Msumbiji: Wanajeshi waukomboa mji wa Palma wanamgambo wauawa

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,001
9,866
Jeshi la Msumbiji linasema kuwa limeukomboa mji wa pwani wa Palma, ikiwa ni wiki moja toka ulipotekwa na wanamgambo wa Kiislamu.

Idadi 'kubwa' ya wanamgambo wameuawa katika shambulio la kuukomboa mji huo, msemaji wa jeshi ameeleza.

Radio ya taifa hilo inaripoti kuwa wakaazi waliokumbia mji huo wameanza kurejea - baadhi wakikuta nyumba zao zikiwa zimeporwa vilivyomo.

Makumi ya raia waliuawa huku zaidi ya 11,000 wakilazimika kuyakimbia makazi yao baada ya wanamgambo hao kuvamia mji huo Machi 24.

Raia mmoja wa Afrika Kusini na Uingereza ni baadhi ya watu waliouawa katika shambulio hilo ambalo ni kubwa zaidi toka wanamgambo hao walipoanzisha uasi wao mwaka 2017 katika jimbo la Kaskazini la Cabo Delgado.

Mawasiliano baina ya mji huo wenye wakaazi 75,000 na sehemu nyengine za nchi bado hayapo.

Kwanini ni vigumu kukabiliana na kundi la IS Msumbiji?

Je, Msumbuji inageuka kuwa ngome ya IS?

Wanamgambo hao ambao wanafahamika na wenyeji wa Cabo Delgado kama al-Shabab ni wafuasi wa kundi la kigaidi la Islamic State (IS).

Shambulio hilo limeilazimu kampuni kubwa ya mafuta ulimwenguni Total kusimamisha mradi wa mabilioni ya dola wa gesi asilia katika eneo la Afungi, umbali mfupi kutoka mji wa Palma.

Maelezo ya picha,
Ujumbe wa kutaka msaada ulionekana katika viwanja vya hoteli ya Amarula mjini Palma

Total iliwaondosha wafanyakazi wake Ijumaa, huku Umoja wa Mataifa ukisitisha safari za ndege za kuwaondosha raia katika eneo hilo kutokana na sababu za kiusalama.

Msemaji wa jeshi, Brigedia Chongo Vidigal amesema mtambo wa gesi upo salama na mji wa Palma pia upo salama.

"Kiwanja cha ndege ndio eneo pekee ambalo tulihitaji kulikomboa na tulifanya hivyo (Jumapili). Ni salama kabisa," Brig Vidigal amenukuliwa akisema na AFP.

Katika mkanda wa kwanza wa video kutoka Palma baada ya kukombolewa, televisheni ya taifa imepeperusha picha za wanajeshi wakizifunika maiti na mifuko myeusi ya plastiki mitaani, anaripoti mwandishi wa BBC Jose Tembe kutoka mji mkuu wa Maputo.

Japo baadhi ya wakaazi wanaripotiwa kuanza kurejea, mitaa ya mji huo ilikuwa kama imetekelezwa kwa kutokuwa na watu.

Hospitali ya mji huo, mabenki na ofisi ya mwendesha mashtaka zote zimeharibiwa, anaeleza ripota wetu.

Gavana wa Cabo Delgado, Valgy Tauabo, alizuru Palma siku ya Jumapili na kuahidi kusaidia wakaazi kuyajenga tena maisha yao.

"Kwa sasa tunahamia katika hatua inayofuata, hatua muhimu zaidi, ambapo tutawakaribisha wakaazi ambao walikimbilia msituni," ameeleza Brig Vidigal.

Maelfu ya wakaazi wengine waliukimbia mji huo kwa mashua kuelekea katika makao makuu ya jimbo hilo, mji wa Pemba.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom