Mtatiro: Mambo matano mazuri ya Magufuli akiwa rais

mcubic

JF-Expert Member
Mar 3, 2011
10,306
6,514
magufuli.jpg

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha Dk John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Kwanza kabisa napenda kumpongeza sana Magufuli kwa hatua aliyofikia na kumtakia kila la heri. Naomba kukiri kwa uwazi kwamba katika uchaguzi unaohusisha vyama vya siasa ni lazima mshindi atapatikana na kwa Tanzania ni lazima mshindi huyo atoke kwenye chama cha siasa.

Tanzania ina vyama 22 vilivyosajiliwa na vinavyofanya kazi sasa, tutake tusitake ni lazima rais wa nchi atatoka katika chama kimojawapo, na kwa sababu CCM imeshapitisha mgombea wake na yeye ana fursa ya kushinda uchaguzi kama ambavyo fursa hiyo ilivyo kwenye vyama vingine. Natumia nafasi hii kufanya uchambuzi wa dhati juu ya taswira ya serikali ya Magufuli ikiwa atafanikiwa kushinda uchaguzi wa mwaka huu. Taswira ya namna hii pia nitaifanya kwa wagombea wengine wa vyama ambavyo vitaamua kuweka wagombea urais.

Katika kulifanya jukumu hili nitachambua masuala 10 ambayo nafikiri kwamba yanaweza kujenga utawala wa Magufuli, ikiwa atachaguliwa na Watanzania kuwa rais wa awamu ijayo.

Mambo matano kati ya hayo nayatazama kama taswira bora na mengine matano yanaweza kuwa taswira hasi. Katika uchambuzi wa leo nitaanza na mambo matano ambayo ni taswira bora.

Usimamizi bora

Taswira ya kwanza ambayo Magufuli anaweza kuirejesha bila wasiwasi ni usimamizi thabiti wa serikali na nidhamu ya utendaji ndani ya serikali. Naamini kuwa serikali ya Magufuli itakuwa ya kiusimamizi na yeye mwenyewe anaweza kulifanya jambo hilo bila kusita. Katika nyadhifa nyingi alizopitia hadi sasa ameijenga taswira hii kila alikopita na bado inambeba hata ikitokea anachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano.

Tukumbuke kuwa moja ya mambo ambayo yameanguka kabisa nchini hivi ni utendaji ndani ya serikali. Tunafahamu kuwa wafanyakazi ndani ya serikali ukiachilia mbali matatizo waliyonayo kwa maana ya vipato, hata mambo madogo ambayo wangeweza kuyasimamia ndani ya dakika au saa chache huchukua wiki kadhaa na hata miezi kadhaa. Utaratibu wa utoaji huduma umekwama sana na nadhani kama akiwa na uwezo huo atafanikiwa kutatua changamoto kubwa na ya siku nyingi. Ikiwa utendaji wa serikali unaimarika na huduma zinatolewa kwa wakati, tutaweza kujenga taifa linalokwenda mbele bila kujali chama gani kiko madarakani.

Msimamo imara

Taswira bora ya pili ya serikali ya Magufuli inaweza kuwa ni misimamo katika masuala ya msingi na kutoyumba sana. Magufuli muda wote ambao amekuwa kiongozi ameonyesha jambo hilo. Kila mara amekuwa na misimamo hata kama siyo sahihi. Kwa tafsiri nyingine hii huwa ni njia bora ya uongozi wa nchi japokuwa misimamo ya serikali au kiongozi mkuu wa serikali huwa haipaswi kuwa juu ya haki na matakwa ya wananchi.

Moja ya mambo ambayo serikali iliyopita ilikosa, ni pamoja na kukosa misimamo na kuwa na “double standard”. Mfano mdogo tu ni kwenye mchakato wa katiba mpya ambapo Rais anayeondoka alisimamia uanzishwaji bora wa mchakato huo, akaunga mkono katika hatua zote na rasimu zote, lakini akaja kuwageuka wajumbe wa tume hiyo na rasimu yao ya pili alipolihutubia Bunge Maalumu la Katiba. Naamini Magufuli si mtu wa kugeuka na kuna masuala mengi anaweza kuyasimamia kwa dhati na kila mmoja wetu akakubali kuwa, naam! Hapa kuna kiongozi anasimamia masuala haya.

Uwezo wa kusimamia miradi


Taswira ya tatu ya serikali inayoweza kuundwa na Magufuli ikiwa atachaguliwa kuwa rais ni uwezo wa kusimamia miradi ya maendeleo. Magufuli ni mtu wa namna hiyo na ametuonyesha katika sekta ya ujenzi na hasa katika eneo la barabara. Moja ya masuala ambayo nayaona kama mafanikio makubwa ya serikali ya Kikwete ni ujenzi wa barabara, ukiniuliza, nitakwambia jambo hili ndilo Kikwete anapaswa kujivunia atakaporudi nyumbani kwake pale ‘Msoga’. Lakini aliyeleta mapinduzi hayo kiusimamizi ni Magufuli.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa “ikitolewa tenda ya ujenzi wa barabara nchini Tanzania na India halafu nchi zote zikakabidhi tenda hizo kwa watoto wa marais wa nchi, kule India walau barabara ya ‘kudanganyishia’ itajengwa lakini hapa Tanzania unaweza usione hata kokoto” (tafsiri yangu). Dhana hiyo ina maana kwamba huku kwetu wizi na kujijazia manoti ndivyo vitu vinavyoshamiri na kwa tafsiri ya Mwalimu “ilipasa Magufuli awe anaongoza kwa kuchukua noti za barabara na kuzijaza tumboni kwake”, jambo ambalo limekuwa nadra kutokea na kama liliwahi kuwepo ndiyo tutajua sasa wakati watu wataanza kutoa taarifa zake kwa sababu anataka kwenda Ikulu. Kwa uwezo huu wa kiusimamizi namuona Magufuli akisimamia miradi ya serikali kwa ustadi mkubwa hata kama siyo “waziri wa miradi” katika serikali atakayoiunda.

Mawaziri imara

Taswira ya nne nayoiona katika serikali ya Magufuli ikitokea anashinda urais wa Tanzania ni uundaji wa Baraza la Mawaziri na nyadhifa za kiutendaji zilizojaa watu wenye uwezo kuliko marafiki. Serikali zetu kadhaa zilizopita ikiwamo hii inayoondoka zimekuwa na sifa ya kubeba marafiki kufa au kupona. Siyo siri kwa JK amelalamikiwa mno na mara kadhaa serikali yake ilionekana kama “imejaa washkaji” watu wanaolindana na kuoneana haya kwa heshima za urafiki kuliko kuangalia maslahi ya nchi.

Magufuli anaweza kuwa dawa ya serikali za ushkaji kwani tangu kwenye mchakato wa kupata wagombea ndani ya CCM hakuonekana kama “kitisho” na hakuwa na makundi nyuma yake, penyeza yake ya kimya kimya hadi anakuwa mgombea urais wa CCM imemsaidia kuanza kujenga marafiki wasio na masharti ya kutaka kubebwa naye. Marais wengi huunda mitandao na mitandao hiyo huwapa fedha mapema na huwasaidia kila jambo, wanapofika madarakani huwa na deni la kuilipa mitandao hiyo, malipo yenyewe ni miradi ya serikali, tenda mbalimbali na vyeo lukuki. Naamini Magufuli hatakuwa na tatizo hilo na itamsaidia kutengeneza serikali isiyo na “washkaji kibao.”

CCM yenye nguvu


Taswira ya tano inayoweza kujitokeza ni uwezekano wa kurejesha nguvu ya CCM ambayo inasambaratika, na naamini hili linaweza kujitokeza sana hasa kwenye kipindi cha kwanza cha uongozi wake. Siamini kama ataweza kurekebisha taswira ya CCM kwa miaka mitano mingine (ikiwa atapata vipindi vyote viwili) kwa sababu hatujaona utendaji halisi wa serikali ijayo, ikiwa CCM ndiyo itashinda. Wananchi wengi hawaiamini tena CCM na jambo hilo linaweza kuipeleka ikaangushwa katika uchaguzi wa mwaka huu, lakini ikitokea CCM inavuka kizingiti na inapona kuangushwa halafu Magufuli anakuwa rais, anaweza kujizatiti na akatumia miaka mitano kufanya mambo makubwa yatakayowafanya wananchi warudishe imani kwa chama hicho. Ila akifanya vibaya sana atazidi kuididimiza. Kwa mtazamo wangu wa msisitizo ni kwamba naona akifanikiwa kwenye eneo hili, japokuwa naweka msisitizo wa pili kuwa ni lazima tusubiri kujua ikiwa atashinda kipindi chake cha kwanza kitakuwaje kiuongozi.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Ana shahada ya uzamili (M.A) na anahitimu shahada ya Sheria (LLB) Julai mwaka huu: +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com). Uchambuzi huu ni maoni yake binafsi.

Source: Mwananchi, July 13, 2015.


 
Kesho atuletee upande wa CUF wakishinda. Why Magufuli kwani uchaguzi ushafanyika? Wewe si mtafiti? Kuna tena kichwa utuletee upande wa CUF wakinda itakuwaje.
 
Hivi Julius Mtatiro Unafanya Uchambuzi au Unafanya Urejea?
hivi huyu Mtatiro ni yule aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF ?
hapo kweli hamna geni ni kwamba anarejea tu maandiko ya nyuma yaliyokwisha pitiwa
Mtatiro andika hivi Mambo ma5 Magufuli akiwa Rais ni haya

  • Afufue Mabwawa yote ya maji kwa kuyaongeza kina na kukarabati vinu vya kufufua umeme, ili hawa Mabosi wake walionunua mitambo ya mafuta na gesi ya kufua umeme wakose soko kwani Hydro-Power ni bei chee sana
  • afufue shirika la simu TTCL ili kuwabana hawa kina Rostam na mabosi wake walio ndani ya chama kwa kuihodhi TTCL na kuipaisha Airtel wakose ulaji (kwani TTCL mpaka leo ndio inagawa na kuuza masafa)
  • afufue Shirika la reli ili kuua biashara ya malori yooooote mizigo iende na treni
  • afufua na kukuza uzalishaji wa mifugo na samaki hata wale wa kina kirefu ili watanzania wapate kieowea tosha,
  • abane mirija yote ya Wabunge kugawana Mashirika kwa kuwa wajumbe wa Bodi
  • apunguze Baraza la Mawaziri hadi 17 na manaibu chini ya 10
Mwenye simu ya Magufuli anisaidie au hata E-mail maana huku na F/B haingii sasa yupo kinjia na GUUFULL
 
Binafsi nilikua mfuatiliaji wa makala za Mtatiro kwenye gazeti la mwananchi akiwachambua wagombea wa ccm na upinzani kwa nafasi ya uraisi na nilizikubali.
Kwa hii post naona ni muendelezo wa makala hizo hivyo sio sahihi kumnyooshea kidole kwamba ni njaa au anajipendekeza kwa Magufuli isipokua kitendo cha kuandika upande chanya tu bila hasi wakati alishaahidi kuandika pande zote inaleta wasiwasi kidogo. Namshauri kama amepitiwa basi aedit hii post ili aondoe huu ukakasi unaoonekana.
 
Kesho atuletee upande wa CUF wakishinda. Why Magufuli kwani uchaguzi ushafanyika? Wewe si mtafiti? Kuna tena kichwa utuletee upande wa CUF wakinda itakuwaje.
Bavicha inaelekea wewe sio mfatiliaji kabisa yani Julius Mtatiro alisha fanya uchambuzi kwa kila aliyekuwa anataka kugombea Urais...jaribu kufatilia..
 
Last edited by a moderator:
Gud mtatiro...a true intellectual... That's what we should do, give facts not bla bla bla and negativity!!
 
Magufuri apunguze ukubwa wa baraza la mawaziri na ajitahidi kutenga bajeti ya maendeleo iwe kubwa walau hata kwa 45% kuliko ilivyo sahivi kati ya 22bn ni 5bn tu ndo zinaenda kwenye miradi ya maendeleo, hili linawezekana akianza na mawaziri wachache na kupunguza manunuzi ya V8 . Afumue mfumo mzima wa manunuzi serikalini kwasababu tenda nyingi zinaendeshwa kwa kujuana na rushwa nene nene, mengine wengine msaidieni.
 
Mkuu Ukwaju hiyo No #3 ya kwamba afufue reli ili kuua biashara ya malori nadhani ndipo hasa pakumpimia mwanzo mwanzo mwa uongozi wake kama akiwa rais.coz akipigia sana kelele hili suala kwamba malori yanaharibu sana barabara sasa ndo tutajua ilikuwa siasa au alimaanisha.
 
Last edited by a moderator:
Mtatiro umesahau kuwa watendaji wengi atakao wachagua watatoka kwa mkapa na jk , wengine umeona mwenyewe jk akimsistiza magufuli kuwa hawa hazina ya chama na serikali na huo ulikuwa ni ujumbe tosha kuwa asije akawaacha, kwahiyo hata wakivurunda atalazimika kuomba ruhusa kwa watangulizi wake ambao kimsingi ndio waajiri wake jpm
 
Magufuri apunguze ukubwa wa baraza la mawaziri na ajitahidi kutenga bajeti ya maendeleo iwe kubwa walau hata kwa 45% kuliko ilivyo sahivi kati ya 22bn ni 5bn tu ndo zinaenda kwenye miradi ya maendeleo, hili linawezekana akianza na mawaziri wachache na kupunguza manunuzi ya V8 . Afumue mfumo mzima wa manunuzi serikalini kwasababu tenda nyingi zinaendeshwa kwa kujuana na rushwa nene nene, mengine wengine msaidieni.
Sna uhakika kama chama kimetenga pesa ya kutosha kampeini, mpaka dk hii wapo ambao wameishajikomba kwake kuwa watatoa helcoptor nk. Kwahiyo hao ni lazma watalipwa kwa njia ya tender fake
 
Mtatiro umesahau kuwa watendaji wengi atakao wachagua watatoka kwa mkapa na jk , wengine umeona mwenyewe jk akimsistiza magufuli kuwa hawa hazina ya chama na serikali na huo ulikuwa ni ujumbe tosha kuwa asije akawaacha, kwahiyo hata wakivurunda atalazimika kuomba ruhusa kwa watangulizi wake ambao kimsingi ndio waajiri wake jpm
 
Back
Top Bottom