Ndugu wanahabari,
Leo tumewaiteni kwa ajili ya kuzungumza nanyi juu ya jambo muhimu ambalo limetokea mwezi huu na likikihusu chama chetu, ulinzi wa fedha kodi za watanzania na mwelekeo wa serikali ya sasa katika kupambana na rushwa, ufisadi, wizi wa fedha za umma, michezo ya utakatishaji wa fedha na makosa mengine ya jinai yanayohusu fedha za umma.
Kwa niaba ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front ambalo liliniteua tarehe 28 Agosti 2016 kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama ambayo ina majukumu ya kufanya kazi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti Taifa, napenda kuwajulisha kuwa chama chetu kimeibiwa fedha za Ruzuku kiasi cha Shilingi za Tanzania 369,378,502.64 (Milioni 369 laki tatu na Elfu Sabini na nane).
Ndugu Waandishi wa Habari,
Fedha hizo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya Alhamisi, tarehe 05 Januari 2017 na kuingizwa kwenye Akaunti ya NMB Tawi la Temeke yenye jina la The Civic United Front ikiwa na akaunti namba 2072300456. Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front ambayo ndiye msimamizi wa jumla wa masuala ya akaunti za fedha na mali za The Civic United Front haiitambui akaunti hiyo na haikuwahi kuiidhinisha ipokee ruzuku ya CUF kutoka Serikali Kuu.
Katibu Mkuu wa The Civic United Front ambaye ndiye muwajibikaji mkuu wa masuala ya fedha na mali za chama haitambui akaunti hiyo na hajawahi kumuandikia Msajili wa Vyama vya Siasa kumpa akaunti hiyo ili iwekewe fedha za Ruzuku ya CUF. Vikao vya kitaifa vya The Civic United Front kwa maana ya Kamati ya Utendaji ya Taifa (ambayo ilikutana hivi karibuni kumpitisha mgombea wa Ubunge jimbo la Dimani) na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa havikuwahi kupitisha maamuzi yoyote kwamba fedha za CUF ziwekwe katika akaunti hiyo ya wilaya iliyoko NMB Temeke.
Baada ya kugundua utoroshwaji huo wa fedha za ruzuku ya CUF ambazo ni fedha za umma na zina masharti na taratibu zake katika kutolewa, tumejiridhisha kuwa akaunti ambayo Hazina ya Serikali Kuu wameshiriki kuitumia kutorosha fedha za umma na mali ya CUF ni akaunti ya CUF ambayo hutumiwa na Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokea mgao wa Ruzuku kutoka kwa Chama Taifa.
Chama cha Wananchi CUF kinazo akaunti katika kila wilaya ya kichama, Kwa mfano Wilaya ya Kinondoni ya CUF wanayo akaunti ya benki ambayo wanaitumia kupokea fedha zilizoidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama kwa mujibu wa Katiba, Wilaya ya Ilala pia ina akaunti ya namna hiyo, Mtwara n.k.
Yaani baada ya watu wanaomsaidia BWANA YULE kuivuruga CUF kuona kuwa Bodi ya Wadhamini ya CUF imezuia njama za ufunguaji wa akaunti mpya ya CUF, wakatumia mbinu ya namna ile ile kwa njia tofauti. Siku mbili kabla ya utoroshaji wa fedha hizo ulisukwa mpango wa kuwaondoa baadhi ya Viongozi wa CUF wa Wilaya ya Temeke kwenye utiaji saini unaoihusu akaunti tajwa. Uondoaji wa Viongozi hao ulikwenda sambamba na kuwageuza baadhi ya Wateule wa Lipumba wanaofanya kazi za kukihujumu chama kutokea Buguruni, kuwa watia saini wa akaunti ya Wilaya. Watia saini wapya walioshiriki kwenye ughushaji huo ni Bi. Magdalena Sakaya (MB) na mtu mwingine aitwaye Thomas Malima.
Hata kama wangelikuwa na uhalali wowote wa kusimamia masuala ya fedha za chama wasingeliweza kuwa watia saini wa akaunti ya NMB Tawi la Temeke ambayo inamilikiwa na CUF Wilaya ya Temeke wakati wote wawili si wanachama wa CUF kutoka wilaya ya Temeke na hata kama wangelikuwa na uhalali wa kuwa watia saini kwenye akaunti hiyo katu hakukuwa na uhalali wowote wa hazina kuweka fedha za ruzuku za chama cha siasa kwenye akaunti ya ngazi ya wilaya bila mifumo rasmi ya kiuongozi ya chama inayohusika na masuala ya fedha kujua au kuidhinisha.
Yaani ni kama vile leo hii, Ruzuku ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itoroshwe na kuwekwa kwenye akaunti ya NMB ya Chama Cha Mapinduzi ngazi ya wilaya huko Kahama. Kisha Fedha hizo ziondolewe kwenye akaunti hiyo ya wilaya na kuingia kwenye akaunti ya mwana CCM aliyesimamishwa uanachama na halafu mwana CCM huyo azitoe fedha hizo na kuzipeleka kusikojulikana. Haya yote yafanyike bila Katibu Mkuu wa CCM kujua, Kamati Kuu ya CCM ikiwa haijui, Halmashauri Kuu ya CCM ikiwa haijui na Bodi ya Wadhamini ya CCM ikiwa haijui chochote.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Siku moja baada ya NMB na wala njama hawa kukamilisha mchakato wa kudilisha watia saini wa Akaunti ya CUF inayomilikiwa na wilaya ya Temeke (Yaani tarehe 05 Januari 2017) ndipo hazina ikaweka mzigo huo wa pesa bila kuchelewa. Siku hiyo hiyo ambapo hazina walitorosha fedha hizo, watia saini wapya wa Akaunti ya NMB ya Wilaya ya Temeke waliulizia kiasi cha fedha kilichomo kwenye akaunti hiyo na walifanya hivyo katika tawi la NMB Mandela Road.
Kesho yake, siku ya Ijumaa, tarehe 06 Januari 2016, Watia saini hao wakiongozwa na Thomas Malima walikwenda katika Benki ya NMB Tawi la Temeke na kufanya mambo mawili. Kwanza wakatoa kiasi cha Shilingi 69,000,000 (Milioni 69) kama pesa Taslimu, kisha wakahamisha Shilingi 300,000,000 (Milioni 300) kwenda kwenye akaunti ya mtu binafsi. Mchezo wote huu umefanyika Chapchap kama zilivyochotwa pesa za ESCROW!
Akaunti ya Mtu Binafsi iliyotumika kutoroshea fedha hizo kutoka kwenye akaunti ya Wilaya ya Temeke ni akaunti ya NMB yenye namba 41401600207 ikimilikiwa na mtu aitwaye MHINA MASUOD OMARY ambaye ni Diwani wa CUF wilayani Handeni, mtu wa karibu wa Lipumba na ni mmoja kati ya wanachama nane waliosimamishwa uanachama na Baraza Kuu lakini kubwa kuliko yote yeye ni mmoja kati ya wanachama wanaoshitakiwa na Bodi ya Wadhamini baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia maamuzi ya Vikao vya CUF na Bodi ya Wadhamini kufungua Shauri namba…lililoko Mahakama Kuu. Wakati akaunti ya ndugu Masoud inawekewa fedha hizo haikuwa na hata senti tano.
Ndugu Waandishi wa Habari, katika historia ya chama chetu hii ni mara ya kwanza tunashuhudia fedha za Ruzuku ya chama zinatoroshwa kutoka Hazina, zinawekwa kwenye akaunti ya chama ngazi ya Wilaya bila Baraka za Baraza Kuu, Kamati ya Utendaji ya Taifa, Bodi ya Wadhamini ya chama na bila ridhaa wala ruhusa ya Katibu Mkuu ambaye ndiye anawajibika kwa masuala yote ya fedha. Na hii ni mara ya kwanza tunashuhudia kuwa fedha za Chama zilizotoroshewa kwenye akaunti ya ngazi ya wilaya zinaondolewa haraka na kuwekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Jana Jumatatu tarehe 09 Januari 2017 na wakati tunapokea taarifa nzima za yanayoendelea, akaunti ya MHINA MASUOD OMARY (mtu binafsi aliyetumiwa kwenye utakatishaji huu wa fedha) ilikuwa kwenye mchakato mkubwa wa kuondoa fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo.
MHINA MASUOD OMARY alianza kazi ya kuondoa fedha hizo majira ya asubuhi ya jana, tarehe 06 Januari 2017, kwanza kwa kuondoa Shilingi 100,000,000 (Milioni 100) kutokea Benki ya NMB tawi la Magomeni, kisha akiwa hapo hapo Magomeni akatoa Shilingi 50,000,000 (Milioni 50) halafu akaelekea tawi la Kariakoo na kutoa Shilingi 100,000,000 (Milioni 100) na mwisho akiwa hapo hapo Kariakoo NMB akatoa tena Shilingi 49,500,000 (Milioni 49.5). Wakati MHINA MASUOD OMARY anazunguka kwenye matawi haya kutoa fedha hizi jana alipewa ulinzi wa POLISI waliokuwa wamevalia kiraia wakiwa kwenye Magari ya CUF na aliambatana na Thomas Malima wakiwa chini ya usimamizi wa watu wengine wawili, Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya.
Baada ya kutorosha fedha hizo zote, Akaunti ya Masoud Mhina imebakia na Shilingi 207,907 (Laki Mbili Elfu Saba Mia Tisa na Saba) kama zawadi maana wakati inawekewa Shilingi Milioni 300 haikuwa na hata senti tano. Kwa hivyo Shilingi Milioni 300 iliyokuwa imetoroshewa kwenye akaunti hiyo imetolewa kama fedha taslimu na kupelekwa kusikojulikana ikiwa ni kabla chama hakijapata taarifa kuhusu wizi huo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Baada ya masuala yote hayo kutokea, tunapenda kuwajulisha watanzania masuala yafuatayo:
1. Kwa niaba ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Kamati ya Utendaji ya Taifa, Bodi ya Wadhamini ya CUF na Katibu Mkuu wa CUF, tumesikitishwa sana na kitendo cha hazina kuacha kabisa maadili ya kazi yake na kushiriki katika utoroshaji wa fedha za chama cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi huku ikitambua kwamba kufanya hivyo ni kuvunja miiko ya masuala ya fedha na sheria za nchi.
Hii ni aibu kubwa sana katika sekta ya fedha na ulinzi wa fedha katika nchi yetu. Tunajiuliza, kama hazina inaweza kukubali kutumika katika michezo michafu tena bila woga, kama Benki ya NMB inaweza kabisa kutumika katika uhuni mkubwa wa namna hii tena dhidi ya taasisi kubwa kama CUF.
Je, mtu mmoja mmoja yuko salama kifedha namna gani? Je, fedha za umma zina ulinzi wa kutosha kiasi gani hapo hazina? Na ni nani anayetoa amri fedha za umma zipelekwe kokote kule bila kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za nchi? Na je, mtu huyo yuko juu ya sheria?
2. Pili, tarehe 10 Oktoba 2016, Msajili wa Vyama vya Siasa alimuandikia “Mwenyekiti” na Katibu Mkuu wa The Civic United Front na kuwajulisha kwamba Ofisi yake inasitisha Ruzuku ya CUF kwa kile alichokiita (namnukuu)
“…Kwa kuwa Fedha za Ruzuku ni fedha za umma ambazo zinahitaji usimamizi mzuri katika matumizi yake, na kwa kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina dhamana ya kugawa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa vinavyostahili na kusimamia uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo, hivyo baada ya tafakuri ya kina nimeona ni busara kwanza kusimamisha kwa muda mgao wa ruzuku kwa chama chenu mpaka hapo chama kitakaporejea katika hali shwari kiutendaji inayowezesha viongozi husika kusimamia matumizi ya fedha hizo ipasavyo”. Barua hiyo yenye Kumb. Namba HA.322/362/14/17 nimewaambatanishia.
3. Wakati Msajili wa Vyama vya Siasa anafanya maamuzi ya kusitisha Ruzuku ya CUF kwa kutomuamini Katibu Mkuu wa CUF, kwa kutoiamini Bodi ya Wadhamini ya CUF, kwa kutoiamini Kamati ya Utendaji ya CUF na kwa kutoliamini Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF – Hazina kwa upande mwingine inatorosha ruzuku hiyo hiyo kwa kumuamini Ibrahim Lipumba, Magdalena Sakaya, Thomas Malima na genge lao.
Wakati Msajili wa Vyama vya Siasa anasema fedha za Ruzuku ya CUF hazitakuwa salama chini ya mifumo ya kitaasisi ya chama ambayo ipo na inafanya kazi, Hazina wanafanya kinyume kabisa, wanatoa fedha za taasisi kwa kuzitorosha na kuwakabidhi watu binafsi ambao hawataweza kuzijibia chochote au kutoa maelezo yoyote ya fedha hizo kwa vyombo vya Ukaguzi wa ndani wa Fedha za chama pamoja na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
4. Kwa mtindo huu The Civic United Front inamuhurumia sana Rais John Pombe Magufuli ambaye amekuwa akijitihadi kwa vitendo kupambana na rushwa, ubadhirifu, wizi wa fedha za umma na vitendo vya utakatishaji wa fedha. Kitendo hiki cha utoroshaji wa fedha za CUF na kuzifikisha mikononi mwa watu binafsi bila kujali kuwa hizo ni fedha za umma na tena kwa kupitia katika vitendo vya jinai si tu kinadhihirisha namna mfumo wetu wa uongozi wan chi ulivyoanguka, bali kinadhihisha kuwa wapo watu wanaishi juu ya Rais wa nchi na wanaweza kufanya chochote anachopambana nacho na watu hao wasiguswe. Kitendo hiki ni kipimo tosha cha utendaji wa ikulu, mifumo ya fedha za nchi yetu na utashi wa Rais katika kupambana na vitendo vya rushwa, ufosadi, matumizi mabaya ya fedha za umma, jinai katika miamala ya fedha n.k.
5. Tunatumia fursa hii kumuuliza Msimamizi Mkuu wa Fedha za Watanzania ambaye ni Rais wa Tanzania, kwamba fedha zilizotoroshwa na Hazina na kuwekwa kwenye akaunti ya chama ya Wilaya kisha zikatoroshwa na kuwekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi zitahakikiwa vipi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali? Zitasimamiwa vipi na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF? Zitasimamiwa vipi na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF? Zitasimamiwa vipi na Bodi ya Wadhamini ya CUF? Na zitasimamiwa vipi na Katibu Mkuu wa CUF (muwajikaji mkuu wa masuala ya fedha za CUF). Na kama Hazina imeipuuza kabisa mifumo ya uongozi wa ndani ya CUF na kuamua kuanza kuwapa watu binafsi fedha za CUF ili wazitumie watakavyo na wajuavyo, je Rais Magufuli amebariki kitendo hicho cha ubadhirifu na uhuni mkubwa? Na kama Rais amebariki kitendo hicho hivi kuna vita dhidi ya wizi, ufisadi na matumizi mabaya ya rasimali na mali za taifa?
6. Nimezungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya CUF, Katibu Mkuu wa CUF, Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Katibu Naibu Katibu Mkuu Bara na Naibu Katibu Mkuu Bara (wanaotambuliwa na vikao halali vya chama; Mkutano Mkuu, Baraza Kuu na Kamati ya Utendaji ya Taifa) na kujiridhisha kuwa hakuna kikao chochote cha chama cha masuala ya usimamizi wa fedha za chama kiliwahi kukaa na kuamua kuwa Hazina iache kupeleka fedha za CUF kwenye akaunti Kuu za CUF na kwamba Hazina ianze kutoroshea fedha hizo kwenda kwenye akaunti za CUF ngazi ya Wilaya kisha kusimamia utoroshaji wa fedha hizo kwenda kwa watu binafsi. Kwa hiyo utoroshaji wa fedha hizo hautambuliki ndani ya mifumo yote ya vikao halali vya CUF na kwa wasimamizi wakuu wa masuala ya fedha na mali za chama ambao ni Katibu Mkuu na Bodi ya Wadhamini.
7. Hadi tuongeavyo na tangu Msajili aiandikie CUF kusitisha Ruzuku ya chama sasa ni yapata miezi mitano ambapo CUF inadai Ruzuku ya Shilingi zipatazo 635,000,000 (Milioni 635). Kwa kuwa Barua ya Usitishaji wa Ruzuku ipo na kwa kuwa CUF haiutambui utaratibu mwingine wa kugawa Ruzuku ya Chama isipokuwa ule wa kupitia kwa Muwajibikaji Mkuu wa masuala ya Fedha za Chama (Katibu Mkuu) na Bodi ya Wadhamini ya Chama (ambayo inasimamia akaunti za chama na mali zake) na kwa kuwa Fedha zilizotoroshwa Hazina zimepelekwa kwenye akaunti isiyotambuliwa na Katibu Mkuu na Bodi ya Wadhamini ya chama, The Civic United Front inatamka rasmi kuwa hadi sasa Ruzuku yake iliyoko hazina ni Shilingi 635,000,000 na kwamba jambo hilo haliwezi kuwa na mjadala.
8. The Civic United Front inamuomba Rais Magufuli, Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa, Gavana wa Benki Kuu (BOT), TAKUKURU, Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na vyombo vingine vinavyohusika, kuchukua hatua za dharura za kuokoa fedha hizo za umma ambazo zimepotezwa kwa na watendaji wa hazina kwani kwa vyovyote vile Bodi ya Wadhamini ya CUF, Vikao halali vya kitaifa vya CUF na Muwajibikaji Mkuu wa masuala ya Fedha ndani ya CUF hawana taarifa na hawakuwahi kupitisha uamuzi wowote wala kuwasiliana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa juu ya kuanza kuiwekea au kuziwekea akaunti za CUF za Wilaya fedha za Ruzuku ya chama ngazi ya Taifa?
9. Tunaujulisha umma wa Watanzania, Serikali na wadau wote kwamba katika “wizi huu” kila mtu atabeba msalaba wake. Waliotumika kutengeneza njama hizo mahali popote pale walipo watabeba misalaba yao. Watendaji wa Hazina ya Serikali Kuu walioidhinisha wizi huu watabeba misalaba yao. Benki ya NMB ambayo imetumika katika wizi huu pia itabeba msalaba wake. Sakaya, Thomas na mtu mwingine yeyote aliyehusika kwenye jinai hii atabeba msalaba wake. Na, mtu aliyetumika kutorosha fedha hizo kwa mara ya mwisho, MHINA MASOUD OMARY lazima abebe msalaba wake. Misalaba hii itahusisha hatua zote muhimu zinazohitajika kuchukuliwa na chama chetu katika kukilinda na kulinda rasilimali zake ambazo ni fedha za walipa kodi dhidi ya ubadhirifu, wizi na aina nyingine yoyote ya jambo linalovunja taratibu na kanuni za kifedha ikiwa Serikali haitachukua hatua za dharura na za haraka.
NA KWA HIYO
10. Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front tayari inakutana, Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF pia inakutana kwa ajili ya kutafakari shambulio hili kubwa la chama na kuelekeza hatua za kiutawala na kisheria za kuchukua haraka. Wanasheria wa chama pia wako tayari kupokea maelekeo yoyote yale kwa ajili ya kukilinda chama dhidi ya shambulio la namna hii.
Julius Mtatiro,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
The Civic United Front,
Jumanne 10, Januari 2017,
Dar Es Salaam