Mtoto Wa Mkulima Na Wasomi Wa Mlimani ( Makala Raia Mwema)

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,500
Na Maggid Mjengwa,WAKATI wa uhai wake, Profesa Abdulrahman Babu alipata kusema kuwa ukichanja mwili wa Mwafrika basi, kwenye damu yake utaona kuna chembe chembe za mkulima. Profesa Babu alimaanisha kuwa kwa asili Mwafrika ni mkulima.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametamka hadharani kuwa yeye ni “Mtoto wa Mkulima”. Lakini, tukimrejea Profesa Babu, tunaona, kuwa tulio wengi tu watoto, au tuna asili ya watoto wa wakulima. Ni bahati mbaya, kuwa watoto wengi wa wakulima wamekuwa wakiionea haya historia yao.


Majuzi hapa Pinda alizuru Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mlimani. Akakutana na bango la watoto wenzake wa wakulima. Walimwambia; ”Mtoto wa Mkulima, tunalala nje!” Iliwachukua dakika kadhaa kwa Pinda na Mkuu wa Chuo hicho Prof. Mukandara kujadili namna wanafunzi hao walivyofaulu kupenyeza bango hilo ndani ya ukumbi ule wa Nkrumah. Hatimaye Pinda akaweka wazi; kuwa ujumbe umefika.Kisha akajibu ujumbe ule wa watoto wenzake wa wakulima kwa kuahidi kutoa shilingi milioni kumi kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.


Labda wanafunzi wale wa Chuo Kikuu walikuwa na ujumbe mzito uliojificha katika maelezo yao yale kupitia bango lile, au ndivyo walivyojipanga; kumwambia tu mtoto mwenzao wa mkulima, kuwa tunalala nje, basi. Maana, kama tatizo ni kulala nje , Mizengo Pinda hakupata tabu sana kuingiza mikono mfukoni kuitafuta milioni kumi kwa mwaka.
Lakini, kama watoto wale wa wakulima pale Mlimani wangemwuliza Waziri Mkuu wao swali lifuatalo; “Mtoto wa Mkulima, kwanini tunalala nje? Ni dhahiri, Pinda asingekimbilia kuingiza mikono mfukoni. Maana, hutokea kwangu nikakutana na kijana anayeniambia; “Braza, sijala tangu asubuhi!” Jibu langu laweza kuwa; chukua elfu moja hii , nenda ukale!


Lakini, kama kijana huyo huyo ataniuliza; “Braza , nimemaliza chuo kikuu, sina ajira wala hakika ya kula yangu ya kila siku. Unaweza kuniambia ni kwa nini katika nchi hii vijana wasomi wanakosa ajira na hakika ya kula yao?” Swali hilo halitaukimbiza mkono wangu mfukoni kuisaka elfu moja ya kumpa kijana huyo. Litanifanya niumize kichwa.


Na katika historia tunasoma, kuwa kuna wakati, nchini Ufaransa, alitokea Malkia aliyeitwa Marie Antoinette. Malkia huyu aliamka asubuhi moja kwenye kasri yake na kukuta maandamano ya wakazi wa jiji la Paris. Waandamanaji walibeba mabango yenye kusema; Hatuna mikate. Naye Malkia aliwatazama wasaidizi wake, kisha akatamka; “ Basi, wapeni keki!” Jibu la Malkia lilikuwa jepesi sana kwa tatizo kubwa.


Watanzania sasa tumepata Waziri Mkuu “Mtoto wa Mkulima”. Tunajisikia yu miongoni mwetu. Huko nyuma nilipata bahati ya kupishana kwa gari na Pinda. Takribani juma moja kabla hajateuliwa kuwa Waziri Mkuu. Ilikuwa ni katika barabara ya Sumbawanga – Mpanda. Nilikuwa nikitokea Nkasi. Nilimwona Pinda akiwa katika gari la kawaida kabisa. Alikuwa njiani kuelekea kwao Mpanda. Nilipofika Sumbawanga mjini nikalikuta shangingi la Waziri Pinda. Wakati huo Pinda alikuwa waziri wa TAMISEMI. Kumbe, hata wakati huo Pinda hakupenda kutinga kijijini kwao na shangingi la kifahari na la gharama kubwa. Ni sahihi, maana mashangingi haya ya waheshimiwa hayafanani kabisa na hali za umasikini mkubwa wa wananchi wanaowaongoza.


Na sisi Waafrika kwenye damu zetu kuna chembechembe za ushamba. Tumetofautiana tu wingi wa chembechembe hizo. Ndiyo maana utamsikia Mwafrika mwenzako anajitambulisha kwa kusema “Mimi ni Dk, Injinia, Profesa au Mheshimiwa Maganga!” Hizi ndizo chembe chembe za ushamba zilizomo kwenye damu ya Mwafrika. Ndiyo hao, akipewa shangingi la Serikali ni lazima awaonyeshe Watanzania wenzake.


Na leo tunaambiwa kuwa Pinda amelikataa shangingi la gharama kubwa. Ni jambo jema, lakini kuna maswali; shangingi hilo alilolikataa Waziri Mkuu Pinda limekwenda wapi? Limerudishwa dukani lilikonunuliwa, au? Tunachohitaji sasa ni mabadiliko ya kimfumo na si jitihada za kuzima moto. Ijulikane wazi Serikali iko tayari kugharamia magari ya kiwango gani. Kule Rwanda Serikali ya Kagame imeliweka wazi suala kama hilo.


Na nyongeza hapa ni ukweli, kuwa Waziri Mkuu Pinda ndiye Waziri Mkuu wetu. Tunadhani anayo mamlaka ya kufanya zaidi ya kukataa shangingi hilo. Si ana mamlaka pia ya kubuni na kuwezesha utekelezaji wa utaratibu mpya wa ununuzi wa magari ya Serikali yanayotumiwa na mawaziri walio chini yake. Maana, mashangingi haya sasa ni kero nyingine kwa wananchi. Hivi ni mwiko kwa waziri wa Serikali ya Tanzania kutumia gari ya aina ya Toyota Prado au Hardtop? Walau hayo yanafanana na hali yetu kama nchi.


Waziri Mkuu wetu Pinda ana fursa ya kufanya maamuzi magumu na kuacha legacy nyuma yake, maana bado ana umma nyuma yake. Umma ambao bado una chembe chembe nyingi za imani juu yake. Machoni mwa wengi, Mizengo Pinda anaonyesha kuishi kama anavyohubiri.


Mizengo Pinda ana ya kuiga kutoka kwa Edward Moringe Sokoine, ambaye kwa Watanzania wengi ataendelea kuishi daima. Sokoine aliguswa kwa dhati na hali za Watanzania aliowaongoza.


Itakumbukwa, katika kikao cha Bunge cha Aprili 11, 1984, Sokoine alisimama kwa mara ya mwisho akiwatetea Watanzania walio wengi. Hata wakati huo, wabunge wetu walidai marupurupu zaidi. Waziri Mkuu Sokoine alisimama na kutamka; “Ndugu Spika, niko tayari kuwaongezea ndugu wabunge ruzuku ya chakula chao wanachokula, lakini siko tayari kuwapa nyongeza ya marupurupu wanayopata. Maana, hali za wabunge hawa zina nafuu kubwa kuliko wananchi wengi”.
Sokoine hakupigiwa makofi na wabunge wengi, na hakuyahitaji makofi yao katika kuifanya kazi yake. Lakini huyo ndiye Sokoine aliyekonga nyoyo za mamilioni ya Watanzania. Bahati mbaya kabisa kwa Watanzania, siku iliyofuatia, Sokoine ambaye hakutaka kupanda ndege, bali alichagua kusafiri kwa gari kujionea hali ya kilimo njiani, akapatwa na mauti , kwa ajali ya gari. Kwa Watanzania, Sokoine ataishi daima.


Ewe, Ndugu Mizengo Pinda, mtoto mwenzetu wa mkulima. Mfano huo juu ni wa aliyekutangulia, miaka mingi iliyopita. Tunatambua jitihada zako za kushuka chini kwa watu. Hata hivyo, uende mbele zaidi katika kushughulika na hao mawaziri walio chini yako. Tunajua kuna mawaziri wanaofanana na wewe, lakini wengi hamfanani kabisa.
Si ni juzi tu tumesoma kuwa baadhi ya mawaziri na wabunge wamekata vibali vya kuvuna magogo kutoka Msitu wa Taifa wa Sao Hill kule Mafinga. Ni Wizara ya Maliasili na Utalii ndio yenye kukatisha vibali hivyo.Tunaambiwa waheshimiwa hawa wana vibali vya kuvuna magogogo ekari kwa ekari.
Wengine wamejitetea, kuwa wanavuna magogo hayo si kwa kufanya biashara, bali kutumia mbao hizo kwa majengo ya shule katika majimbo yao ya uchaguzi. Labda shule wanazojenga ni za mbao tupu! Hivi ni wabunge hawa hawa wa bunge letu tukufu waliojiwa na ukarimu huu wa ghafla; kuvuna magogo yao na kuwapa bure wananchi waezekee paa za shule zao? Ni kama vile tunasoma Hekaya za Abunuwasi.


Ni ukweli sasa, kuwa umma umeanza kuhisi, kuwa wale waliodhani ni wakombozi wao sasa wamewasaliti. Wanazunguka na mashangingi yao ya kifahari na huku wakijilimbikizia na kujinyakulia mali na rasilimali za nchi. Wanajijengea mahekalu, wanaishi kwenye fahari kubwa katikati ya umasikini mkubwa wa walio wengi.


Nikiwa Dar es Salaam majuzi nilikutana na mkazi mwenzangu wa Iringa. Kabla ya kumsindikiza kwenda Ubungo kupanda basi la Iringa, nilimwonyesha moja ya nyumba za Serikali zilizonunuliwa kwa bei chee na mmoja wa mawaziri wetu wa sasa. Ni hekalu la kifahari. Na ndani yake kumejengwa mahekalu mengine ya kifahari. Kijana yule uso ulimbadilika, alikumbwa na simanzi kubwa. Hakuamini alichokiona. Akanitamkia; “ Ni afadhali ningebaki nikisikia tu, na hili ni jambo kubwa katika safari yangu hii ya Dar es Salaam, ahsante sana.”


Hakika, binadamu tunasahau, kuwa shida ni mwalimu mzuri sana. Katika shida zao hizi, Watanzania wa leo wanafikiri zaidi. Wameanza kung’amua ulaghai wa baadhi ya viongozi wao. Tatizo ni viongozi hao kudhani walio kwenye shida ni wajinga pia, hawafikiri. Ni nani hasa asiyefikiri?mjengwa
 

Opaque

JF-Expert Member
Oct 24, 2008
1,133
1,500
Na Maggid Mjengwa,... Labda wanafunzi wale wa Chuo Kikuu walikuwa na ujumbe mzito uliojificha katika maelezo yao yale kupitia bango lile, au ndivyo walivyojipanga; kumwambia tu mtoto mwenzao wa mkulima, kuwa tunalala nje, basi. Maana, kama tatizo ni kulala nje , Mizengo Pinda hakupata tabu sana kuingiza mikono mfukoni kuitafuta milioni kumi kwa mwaka.
Lakini, kama watoto wale wa wakulima pale Mlimani wangemwuliza Waziri Mkuu wao swali lifuatalo; "Mtoto wa Mkulima, kwanini tunalala nje? Ni dhahiri, Pinda asingekimbilia kuingiza mikono mfukoni. Maana, hutokea kwangu nikakutana na kijana anayeniambia; "Braza, sijala tangu asubuhi!" Jibu langu laweza kuwa; chukua elfu moja hii , nenda ukale!...
Bahati nzuri mimi nilikuwemo ndani ya ukumbi wa Nkurumah. Waandishi wa habari (akina Mjengwa) muwe mnahudhuria matamasha au sherehe za namna hii ili muwe mnapata habari zilizo sahihi.
Kilichotokea ni hiki:
Siku hiyo ilikuwa ni ufunguzi wa sherehe za miaka 50 ya UDSM, ambayo kilele chake kitakuwa 25th October, mwakani 2011. Pia siku hiyo ikaunganishwa na Mkutano wa wana UDSM waliosoma pale i.e alumni ambayo waliita Convocation Day. Kwa hiyo matukio yote mawili wakayaunganisha yakaenda sambamba. Katika ratiba ya sherehe hizo, kilikuwapo kipengele cha HARAMBEE YA KUCHANGIA KITUO CHA ELIMU. Kwa hiyo Pinda aliahidi kutoa milioni 10 kila mwaka mpaka uwaziri Mkuu wake utakapoisha, akambana na Membe ambaye naye akaahidi milioni 5 kila mwaka ambao Pinda atakuwa Waziri Mkuu! Kwa hiyo hizo milioni 10 si za kuchangia malazi ya wanachuo, usipotoshe watu kabisa! Alichoahidi baada ya kuliona bango ni kutoa kauli tu kwamba "atashughulikia". Kwa lugha nyepesi ni kwamba, hata kama kusingekuwapo na kuonyeshwa kwa bango mle Nkurumah, bado Waziri Mkuu angeahidi hiyo 10M kwani HARAMBEE ilikuwa ni sehemu ya ratiba ya sherehe, wala hakwenda kusikiliza matatizo ya wanafunzi, na wala wanafunzi hawakualikwa ndio maana masomo yalikuwa yanaendelea kama kawaida isipokuwa yale tu yaliyokuwa yanatakiwa yatolewe Nkurumah. Kama mwandishi (Maggid Mjengwa) atahitaji ratiba, nipo tayari kumtumia kwani hadi leo ninayo!
 

jyfranca

JF-Expert Member
Oct 3, 2010
297
0
Mtoto wa mkulima hakufanya vibaya kuchangia, namkubali kutoa mfano na kila mtu akifanya ivyo tutafika, tatizo hatuna moyo wa kuchangia tunafikiria serikali inaweza kutatua kila kitu. Namkumbuka mzee mwenzangu Ronald Reagan alipowaambia serikali si suluhisho la matatizo bali serikali inaongeza matatizo.
 

Opaque

JF-Expert Member
Oct 24, 2008
1,133
1,500
Maggid mbona nakuona hapo lakini hutaki kusahihisha habari yako kwamba Pinda hakuwahi kuchangia hela kwa ajili ya malazi ya wanachuo UDSM, ila zile zilikuwa ni hela za harambee? Utaacha lini kuandika habari za uongo? kama hutaki kusahihisha, nitareport kwa Invisible kuwa habari za Maggid ni za uongo na anastahili kupewa ban.


attachment.php
 

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,500
Maggid mbona nakuona hapo lakini hutaki kusahihisha habari yako kwamba Pinda hakuwahi kuchangia hela kwa ajili ya malazi ya wanachuo UDSM, ila zile zilikuwa ni hela za harambee? Utaacha lini kuandika habari za uongo? kama hutaki kusahihisha, nitareport kwa Invisible kuwa habari za Maggid ni za uongo na anastahili kupewa ban.


attachment.php
Opaque,
Asante kwa tafsiri yako.
Nakuomba Unisome kwa makini, kisha jadili hoja yangu ya msingi, ukipenda.
 

Opaque

JF-Expert Member
Oct 24, 2008
1,133
1,500
Opaque,
Asante kwa tafsiri yako.
Nakuomba Unisome kwa makini, kisha jadili hoja yangu ya msingi, ukipenda.
Nimesoma kwa makini, lakini nimegundua uongo ndani ya habari ndio maana sijadili makala yako ila naisahihisha. Nijadili nini, uongo? Nasema hivi, sahihisha habari yako. Pinda hakutoa zile 10M kwa response ya bango la wanachuo, alitoa kwa sababu ilikuwa harambee. Hata kama asingeingia hata mwanachuo mmoja pale Nkurumah, Pinda angetoa 10M kwani kulikuwa na harambee ya kitu kingine kabisa. Sahihisha kipengele hicho chini ili tuziamini makala zako!

.... Hatimaye Pinda akaweka wazi; kuwa ujumbe umefika.Kisha akajibu ujumbe ule wa watoto wenzake wa wakulima kwa kuahidi kutoa shilingi milioni kumi kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.
 

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,500
Nimesoma kwa makini, lakini nimegundua uongo ndani ya habari ndio maana sijadili makala yako ila naisahihisha. Nijadili nini, uongo? Nasema hivi, sahihisha habari yako. Pinda hakutoa zile 10M kwa response ya bango la wanachuo, alitoa kwa sababu ilikuwa harambee. Hata kama asingeingia hata mwanachuo mmoja pale Nkurumah, Pinda angetoa 10M kwani kulikuwa na harambee ya kitu kingine kabisa. Sahihisha kipengele hicho chini ili tuziamini makala zako!

Opaque,
Ahsante sana, lakini sikioni cha kusahihisha, nadhani tatizo liko kwako. Na bado unaamini hata kama asingeingia hata mwanachuo mmoja pale Nkrumah, Pinda angetoa 10M, nilidhani hiyo nayo ingekuwa habari kubwa.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom