Mtutura: Tunataka chakula Mezani kwa Kila Mtanzania

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
606
1,540
Uchambuzi wa Bajeti ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/24

Utangulizi
Jana Jumatatu Mei 08, 2023 Waziri wa Kilimo Ndg. Hussein Bashe (Mb) aliwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo katika Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania. Bajeti ambayo imeanza kujadilia siku jana na leo watajadili na kuipitisha bajeti.

Kwa kutumia fursa hii ya kuendelea kujadiliana ili kwa wakati uliopo yapo mambo yanaweza kufanyiwa marekebisho madogo ili kuhakikisha mpango na bajeti unaakisi mahitaji ya wananchi.

Kutokana na umuhimu huo, ACT Wazalendo kupitia kwa Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi tumefuatilia hotuba hiyo na kuifanyia uchambuzi wa kina ili kubaini kama hotuba hiyo inaakisi hali halisi ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima hapa nchini.

Kupitia uchambuzi huu tumekuja na hoja kubwa nane (8) kuhusu bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

1. Hali ya upatikanaji na uzalishaji wa chakula
Kwa misimu miwili (Msimu wa mwaka 2021/22 na 2022/23) mwenendo wa bei za chakula (nafaka) umekuwa ukiendelea kupanda zaidi. Bei za mazao ya nafaka na bidhaa zingine za chakula katika miji mikubwa na mikoa nchini bado zipo juu hadi sasa katika msimu wa mavuno. Uchambuzi wa bei za vyakula unaonyesha kuwa; Mchele- 2021 ulikuwa Shilingi 1500-2000 bei ya Sasa ni Shilingi 2900-4,000; Unga wa Ugali ni Shilingi 800-1000 (2021) kwa sasa Shilingi 1800-2200; Ngano- Shiling1500-1800 (2021) kwa sasa- Shilingi 2000-2500; Maharage-Shilingi 1600-2000 (2021) kwa sasa (Shilingi 3500-4000);

Tathimini ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini kwa mwaka 2021/22 kwa mujibu wa taarifa za Wizara zinaonyesha umeshuka sana hadi kufikia tani Milioni 17.1 kutoka tani milioni 18 za msimu wa 2020/21. Uzalishaji wa mazao ya chakula umeshuka asilimia 15, upungufu huu una mchango mkubwa kwenye kuathiri mwenendo wa bei za vyakula na kuwepo kwa uhaba wa chakula nchi kwa baadhi ya maeneo. Ingawa, mahitaji ya chakula katika msimu wa 2022/23 yalikuwa tani milioni 15.0 hivyo kuwa na ziada ya tani milioni 2.0.

Hii ndio maana tumeona pamoja na hali ya uzalishaji wa chakula kwa ujumla umeonyesha tumejitosheleza, lakini kuna baadhi ya maeneo yamekumbwa na uhaba wa chakula na kusababisha mfumuko mkubwa wa bei za chakula katika nchi kwa ujumla wake. Ni wazi kuwa uwezo wetu kama nchi wa kuhifadhi chakula cha kutosha ni mdogo sana (kwa sasa tunaweza kuhifadhi tani laki 4 hadi 5) kiasi cha kuathiri usambazaji na upatikanaji wa chakula kwenye maeneo yenye mavuno hafifu.

Hofu yetu ni kuwa mwelekeo wa Serikali unaweza kupelekea msimu huu wa kilimo kuwa na hali mbaya zaidi kutokana na hali ya hewa na upatikanaji wa mvua nchini. Hivyo, tutakuwa kwenye hali ngumu zaidi kwa kuwa hakuna hatua madhubuti za kutoa nafuu kwa wananchi. Katika hotuba ya Waziri wa Kilimo ameeleza nia ya Serikali kuongeza uwezo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wa kununua chakula kutoka kwa wakulima kiasi cha tani 500,000 kama akiba ya chakula (Nyongeza ya tani lakini 4). Hatua hii bado haitoshi kujiandaa na baa la njaa au kuweza kusaidia kukabiliana na mfumuko wa bei.

Utafiti uliofanywa na ACT Wazalendo mwezi Machi-April 2023 unaonyesha kuwa jambo moja kubwa linalotia hofu Watanzania ni kupanda kwa gharama ya maisha na hasa gharama za chakula. Asilimia 75 ya Watanzania walisema hofu yao kuu ni hiyo. Serikali ya CCM haijajihangaisha kukabiliana na changamoto hii ili mwaka huu na miaka inayofuata kusiwe na changamoto hii au ipungue kwa kiwango cha kutoa nafuu kwa wananchi. Wakati umefika sasa Serikali ianze kuhangaika na NJAA. Siasa bora ni siasa inayoweka chakula mezani kwa wananchi.

ACT Wazalendo tunaisisitiza Serikali kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha angalau miezi 3 kutoka kwenye chakula kitachovunwa mwaka huu ili kujilinda na upungufu wa chakula. Ukweli uko dhahiri sasa kuwa maeneo mengi ya nchi yetu uzalishaji wake unaweza kuwa sio mzuri kwa mwaka huu.

Hatua hii itawezakana kwa Serikali kuongeza bajeti kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ya kutosha kununua chakula (Tani Milioni 1.5 za Mahindi, Tani laki 5 za Mpunga, Maharagwe tani Milioni 1) badala ya tani laki 5 pekee. Aidha, kuwezeshwa Bodi ya mazao mchanganyiko kununua na kusambaza chakula kwenye eneo linaloonyesha uhaba/upungufu wa chakula.

Mwisho, Serikali iweke mazingira bora kwa wakulima wadogo ili kuongeza uzalishaji zaidi; kwa kuendelea kutoa ruzuku katika mbolea na kusimamia usambazaji wake; kuhakikisha usalama wa ardhi kwa wakulima wadogo kwa kushughulikia migogoro ya ardhi.

2. Ukuaji wa Sekta ya Kilimo ni mdogo sana kusukuma maendeleo ya Kilimo.
Chama cha ACT Wazalendo hakiridhishwi na usimamizi wa sekta ya Kilimo katika kuelekea kufikia malengo ambayo Serikali yenyewe imejiwekea. Serikali inataka sekta ya Kilimo iwe na kasi ya ukuaji wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Hata hivyo ukisoma hotuba ya Waziri wa Kilimo Ndg. Hussein Bashe huoni mtitiriko wa mabadiliko katika kufikia lengo hilo. Kwa mfano mwaka 2021 kasi ya ukuaji wa sekta ilikuwa ni 3.9%, Waziri hajaiambia nchi mwaka huu 2023 wanatarajia kasi ya ukuaji kufikia asilimia ngapi? Kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo haiwezi kufika tu 10% mwaka 2030. Lazima ipande kutoka ilipo sasa hadi kufikia huko. Waziri hajalieleza bunge tunafikaje 10% Mwaka 2030.

Sisi, ACT Wazalendo tunakiweka Kilimo katikati ya vita kupambana na umaskini. Tanzania haiwezi kuondoa umaskini kwa kauili mbiu tu bali kwa kuwa na mwono wa wazi katika mipango ya kilimo. Sura ya umaskini wa watu wetu ni MKULIMA! Tunahitaji kuongeza pato la mtu mmoja mmoja, kama tunahitaji kuongeza maradufu pato la mtu mmoja ifikapo 2050, tunapaswa kuwa na pato la taifa yaani GDP ya dola za Kimarekani bilioni 455. Hii ni sawa na kuongeza pato la taifa mara 6.5 kutoka sasa. Lakini kazi kubwa ya kufanya mageuzi ya uchumi wetu inahitaji kuambatana na nidhamu ya hali ya juu.

Tunahitaji uchumi wetu ukue kwa kasi ya wastani wa 8% kwa mwaka, kwa miaka miaka 10 mfululizo ya mwanzo na kasi isipungue asilimia 6 kwa miaka mingine 10 hadi kufikia 2050. Miaka 10 ya mwanzo, kilimo kinapaswa kuwa sekta kuu ya kuchochea ukuaji isiwe chini ya asilimi 6 hadi 8 kwa hiyo miaka 10 mfululizo.

Waziri anapaswa kulieleza Taifa tunafikaje kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kuanzia mwaka huu na kuendelea? Mwaka jana tumeona uzalishaji wa mazao umeshuka kwa asilimia 15 katika hali kama hii Sekta ya Kilimo itawezaje kuwa injini ya kuondoa umaskini?

3. Hali ya usambazaji wa pembejeo za kilimo
Hali ya upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa mwaka 2022/23 imekuwa sio nzuri hususani mbolea ya ruzuku na viuatilifu vya maji na unga (salfa) kwa zao la korosho. Upatikanaji wa mbolea na pembejeo zingine za kilimo kwenye misimu miwili mfululizo umekabiliwa na changamoto za kupaa kwa bei kiasi cha kutishia kabisa uzalishaji na kupelekea kupanda kwa bei za vyakula kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.

Chama chetu kilitoa mapendekezo kadhaa ya kukabiliana na hali ya kupanda kwa bei za pembejeo ikiwemo kuitaka Serikali iweke ruzuku ili kushusha bei za mbolea kwa wakulima. Serikali ilichukua pendekezo letu, kwetu ilikuwa hatua muhimu na ilibeba matumaini makubwa kwa wakulima kwa matarajio ya kupunguziwa gharama (zilizokuwa zinaendelea kupaa) na kuhakikishiwa urahisi wa upatikanaji.

Hata hivyo utekelezaji wake ulikuwa na changamoto nyingi zilizoathiri usambazaji, upatikanaji na matumizi ya mbolea kwa wakulima. Changamoto kubwa zilizoibua vilio na malalamiko ni kama zifuatazo;

Mosi, umbali wa vituo vilivyotumika kusambaza mbolea, kuna baadhi ya maeneo bei ya mbolea ya ruzuku iliuzwa kwa gharama kubwa zaidi (dola 59, 63 na 70) na kwa kutumia fedha za kigeni (dola); mawakala wengi walikuwa wanapatikana maeneo ya mijini wakati wakulima wapo vijijini, wakulima walilazimika kutumia gharama zaidi ili kuweza kutapa mbolea. Pia, mawakala wasio waaminifu kusambaza mbolea bandia na zilizokosa ubora. Idadi ya mawakala kuwa ni chache ukilinganisha na uhitaji.

Pili, changamoto za Usimamizi; Serikali kutosimamia na kufuatilia kwa karibu mfumo wenyewe kiasi cha baadhi ya wafanyabiashara waagizaji na wasambazaji kuhujumu kwa kuweka mgomo baridi uliopelekea kuwepo kwa shida ya upatikanaji na usambazaji wa mbolea. Pia, usajili wa wakulima kutumika kama vile ndio kigezo cha kupata mbolea ya ruzuku badala ya kuwa na mfumo wa kutambua mahitaji halisi.

Kwa upande wa usambazaji wa viuatilifu (pembejeo za korosho) nao ulikuwa na changamoto kadhaa zilizoathiri mazao ya korosho hata kushusha kufikia tani 175,000 mwaka 2022/23. Changamoto hizo zikiwemo ni kucheleweshwa kwa pembejeo, mfumo mbovu wa usambazaji, kusambazwa kwa pembejeo bandia na baadhi ya maeneo (Tunduru, Tandahimba, Newala) kupata mbolea kiduchu.

Katika mpango wa Serikali 2023/24 umeonyesha nia ya kuendelea kutoa ruzuku lakini haujaonesha namna utakavyoenda kukabiliana na changamoto zilizobainika. Ni wazi ruzuku inaweza kutafunwa tu bila kuleta matokeo tarajiwa ya kukuza maendeleo ya kilimo.

Aidha, tumeona Serikali imefanyia kazi mapendekezo yetu ya kuiwezesha Kampuni ya Taifa ya mbolea (TFC) kwa kutengewa bajeti kiasi cha shilingi bilioni 40 (kuifanya kuwa na mtaji wa bilioni 46) ili iweze kushiriki kwenye soko la mbolea (kuagiza na kusambaza).

ACT Wazalendo tunaendelea kuitaka Serikali kuiwezesha Kampuni hii kuagiza kiasi kikubwa zaidi (angalau iwe na uwezo wa kuagiza nusu ya mahitaji ya mbolea nchini). Hivyo, iiongezee TFC bajeti ili kushiriki kikamilifu kwenye ununuzi wa mbolea (uagizaji nje) na usambazaji wake kwenda ngazi za chini kwa ajili ya kuongeza uwezo wa usambazaji wa mbolea na kuondosha upungufu unaosababishwa na kulegalega kwa waagizaji na wasambazaji binafsi.

Vilevile, kwa hatua za muda mrefu Serikali isimamie ukamilishaji wa uwekezaji wa viwanda vya mbolea nchini ili kuondoa utegemezi wa kuagiza mbolea nje ya nchi,

4. Kutofungamana kwa Kilimo na sekta ya Viwanda
Muundo na sifa za uchumi wa nchi yetu, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika unatawaliwa kwa sehemu kubwa na sekta ya uzalishaji wa malighafi (Extractive Industry) hususani kilimo, uvuvi, misitu na madini. Kwa upande wa kilimo sehemu kubwa ya mazao yanayoingiza au kuchangia pato la taifa ni mazao ambayo yanatumika kama malighafi inayotegemea soko la nje.

Uzalishaji wa mazao unaofanywa na wakulima hauna uhusiano mkubwa na sekta ya viwanda vilivyopo nchini, jambo ambalo linaathiri, maendeleo ya kilimo chetu kwa namna mbalimbali.

Kwanza bidhaa zinazozalishwa viwandani hazijibu changamoto zinazokikabili kilimo Chetu. Kama tulivyobainisha hapo mwanzo, asilimia 95 ya mbolea inayotumiwa na wakulima nchini haizalishwi ndani, pia viuatilifu na zana za kazi nazo zinaagizwa kutoka nje. Hivyo hivyo, kwa upande wa kilimo malighafi zinazozalishwa zinasafirishwa nje kwa ajili ya viwanda vya ughaibuni. Mazao kama pamba, korosho, mbaazi, katani n.k ni mifano michache kuthibitisha hoja.

Pili, kuhusu zana za kilimo, kwa mwaka 2022/2023 ni matrekta makubwa 1,700 na madogo 1,959 ndio yaliyoingizwa nchini taarifa za TRA zinaonesha ni mashine za kuvunia 22 plau za matrektani 37,840, haro za matrekta 6,258, mashine za kupura 82,802 zana za kupandia 10,725 majembe ya kukokotwa na wanyamakazi 603,57 hii ni idadi ndogo mno.
Kwa kutazama mipango ya Serikali ni wazi haina dhamira ya dhati ya kumaliza muundo huu wa uzalishaji wa uchumi wetu ili kukisaidia kilimo na wakulima wetu.

ACT Wazalendo, tunaendelea kusisitiza kuwa ni wakati sasa wa kuunganisha maendeleo ya viwanda na ukuwaji wa kilimo. Pia, Serikali iweke mkazo kwenye viwanda vidogo maeneo ya vijijini vinavyoendeshwa, kumilikiwa na kusimamiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vya ushirika ambavyo vitaweza kuzalisha ajira na kuchakata mazao kwa dhamira ya kuyaongezea thamani.

Tunaitaka serikali, kupitia taasisi zake, kuingiza matrekta (imara) na kuyauza kwa ruzuku na kwa mkopo wa masharti nafuu kwa wakulima.

5. Uporaji wa ardhi ya wakulima na migogoro ya wakulima na watumiaji wengine.
Changamoto ya migogoro ya ardhi inazidi kuwa kubwa kila uchao. Kiasi cha kuwa na mchango mkubwa wa kuathiri mwenendo wa kilimo na usalama wa chakula nchini. Miongoni mwa sababu ni wimbi kubwa la uwekezaji wa mashamba makubwa. Migogoro inatokana na dhana iliyojengwa kuona kwamba ardhi ni mtaji au bidhaa. Kwa mtazamo huu, ardhi inachukuliwa kwamba inapaswa kutengeneza faida zaidi kuliko kukidhi mahitaji ya kijamii.

Ndio maana tunashuhudia Serikali ya CCM inapora ardhi kutoka kwa wananchi wazawa kwa ajili ya wawekezaji au inachukuliwa kutoka kwenye miliki ya vijiji au wanavijiji ili kupatiwa mtu mmoja atakayetumia kwa ajili ya kupata faida. Migogoro ya wakulima na wawekezaji ni mingi sana na mingine inachukua muda mrefu.

Pili, Migogoro ya wakulima na wafugaji kwa miaka ya hivi karibu imezidi kushika kasi kubwa hapa nchini. Migogoro hii kwa sehemu kubwa hutokana na mifumo ya umiliki na matumizi ya ardhi miongoni mwa makundi haya mawili. Athari za migogoro hiyo imepelekea kuwa na mapigano baina ya wakulima na wafugaji, mauaji, uharibifu wa mali, ulemavu na kutoa matishio ya amani na usalama nchini. Mikoa ambayo inaonyesha kuchomoza kwa kasi ya Migogoro hiyo kwa sasa ni Mikoa ya Kusini (Lindi, Mtwara, Ruvuma), Magharibi Kigoma na Katavi ambayo zamani hakukuwa na migogoro hiyo kabisa.
Sababu kubwa ya migogoro ni kutokuwa na mazingira mazuri ya ufugaji hususani malisho na malambo ya kunyweshea mifugo yao.

Serikali inakwepa jukumu la kusimamia uboreshaji wa mazingira ya ufugaji ili kuwa na huduma hizo kwa wafugaji wadogo. Uzoefu unaonyesha migogoro inatokea kuanzia mwezi wa Juni hadi mwanzoni mwa mwezi Januari kila mwaka. Kipindi ambacho mito, mabwawa na nyasi hazipatikani kwa urahisi kwenye maeneo ya malisho ya mifugo. Hivyo, wafugaji kuswaga mifugo yao kwenye maeneo ya wakulima ili wapate maji na malisho ya kutosha.

Tatu, migogoro kati ya wananchi Wafugaji na Mamlaka za hifadhi imezidi kushika Kasi hapa nchini, Mamlaka za Hifadhi bila kujali athari kwa wananchi zimekua zikichuka maamuzi ya kumega maeneo ya wananchi na kuyatia kwenye Hifadhi jambo linaloacha madhara makubwa sana kwa wananchi mfano mzuri wa kadhia hii ni Mgogoro kati ya Wafugaji wa eneo la Ngorongoro. Migogoro ya wafugaji na hifadhi Kigoma (Kageramkanda Kasulu, Mpeta Nguruka), Tunduru hifadhi ya Selous.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iharakishe na kukamilisha zoezi la kupima, kurasimisha na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili kuepusha migongano na mivutano. Vilevile, Mamlaka za Halmashauri zijengewe uwezo stahiki na kuwezeshwa ipasavyo ili ziweze kushugulikia migogoro ya ardhi upesi na kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha ardhi imepimwa na kurasimishwa kwa wananchi

Pia, tunaitaka Serikali iainishe umiliki wa ardhi na kuwarejeshea maeneo yaliyobinafsishwa ili kuondoa migogoro inayoendelea hapa nchini.
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali isitishe kabisa tabia ya kupanuwa maeneo ya hifadhi kwa kuwanyang’anya wananchi maeneo yao ya kulisha mifungo na kilimo. Kwani upanuzi huo unafifisha jitihada za wafugaji na wakulima katika uendeshaji wa shughuli zao za uchumi.

6. Kilimo cha Umwagiliaji.
Pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji (Irrigation Development Fund (IDF)) Kupitia tume ya Taifa ya umwagiliaji (NIRC), bado sekta hii ya umwagiliaji haiwanufaishi wakulima. Tanzania ina mabonde mengi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, hivyo ni mhimu kwa nchi kuwekeza katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji ili sekta hii iwe na tija kwa taifa.
Tunaamini kuwa mabonde tuliyonayo Tanzania, yakitumika ipasavyo tuna uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha hapa nchini na ziada tukauza katika mataifa mbalimbali Afrika na ulimwenguni kote.

Hapa nchini hakuna haja yoyote ya kutegemea mvua za misimu Ili kusukuma maendeleo ya Kilimo kwani Kuna vyanzo vingi na vikubwa vya maji Mfano bonde la mto Rufiji lina ardhi nzuri na yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha mpunga. Bonde hilo likitumika kisayansi linaweza kuzalisha mchele wa kutosha na ziada.

Mabonde mengine ni pamoja mabonde ya mwambao wa ziwa Victoria, Nyasa, Tanganyika, mto Ruvuma, mto Ruvu, mto Pangani na mto Malagalasi.

Chama cha ACT Wazalendo tunaiagiza Serikali kuwekeza nguvu zaidi kwenye mabonde ya Mto Ruvu, Rufiji, Pangani, Kilombero, Ruvuma, Mbwenkuru, Ruaha, Kihansi, Mara, na mabonde ya ziwa Tanganyika na Victoria. Kama Taifa litawekeza nguvu na maarifa ya kutosha maeneo hayo Taifa litajihakikishia akiba ya chakula cha kutosha na ziada kujipatia pesa za kigeni.

7. Kusuasua na ubadhirifu katika miradi ya ujenzi wa maghala na Vihenge vya kuhifadhia chakula
Kwa miaka mitatu mfululizo Serikali imekuwa ikitaja kuweka kipaumbele cha kuimarisha miundombinu ya uhifadhi ya chakula kwa kujenga maghala mapya na vihenge kwa lengo la kuongeza uweza wa nchi wa kuweka akiba ya chakula. Lakini, imekuwa kama sehemu ya viongozi na wasimamizi kufanya ubadhirifu na kupelekea miradi kutokamilika kwa muda mrefu.

Katika uchambuzi wa ripoti ya CAG mwaka jana tulionyesha namna CAG alivyobaini kutojengwa kwa vihenge wala maghala na kutapeliwa kiasi cha shilingi bilioni 87.2 na Mradi uliopaswa kukamilika mwaka 2017 na kusogezwa mbele hadi 2020 hata hivyo hadi mwaka 2021 ulikuwa haujakamilika.

Katika ripoti ya CAG iliyotolewa mwaka huu inaonyesha kutelekezwa kwa vihenge na magahala 14 kwenye Kijiji cha Endanoga katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara. Thamani ya mkataba ilikuwa Shilingi bilioni 1.1 na tarehe ya kukamilika ilipaswa kuwa tarehe 30 Agosti 2022 lakini sasa haujakamilika na Mkandarasi alilipwa kiasi cha Shilingi Milioni 241.5 sawa na asilimia 22.5 ya thamani ya mkataba.

Pamoja na kupewa kiasi hicho mkandarasi hakuwepo eneo la ujenzi tangu alipoondoka mwezi Aprili 2022 pasipo kutoa taarifa kwa Wizara husika kinyume na kifungu 6.7.1 (a) (b) cha Masharti ya Jumla ya Mkataba ambacho kinamuhitaji mkandarasi kumuarifu mwajiri ikiwa ameshindwa kutimiza majukumu yake ya mkataba au kama anataka kusitisha mkataba.
Mapungufu haya yametokana na Menejimenti ya Wizara kushindwa kusimamia vipengele vya mkataba vinavyomtaka mkandarasi kuwepo eneo la ujenzi au kutoa taarifa ya kutokuwepo kwake na hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo hatatekeleza vipengele hivyo.

ACT Wazalendo tunaitaka Wizara ya Kilimo ichukue hatua zifuatazo; Mosi, iwasiliane na mkandarasi ili arudi kuendelea na ujenzi bila ya kuchelewa zaidi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maghala 14 na miundombinu ya nje saidizi.
Pili, ichukue hatua za kimkataba dhidi ya mkandarasi kwa kuvunja kifungu 6.7.1 (a) na (b) cha Masharti ya Jumla ya Mkataba.

Tatu, unataka uchunguzi ufanyike ili kubaini anayekwamisha mradi huu muhimu kwa taifa na hatua za kisheria zichukuliwe baada ya uchunguzi kufanyika na kubaini wahusika.

