Mswada mpya jeneza la upinzani...

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,238
Mswada mpya jeneza la upinzani

Na Ahmed Rajab

MFUMO wa demokrasia ya vyama vingi haukukaa sawa katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Kuna dalili kuwa nchi hizo zinaelekea kuwa sawa na nchi zenye mfumo wa chama kimoja.

Kenya na Tanzania ni miongoni mwazo. Lakini zinatofautiana.

Kenya imekuwa kama taifa la chama kimoja kwa viongozi wa upinzani kupewa mifupa waing’ong’one huku wakicheza ngoma ya mdundo mmoja na viongozi wa chama kinachotawala. Tanzania inageuka kuwa taifa la chama kimoja kwa serikali kuvikandamiza vyama vya upinzani visiweze kuvuta pumzi.

Kila kukicha serikali inavifanyia ngumu vyama vya upinzani visifurukute na kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kuikosoa serikali inapohitaji kukosolewa au kuwapa wananchi sera mbadala za kuiendesha nchi.

Majuzi serikali ya Tanzania iliufikisha bungeni Mswada kuhusu Sheria Mpya ya Vyama vya Siasa. Mswada huo utajadiliwa katika kikao cha bunge cha Januari 2019. Ukipitishwa, utakuwa jeneza la kuvibebea vyama vya upinzani hadi makaburini vitakozikwa.

Mswada huo unampa madaraka makubwa mno Msajili wa Vyama na, kwa kupitia yeye, Rais wa Jamhuri, anayemteua. Vyama vitakuwa chini ya udhibiti na ukaguzi wa Msajili.

Atakuwa na haki ya kuviingilia moja kwa moja vyama vya siasa. Kwa kufuatilia chaguzi za ndani ya vyama atakuwa na uwezo wa kuamua nani awe kiongozi wa chama.

Sheria hiyo mpya pia itampa Msajili mamlaka ya kuziingilia katiba za vyama na hata kuamuru chama cha siasa kiirekebishe katiba yake katika muda wa miezi sita, ikiwa ataona kuwa hayo anayotaka yarekebishwe hayalingani na masharti ya Sheria.

Akitaka, Msajili anaweza akadai apewe taarifa yoyote kutoka chama cha siasa, kiongozi au mwanachama yeyote juu ya chama hicho.

Hata uendeshaji wa elimu ya uraia utakuwa chini yake. Inadhaniwa kwamba lengo ni kuzuia ushirikiano wa vyama rafiki, hasa vitokavyo nje ya nchi.

Kwenda kinyume na masharti ya elimu ya uraia kunaweza kupelekea kutozwa faini ya juu ya shilingi milioni 30 au kifungo kisichopungua miezi sita.

Uamuzi wa Msajili na maofisa wake ni wa mwisho na hawawezi kufunguliwa mashitaka. Wamewekewa kinga hiyo licha ya kwamba wanaweza wakayatumia vibaya madaraka yao.

Ni dhahir kwamba macho ya Chama cha Mapinduzi na serikali yake yanauangalia uchaguzi mkuu ujao wa 2020. Ndio maana Sheria iliyopendekezwa itampa waziri anayehusika na vyama vya siasa mamlaka ya kuamua juu ya ushirikiano wa vyama vya siasa.

Tathmini ya mkato ya wachambuzi wa ndani na nje ya nchi kuhusu afya ya demokrasia ya vyama vingi Tanzania ni kwamba demokrasia hiyo ni mahututi.

Tanzania ya leo sio tena ile Tanzania iliyokuwa ikichemka kwa mijadala ya siasa hata katika miaka ya 1960 taifa lilipokuwa chini ya mfumo wa chama kimoja hadi uliporejelewa mfumo wa vyama vingi na baadaye.

Tanzania ya leo ni Tanzania yenye siasa zilizopwaya na zimekuwa zikipwaya polepole tangu ianze awamu ya tano. Kuna sababu zilizozifanya siasa zipwaye. Sababu kubwa ni kuwa mazingira yake yamebadilika na yamekuwa mazingira ya woga.

Naitoshe kusema kwamba serikali inaziogopa siasa, watu wanaziogopa siasa na kuna watu fulani wanaowafanya watu wengi waziogope siasa. Wanafanya hivyo kwa kusudi, kwa sababu zao na kwa maslahi yao.

Hao watu fulani wanawafanya watu waziogope siasa kwa sababu wanataka wao wawe wanaogopwa. Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere, katika tafakari zake, aliligusia suala hili la woga wa kisiasa na viongozi wenye kutaka waogopwe.

Nyerere aliiona hatari ya wananchi kuwanyenyekea viongozi. Kwa mujibu wake madikteta ndio wenye sifa na ada ya kuogopwa. Viongozi wenye kujiona kuwa wao ni viongozi wa umma, huwa hawapendi waogopwe.

Nyerere pia aliwatahadharisha watu wasiwe na mazoea ya kuwatii viongozi katika mambo ya haramu. Katika muktadha wa kisiasa, hasa siasa za kidemokrasia, mambo ya haramu huwa pamoja na kwenda kinyume na katiba ya nchi, kukiuka haki za binadamu, kuyatumia vibaya mahakama, majeshi na polisi.

Nyerere akiamini kwamba kuwatii viongozi katika mambo ya haramu ni dalili ya woga na kwamba kufanya hivyo ni kuukaribisha udikteta.

Bila ya shaka, si watu wote wenye kuogopa kutoa maoni yao na kuyasema yale watawala wasiotaka kuyasikia. Wapo wachache wenye ujasiri wa kujitokeza na kuthubutu kusema bila ya kujali yatayowafika.

Sijui, au pengine najua, nini kilichomfanya John Pombe Magufuli azikanye siasa mara baada ya kuchaguliwa Rais wa Tanzania. Nadhani anaziogopa.

Anazoziogopa ni siasa za wapinzani wake kwa sababu yeye amekuwa akiziongoza za chama chake lakini alichofanya ni kuwazuia wapinzani wasiendelee na harakati zao za kisiasa.

Alijipa haki ya kufanya uamuzi wa ajabu kwamba wakati wa siasa ulikwisha baada ya yeye kuchaguliwa rais. Akakiuka katiba ya nchi kwa kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Akasema kuwa siasa zitaanza tena kwenye kampeni ya kuwania uchaguzi ujao wa 2020. Aonavyo yeye ni kwamba wakati huu ni wakati wa kufanya kazi za kuleta maendeleo nchini. Inawezekana kwamba hajui nini maana ya “siasa” au anajua lakini anaziona kuwa zinawababaisha wananchi wasishughulikie maendeleo yao.

Naye si kiongozi peke yake mwenye msimamo huo. Kila kukicha tunashuhudia njama zaidi za watawala wa nchi kadhaa za Kiafrika za kuufanya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ama udhoufike au ufe kabisa.

Katika baadhi ya nchi si vyama vya siasa bali ni asasi zisizo za kiserikali zinazoshika bendera za upinzani zikiwa pamoja na wanaharakati wa mrengo wa kushoto.

Siku hizi ni nadra kuvisikia vyama vya siasa vikipaza sauti za itikadi za mrengo wa kushoto. Hili ni jambo lenye kushangaza na kutia wasiwasi.

Linatia wasiwasi kwa sababu kukosekana kwa sauti hizo ni kukosekana sauti mbadala ya zile zenye kuipigia debe itikadi moja. Itikadi yenyewe ikiwa ileile yenye kuhubiriwa na vyama vya serikali na vya upinzani.

Linashangaza kwa sababu katika enzi za ukoloni wanaharakati wa mrengo wa kushoto ndio waliokuwa safu ya mbele katika harakati za kupigania uhuru.

Si hayo tu lakini hata baada ya ukoloni kufurushwa, mataifa huru ya Kiafrika yalipojikuta yametekwa na ukoloni mamboleo walikuwa ni wao wanaharakati wa mrengo wa kushoto waliojitokeza kuongoza harakati za kupigania haki, usawa na utawala wa sheria.

Kaulimbiu yao ilikuwa “ukombozi wa pili”. Waliamini kwamba palikuwa na haja ya kuongoza vuguvugu dhidi ya mfumo uliokuwako wa chama kimoja cha siasa, dhidi ya udikteta na dhidi ya taasisi za kimataifa, zikiwa pamoja na Benki ya Dunia, ambazo zikionekana kuwa na ajenda ya kuziingilia chumi za nchi za Kiafrika kwa mlango wa nyuma na kuzifisidi kwa maslahi ya ubepari wa kimataifa.

Wanaharakati hao wa mrengo wa kushoto waliungwa mkono na wasanii, wakiwa pamoja na wachoraji, waimbaji, washairi, waandishi wa riwaya, makasisi na mashekhe wa kimapinduzi.

Katika baadhi ya nchi palifanywa juhudi za kuzifufua harakati za wakulima na wafanyakazi wa mijini waliokuwa hawana tena wa kuwatetea kwa vile vyama vyao vilikuwa vimekabwa au vilikuwa vimepigwa marufuku kabisa katika nchi zilizokuwa na mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Kuna wanaharakati wa mrengo wa kushoto katika baadhi ya nchi wenye kuhoji kwamba wanaweza kuzipenyeza fikra zao za kiitikadi katika vyama vikuu vilivyo katika nchi zao. Wanafikiri kwamba kwa kufanya hivyo wataweza kuleta mapinduzi ya kifikra ndani ya vyama hivyo licha ya kuwa vyama vyenyewe ni vya mrengo wa kulia. Hadi sasa jitihada zao hazijafanikiwa.

Ninawajua wanaharakati katika nchi kadhaa za Kiafrika waliojaribu kujiingiza katika vyama vikuu nchini mwao. Lililotokea ni kwamba badala ya wao kuweza kuvibadili vyama vyao vipya, hivyo vyama viliwabadili wao. Viliwageuza dagaa vikawameza. Wanazungumza lugha ileile ya mahasimu wao wa kiitikadi na wanazitetea sera zilezile walizokuwa wakizipinga walipokuwa nje ya vyama hivyo.

Siku hizi siasa za mrengo wa kushoto zimekuwa kama zilizokufa katika nyingi ya nchi za Kiafrika. Hakuna vyama vikuu vya siasa vinavyohubiri kwa dhati itikadi ya mrengo wa kushoto. Takriban kote Afrika kwenye vyama vingi vya siasa, vyama hivyo vinafuata itikadi moja: itikadi ya ulibirali mamboleo. Itikadi hii imejikita zaidi juu ya sera za kiuchumi.

Kweli wanaharakati hao wana kazi kubwa ya kuwapata wafuasi. Lazima tukubali kwamba siku hizi siasa za mrengo wa kushoto haziwavutii wengi barani Afrika. Waafrika wengi wamezugwa waamini kwamba sera pekee zitazoweza kuziokoa nchi zao ni zile za ulibirali mamboleo. Wamezugwa, nao wakazugika.
 
Kwa nini Mtikila alifariki? Yaani angekuwa hai sijui ingekuwa aje. Wakati mwingine najiuliza kama ajali ilificha ukweli wa kifo chake.
 
Kweli kabisa, hii sheria ni ya kuua chama ambazo ni za upizani, lakini madictator wengi duniani huwa wanajioni wao ni kaa miungu ya kuabudiwa, mimi vile naona magufuli anaona kaa ataishi milele, lakini hakuna ajuae kesho,ombi langu ni moja , mungu kwa njia aiujuae yeye weyewe amuondoe magufuli hata kaa ni kwa hii dunia, hawezi haribu maisha ya watanzania zaidi ya 55milioni
 
Kwa nini Mtikila alifariki? Yaani angekuwa hai sijui ingekuwa aje. Wakati mwingine najiuliza kama ajali ilificha ukweli wa kifo chake.
Mwingine ni mbunge wa Bihalamulo mzee Kasusura alikuwa mwiba ndani ya Tanu na CCM yenyewe. Tuntemeke Sanga, yule aliyeanzisha group jina nimesahau wa mbeya au Iringa baadaye akapewa uwaziri akanyamazishwa. Kulikuwa na watu wakiongea bungeni wakati huo tunalisikiliza na pesa zetu za kodi ambazo sasa tumeambiwa hazitoshi kusikiliza bunge live!
 
Ukiangalia kwa jujuu unaweza fikiri hizo sheria zinakandamiza vyama vya siasa tu. Ukweli ni kwamba demokrasia inapigwa chini ili dola ianue mambo yake ya dhuruma bila kupigiwa kelele na wakandamizwaji. Anglia issue ya watumishi wastaafu, dola kupitia bunge imeamua kukata hela za mstaafu na kumpa 25% tu. Wanafanya hivyo bila hofu kwa kuwa wamewanyamazisha wapiga kelele na wala hawana hofu ya upinzani wa jambo hilo.
 
Back
Top Bottom