henry Tandau, Philemon Ntahilaja* na wengine wengi ambao nashindwa kuwataja wote kwa ufinyu wa nafasi. Hawa wakutanapo unakuwa hutaki kuondoka…

Yote tisa. *Cisco pia alikuwa hodari katika kuhamasisha wadau kushiriki katika shughuli za mwenzetu wakati wa shida ama raha, iwe harusi ama msiba*.

Huyu braza hatosahaulika pale alipoasisi kufanyika kwa michezo baina ya timu za veteran kutoka kila pembe ya jiji iliyokuja kujulikana kama Sunday Soccer Bonanza. Yaani kila Jumapili wachezaji wa vilabu vya Veterans kutoka Sinza, Kinondoni, Ilala, Temeke walikutanika Leaders Club na kuchuana katika mchezo wa soka na baada ya hapo burudani ya muziki wa aidha Msondo ngoma ama Twanga Pepeta ilifuata. Umati uliokuwa unajaa hapo mahali si mchezo. Hakika Bonanza hilo lilifanikisha kwa kiasi kikubwa kuunganisha na kudumisha undugu miongoni vijana na watu wazima wa sehemu mbalimbali za Dar es salaam. Kama kuna mtu aliyekuwa ananung’unika san asana kwa kufifia kwa Bonanza hilo hivi sasa, basi wa kwanza alikuwa Cisco.

Kama hilo Bonanza lilikuwa halitoshi, Cisco na wanachama wenzie wa TAZARA Club wakabuni hadhara ya kukutana mara moja kila mwaka kuwakumbuka na kuwaombea wenzetu wote waliotangulia mbele za haki kwa kisomo na dua za dini zote. Baada ya hapo ‘mpunga’ ulifinywa huku Balozi akichana mbavu za wadau kutwa nzima kwa vichekesho na stori za mjini.

*Nashindwa kukubali kwamba katika kisomo kifuatacho hapo Leaders Club jina la Abdul Omar Cisco Mtiro litatajwa katika orodha ya kuwarehemu wenzetu wote waliotangulia mbele ya haki*.

Kama nilivyosema hapo awali, ugumu wa kumueleza mtu kama Cisco hauna tofauti na kuelezea jiji lolote kwa kutumia ukurasa mmoja tu. Yaani naweza kuandika kurasa mia kama hizi lakini bado nisiweze kusimulia robo tu ya Cisco alikuwa ni mtu wa aina gani huku 'uraiani'.

Itoshe tu kusema kwamba kifo kimetupoka mtu mmoja muhimu sana sana katika maisha yetu, na daima jina lake litabaki kuwa midomoni na ndani ya vilindi vya mioyo yetu daima.

*ADIOS AMIGO, BRAZA CISCO!*Cisco akiwa katika kutekeleza majukumu yake kama Balozi akiwa Malaysia


Cisco aliketi pembeni yangu kuniliwaza nilipoondokewa na mwanagu Maggid mwaka jana

Cisco akitaniana na Franco Kabigi (RiP) wakati wa 'kuufinya' baada ya kisomo cha kurehemu waliotangulia mbele ya haki Leaders Club

Umati wakati wa Sunday Soccer Bonaza Leaders Club

Mwadila Investments ilikuwa mojawapo ya timu za Kinondoni zilizoshiriki Bonanza hilo

Uncle Phil akiwa tayari 'kuufinya'

Wadau kutoka kila pembe ya jiji walishiriki hafla ya kurehemu waliotangulia mbele ya haki

Umoja wa wana Dar es salaam usioweza kusahaulika

Mpunga ukifinywa

Umoja wa wana Dar es salaam

Cisco (kulia, mwenye shati la Bluu) akipiga stori zake

Cisco akiwa kazini siku Rais wa Marekani Bill Clinton alipozuru Tanzania

Balozi Cisco akiwa kazini Lagos, Nigeria, kwenye mkutano uliohudhuriwa na Baba wa Taifa ma viongozi wengine wa AfrikaCisco akiwa katika kisomo klabu ya Saigon ambako alikuwa mwanachama

Cisco akiwa kazini kama mkuu wa Itifaki

Cisco akiwa na Mwalimu na Madiba
 

GENTAMYCINE

JF-Expert Member
Jul 13, 2013
36,840
2,000
Kuna Watu mnajifanya Masela / Watoto wa Mjini ila kwa taarifa za Watu wa zamani wanakuambia kuwa huyu Marehemu ndiyo alikuwa Msela / Mtoto wa Mjini hasa na uzuri wake alikuwa pia ni Msomi mzuri mno tofauti na Masela wa sasa hivi ambao Vichwani mwenu kumejaa tu maji machafu na Elimu hamna labda ya Kuiba / Kukaba tu.
 

MLAU

JF-Expert Member
Aug 23, 2007
4,727
2,000
Uncle Issa Muhidini Michuzi umemuelezea vizuri sana Balozi Cisco ktk wasifu wake kwa jamii na kipindi kile maisha yalikuwa poa sana Dar.

Jamaa alikuwa mtoto wa mjini na alijua kuishi na jamii za aina zote.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom