Mtanzania apora Sh. bilioni 400 za Aga Khan

Simon Martha Mkina

Investigative Journalist
Sep 5, 2020
21
110
aga.family.PNG

Familia ya Aga Khan ikiwa katika picha ya pamoja. Aliyeketi ndiye kiongozi wa sasa


Na Simon Mkina

Nyaraka za akaunti zilizoko Benki ya Barclays zinazoonyesha mmiliki wake ni Mtanzania – kwa miaka mitatu mfululizo, zimetumika kutakatisha zaidi ya Sh. bilioni 400, fedha zilizokwapuliwa kutoka Taasisi ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), uchunguzi umethibitisha.

Kiasi hiki ambacho ni zaidi Dola za Marekani milioni 176, zinatosha kujenga vyumba vya madarasa ya kisasa 10,000 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 450,000 wa shule za sekondari nchini – ikiwa kila darasa litabeba wanafunzi 45. Darasa la kisasa lenye samani zake linaweza kufikia Sh. milioni 40,000.

Pia fedha hizi ni sawa na mapato ya serikali kwenye mauzo ya makaa ya mawe Ruvuma kwa kipindi cha miaka mitatu (2017-2020) ambako zaidi ya vijana 700 wameajiriwa. Ni sawa na gharama za kujenga barabara ya kilomita 270 kwa kiwango cha lami, ikiwa kilometa moja itajengwa kwa Sh. bilioni 1.5.

Hata hivyo, kiasi hicho kikubwa cha fedha kiliingia mfukoni mwa Mtanzania anayejulikana kwa majina ya Janmohammed Mohamed Ali Rahemtulla, mkazi wa Dar es Salaam.

Uchunguzi wa Jamii Forums unaonyesha kuwa tawi la benki ya Barclays, New York, Marekani tayari limetoa ripoti inayoonyesha kutilia shaka Mtanzania huyo, Janmohamed Mohamed Ali Rahemtulla, na uchunguzi wa kumsaka umeanza kwa kutumia taasisi za uchunguzi za nchi hiyo, ikiwamo FBI.

Nyaraka zilizoonwa na mwandishi wa habari hii zinaonyesha kuwa Mtanzania huyo, anaishi Dar es Salaam, Barabara ya Uganda, maeneo ya Masaki, nyumba nambari 124.

Kazi ya Rahemtulla, kama inavyooekana katika nyaraka hizo za benki ni 'Mhazini Mwandamizi wa Aga Khan,’ na kwamba alikuwa akipokea fedha hizo kwa ajili ya taasisi hiyo kubwa ya kusaidia wenye uhitaji kwenye nchi 30 duniani.

Taarifa za benki hiyo zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2016, Rahemtulla alipokea dola 175,851,858 katika akaunti yake iliyoko katika benki hiyo, tawi la Geneva nchini Uswisi (Switzerland), kutoka tawi la New York.

rahemtulla.PNG

Baadhi ya nyaraka zilizoungwa zikionyesha Rahemtulla alivyopiga dili
Nyaraka za benki zilizoonwa na mwandishi wa habari hii zinaonyesha kuwa Rahemtulla alipokea pesa zote zilizokusudiwa kwa ajili ya AKDN, lakini uchunguzi umebaini kuwa hazikufika kwenye majukumu yoyote ya AKDN, hivyo kuwepo uwezekano mkubwa wa kumnufaisha Rahemtulla na makundi yanayohisiwa kujihusisha na utakatishaji fedha wa kimataifa, yakiwamo yale “yenye msimamo mkali.”

Fedha zilizopokelewa Geneva na Rahemtulla zilionekana kutoka benki za nchi kadhaa kupitia miamala 535. Benki hizo ni kutoka Seychelles, Oman, Mauritius, DR-Congo, Madagascar, Angola, Kenya, China na Uswisi.

Taarifa zinaonyesha kuwa kiwango cha juu ambacho Rahemtulla alitoa kwa siku ni dola milioni 2, huku cha chini kabisa kikiwa dola 2,443. Na kwamba katika kutoa fedha alieleza sababu ni “kupelekea msaada kwa wahitaji,” "ushuru wa kidini" au "mchango."

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi umebaini kuwa Rahemtulla hajawahi kukaa kwenye nyumba namba 124 iliyopo Barabara ya Uganda. Imebainika kuwa awali kulikuwapo nyumba ndogo ambayo ilibomolewa mwaka 2015 kupisha ujenzi wa jumba kubwa ambalo sasa kuna maduka chini ya Shoppers Plaza, ambayo inahusisha ‘Supermarket.’

Majirani wa muda mrefu wa kiwanja hicho namba 124, walisema kwenye kiwanja hicho kulikuwa na nyumba ndogo kabla ya kuvunjwa na kwamba wale walioishi hapo ni Watanzania, waliotokea Mtwara, na hawafanani kamwe kwa sura wala majina yenye asili ya Asia au Uajemi; Janmohammed ama Rahemtulla.

Uchunguzi zaidi unathibitisha kuwa Rahemtulla hajulikani popote ndani ya ofisi za Aga Khan na hajawahi kufanya kazi na AKDN nchini Tanzania au mahali pengine kama nyaraka za benki zinavyoonyesha.

Uchunguzi kupitia mitandao ya kijamii, udukuzi wa intaneti na njia zingine ikiwamo kupitia idara za uhamiaji Tanzania na Kenya, hazina taarifa za jina hilo.

2669699_Rew-Revealed.jpg

Rew-Revealed

Rew-Revealed Kataru, Mkurugenzi wa Aga Khan Foundation (AKF) - Tanzania, anasema hajawahi kusikia jina la Rahemtulla akifanya kazi katika shirika hilo. AKF ni moja ya vitengo vya misaada chini ya AKDN.

"Sijawahi kukutana na jina kama hili tangu nianze kazi hapa na nchi zingine ambako nimetumikia taasisi hii kwa zaidi ya miaka 10, kifupi, simfahamu,” alisema Rew-Revealed na kushauri kutafutwa kwa mwakilishi mkazi wa Aga Khan nchini Tanzania.

Mwandishi alikutana na kumhoji Amin Kurji, mwakilishi huyo mkazi ofisini kwake Upanga, Dar es Salaam ambaye alisema mara moja “huyo mtu hayupo, ni wa uwongo; hatuna mtu kama huyo ambaye anaweza kufanya jambo hilo la kutia shaka."

2669706_Amin.jpg

Kurji

Kurji alisema AKDN ina mifumo ya kifedha na uhasibu thabiti ambayo haiwezi kuchakachuliwa kwa urahisi kwa ajili ya kufanikisha utakatishaji wa fedha au manufaa ya mtu binafsi.

Alisema, AKDN yenye makao makuu ya Afrika Mashariki, Nairobi, Kenya michango yake kutoka kwa wasamaria wema, serikali au taasisi, hupokelewa na kutunzwa na watu wenye hofu, ustaarabu na heshima kubwa, hivyo siyo rahisi kuwa na “mtu hovyo.”

Alisema kiongozi wa AKDN kwa Afrika Mashariki kwa sasa ni Mohamed Lalji, mwenye makazi yake Nairobi, Kenya.

Mwandishi alitembelea ofisi za AKDN katikati ya jijini Nairobi, ndani ya Jengo la IPS, ghorofa ya nne na kukutana na binti aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wa ofisi na kueleza kuwa maofisa wote wako likizo ya lazima kutokana na kuwepo kwa janga la ugonjwa wa Corona. Alikataa kutoa namba za wahusika kwa maelezo kwamba “haruhusiwi.”

Baada ya siku tatu, ofisa mmoja mwandamizi ambaye hakutaka kunukuliwa kwenye vyombo vya habari alisema hajawahi kusikia mwenye jina hilo la Rahemtulla akifanya kazi AKDN na kueleza; "Nadhani watu hawa walikuwa wakitumia jina la Aga Khan kufyonza pesa kutoka vyanzo vingine kupitia akaunti zetu au walidanganya wanavyojua wao kwa faida yao ya kishetani, lakini hatuwajui. Inasikitisha!”

Alimtaja mwakilishi wa Aga Khan Afrika Mashariki kuwa ni Dk. Azim Lakhan ambapo aliahidi kumfikishia ujumbe na kwamba angepiga simu mapema. Lakini hadi habari hii inaenda hewani hakuna mawasiliano yoyote kutoka kwake wala ofisi za AKDN.

Mfanyakazi mwandamizi wa sekta ya benki Tanzania, Masoud Hillary, aliyewahi kuajiriwa na benki kadhaa, ikiwamo FBME Tanzania akielezea namna wizi wa fedha unavyoweza kufanywa alisema; “wizi mkubwa kutoka kwenye akaunti zenye fedha nyingi, umekuwa ukifanywa mahali pengi, lakini lazima uhusishe wafanyakazi wa benki husika.”

Anasema hata Tanzania kumewahi kuwepo historia ya namna fedha zinavyoweza kuchotwa na wahusika wasigundue mapema, hasa kama ni fedha za taasisi zinazokaa muda mrefu kwenye akaunti bila kutolewa.

Masoud alitoa mfano wa wizi wa aina ya Rahemulla akiufananisha na ule uliofanyika mwaka 2012 katika Benki ya Exim tawi la Arusha, ambapo meneja wa tawi hilo, Livingstone Mwakihaba alikwapua zaidi ya Sh. milioni 550 kutoka akaunti ya mteja kwa kumpatia nyaraka za kugushi. Meneja huyo alikamatwa, kushtakiwa na kupatikana na hatia ambapo alifungwa jela maisha.

Pesa jijini Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Nairobi

Uchunguzi unaonyesha kuwa pesa zingine kutoka kwa Rahemtulla zilitumwa kwa Garetus Ruto wa Nairobi, Kenya, kupitia benki ya FBME Tanzania Limited. Maelezo yanaonyesha kwamba mpokeaji alikuwa mfanyabiashara anayeshughulikia kampuni ya ujenzi akiwa na ofisi katika majengo ya Maser Ensuite, Waiyaki Way, eneo la Westlands. Hata hivo uchunguzi Zaidi unaonyesha kuwa jengo hilo ni makazi ya watu na hakuna ofisi.

Akaunti za Garetus zilipokea na kuondoa dola 320,915 katika tarehe tofauti kuanzia Julai 17, 2014 hadi Aprili 12, 2016.

uknown1.PNG

Garetus Ruto

Kampuni yake, GR Construction Company Limited haikupatikana katika taasisi zozote za usajili nchini Kenya; kumbukumbu katika Ofisi ya Msajili wa Biashara (BRS) hazina maelezo yake kama ilivyo kwa Mamlaka ya Ujenzi ya Kitaifa ya Kenya (NCA).

Ruto ni jina la ukoo maarufu nchini Kenya. Miongoni mwa wakubwa wenye jina hilo ni Makamu wa Rais William Ruto. Lakini imebainika kuwa Garetus hana uhusiano wowote na makamu huyo wa rais.

Kulingana na habari zilizopokelewa kutoka kwa taasisi mbali mbali, mtu mwingine ambaye ni mfanyabiashara wa Kitanzania, Juma Salum Isiko, alipokea pesa kutoka kwa Rahemtulla kupitia Benki ya FBME Bank Limited - Tanzania kutoka Julai 17, 2014 hadi Aprili 12, 2016. Isiko alidai kuwa mkurugenzi wa Isman General Traders yenye ofisi katika miji ya Arusha, Zanzibar na Mwanza.

Maelezo ya benki hiyo yanaonyesha kuwa kampuni ya Isman ina anwani iliyosajiliwa ya S.L.P 18834, Dar Es Salaam, Tanzania, na imeainishwa kuwa inafanya biashara ya usafirishaji mizigo. Kanzidata ya Kidigitali ya Mjue Mteja Wako (eKYC) inaonyesha kwamba taarifa za kampuni hiyo ziliboreshwa mara ya mwisho Oktoba 9, 2015.

Uchunguzi wa mwandishi unaonyesha kuwa kampuni hiyo inajitanabaisha katika taarifa za benki kuwa ni "kampuni ya kimataifa ya usafirishaji mizigo iliyobobea katika usafirishaji kupitia anga, bahari na barabara na inahudumia zaidi nchi za DR-Congo, Rwanda na Zambia.”

Kanzidata inaonyesha kuwa kampuni inaajiri watu kumi (10), ina mali ya dola milioni 20, madeni yanayofikia dola milioni 10 za madeni na kuwa na mapato ya faida yanayofikia dola milioni nane “baada ya makato ya kodi.”

Uchunguzi unaonyesha kuwa akaunti za kampuni hiyo zilipitisha na kutolewa dola 384,917.59 katika kipindi hicho.

Aidha, Kanzidata ya inaonyesha kuwa Isiko alizaliwa Tabora, Tanzania, na kutambuliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo tangu 2012 na kwamba mkurugenzi huyo ni mshauri mwandamizi wa tasnia ya usafirishaji nchini Tanzania tangu 2010.

Uchunguzi umebaini kuwa kampuni hiyo haijawahi kusajiliwa popote na serikali na kwamba hakuna ofisi za kampuni ya Isman zilizopatikana katika maeneo yafuatayo kama ilivyodaiwa katika nyaraka za benki; Mwanza (Pamba House), kando ya Barabara ya Pamba; jengo la AICC, jijini Arusha; na katika Hoteli ya Bwawani, Zanzibar.

Serikali ya Tanzania kupitia Benki Kuu (BoT) ilinyang’anya leseni ya kuendesha shughuli za Benki ya FBME baada ya kubainika kutofuata taratibu za kibenki na kushindwa kuzingatia makatazo ya utakatishaji fedha, hivyo kuwekwa chini ya uangalizi. Hadi sasa benki hiyo iliyokuwa na tawi lake Barabara ya Samora, Dar es Salaam haijafunguliwa. Baadaye ilibainika kuwa benki hiyo, Pamoja na kuwa na ofisi kubwa Tanzania, fedha zake zilikuwa zikihifadhiwa Cyprus, nchi inayohusishwa na wepesi wa kuhifadhi fedha zenye shaka.

Nyaraka kutoka serikali ya Marekani na kupatikana mikononi mwa Shirika la Habari la BuzzFeed News la nchini humo na baadaye kufika kwa Taasisi ya Kimataifa ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ), ambamo mwandishi ni mshirika, zinaonyesha kwamba kuna mawasiliano yanaendelea kati ya matawi ya benki ya Barclays Uswisi na Barclays New York kuhusu sakata hili.

Hata hivyo, Barclays Uswisi ilipoulizwa kuhusu suala hili haikuwa tayari kuweka wazi na kueleza kwamba “usiri wa wateja na taratibu za benki haziruhusu na pia bado kuna uchunguzi unaendelea.”

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya Rahemtulla kutiliwa shaka na kuanza kufuatiliwa, aliitwa kuhojiwa juu ya uhalali wake kutoa kiasi kikubwa cha fedha mara kwa mara kwa maelezo kuwa ni fedha za misaada kwa ajili ya Aga Khan, “alipotea na hakuonekana tena.”

Katika maelezo yake, benki hiyo ilieleza kwamba Rahemtulla huenda alikuwa akishirikiana na wahalifu na makundi hatari, yakiwamo ya kigaidia kufanya wizi ambao haukugundulika mapema, ndiyo maana baada ya kushukiwa alipotea.

“Utaratibu wa kuchukua fedha kupitia kwa Rahemtulla ulisimama ghafla baada ya mteja huyo kuitwa na kutakiwa kuelezea sababu za kuchukua kiasi kikubwa cha fedha,” ilieleza taarifa ya benki hiyo na kuongeza kwamba siku alipoulizwa na kuahidi kurejea kwa mazungumzo Zaidi, hakupatikana na taarifa zake zilizoko benki, hazijaweza kusaidia kukamatwa kwake,”.

Mwanasheria mwandamizi wa Taasisi za Aga Khan, aliyeko Geneva, Uswisi, Daniel Schafer baada ya kuulizwa kuhusu wizi huu na hatua ambazo AKDN imechukua kuhusu upotevu wa fedha hizo hakujibu maswali aliyotumiwa, isipokuwa alijikita kueleza sifa nyingi za taasisi hiyo katika kusaidia jamii zenye uhitaji. Hakutoa maelezo yoyote juu ya upotevu wa dola milioni 176 zilizolipitia kwenye akaunti za Rahemtulla kutoka akaunti za AKDN.

Sehemu ya barua yake aliandika; “Mtukufu Aga Khan hutoa ufadhili wa mara kwa mara kwa shughuli za maendeleo katika sekta za afya, elimu, kilimo na huduma zingine muhimu kwa nchi mbalimbali, hasa zenye kiwango kikbwa cha umasikini. Pia alielezea namna AKDN inavyopokea fedha zake kutoka vyanzo mbalimbali.

Aga Khan, ni Imam wa urithi wa watu wa Ismailia, dhamana ambayo hurithiwa kutoka kwa baba kwenda kwa mtoto au mjukuu, ikiwa na hadhi saw ana mkuu wa nchi. Mtu anaweza kumlinganisha Aga Khan na Dalai Lama – kiongozi wa mabuda wa Tibet au hata Papa – kiongozi wa Katoliki duniani.

Miaka iliyopita, Aga Khan (neno ambalo linamaanisha "Chifu Mkuu") alipokea zawadi za vito vya thamani ikiwamo dhahabu na hata almasi kutoka kwa wafuasi wake ili kusherehekea maadhimisho ya miaka ya utawala kila mwaka. Utajiri huu uliwawezesha familia hiyo kuunda himaya kubwa na inayoheshimiwa.

Aga Khan wa sasa; Karim (84) anayeishi Paris, Ufaransa ni tajiri mkubwa. Kila mwaka, anapokea “zawadi” ya asilimia 10 hadi 12 kutoka kwenye mapato ya kila muumini wa Ismailia duniani. Inakadiriwa kuwa wapo waumini wanaofikia milioni 15 duniani, wengi wakiwa wafanyabiashara na matajiri wakubwa.

jfund.logo.png


Habari hii ya uchunguzi imefadhiliwa na Mradi wa Money Trail chini ya taasisi ya Jornalismfund.eu (www.money-trail.org)
 
Nimesoma hapo kwa huyo jamaa wa Nairobi mwenye hiyo kampuni ambayo imethibitika haijasajiliwa Kenya (GR Construction Limited) nime- conclude hao Aga Khan nao wanastahili lawama, haiwezekani wafanye kazi na kampuni isiyosajiliwa, hapa nahisi baadhi ya maofisa wake watakuwa wanahusika na huo mchezo mchafu.

Lakini pia, kitendo cha FBI kutilia shaka nyendo za huyo jamaa mpaka waanze kumtafuta inaonesha jinsi taasisi zetu za kiuchunguzi hapa ndani zilivyolala, au inawezekana nao ni sehemu ya hilo dili kuna kitu walipewa wakafungwa midomo.

Nasema hivi kwasababu mabenki yetu mara nyingi yamekuwa yakitoa taarifa za wateja wao kwa serikali, na hao Baclays wana tawi Tz, sasa vipi kwa huyo muhusika ishindikane kumgundua mapema? hapa wafanyakazi wa hiyo benki wanatakiwa kujibu maswali.
 
