UZUSHI Mtoto mchanga ukimtazamisha kwenye kioo au Mwanga wa jua kabla ya siku 40 hupata Makengeza

Baada ya tathmini, tumebaini kuwa taarifa hii ni ya uzushi
Kwa muda mrefu sasa yamekuwepo madai yanayosema kuwa Mtoto mchanga ukimtazamisha kwenye kioo au Mwanga wa jua kabla ya siku 40 hupata Makengeza.

Strabismus1-AdobeStock_279983412.jpg

Naomba kufahamu ukweli kuhusu jambo hili.
 
Tunachokijua
Makengeza au macho yaliyopishana kwa lugha ya kitaalam huitwa Strabismus.

Ni hali inayotokea baada ya kukosekana kwa uswa wa macho katika kujenga taswira ya vitu. Katika hali ya kawaida, macho yote mawili ya binadamu hupaswa kutazama sehemu moja kwa wakati, lakini hali haipo hivyo kwa watu wenye makengeza ambao macho yao hutazama pande (sehemu) mbili tofauti kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa tafiti, 2-5% ya watu duniani wapo na makengeza. Hutokea zaidi kwa watoto, lakini watu wazima wanaweza pia kupatwa na hali hii.

Makengeza yanaweza kusababishwa na Kutazama kioo au Mwanga wa jua?
Kupitia vyanzo vya kuaminika, JamiiForums imebaini kuwa makengeza hayawezi kusababishwa na kutazama kioo au mwanga wa jua.

Macho ya binadamu hulindwa na aina tofauti 6 za misuli inayoongoza mijongeo yake. Misuli hii hupokea taarifa na amri kutoka kwenye ubongo ya jinsi inavyopaswa kufanya kazi.

Sababu yoyote inayopunguza ufanisi wa misuli hii katika kutekeleza majukumu yake husababisha kutokea kwa makengeza. Baadhi yake ni;
  • Kurithi
  • Kupatwa na ajali yenye kuleta madhara makubwa sehemu ya kichwa
  • Kusagika kwa mishipa ya fahamu (cranial nerves)
  • Changamoto za kuzaliwa, mfano kichwa kikubwa, maambukizi ya magonjwa mfano Surua pamoja na uwepo wa uvimbe kwenye ubongo
  • Kiharusi na Changamoto ya ugonjwa wa Downs unaotokana na uwepo wa kromosomu ya ziada (namba 21)
  • Utindio wa ubongo
Aidha, hakuna njia maalum ya kujikinga na Makengeza isipokuwa kupunguza ukubwa wa madhara yanayoweza kutokea kwa mhusika baada ya kugundulika kuwa na tatizo hili.

Tofauti na jinsi inavyotajwa, Matumizi ya kioo huwaongezea watoto uwezo wa kujitambua wao binafsi pamoja na kuboresha uwezo wa kujifunza mambo mbalimbali katika umri mdogo.

Makengeza yanatibika hasa ikiwa yatagunduliwa katika umri mdogo. Baadhi ya njia zinazoweza kutumika kama sehemu ya tiba ni kutumia miwani maalum, prism au kwa njia ya upasuaji unaohusisha misuli ya macho.
3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom