Mtazamo binafsi: Tatizo kuu la mkwamo wa Katiba mpya na mambo mbalimbali ya kisiasa na kijamii ni 'kwanini ianzie kwangu? Kwanini nianze mimi?'

Petro E. Mselewa

JF-Expert Member
Dec 27, 2012
10,197
25,516
Nimekuwa nikifuatilia na kutafakari sana kuhusu siasa na mambo ya nchi yangu kwa ujumla. Kiukweli, naipenda sana Tanzania yangu na sijawahi kuiwazia wala kuifanyia mabaya hadi hapa nilipofikia. Na naendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kila uchao kuniachia na kuniimarishia uzalendo wangu kwa nchi yangu Tanzania. Kimsingi, kama nchi, tuna tatizo kubwa la uthubutu. Nitatoa mifano michache kuhusu Katiba mpya na Uenyekiti wa CCM/Urais.

Mchakato wa Katiba mpya ulianzishwa na kusimamiwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mzee Jakaya Mrisho Kikwete. Aliuanzisha mchakato huo mwaka 2011 kwa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 na Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013. Mchakato huo, pamoja na hatua na gharama kubwa zilizotumika ulikwama tangu mwaka 2014 katika ngazi ya Katiba Inayopendekezwa.

Iko wazi hadi hapo kuwa mchakato huo ulianza na hata kukwama wakati wa awamu ya pili ya Mzee Kikwete. Kimahesabu, kama Katiba mpya ingepatikana, katiba husika ingeanza kutumika kuanzia awamu ya tano iliyoanza mwaka 2015. Katiba ya sasa inatoa nguvu kubwa kimamlaka kwa Rais tofauti na Katiba Iliyopendekezwa. Ilisemwasemwa kuwa wakati wa kukusanya maoni kutoka kwa viongozi waandamizi wa kiserikali, baadhi yao 'walipinga' katiba mpya kwa hofu ya kuwa 'Urais' wao ugepungua nguvu na 'kwanini hilo lianzie kwao'?

Naweza kuamini binafsi kuwa kati ya mambo yaliyokwamisha kumalizika kwa mchakato wa katiba mpya ni hofu ya 'kupungua kwa utamu/nguvu kubwa ya Urais' tofauti ya ilivyo sasa kwenye Katiba yetu iliyotungwa mwaka 1977 na kufanyiwa mabadiliko mbalimbali. Kila kiongozi anajiuliza: 'kwanini Katiba mpya ianzie kwangu/kwetu ikiwa wenzetu wameongoza kwa Katiba ya sasa?' Uthubutu wa kuanza na Katiba mpya yenye mambo mapya unakosekana.

Kuhusu Uenyekiti wa CCM Taifa na Urais wa Tanzania kushikwa na mtu mmoja, huu ni utamaduni ulikuwepo tangu wakati wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere. Utaratibu huu ulisimama kwa muda kidogo kuanzia mwaka 1984 hadi 1990 ambapo Mwenyekiti wa CCM alikuwa Mwalimu Nyerere na Rais alikuwa Mzee Mwinyi. Mwaka 1990 utaratibu wa Rais na Mwenyekiti wa CCM kuwa mtu mmoja ulirejea na kubakia hadi leo. Mzee Mwinyi aliiongoza CCM hadi mwaka 1995 alipokabidhi uenyekiti kwa Hayati Mkapa ambaye ndiye aliyekuwa Rais.

Kisiasa, utaratibu huu, ingawa unamhitaji mthubutu kuubadili, una mashiko. Chama kinachoshinda uchaguzini ndicho kinachounda Serikali. Hadi hapo, chama kinaanza kabla ya Serikali. Pia, chama kinachounda Serikali kinaielekeza/kuishauri Serikali husika. Mamlaka ya juu kichama ni Mwenyekiti; mamlaka ya juu kiserikali ni Rais. Itakuwaje ikiwa ni watu tofauti na kumejitokeza tofauti baina yao? Kwa vyovyote vile, chama kitaibuka mshindi. Hali itakuwaje?

Nguvu ya chama ndiyo inayolazimu mtu mmoja awe kiongozi wa chama na Serikali. Nguvu hii kubwa ya chama ina baraka za kikatiba na kisheria. Katiba na sheria zetu zinabainisha wazi kuwa kiongozi yeyote wa kuchaguliwa (mfano Rais, Mbunge au Diwani) anapofukuzwa uanachama wa chama chake hupoteza nafasi yake ya Urais, Ubunge au Udiwani. Uenyekiti wa CCM Taifa na Urais kuwa kwa mtu mmoja ni njia ya udhibiti na kuepusha switafahamu ambazo zinaweza kujitokeza.

Kila awaye hujisemea na kujiuliza: kwanini utaratibu mpya uanzie kwangu? Uthubutu unakosekana na utamaduni unabakia.
 
Kinachokwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya hasa ni hili jukumu kukabidhiwa chama cha siasa kinachounda serikali kuliendesha ambacho ni mnufaika wa moja kwa moja wa hii Katiba mbovu iliyopo.

Tukitaka Katiba Mpya ipatikane sharti hili jukumu liachwe kwa taasisi huru, kama itakuwa ni amri kutoka mahakama kuu itakayotoa maelekezo ya nini cha kufanya ili katiba ipatikane, lakini kuendelea kuwaachia CCM kusimamia huo mchakato tunajidanganya, haitapatikana kamwe.

Kwa sababu CCM kama chama cha siasa kina haki sawa na vyama vingine vya siasa, huu ukiritimba wao wa kujiona kwakuwa ndio wanaunda serikali basi wana kura ya turufu kwenye maamuzi ya kuunda Katiba Mpya haufai, vyama vipige kura vingapi vinataka Katiba Mpya wengi wapewe.
 
Kinachokwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya hasa ni hili jukumu kukabidhiwa chama cha siasa kinachounda serikali kuliendesha ambacho ni mnufaika wa moja kwa moja wa hii Katiba mbovu iliyopo.

Tukitaka Katiba Mpya ipatikane sharti hili jukumu liachwe kwa taasisi huru, kama itakuwa ni amri kutoka mahakama kuu itakayotoa maelekezo ya nini cha kufanya ili katiba ipatikane, lakini kuendelea kuwaachia CCM kusimamia huo mchakato tunajidanganya, haitapatikana kamwe.

Kwa sababu CCM kama chama cha siasa kina haki sawa na vyama vingine vya siasa, huu ukiritimba wao wa kujiona kwakuwa ndio wanaunda serikali basi wana kura ya turufu kwenye maamuzi ya kuunda Katiba Mpya haufai, vyama vipige kura vingapi vinataka Katiba Mpya wengi wapewe.
Asante Mkuu kwa mchango wako mzuri
 
Back
Top Bottom