Duuh hii habari usome mwanzo mwisho huelewi. Mtu hajulikani ni nani na anaishi wapi ila kuna waliomwita wakitaka maelezo toka kwake akaahidi kurudi na hajawahi kuonekana tena?

Hao waliomwita walimpata vipi mpaka wakamhoji na sasa hawajui alipo na anapatikana wapi?

Hii ni michezo ya watu wakubwa wa dunia maana ni hela nyinyi sana hiyo
 
Nimesoma hapo kwa huyo jamaa wa Nairobi mwenye hiyo kampuni ambayo imethibitika haijasajiliwa Kenya (GR Construction Limited) nime- conclude hao Aga Khan nao wanastahili lawama, haiwezekani wafanye kazi na kampuni isiyosajiliwa, hapa nahisi baadhi ya maofisa wake watakuwa wanahusika na huo mchezo mchafu...
Huu ni mchezo sio mchafu ila ni umafia uliohalalishwa. Huyo jamaa hao waliomhoji akaahidi kurudi kwa mahojiano zaidi na akapotea mpaka leo walimpata vipi ndo wakamhoji?

Mtu hajulikani kila adress yake ni fake ila kuna waliofanikiwa kumpata na kumhoji kidogo.
 
Huu ni mchezo sio mchafu ila ni umafia uliohalalishwa. Huyo jamaa hao waliomhoji akaahidi kurudi kwa mahojiano zaidi na akapotea mpaka leo walimpata vipi ndo wakamhoji?....
Pamoja na kwamba maelezo ya awali ya benki yanakanganya, lakini inawezekana siku alipokwenda kutoa fedha, dirishani, aliitwa na uongozi na akaahidi kurejea siku inayofuata.

Lakini hakutokea na hakuna traces. Akapotea. Kama unavyosema, ni mchezo unaohusisha idadi kubwa ya watu wakiwamo maofisa wa benki na hata taasisi
 
Aisee Habari inasisimua na kupendeza kama movie za Hollywood
Zinaanza mtu anakura bata
Kisha wazee wa kazi FBI wanaingia kati
Sasa ule mchezo mara tanzania mara kenya kutafuta EVIDENCE ndo inafanya MOVIE kuwa moto

sasa hukute hollywood wameitengenezea MOVIE hii utaenjoy
 
Pamoja na kwamba maelezo ya awali ya benki yanakanganya, lakini inawezekana siku alipokwenda kutoa fedha, dirishani, aliitwa na uongozi na akaahidi kurejea siku inayofuata. Lakini hakutokea na hakuna traces. Akapotea. Kama unavyosema, ni mchezo unaohusisha idadi kubwa ya watu wakiwamo maofisa wa benki na hata taasisi
Kwa miamala yote iliyofanyika kama ni mtu wa kutolea hela dirishani badi ana adress inayoleweka maana bank kuna mambo za fingerprint, cctv camera n.k ina maana bank walifuta hata footage za cctv camera?

Mtu kama huyo unafanya naye mahojiano ambayo hayana hata traces? Hii ni michongo ya watu na inasisha kama hivyo maana biashara yao ishamalizika.

Kama biashara ingekua haijamalizika ungesikia balaa lake na mpaka wangemtia mkononi
 
Network hii kui-crack ni ngumu kuliko ya Q-NET!

Hawa Aga Khan Foundation, watakuwepo watumishi wao wa chini, wasiodhaniwa wanaohusika na hili.

CCTV hazina picha ya Rehmtullah??

Bahati mbaya yawezekana mpaka taarifa na uchunguzi umesambaa kwa kiwango hiki, naamini wengi watakuwa wameshawanyamazisha mazima!

Everyday is Saturday.............................. :cool:
 
30 Reactions
Reply
Back
Top Bottom