Mtandao wa kuwalinda ofisi ya DPP wabainika, Vigogo wa ufisadi waanza kutikiswa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mtandao wa kuwalinda ofisi ya DPP wabainika, Vigogo wa ufisadi waanza kutikiswa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by abdulahsaf, May 24, 2012.

 1. a

  abdulahsaf JF-Expert Member

  #1
  May 24, 2012
  Joined: Aug 31, 2010
  Messages: 859
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  WAKATI Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, akijiandaa kuanza kuwahoji vigogo watuhumiwa wa ufisadi, zipo taarifa kwamba kuna mtandao ndani ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) unaokwamisha kazi hiyo, Raia Mwema imeambiwa.

  Taarifa zinasema ukwamishaji huo unafanywa na baadhi ya watendaji wa ofisi ya DPP katika mazingira yanayoashiria rushwa ili vigogo watuhumiwa wasishitakiwe.

  Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili ambao umehusisha baadhi ya maofisa katika ofisi za DPP na TAKUKURU, kwa muda mrefu sasa, baadhi ya mafaili yanayohusu vigogo wala rushwa na wengine wakiwa rafiki zao, yamekuwa yakikwamishwa katika ofisi ya DPP kwa maelezo ya "uchunguzi" kutokukamilika, hatua ambayo wakati fulani iliwahi kuleta mvutano kati ya Dk. Hosea na DPP Dk. Eliezer Feleshi.

  Mara kwa mara, TAKUKURU imekuwa ikiwasilisha mafaili ya baadhi ya vigogo kwa DPP lakini badala ya kutolewa idhini ya mashitaka, mafaili hayo yamekuwa yakirudishwa TAKUKURU kwa madai kuwa uchunguzi zaidi unahitajika wakati maofisa wa TAKUKURU wakiamini kuwa kwa kuzingatia utaalamu wao, uchunguzi umekamilika na mashitaka yamebeba uzito mkubwa wa kufungua kesi mahakamani.

  Gazeti hili halitachapisha kwa sasa majina ya maofisa wanaohusika katika kadhia hiyo ndani ya ofisi ya DPP kutokana na kutopata maelezo ya wahusika lakini kwa upande mwingine, imefahamika kwamba kati ya mafaili yanayopigwa danadana kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili ni la kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi kutoka katika kampuni ya BAE Systems ya Uingereza.

  Hata hivyo, katika hali inayozidi kuthibitisha kuwa hamkani si shwari katika ofisi ya DPP, ofisa katika Wizara ya Katiba na Sheria amemweleza mwandishi wetu: "Hatua zimekwishawahi kuchukuliwa kwa baadhi ya watendaji" lakini akishindwa kueleza kwa kina namna tatizo la uadilifu katika ofisi ya DPP linavyochafua taswira ya ofisi hiyo.

  Mbali na hali hiyo, kwa upande mwingine utafiti umebainika kuwa tatizo la ufanisi wa taasisi hiyo ni sheria inayoendesha chombo hicho na Mkurugenzi wa Mashitaka (DDP), akitajwa kuiendesha TAKUKURU kwa mlango wa nyuma.

  Kwa mujibu wa ripoti za Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) ambayo umeendesha utafiti wake nchini ikiwa ni pamoja na kuwahoji wadau mbalimbali, TAKUKURU inakwamishwa na sheria inayoilazimu kupata kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) katika kuwashitaki watuhumiwa wakubwa wa rushwa nchini.

  Matokeo ya Utafiti wa APRM

  Katika utafiti wake, APRM inaeleza kizingiti cha ufanisi katika utendaji kazi wa TAKUKURU kuwa ni sheria ya chombo hicho nyeti sehemu ya 57, ambayo inatamka kwamba TAKUKURU ni lazima wapate kibali cha DPP ili waweze kufungua kesi za wala rushwa wakubwa.

  "Ni wala rushwa wadogo wadogo tu ndio wanaoweza kushitakiwa bila mizengwe. Makosa makubwa ya rushwa yanayohusu viongozi au marafiki wa viongozi wakubwa ni nadra kushughulikiwa kwa maana ya kufunguliwa kesi.

  "Rais ndiye anayemteua DPP. Na huyo DPP ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuua kesi yoyote bila kutoa sababu (nolle proseque prerogative). Mfumo huu wa kitaasisi wa kutenganisha kati ya mamlaka ya uchunguzi na uendeshaji mashitaka unafanana na Azimio la Havana la mwaka 1990.

  "Azimio hilo linataka mamlaka ya mashitaka iwe tofauti na mamlaka ya uchunguzi ili kulinda haki za watu ambazo zinaweza kupuuzwa kama mamlaka hayo yatakuwa upande mmoja.

  "Hata hivyo, mfumo huu unaelekea kuinyima mamlaka ya kiutendaji TAKUKURU na kimsingi, unakandamiza juhudi za TAKUKURU," inaeleza ripoti hiyo ya utafiti wa APRM.

  Mgongano kati ya TAKUKURU na DPP

  Kama ambavyo imewahi kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuhusu mvutano kati ya Dk. Hosea na Dk. Feleshi, ndivyo ambavyo ripoti za APRM zinavyoeleza.

  "Kumewahi kuwa na mgongano kati ya ofisi hizi mbili katika taarifa zao kwa umma kuhusu mafaili ya kesi. Kuinyima TAKUKURU mamlaka ya kushitaki moja kwa moja kunakinyima chombo hicho nguvu za kutosha kukabili rushwa kubwa.

  Maelezo ya Wizara ya Katiba na Sheria

  Ofisa mmoja katika Wizara ya Katiba na Sheria, akizungumzia masuala hayo anasema: "Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa ofisi hizi mbili zinafanya kazi kwa ushirikiano mzuri. Lakini pili, msingi wa sheria kumtaka DPP atoe kibali (consent) cha mashtaka ni kutekeleza matakwa ya utawala bora na kuufanya mfumo wetu wa haki jinai uonekane unatenda haki.

  "Vyombo vya uchunguzi ikiwamo TAKUKURU vifanye uchunguzi kwa kina, DPP aendeshe mashtaka yaliyofanyiwa uchunguzi wa kina ili hatimaye Mahakama itoe uamuzi wa haki. Huwezi kuwa na chombo kimoja kinafanya yote au mawili, huu ndio mfumo bora duniani kote na kwa Tanzania umesaidia sana kupunguza mlundikano wa mashauri na mahabusu kwa kuwa yale yenye ushahidi usio na shaka ndio hupelekwa mahakamani baada ya kuchambuliwa ...Kiingereza inaitwa investigation-led prosecution".

  Kuhusu baadhi ya watumishi ndani ya ofisi ya DPP kujihusiha na mchezo mchafu wa kuchelewesha kesi, ofisa huyo anasema: "Ndiyo nasikia kwako, ni vema tukajua ni nani na anahusika na shauri gani. Lakini sheria na taratibu zipo za kushughulikia watumishi kama hao mara ikithibitika na kuna baadhi wameshawahi kuchukuliwa hatua stahili. Hii taarifa nitazipa mamlaka za nidhamu."

  Dk. Hosea na uchunguzi TAZARA

  Katika hatua nyingine, Dk. Hosea amemweleza mwandishi wetu kwamba taasisi yake ilikwishakuanza kuchunguza tuhuma za rushwa katika Mamlaka ya Reli ya Zambia na Tanzania (TAZARA).

  Maelezo hayo ya Dk. Hosea ni sehemu ya majibu kwa kauli ya hivi karibuni ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba akishirikiana na Waziri wa wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambao kwa pamoja walikuwa wakijiandaa kuipa taarifa TAKUKURU ichunguze kadhia ya rushwa TAZARA.

  Akizungumzia hatua zilizokwishaanza kuchukuliwa muda mrefu na TAKUKURU kwa TAZARA, Dk. Hosea alisema: "Uuzwaji wa waziwazi wa vitega uchumi, hujuma katika miundombinu ya reli pamoja na uuzwaji wa nyumba za TAZARA zilizoko mkoani Mbeya ni kati ya mambo tuliyokwishaanza kuyachunguza muda mrefu."

  Hata hivyo, pamoja na Dk. Hosea kueleza kuanza uchunguzi naye ameeleza namna kifungu namba 57 cha sheria ya TAKUKURU kinavyowapa wakati mgumu katika kujijengea imani kwa umma. Kifungu hicho ndicho kinaelekeza taasisi hiyo iwasilishe uchunguzi wake kwa DPP na kisha kusubiri ‘utashi' wa ofisi ya DPP.

  Hosea na uuzaji nyumba TAZARA

  Kinyume cha matamko yake ya mara kwa mara bila kulaumu, safari hii Dk. Hosea amemweleza mwandishi wetu: "TAZARA ilikuwa ikitoa huduma nzuri sana si kama ilivyo sasa, baadhi ya nyumba zake zimeuzwa kiholela mkoani Mbeya na kusababisha baadhi ya wafanyakazi kukosa nyumba za kuishi.

  "Tumeanza uchunguzi mapema lakini kama unavyofahamu mchakato huu unazo hatua ambazo ni pamoja na uthibitishaji wa taarifa, watu kutoa ushirikiano wa kutosha pamoja na vielelezo vya kuthibitisha hayo tunayoyachunguza."

  Mbali na mawaziri wapya na hatua za TAKUKURU kuichunguza TAZARA, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu naye aliwahi kuitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo kuisimamisha kazi menejimenti kwa sababu za kukosa ufanisi uliotarajiwa.

  Miongoni mwa mambo yanayoiondolea sifa Menejimenti ya TAZARA kwa sasa ni pamoja na kudaiwa kushindwa kulipa mishahara kwa wakati, kushindwa kuwasilisha makato ya wafanyakazi kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kushindwa kushughulikia changamoto nyinginezo.

  Mbali na hayo, udanganyifu mkubwa umeripotiwa katika mizani ya kupima mizigo, ikielezwa kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakirekodi kiwango kidogo cha uzito wa mizigo wakati uhalisia ni kwamba mzigo husika ni mkubwa kwa tani nyingi zaidi.

  Mizigo inayohusishwa na udanganyifu huo ni shaba ambayo imekuwa ikisafirishwa kutoka New Kapirimposhi Zambia kwenda Dar es Salaam, ikibainika kuwa katika baadhi ya mizigo kumekuwa na uzidishaji wa tani hadi saba. Mkurugenzi wa TAZARA ndiye anayetuhumiwa kuwa na tabia ya kunufaika na uchakachuaji huo wa uzito wa mizigo.

  Mwandishi wetu amezungumza na Mkurugenzi huyo wa TAZARA, Akashambatwa Mbikusita, ambaye hakuwa na majibu ya moja kwa moja kukiri au kukanusha kuhusika kwake katika tuhuma hizo na badala yake akatoa maelezo ya ufafanuzi na hatua zilizochukuliwa kuzuia tatizo hilo.

  "Nakiri kuwapo kwa tatizo hili (uchakachuaji wa uzito wa mizigo) na nimechukua hatua za kubuni utaratibu mpya unaohusisha Benki Kuu ya Zambia katika kuhakiki mizigo yote kabla haijasafirishwa kwenda nje ya nchi," alisema.

  Akashambatwa alitoa ufafanuzi huo kupitia taarifa aliyoituma kwa njia ya baruapepe kwa mwandishi wetu.

  Mbali na matatizo hayo, TAZARA imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingine mbalimbali ikiwamo wizi wa mafuta ya kuendeshea treni.

  Kwa upande wake, Waziri mpya wa Uchukuzi, Dk. Mwakyembe amekiri kuwapo kwa usimamiaji mbovu wa rasilimali pamoja na uongozi usiowajibika katika TAZARA.

  "Ni ujinga kufanya kazi na watu walewale, mbinu zile zile huku ukitegemea kupata matokeo tofauti, lazima tuondoe changamoto za kipuuzi puuzi TAZARA," alisema Mwakyembe.

  Miongoni mwa kasoro zilizopo TAZARA ziliwahi kuainishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Erasto Kihwele, kwa niaba ya wafanyakazi.

  Chanzo:Raia Mwema

   
 2. Kakke

  Kakke JF-Expert Member

  #2
  May 24, 2012
  Joined: Dec 4, 2010
  Messages: 1,797
  Likes Received: 389
  Trophy Points: 180
  abdulahsaf

  KATIKA ukurasa wa kwanza wa gazeti hili, kuna habari kuhusiana na mvutano mkubwa uliopo kati ya taasisi mbili nyeti nchini: Ofisi ya Mwendasha Mashitaka (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
  Mvutano huo unatokana na kigugumizi kilichopo cha kuwafikisha mbele ya sheria wenye tuhuma kubwakubwa za rushwa na ufisadi mwingine ambao TAKUKURU imewachunguza.
  Habari hiyo inatoa mwanga ni kwa nini Taifa linatwanga maji kwenye kinu katika vita ya kupambana na rushwa kwa kisingizio cha ‘utawala bora.'
  Hicho kinachoitwa utawala bora ndicho kinachofanya vigogo wa rushwa kubwa nchini ambao wana maswahiba serikalini kuwa na kinga ya kushitakiwa.
  Na kinga yao ni ‘utawala bora' unaofanya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuwa mwenye mamlaka pekee ya kutoa kibali cha kuwafikisha mahakamani au la.
  Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba walioko serikalini na wenye marafiki serikalini ni rahisi ‘kucheza' na ofisi ya DPP kuepuka mkono wa chuma dhidi yao.
  Na hilo ndilo linalofanyika, hivyo haishangazi kuona kwamba baadhi ya vigogo wenye tuhuma kubwa za rushwa ambao TAKUKURU imemaliza kuwachunguza, wamepiga kambi kwenye ofisi za DPP kutaka kuokolewa.
  Tunasikitika kusema kwamba pamoja na ukweli kwamba sheria kumtaka DPP atoe kibali cha mashtaka ni kutekeleza matakwa ya utawala bora na kuufanya mfumo wetu wa haki jinai uonekane unatenda haki, kinachofanyika ni kinyume chake.
  Kutokana na kile kinachofanyika, hatupaswi kutamba kwamba TAKUKURU tumeipa meno. Meno gani wakati mambo yote yako kwenye ofisi ya DPP?
  Hatuwaoni watuhumiwa wakubwa nchini kwa mfano wa kesi ya rada, wakifikishwa mahakamani. Bila shaka ni kutokana na mfumo huo unaotoa nafasi ya ‘wakubwa' kulindana.
  Ni imani yetu kwamba katika mchakato wa kuandika Katiba mpya, suala hili litajitokeza kwa nia ya kulirekebisha ili watoa rushwa wakubwa nao washughulikiwe kama wadogo ambao hushukiwa kama mwewe kwa utaratibu wa sasa.
  Tunaamini kwamba hakuna hali ambayo ni ya kudumu. Kama ufumbuzi hautakuwa kwenye Katiba mpya basi, utatokana na sababu nyingine.


  KUTOKA KWA John Bwire   
 3. jmushi1

  jmushi1 JF-Expert Member

  #3
  May 23, 2014
  Joined: Nov 2, 2007
  Messages: 17,543
  Likes Received: 1,892
  Trophy Points: 280
  Katiba mpya iangalie hi issue!
   
 4. Kibanga Ampiga Mkoloni

  Kibanga Ampiga Mkoloni JF-Expert Member

  #4
  May 23, 2014
  Joined: Aug 9, 2007
  Messages: 14,565
  Likes Received: 1,649
  Trophy Points: 280
  We acha tu, Ipo siku!
   
 5. Chakaza

  Chakaza JF-Expert Member

  #5
  May 23, 2014
  Joined: Mar 10, 2007
  Messages: 23,643
  Likes Received: 21,854
  Trophy Points: 280
  Bwana mkubwa mwenyewe yupo tuu pale karibu na Ferry anaangalia kama vile mtu anayetazama filamu ya katuni. Tuzunguke kote ila tatizo ni kwa mkulu mwenyewe kutokuwa na nia ya dhati katika mambo kama hayo.
  Pamoja na sheria kuwa na mapungufu,bado kashfa kubwa kubwa kama za Rada,EPA na haya madudu ya IPTL ilikuwa ni lazima mkuu mwenyewe aingilie kati na kuona kipi kinafanyika. Hawezi kuwa kila siku kiguu na njia kwenda kutembeza bakuli kwa fedheha huku nyuma fedha zinazoibiwa ni nyingi kuliko alizokwenda kuomba. Unless kama yeye mwenyewe hana mshipa wa aibu.
  Huwezi kwenda kuomba debe la unga kwa jirani wakati huku nyumbani watoto wanachezea gunia la unga.


  Sent from my iPad using JamiiForums
   
Loading...