Mtikila Amtaka Butiku Aende Mahakamani

Ufunuo wa Yohana

JF-Expert Member
Oct 9, 2007
319
70
*Apinga Mahakama ya Kadhi, afungua kesi
*Adai inakiuka Katiba ya nchi, italeta vurugu

Na Grace Michael

MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amemkosoa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku, kwa kumtaka Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ajitokeze kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mchungaji huyo wa Kanisa la Uokovu Kamili, badala yake amemtaka Bw. Butiku afungue kesi ya kikatiba, ili kuondoa kinga ya kisheria inayozuia kuchunguzwa au kushitakiwa Rais.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam jana, Mchungaji Mtikila alisema anachofanya Bw. Butiku ni uoga na kutojua kuwa Rais ana kinga kisheria ya kutochunguzwa tuhuma zake.

"Anachotakiwa kufanya yeye Butiku ni kuja hapa mahakamani na kufungua kesi ya kikatiba, ili hizo sheria za kizamani wanazodai zinawalinda hao marais zifutwe na kutungwa mpya ambazo zitawabana na kuwafanya waogope yale maovu wanayoyafanya kwa sasa wakijua kuna nguzo inawalinda," alisema Mchungaji Mtikila.

Alisema sheria inayowalinda marais imepitwa na wakati na inatakiwa kufutwa ili itungwe nyingine itakayowezesha Rais kuchunguzwa na kushitakiwa kama raia wengine, hii italeta heshima katika utendaji kazi wao.

"Kukiwa na sheria ya kuwabana, mtawaona, watafanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na haya mambo ya kuingia mikataba mibovu kama ya Buzwagi na mambo mengine machafu yatakwisha, kwani atakuwa anatambua kuwa kuna siku atafikishwa mahakamani na ikibidi kufungwa jela," alisema Mchungaji Mtikila.

Juzi Bw. Butiku alikaririwa na vyombo vya habari akimtaka Rais mstaafu Mkapa kujitokeza kuujibu umma dhidi ya tuhuma zinazomkabili ili kuondoa utata ndani ya jamii.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini vimekuwa vikidai kuwa Rais Mkapa alifanya biashara akiwa Ikulu na kukiuka sheria za nchi na baadhi yao wakimtaka ajitokeze hadharani kujibu tuhuma hizo.

Wakati huo huo, Mchungaji Mtikila alitinga mahakamani kupinga kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Mchungaji Mtikila alifungua kesi ya kikatiba jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, akipinga kuanzishwa kwa Mahakama hiyo kwa madai kuwa ni kinyume cha Katiba ya nchi.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo, anaiomba Mahakama kuilinda Katiba ya nchi kutokana na vitendo vya Serikali ya Awamu ya nne na Bunge kuanzisha mahakama hiyo, ambayo anadai itasababisha vurugu kwa wananchi.

Hati hiyo inasema kifungu 26 (1) cha Katiba, kinatamka kuwa kila raia akiwamo Rais, Mahakama na Bunge ambao waliapa kuilinda na kifungu kidogo cha (2) kinampa haki mlalamikaji kuhakikisha Katiba inalindwa kwa mujibu wa sheria.

Inasema vifungu 19 na 20 (1) vinasema nchi ya Tanzania si ya kiislamu, na Mahakama ya Kadhi ni chombo cha kidini cha kiislamu kilichopo ndani ya Korani, hivyo kuundwa kwake si lazima kihusishe Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mchungaji Mtikila anadai kuwa kutokana na CCM kuingiza suala la Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani yake ya Uchaguzi mwaka juzi, chama hicho kimepoteza sifa ya kuwa chama cha kisiasa na badala yake kujiingiza kwenye udini zaidi.

Anadai kuwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, kutaruhusu kuwapo kwa sheria za kiislamu, ambazo zinakiuka haki za binadamu, vinginevyo Waislamu walindwe kwa sheria za nchi, ambazo zinaendana na Katiba.

Katika hati ya mashitaka, Mchungaji Mtikila amenukuu aya mbalimbali za Korani na Hadithi kusisitiza madai yake, huku akituhumu kuwa mahakama hizo zinaweza kuwa za kueneza Jihad.

"Mahakama ya Kadhi ni njia ya kufanya Jihad...kama ilivyoainishwa katika Mintaj il Muslim Vol. 3 Muamalaat...na kwa mujibu wa sura ya 9:30 (Surat at-tauba) Kadhi huongoza mauaji ya Wakristo..."

Akizungumza baada ya kufungua kesi hiyo, Mchungaji Mtikila alisema haiwezekani kila kikundi cha dini kikawa na mfumo wake kisheria, kwani kwa kufanya hivyo, itakuwa ni nchi yenye vurugu.

"Mahakama ya Kadhi ina vipengele ambavyo hata Waislamu wengine sidhani kama wanaitaka, kwani bado wanahitaji," alisema Mchungaji Mtikila.

Alisema wana CCM waliohusika kuingiza kipengee hicho katika Ilani, inabidi wachukuliwe hatua kali na endapo itashindikana, basi wananchi wataingia barabarani kulalamikia hilo
 
Katika hilo, mi naona bado Butiku ana hoja ya msingi kabisa...anawafumbua watu macho kuwa hii vita hata ndani ya CCM ipo, ndani ya watendaji wa serikali ipo, kinachoonekana hapa ni wogawa baadhi ya walio na uwezo wa kusema kujitokeza hadharani kusema kuwa kuna ufisadi, sasa anapojitokeza Butiku na barua yake mi nadhani ni hatua muhimu sana...ujumbe umewafikia wananchi na hilo ni la Muhimu zaidi
Mtikila na 'siasa zake za mahakamani' anaweza pia kufungua yeye hiyo kesi kama alivofungua hii..kwani nani kamtuma? ni suala la kugawana majukumu katika kupambana na hili jinamizi la ufisani, ni 'kumkoma nyani giladi' kutoka pande zote kama inavosemwa(ga) hapa japo sijui maana yake kamili!
 
Back
Top Bottom