8. Kukosekana kwa mfumo wa kodi na sheria ya kusimamia kilimo
Kukosekana kwa mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka katika kuisimamia sekta ya Kilimo inarudisha nyuma maendeleo ya wakulima. Kilio cha kuporomoka kwa bei ya mazao, wakulima kutooana tija ya jasho lao ni kutokana na Serikali kutoweka mkazo na kuipuuza sekta ya kilimo kwa kutowekwa mfumo mzuri wa Usimamizi, sheria na kodi ili kuhakikisha wakulima wananufaika.

Ingawa Tanzania imeendelea kutegemea Sekta ya Kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake kwa kuajiri asilimia 65 ya nguvu kazi ya Watanzania wote na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye miaka yenye mvua za kutosha. Lakini bado hali za wakulima hazijabadilika na kunufaika na kilimo chao. Mfano wakati wa ziara zetu za chama tulipofika Tabora tulikuta malalamiko kutoka wakulima wa Tumbaku wa Urambo Tabora kwamba bei ya sasa ya Tumbaku, mkulima ananufaika sio zaidi ya asilimia 35 ya bei ya soko la dunia, zote zinazobaki zinapita kwenye mikono ya wajanja.

Inashangaza katika nchini moja, Sheria ya madini ipo na mfumo wa kodi wa madini upo, sheria ya mafuta na Gesi ipo na mfumo wa kodi wa Mafuta na Gesi upo, nchi hii asilimia sitini na saba (67%) ya watu wanategemea kilimo lakini hakuna sheria ya Kilimo wala hakuna mfumo wa kodi maalum kwa ajili ya sekta ya kilimo, ndio maana tunasema CCM imechoka.

Hivyo basi, Wito wetu, ACT Wazalendo ni kuwa Serikali itunge mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka (stable fiscal regime) katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa mkulima anabakia na sehemu kubwa ya mapato yake
Hitimisho.

Tanzania imeendelea kutegemea Sekta ya Kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake kwa kutoa ajira kwa asilimia 61.1 ya nguvu kazi za watanzania wote na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye miaka yenye mvua za kutosha. Hivyo, mpango wa bajeti unapaswa kubeba dhima hiyo kukabiliana na changamoto za uzalishaji, uhifadhi na mauzo ya chakula. Kuhakikisha wakulima wanapata kwa wakati pembejeo za kilimo kwa kuwekewa ruzuku ili kuwawezesha kumudu gharama na kuongeza tija katika uzalishaji. Aidha, mikakati ya kilimo lazima ifungamanishwe na viwanda ili kuongeza thamani, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha kunakuwa na masoko ya uhakika wa bidhaa za mazao ndani ya nchini na zaida kusafirishwa nje.

Katika uchambuzi wetu tumeona Mwenendo wa bei za vyakula utaendelea kupanda ikiwa bajeti ya kilimo haitongezwa hususani kuiwezesha NFRA kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha. Bado miradi mingi ya umwagiliaji ipo katika hatua ya ndoto, na hata iliyokwisha kuanza kutekelezwa inaenda mwendo wa konokono. Hali na Mwenendo huu wa bajeti ya kilimo itachukua muda mrefu zaidi kupiga hatua ya maana katika nchi yetu.

Imetolewa na;
Ndg. Mtutura Abdallah Mtutura
Twitter: @MtuturaAbdallah
Waziri Kivuli wa Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi
ACT Wazalendo.
09 Mei, 2023
IMG-20230509-WA0057.jpg
 

A chicken in every pot, and a car in every backyard - Herbert Hoover


Huu msemo ulitumiwa sana na Raisi wa Marekani Herbert Hoover wakati wa kampeni zake za kutafuta uraisi, akimaanisha akipewa nchi ataleta maisha bora kwa kila raia wa Marekani. Akataja matatizo ya kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei yaliokuwepo kwenye serikali ya Raisi Calvin Coolidge. Alikosoa kwelikweli na wamarekani wakamwamini.

Kimbembe kilianza pale alipopewa nchi na kugeuka kuwa kichekesho na kushindwa kudhibiti mfumuko wa bei, huku akifahamu kwamba matatizo ya mfumuko wa bei hayakuwa ya Marekani peke yake kwasababu dunia nzima ilikuwa kwenye mdororo mkubwa wa kiuchumi (The Great Economic Depression) ambao uliikumba dunia tokea mwaka 1928.

Nilichokuja kujifunza ni kwamba, ndani ya karne ya 21 sekta nyeti za nchi kama kilimo huathiriwa na mambo yaliyokuwa ndani na nje ya nchi. Hivyo ukiangalia sababu za ndani peke yake bila kuzingatia mwelekeo wa dunia na jinsi unavyoathiri hii sekta utaangukia pua, lakini pia vivyo hivyo ukiangalia sababu za nje peke yake na kutozingatia zile za ndani pua lazima utaangukia.

Nimefurahishwa sana na hoja ya nne, ya kutofungamana baina ya wizara ya kilimo na viwanda. Mmegusia mambo ya msingi sana, japo binafsi naona zaidi ya hapo. Wizara nyeti kama kilimo haitakiwi iungwe na wizara ya viwanda peke yake. Matatizo kama mfumuko wa bei yanapoikumba nchi ambayo asilimia zaidi 70% ya wananchi wake hutegemea kilimo, hadi kutishia usalama wa chakula (Food Security) huwezi kuzitegemea hizi wazara mbili peke yake. Juhudi za ziada zinatakiwa kufanywa..

Binafsi naamini Tanzania iko vizuri, tatizo ni kushindwa kupangalia mambo vizuri na kusisitiza ufuatiliaji. Sekta kama kilimo haitakiwi iachwe chini ya waziri na makatibu wake wakiwa wao ndiyo wanaopanga na kutunga sera mpya kila siku. Tena wao ndiyo wasimamie karibia kila bodi ya kilimo hapa nchini, huku wizara ikiwa na nguvu ya kutegea wanabodi na kupewa mamlaka makubwa kuingilia kisiasa utendaji wa hizi bodi. Hili haliwezi kuisaidia nchi hata siku moja.

Leo Raisi Samia na Ndugu Bashe wanaweza kushaurina tu waende kwenye maghala ya korosho Mtwara na kufanya wanachotaka na hayo mazao bila kuwajibishwa na mtu kwasababu sheria inawahusu. Nchi nyingine kilimo ni kitu muhimu, lakini wameamua kufanya DECENTRALIZATION THROUGH AUTONOMIZATION. Mikoa inapangiwa mazao ya kuzalisha kutokana na uhitaji wa soko. Mfano, mkoa wa Kagera unakuwa na bodi maalumu ya wataalamu wa zao la tumbaku ambayo inakuwa ni FULLY AUTONOMOUS, BEARING IT'S OWN SEAL and CAPABLE OF SUING AND BEING SUED, bila kuingiliwa na wanasiasa.

Kazi ya hii bodi ndiyo itakuwa na kazi maalumu ya kushauri na kusimamia wakulima wa zao husika pamoja na kutoa pembe-jeo za kilimo, mikopo na mambo mengine kwa wakulima wakubwa na wadogo ikishirikiana na mabenki ya kilimo kama TADB na benki taasisi nyingine muhimu za kifedha. Mwisho wa siku bodi hizi, zitatakiwa kuwa na BOARD OF TRUSTEES ambao ndiyo humiliki mali za wakulimu kama mapato, maghala na fedha huku zikiwajibika kwa wizara ya kilimo.

Wizara ya kilimo iwe mwamvuli tu unaosimamia katika kisera taasisi za kilimo ambazo zinajiendesha zenyewe. Upande mwingine serikali iwe inanua mazao kwa hizi bodi ambazo pia zitakuwa zinalipa kodi kwasababu ni taasisi huru zinazojiendesha zenyewe. Kuna baadhi ya mambo wakoloni waliyaona na kuyafanya lakini serikali ya kijamaa ikaamua kuyavunja na kusababisha umasikini mkubwa kwa watu.
 
Back
Top Bottom