Mtandao wa wanafunzi Tanzania TSNP, umetoa angalizo katika maeneo kadhaa kuelekea kufunguliwa kwa vyuo na kidato cha sita nchini

Dec 13, 2016
8
5
Kufuatia tamko la Serikali juu ya kufunguliwa kwa vyuo na vyuo vikuu vyote nchini pamoja na
wanafunzi wa kidato cha sita hapo Tarehe 1 Juni 2020, Mtandao wa Wanafunzi Tanzania – TSNP
unapenda kutoa angalizo katika maeneo kadhaa ili kuhakikisha haki na ustawi wa wanafunzi
unazingatiwa kikamilifu hasa katika kipindi hiki cha dharura ya mlipuko wa ugonjwa wa
COVID19;

1. Serikali ilifunga shule Tarehe 17 Machi 2020 sawa na siku 50 kabla ya mitihani ya Taifa
kidato cha sita haijaanza mwezi Mei 4, 2020 kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa awali na
Baraza la Taifa la Mitihani – NECTA. Hata hivyo, tamko la kurudi shuleni kwa wanafunzi
wa kidato cha sita linaelekeza kwamba, mitihani ya Taifa itaanza Tarehe 29 Juni 2019 sawa
na siku 28 tu za maandalizi mara baada ya kurudi shuleni. TSNP tunaona muda wanaopewa
kujiandaa na Mitihani ya Taifa utawaumiza wanafunzi wa kidato cha sita hasa wanaoishi
vijijini pamoja na wanafunzi wa sayansi ambao huenda hawakupata fursa nzuri ya kujiandaa
na mitihani muda huo wa dharura. Serikali ione umuhimu wa kuongeza muda wa maandalizi
ya wanafunzi wa kidato cha sita kabla ya mitihani.

2. Kwakuwa bado haijathibitika ni kwa kiasi gani ugonjwa wa CORONA umepungua nchini,
kwa namna yeyote ile, kufungua vyuo na vyuo vikuu hapo Juni 1, 2020 kutawaweka
wanafunzi katika hatari ya maambukizi kutokana na uhalisia kwamba shughuli nyingi za
kitaaluma huwaleta wanafunzi wengi pamoja. TSNP inatoa angalizo kwa wanafunzi
wenyewe kujilinda na maambukizi ya virusi vya CORONA kwa kadiri iwezekanavyo ili
kulinda uhai wao. Tunatoa angalizo pia kwa uongozi wa vyuo na Serikali za wanafunzi
vyuoni kuhakikisha kwamba, zinajiridhisha kuwa vyuo vyao vina mazingira salama ya
kujikinga na maambukizi ili kuwalinda wanafunzi.

3. Mlipuko wa ugonjwa wa COVID19 umeathiri uchumi wa wananchi kutokana na kudorora
kwa shughuli za uzajilishaji na biashara. Mamlaka za TCU na NACTE ni vyema zikaweka
utaratibu elekezi wa Tarehe ya mwisho ya usajili wa wanafunzi ambayo inahusisha
kulipia/kulipiwa ada ya muhula wa pili ili kuwalinda wanafunzi wanaojigharamia ada
(wasiolipiwa na Bodi ya Mikopo) waweze kuwa na muda wa kutosha kulipia.

4. Vile vile, TSNP inatoa angalizo ya kwamba, jitihada zinazofanywa na vyuo na vyuo vikuu
nchini katika kufidia muda uliopotea zisihusishe kabisa kulimbikiza mfululizo wa vipindi
vya masomo kuliko kawaida ili tu kumaliza mhula mapema. Hii ni hatari kwa ustawi wa
kitaaluma wa mwanafunzi kwakuwa kila binadamu ana kiwango cha mwisho cha kujifunza
na kuelewa darasani kwa wakati mmoja.

Mtandao wa wanafunzi Tanzania – TSNP unathamini sana jitihada zinazofanywa na serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongoza mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa
wa COVID19, kulinda uchumi wa nchi na kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa ya kuendelea na
masomo. TSNP inatoa wito kwa wanafunzi kutumia vyema fursa ya kurudi shuleni (kwa kidato
cha sita) na vyuoni kupambania taaluma zao ambazo ni za muhimu sana bila kusahau kuwa uhai
wao ni muhimu zaidi.

Imetolewa na;

Davis Betram Komba
Mwenyekiti
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania – TSNP
Mei 23, 2020
IMG-20200523-WA0094.jpg
IMG-20200523-WA0095.jpg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom